Kwanza unisamehe kwa kuchelewa kukujibu swali lako ila wakati wa Mungu ni wakati sahihi zaidi. Turudi kwenye swali lako katika agano jipya wapi Yesu alifundisha kuhusu kutoa zaka? Kama kawaida twende taratibu mpaka tupate kweli yote imeandikwa tena mtaifahamu, nayo iyo kweli itawaweka huru na kweli ni neno la Mungu.
Mathayo 23:23 Ole wenu walimu wa sheria nanyi Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki!
Mnampa Mungu sehemu ya kumi ya chakula mnachopata, hata mnanaa, binzari na jira Lakini hamtii mambo ya muhimu katika mafundisho ya sheria; kuishi kwa haki, kuwa wenye huruma, na kuwa waaminifu. Haya ndiyo mambo mnayopaswa kufanya.
Na mwendelee pia kufanya mambo hayo mengine.
Haya ni maneno ya Yesu mwenyewe alipokuwa akisema na waandishi na mafarisayo Yesu alikuwa akiwaambia wafarisayo kuwa wao mafarisayo wanalipa zaka ya kila wapatacho lakini hawatii mambo ya muhimu. Yesu alikuwa anawaonya mafarisayo kwamba wanashika vitu flani flani na kuacha vitu vya muhimu zaidi kama kuishi kwa haki, kuwa na huruma na kuwa waaminifu lakini pia aliendelea kusisitiza waendelee pia kufanya na hayo mengine ambayo ni yapi? (Mnampa Mungu sehemu ya kumi ya chakula mnachopata, hata mnanaa, binzari na jira). Hivyo kwa andiko hili Yesu anatuambia pamoja na kuwa tunapaswa kulipa zaka lakini ni muhimu sana kuishi kwa haki, kuwa wenye huruma, na kuwa waaminifu. Tambua ya kuwa zaka haikupeleki mbinguni, zaka itakufanikisha hapa duniani tu.
Zaka imetajwa tena katika Luka 18:9-12 9 Walikuwepo baadhi ya watu waliojiona kuwa wenye haki na waliwadharau wengine. Yesu alitumia simulizi hii kuwafundisha: 10 “Siku moja Farisayo na mtoza ushuru walikwenda Hekaluni kuomba. 11 Farisayo alisimama peke yake mbali na mtoza ushuru. Farisayo aliomba akisema, ‘Ee Mungu, ninakushukuru kwa kuwa mimi si mwovu kama watu wengine. Mimi siyo kama wezi, waongo au wazinzi. Ninakushukuru kwa kuwa mimi ni bora kuliko huyu mtoza ushuru. 12 Ninafunga mara mbili kwa wiki na kutoa sehemu ya kumi ya vyote ninavyopata!’
Yesu alitoa mfano wa Farisayo na mtoza ushuru yule Farisayo alijigamba maana aliona anafanya yote kwa usahihi na Yesu hakukosoa kufanya hayo bali akosoa kujikweza kwa yule mfarisayo.
Kwa muda wako utasoma Waebrania 7: 1-6 ili ujue kwanini haipaswi kutoa fungu la kumi kwa kila mtu isipo kuwa kwa watumishi wa Mungu au kanisani tu.
Asante na Ubarikiwe sana