Sijui wewe ni wa imani ipi ila kama imani yako iko kwenye maandiko ya Biblia basi hicho unachota sio fungu la kumi.
Twende taratibu nitakuonesha fungu la kumi ni nini kisha utajua kwanini ninasema hicho unachotoa sio fungu la kumi.
Kwa mara ya kwanza fungu la kumi limeandikwa katika Biblia kwenye kitabu cha Mwanzo 14:20, ambapo Abraham akampatia Mfalme wa Salemu, ambaye alikuwa ni Kuhani wa Mungu aliye juu sana aliyeitwa Melkizedeki fungu la kumi la nyara zote alizozipata kutokana na ushindi katika vita alivyopigana.
Sasa turudi nyuma kidogo kabla ya Abraham kutoa fungu la kumi nini kilitokea mpaka Abrahamu akatoa fungu la kumi?
Abrahamu alikuwa na mpwa wake aliyeitwa Lutu aliyekaa Sodoma. Kulikuwa na vita baina ya falme (Sodoma, Gomora, Adma, Seboimu na Bela) famle tano zilishindana na falme nne (Elamu, Goimu, Shinari, Elasari) na hizi tano zikapigwa na ufalme wa Sodoma na Gomora mahali ambapo Lutu alikuwa anakaa wakachukuliwa mateka na kila kitu walicho nacho kikanyang’anywa soma Mwanzo 14:1-14
Abrahamu aliposikia kwamba Lutu nduguye ametekwa na mali zake zote zimechukuliwa akatoka ili kumkomboa ndugu yake akiwa na vijakazi wake akawafuata na kuwapiga na kumkomboa ndugu yake Lutu na alifanikiwa kurudisha vyote. Alipokuwa njiani kurudi nyumbani kwake akiwa na mateka wake na mali zao mfalme wa Salemu Melkizedeki akaleta mkate na divai kisha akasema Abraham na abarikiwe na Mungu aliye juu sana Muumba wa Mbingu na nchi, Ahidimiwe Mungu aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako (Mwanzo 14:19-20)
Kumbuka Abrahamu alienda kupigana na majeshi ya nchi nne yaliyo zishinda nchi tano na Abrahamu hakuwa na jeshi bali vijana mia tatu na kumi na nane waliozaliwa kwenye nyumba yake, kitendo cha Abrahamu kuwapiga majeshi ya nchi nne tena akiwa hana jeshi kilimfanya Mungu amtume Melkizedeki kumkumbusha Abrahamu kwamba si yeye Abrahamu amewapiga wale Wafalme bali Mungu aliemtangulia ndio amewapiga wale Wafalme. Kwasababu hiyo Abrahamu aliamua kumtolea Mungu fungu la kumi la mali yote aliyoipata kama ishara ya kutambua ukuu wa Mungu aliovyomshindia katika vita yake na kwasababu Mungu haonekani Abrahamu alimpa Melkizedeki hilo fungu la kumi sababu Melkizdedki alikuwa kuhani wa Mungu aliye juu sana.
Utaona kuwa Melkizedeki alimbariki Abrahamu kisha Abrahamu akampa fungu la kumi. Hivyo sehemu ya kwanza fungu la kumi linatolewa kwa mtumishi wa Mungu na mtumishi wa Mungu anatakiwa kutamka maneno ya baraka kwa mtoaji. Ongeza na andiko la msisitizo Hesabu 18:21-24 Mungu ameweka mkazo fungu la kumi ni urithi wa Walawi ambao ni watumishi wa Mungu.
Sehemu ya Pili ya kutoa fungu la kumi tunaipata Malaki 3: 8-12 Mungu ametutaka tutoe zaka kamili nyumbani mwake ambapo kimsingi ndipo watumishi wa Mungu wanapatikana.
Hivyo ni makossa kutoa fungu la kumi nje na hapo na pia ni makossa kutoa fungu la kumi pungufu. Hatari ya kutoa fungu la kumi pungufu tunaisoma katika Matendo ya Mitume 5:1-10 Anania na mkewe walikufa sababu walidanganya katika kutoa fungu la kumi.
Fungu la kumi sio Sadaka hivyo usitoe kama upendavyo ni amri na utekelezaji wake ni wa kisheria. Wala usichepushe kwa kuwapa wale unaoona wanafaa. Fungu la kumi linalipwa kwa;
1. Mtumishi wa Mungu na yeye anapaswa kumshukuru Mungu kwa ajili yako na kisha kukubariki.
mfano;
Baba yako wa Kiroho
Mchungaji
Askofu
Nabii
Mwalimu wa neo la Mungu
Mwinjilisti
Mtume
Kuhani
2. Kanisani ili itumike katika ujenzi wa ufalme wa Mungu
Sadaka hazina ahadi ya Mungu ila fungu la kumi lina ahadi ya Mungu juu ya kufanikiwa kwetu. Lipa zaka kamili na ukumbuke na dhabihu ili ufanikiwe katika Maisha yako. Mungu wa Bwana wangu Yesu Kristo akubariki sana.