Kwa sisi Wakristo, ukisoma Kitabu cha Mwanzo 1:28 Biblia inasema, "Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi na kuitiisha;...".
Sikatai kwamba tunaweza tukaziliana bila ndoa, lakini huu ni uzinzi ambao ni dhambi machoni pa Mungu, na watoto ambao ni zao la uzinzi ni chukizo kwa Mungu. Soma 1Wakorintho 7:1-2, neno la Mungu linasema, "...heri mwanamume asimguse mwanamke. Lakini kwasababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe" (mume au mke anayezungumziwa hapa ni yule wa ndoa).
Ukisoma Mithali 18:22 neno linasema, "Apataye mke apata kitu chema, naye ajipatia kibali kwa Bwana".
Kibali ni nini? Kibali ni hali ya kukubalika katika jambo/kitu fulani. Kumbe ukioa unapata kibali kutoka kwa Mungu, hii ina maana hakuna jambo/kitu ambacho utatia mkono wako kisifanikiwe.
Kwanini vijana tunadanganyana kwamba tusioe?
Shida ni moja tu, mifarakano kwenye Taasisi ya ndoa ndiyo imesababisha kampeni hii huku wanaume tukiwatupia lawama wanawake kwamba wao ndiyo chanzo cha mifarakano hii, jambo ambalo si kweli.
Ukisoma 1Petro 3:7 neno linasema, "Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe". Acha kushindana na mwanamke, Biblia imeshasema kwamba mwanamke ni chombo kisicho na nguvu, usishindane naye.
Sasa ni wanaume wangapi wanakaa na wake zao kwa akili? Wangapi wanawapa wake zao heshima kama neno linavyotufundisha? Wangapi hawashindani nao? Interesting part ya andiko hilo hapo juu ni kwamba ukilitii au ukilitimiza basi KUOMBA KWAKO HAKUTAZUILIWA, yani hakuna kitu utaomba kwa Mungu kisitimie, hapa najifunza kwamba wake zetu wanabeba mafanikio yetu endapo tukiwaheshimu na kuishi nao kwa akili.
Aidha, ukisoma 1Petro 3:1, wanawake wanaaswa KUTUTII WAUME ZAO. Sasa ni wanawake wangapi wanawatii waume zao? Lakini pia ukisoma Mithali 14:1 Biblia inasema "Mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake, bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe". Je, ni wanawake wangapi wenye hekima za kujenga nyumba zao kwa kutofuata ushauri mbaya wanaoshauriwa na marafiki zao ambao pengine wao hawajaolewa?
Hapa najifunza kwamba kila upande (ME na KE) unapaswa kuishi kwenye misingi yake ili Taasisi ya ndoa ilete tija iliyokusudiwa. Shida haiko kwa wanaume au wanawake tu; ingawa kuna upande unaweza ukawa una matatizo zaidi.
Niwe mkweli tu, upande wenye matatizo zaidi ni upande wetu wa ME. Mwanamke ukimpenda, ukimthamini, ukimtunza kwa kadiri ya kipato chako, ukimheshimu, NAKUHAKIKISHIA kwamba mwanamke huyu hawezi kukukosea heshima. Ukiona mwanamke amekengeuka ujue kuna shida mahali, na kwa kawaida mwanamke huwa anapenda mara moja tu, akichoka amechoka, huwa harudi nyuma.
Ni rai yangu kwa wanaume wenzangu kwamba tusiogope kuoa. Na unapomtafuta mwenza nakusihi usitumie macho na hekima ya kibinadamu bali umtangulize Mungu mbele. Usioe makalio, sura n.k. Sura siyo roho; kwamba akiwa na sura nzuri basi ana roho nzuri.
Mimi sijaoa ila I am on the way. Niko single but seriously searching. Mungu atusaidie vijana wote wenye dhamira ya dhati ya kuoa. Muwe na week end njema.