...kwanini hatuchangii Elimu?
" Siku hizi hata sherehe ya
ubarikio zinachapishwa kadi na
kusambazwa, sherehe ya mahafali
na bethidei mambo na hivyo hivyo.
Na jamii yetu iko tayari kabisa
kuchanga kwa ajili ya sherehe ya
siku moja.
Wanajamii wenzangu,
ninashangazwa jinsi tulivyo na
umoja huu wa kuchangishana
kwenye sherehe mbalimbali,
ambako wengine wetu hufanya kwa
sifa ili tuonekane tunazo na
kusifiwa sana. Tunachanga ili
tukale na kunywa siku moja,
tunasahau.
Lakini linapokuja suala la
kuchangia maendeleo, watu wale
wale wanaochanga maelfu kwa
mamilioni kwa ajili ya shughuli za
maendeleo yetu ndio huwa wa
kwanza kubeza na kusema kwamba
wao hawahusiki, bali serikali ndiyo
yenye wajibu wa kuchangia.
Fikiria kijiji kina mashine ya maji,
lakini mashine hii imekosa kipuri
kidogo tu ambacho kikifungwa
itapona na jamii itapata huduma ya
maji. Wananchi hawako tayari
kuchanga fedha kwa ajili ya
huduma hii ya kudumu, bali
wanaitaka serikali ndiyo ije
iwatengenezee.
Watoto wetu wanaketi kwenye
vumbi kwa sababu hakuna
madawati, shule zetu nyingi za
vijijini zinakosa walimu makini kwa
sababu wengi wanakataa kuja kwa
kuwa hakuna nyumba za kuishi
walimu, watoto hawana rejea
yoyote kwa kuwa vitabu hakuna,
lakini mbaya zaidi, shule zetu
hazina hata chaki!
Mwanajamii huyu anayaona yote
haya, lakini anasema siyo jukumu
lake, bali ni la serikali. Sikatai,
kwamba serikali ina wajibu mkubwa
wa kuhakikisha huduma zinawafikia
wanajamii wake. Lakini hivi hata
kujenga ukuta wa choo cha shule
tusubiri serikali ije itujengee? Sisi
wanajamii hatuyaoni hayo?
Mbona kwenye sherehe hatusemi
bwana na bibi harusi ndio wajibu
wao kutuandalia chakula na
vinywaji, sisi hatuna haja ya
kuchangia? Mbona tunakuwa
wepesi wa kutafuta sifa ya mara
moja badala ya kufikiria mipango ya
maendeleo yetu?"