TAARIFA YA MBUNGE WA KIGAMBONI DKT FAUSTINE NDUGULILE KUHUSU MIRADI YA MAENDELEO KIGAMBONI
Napenda kutoa taarifa ya wapi tulipofikia kwenye utekelezaji wa miradi tuliyokubaliana kwenye kikao chetu.
1. Barabara ya kutoka Darajani hadi kwa Msomali
Mkandarasi ameshapatikana kazi ya ujenzi kuanza muda wowote kuanzia sasa.
2. Upatikanaji wa nguzo za umeme
Kumekuwa na changamoto wa upatikanaji wa nguzo za moto mdogo (Low Tension-LT) toka Tanesco Makao Makuu. Nguzo za umeme mkubwa (High Tension-HT) zipo. Kazi ya usambazaji wa umeme mkubwa unaendelea. Kazi ya kuunganisha umeme majumbani unasuasua kutokana na uhaba wa nguzo. Mara ya mwisho Wilaya ya Kigamboni ilipata nguzo 50 wakati mahitaji no zaidi ya nguzo 500. Ninaendelea kufuatilia ili mgawo wa nguzo uongezeke.
3. Barabara ya Feri-Tungi-Kisiwani-Kibada
Zabuni ya barabara hii ilitangazwa mapema mwaka huu. Hadi zabuni zinafunguliwa ni kampuni moja ilijitokeza na gharama zake zilikuwa juu sana.
Gharama zimekuwa juu kutokana na hali ya upatikanaji wa kifusi kutokuwa na uhakika baada ya kuzuia machimbo katika Wilaya Mpya ya Kigamboni.
Hata hivyo, kama Uongozi wa Wilaya tumeshakubaliana kuhusu kuwa na maeneo mahsusi ya uchimbaji kifusi ambayo yatasimamiwa na Halmashauri na kwa ajili ya miundombinu ya Halmashauri na ile ya Tanroads.
Baada ya maafikiano haya, ninatarajia zabuni hii itatangazwa tena baada ya kupata uhakika wa upatikanaji wa kifusi.
4. Barabara ya Feri-Mjimwema-Kimbiji-P'Mnazi
Barabara hii itaendelea kujengwa. Makisio ya gharama yapo kwenye bajeti itakayowasilishwa Bungeni hivi karibuni.
5. Barabara ya Kibada-Mwasonga-Kimbiji
Kazi ya usanifu na upembuzi yakinifu unaendelea kwa saaa. Hakuna maoteo ya kujenga barabara hii kwa mwaka wa fedha 2017/18. Tunajaribu kuangalia wapi tunaweza kupata hela ya kujenga barabara yote kwa mpigo.
6. Suala la Kituo kidogo cha umeme
Ununuzi wa eneo umekamilika. Bajeti ya ujenzi wa kituo iko kwenye bajeti ya mwaka 2017/18 ambayo utekelezaji wake unaanza Julai 2017.
Aidha, maeneo ambayo hayana umeme tumeyaingiza kwenye mradi wa REA awamu ya Tatu. Tunasubiri utekelezaji baada ya kuzinduliwa.
Aidha, tunatarajia kukatika katika kwa umeme kutapungua sana baada ya vituo cha kupoozea umeme cha Mbagala na Kurasini vitakapokamilika.
Umeme tunaopata unaanzia Kipawa na unahudumia baadhi ya maeneo ya Ilala, Temeke, Mbagala yote, Mkuranga yote na Kigamboni yoye.
Mfano, jana umeme ulikatika jana usiku kutokana na tatizo lililotokea huko Tazara.
Ujenzi wa kituo cha Kigamboni ndio suluhu ya kudumu.
Suala la utitiri wa leseni, wavuvi kupewa nyenzo na uvuvi haramu nililifikisha kwa Waziri wa Sekta. Nikiri sijapata mrejesho wa kutosheleza kuleta majibu. Ninaendelea kufuatilia.
Dkt Faustine Ndugulile Mb
Mbunge
15.04.2017