Kimahesabu serikali yetu imefanya jambo la maana sana maana piga ua bandari yetu itakuwa chaguo rahisi kwa Rwanda Burundi na DRC, hata kama ya Lamu itakuwa kubwa na nzuri kiasi gani. Arguments za Zitto ni za kisiasa tu, ndio maana akiposto huwa harudi kuleta ufafanuzi.
'Bongolander' nimekusoma kwa makini sana.
Naomba nitumie hoja yako hapa nami nieleze ninavyoona yanayojifunua kuhusu Bandari zetu hizi za Afrika Mashariki - yaani,
Mombasa, Dar es Salaam na sasa Lamu. Na pengine hapo baadae Bagamoyo.
Imani yangu ni kwamba Bagamoyo itajengwa, kama sio chini ya utawala huu wa Magufuli, tawala zitakazofuata lazima Bagamoyo (au mbadala wake), kama kule Mwambani Tanga. Vinginevyo tutakuwa tumekubali kuwaachia Kenya uwanja, wacheze wenyewe wanavyopenda.
Bandari ya Dar es Salaam haina nafasi kabisa katika ushindani huo peke yake.
Ningeweza kuchora ramani hapa ningetumia kukupa picha halisi ya biashara ya bandari itakavyokuwa katika ukanda huu, tokea sasa na kwenda mbele. Lakini ngoja nieleze tu, na unaweza ukatoa ramani kufuatilia ninayoyaeleza.
Bandari ya Lamu (bila ya ushindani) itakuwa mhimu sana. Meli kubwa zenye uwezo wa kupakia makasha zaidi ya 20,000 zitaitumia bandari hiyo, hasa kutoka China na nchi nyingi za maeneo ya huko. Haya mameli makubwa kituo chao kitakuwa Lamu. Makasha yatapakuliwa na kupakiwa kwenye meli ndogo ndogo zitakazosambaza kwenye bandari kama Mombasa, Dar es Slaam, na kwingineko. Hili sote sasa tunalijua vizuri.
Sasa ngoja nikupe habari ya Mombasa, ambayo wengi bado hatujaiwekea maanani, lakini wenzetu Kenya tayari wamelinasa vizuri sana.
Mombasa itakuwa Bandari mhimu sana (kuliko Dar es Salaam mara dufu), katika kusambaza mizigo toka Lamu na kuipeleka Kenya kwenyewe; Uganda, Sudan Kusini, TANZANIA, Burundi, Rwanda, DRC.
Hapa ndipo inapokupasa uchukue ramani ya maeneo ya nchi hizi na kuisoma vizuri. Eneo lote la Kaskazini mwa Tanzania litakuwa eneo la kusambazia mizigo na kupitisha mizigo toka Bandari ya Mombasa. Nazungumzia mikoa hii yote ya Tanzania kuhudumiwa na Mombasa, na sio Dar es Salaam: Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida, Shinyanga, Simiyu, Mara, Mwanza, Geita, Kagera... Tazama ramani. Kuna barabara nzuri kabisa ya lami tupu, toka Mombasa, Voi, Taita Taveta, inavuka mpaka pale Holili, inaingia Moshi, Arusha, inateremka chini kuja kuunganisha Singida. Tokea hapo, inapandisha kuelekea Shinyanga na kutokomea zake kwenda Rwanda na Burundi.
Barabara hii ni fupi, kuliko kutoka Dar es Salaam.
Hiyo ni mosi.
Bandari ya Kisumu imefanyiwa ukarabati mkubwa na tayari imekwisha kamilika inasubiri tu kuzinduliwa. Meli kubwa la mizigo, MV Uhuru, nalo limekarabatiwa na tayari linasafiri kwenda Port Bell Uganda.
Ziwa Victoria itakuwa njia nzuri sana ya kusambazia mizigo toka Bandari ya Mombasa hadi mikoa yote ya Tanzania inayolizunguka ziwa - Mara, Mwanza, Simiyu, Geita na Kagera. Mikoa hii nayo ipo karibu na Mombasa kuliko ilivyo karibu na Dar es Salaam.
Sasa lililobaki ni wewe, na wengine kunieleza kwamba sheria haitawaruhusu Mombasa kusambaza mizigo yao Tanzania.
Kama sheria hii ipo, itabidi mnieleze, na kwa maoni yangu ni kwamba, sheria hiyo itakuwa inapingana na kila kitu kinachosimamiwa katika umoja wetu wa EAC. Je, tutaamua kupinga na kujiondoa kwenye umoja huo?
Mfanya biashara yeyote hutafuta njia nafuu ya kufanya biashara yake. Mombasa wamekwishaweka miundombinu bora ya kusambaza mizigo; nasi pia tumewasaidia kwa kuwajengea barabara za kupitisha mizigo yao kwa urahisi, hadi kufikia nchi jirani za Burundi, Rwanda na Congo.
Nadhani nimekwishajieleza vya kutosha. Ngoja niishie hapa nisiwachoshe. Ambayo sikuyasema hapa jazieni wenyewe kuangalia fursa tuliyowapatia Kenya, na hasa kama tutaendelea kuchelewa kuijenga Bagamoyo au Bandari nyingine yoyote mbadala wake.
Dar es Salaam itaendelea kuhudumia mikoa iliyokaribu nayo, na nchi za jirani kama Zambia Malawi, na Kusini mwa Congo.