Waandishi Wetu
HabariLeo; Saturday,March 10, 2007 @00:07
MAHAKAMA Kuu imeagiza Jeshi la Polisi kuchukua hatua haraka dhidi ya waliohusika kumpitisha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile-Mzuzuri katika mlango wa kuingilia majaji wa mahakama hiyo. Imesema iwapo polisi watazembea kuwachuliwa hatua, yenyewe itachukua hatua za kisheria dhidi yao.
Msajili wa Mahakama Kuu, Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Prophir Lyimo aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa bado mahakama inalitathimini suala hilo la mlango huo kutumiwa na mshitakiwa, kitendo ambacho hakijawahi kufanyika nchini na ni kinyume cha taratibu na sheria za mahakama.
Alisisitiza kuwa polisi walifanya makosa kumpitisha mlangoni hapo Ditopile-Mzuzuri anayekabiliwa na kesi ya kuumua bila kukusudia, dereva wa daladala, Hassan Mbonde.
Hakuna mshitakiwa yeyote aliyewahi kupitishwa katika mlango huo ambao hutumiwa na majaji pekee. Polisi walifanya makosa makubwa kumpitisha mshitakiwa hapo na waliingilia na kuvuruga utaratibu wa Mahakama, alisema Lyimo.
Alisema pia kuwa Mahakama wiki ijayo itatoa tamko juu ya vurugu zinazodaiwa kusababishwa na ndugu wa Ditopile-Mzuzuri dhidi ya waandishi wa habari na wapiga picha. Polisi waliokuwa katika sare na raia wanaodaiwa kuwa ndugu zake Ditopile - Mzuzuri walimpitisha katika mlango wa majaji kwa nguvu baada ya kudaiwa kumpiga kikumbo mlinzi wa Mahakama Kuu.
Mlinzi huyo naye alisikika akieleza kuwa anahofia kupoteza kazi baada ya kuamriwa kuandika barua ya kujieleza alikuwa wapi wakati lango hilo likitumika kwa watu wasio majaji.
Jumatano ya wiki hii, Ditopile- Mzuzuri alipelekwa mahakamani hapo akiwa amechelewa na kurudishwa tena rumande Keko na ilielezwa kuwa gari aina ya Baloon iliyompeleka hapo iliegesha upande huo wa majaji hadi ilipoondoka. Naye Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, ameiomba radhi Mahakama Kuu na waandishi wa habari kutokana na vitendo vya vurugu na uvunjaji wa sheria vilivyotokea wakati wa kesi ya Ditopile-
Mzuzuri juzi.
Tibaigana alisema amekwisha kuliagiza jeshi lake kufungua jalada kwa ajili ya uchunguzi utakaoliwezesha kuchukua hatua za nidhamu dhidi ya wote waliohusika, ikibainika walitenda makosa.
Kamanda huyo pia aliwaonya ndugu wa mtuhumiwa Ditopile Mzuzuri kwa kitendo chao cha kufanya vurugu katika eneo la Mahakama na kuwatahadharisha kuwa kitendo hicho kikitokea tena asilaumiwe yeye binafsi kwa hatua atakazochukua dhidi yao.
Nawapa pole wote mliopatwa na adha hii lakini pia napenda kuwaonya ndugu wa mtuhumiwa kwa vitendo vyao vya ubabe waliovionyesha. Watambue kuwa kesi ni kesi, sasa hivi Ditopile-Mzuzuri atakuwa anakuja mahakamani mwenyewe bila usimamizi wa polisi kwa sababu ya dhamana. Wakifanya tena vurugu, wasimlaumu Tibaigana kwa hatua atakayowachukuliwa, alisema.
Alisema kujaa mahakamani hapo na kusababisha vurugu hizo inaonyesha dhahiri ndugu hao wa Ditopile- Mzuzuri walijua ndugu yao angetolewa kwa dhamana, jambo ambalo lilimshangaza Tibaigana.
Alisema kwa mujibu wa taarifa alizopewa na askari hao, uamuzi wa kumpitisha Ditopile-Mzuzuri katika mlango huo wa nyuma wa jengo la Mahakama Kuu, ulitokana na taarifa walizopata askari hao walipokuwa gerezani kuwa mahakamani hapo kumejaa watu.
Kesi hii tangu mwanzo imekuwa na mvuto mkubwa kwa wananchi hali ambayo tangu mwanzo imekuwa ikiwapa shida askari kudhibiti hali ya usalama wakiwamo ndugu zake mtuhumiwa, alisema Tibaigana.
Aliwataka wajirudi akisema si vema polisi kuonyeshana ubabe na familia hiyo na pia hadhani kama ni sawa jeshi hilo kutumia askari wengi kushughulikia ulinzi wa mtu mmoja. Ditopile-Mzuzuri anakabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia dereva wa daladala Hassan Mbonde, Novemba 4, mwaka jana .
Naye Ikunda Erick anaripoti kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP), Christopher Mtikila amesema vurugu na kuwapiga waandishi zilizofanywa juzi eneo la Mahakama Kuu zilifanywa na polisi waliovaa kiraia.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mtikila alisema polisi waliovaa sare na wengine waliovaa kiraia ndiyo walihusika kufanya vurugu kwa kile kilichoelezwa ni kuwapa hofu wananchi wasihoji masuala ya kesi hiyo.