Maimamu Dar wamjia juu Rais Kikwete, Mtikila
na Prisca Nsemwa
KAMATI ya Maimamu wa Kiislamu, wamewajia juu Rais Jakaya Kikwete na Mchungaji Christopher Mtikila katika masuala mawili nyeti.
Kubwa lililosababisha maimamu hao kumjia kuu Rais Kikwete ni kushindwa kwa serikali yake kuanzisha Mahakama ya Kadhi kama ilivyoahidiwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2005.
Maimamu hao walimlaumu Kikwete na CCM kwa kile walichokieleza kutumia ajenda ya kuanzisha Mahakama ya Kadhi ili kujihakikishia kura zao kabla ya kuiweka ahadi hiyo kando.
Kwa upande wa Mtikila, maimamu hao, walieleza kushangazwa na uamuzi wa kiongozi huyo wa kisiasa kuivalia njuga kesi inayomkabilia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditoplie Mzuzuri.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Msikiti wa Mtoro jana, Katibu wa Kamati ya Maimamu, Sheikh Khalifa Khamisi, alimtaka Rais Kikwete kuhakikisha anatekeleza haraka, ahadi yake ya kuanzisha Mahakama ya Kadhi.
Sheikh Khamis alisema kuwa ahadi hiyo iliwavuta Waislamu wengi ambao walimchagua Kikwete kwa matarajio kuwa hamu yao ya kuwa na mahakama yao, itatimia. Hata hivyo, Sheikh Khamis alisema kuwa muda unapita sasa na hakuna dalili kuwa Kikwete ana mpango wa kutekeleza ahadi hiyo hivyo wameona ni vema wamkumbushe.
Alisema kuwa ni vema Kikwete akahakikisha kuwa Mahakama ya Kadhi inaanzishwa kama alivyoahidi la sivyo, watazidai kura zao kwani walizitoa wakiwa na matumaini kuwa zitawasaidia kupata chombo hicho muhimu katika masuala ya dini yao.
Alisema kuwa mahakama hiyo ni jambo la msingi kwa Waislamu na ndiyo maana hawakutilia maanani ahadi zilizotolewa na wagombea wengine wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita.
Tunashangaa sana, tunaona shule zinajengwa na misaada inapelekwa katika mikoa mbalimbali kuwasaidia watu wenye shida, lakini Mahakama ya Kadhi imesahaulika. Sasa ahadi hii isipotimizwa kura zetu tulizompa Kikwete tutazitaka, alisema Sheikh Khamis.
Alisema wakati ahadi nyingine zikitekelezwa moja baada ya nyingine, suala la Mahakama ya Kadhi limesahaulika kabisa. Alisema kuwa kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi kutawasaidia Waislamu kote nchini, kwa kuwa itashughulikia mambo ya ndoa, mirathi na mambo mengine yatakayowahusu Waislamu.
Sheikh Khamis alipogeukia suala la Mchungaji Mtikila, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Democratic, alimtaka aache mara moja kujihusisha na kesi inayomhusu Ditopile. Sheikh Khamis alisema Waislamu na watu wengine wote wanatambua kuwa tuhuma zinazomkabili Ditopile ni za jinai na inapendeza kuona kuwa suala hilo lililokwishafikishwa katika mahakama ambacho ndicho chombo kinachoshughulikia masuala ya kijinai likiachwa huko huko.
Mtikila hana haja ya kuingilia uwezo wa mahakama kuhusu kesi ya Ditopile, anatakiwa asubiri (uamuzi wa mahakama) ndipo akate rufaa
haina haja kwa wanasiasa kujiingiza kwenye kesi hiyo, waiachie mahakama ifanye kazi yake, alisema Khamis.
Kauli hiyo inakuja wakati Mtikila akiwa ameshatangaza azima yake ya kufungua kesi mahakamani kupinga kubadilishwa kwa mashitaka yanayomkabili Ditopile kutoka mauaji na kuwa mauaji ya bila kukusudia.
Katika hoja zake, Mtikila anaeleza kuwa duniani kote, hakuna kosa lijulikanalo kama mauaji bila kukusudia bali linalotambulika ni la mauaji. Jaji anayesikiliza kesi ndiye mwenye uwezo wa kutamka baada ya kusikiliza ushahidi wote kuwa mtuhumiwa hakuua kwa kukusudia
tunashangaa, mwendesha mashitaka amepata wapi mamlaka ya kuamua kuwa Ditopile aliua bila kukusudia, alisema Mtikila alipozungumza na gazeti hili juzi.
Hata hivyo, Sheikh Khamis alisema kuwa Mtikila hana uwezo wa kuilazimisha mahakama kufanya kazi kama anavyotaka yeye, bali mahakama inafuata taratibu za kisheria.
Alisema kuwa si kwamba Waislamu wanamtetea Ditopile, bali katika uongozi wake hakuwahi kupatikana na tuhuma za ujambazi wala ukatili, na kuamini kuwa tukio hilo lilikuwa ni bahati mbaya.
Aidha, alisema hakuna sababu za kuonyesha chuki kwa Ditopile na mahakama inatakiwa ipewe fursa ya kufuata sheria inavyosema kabla ya kufanya maamuzi yanayostahili.
dini nayo imo...