KUNA KITU SERIKALI HAISEMI KUHUSU CORONA. NATAMANI KUKISIKIA..
Na, Robert Heriel.
Mara nyingi namsikiaga Mhe. Rais Magufuli akisemaga kuwa "Tanzania tunaweza" Ni kauli ya kiume, yenye matumaini na yenye mtazamo chanya kifikra. Napenda watu wenye mitazamo wa namna hiyo.
Rais Magufuli kama kiongozi wa nchi kwa sasa, ameweza kukabiliana na changamoto lukuki, na sasa tupo na huyu Corona ambaye tayari athari zake kiuchumi tumeanza kuziona.
Nimependa hatua zilizochukuliwa na serikali, na naunga mkono kwa 90%, japo nisingeshauri shule, na vyuo vifungwe lakini sio mbaya kwa kuwa kila kiongozi anamuono wake.
Tokea Corona ianze nimesikia matamko mengi kutoka kwa serikali, viongozi wa dini,vyombo vya habari, na wananchi kwa ujumla. Kila mtu kwa nafasi yake na maoni yake ameweza kuzungumzia kuhusu janga hili la Corona. Wapo wanaochukulia ni jambo hatari na wapo wanaoona ni jambo la kawaida mpaka kufikia kulifanyia mzaha. Ni sawa kwenye jamii lazima kuwe na makundi tofauti lakini haimaanishi utofauti wa kuvunja sheria.
Serikali imekuwa mstari wa mbele kutoa tahadhari, ni sawa kabisa.
Serikali imekuwa iktoa kila siku taarifa ya kile kinachojiri kuhusu waathirika wapya wa Corona, ni sawa kabisa.
Serikali imekuwa mstari wa mbele kuwaonya, kukaripia na kuwatisha wale wote watakaoleta mzaha, kupotosha, watakao kujipatia faida kwenye biashara za sanitizer, Ni sawa kabisa.
Serikali imekuwa mstari wa mbele kabisa, kuelimisha na kuwapa wananchi uelewa wa jinsi ya kujikinga na Corona, Ni sawa kabisa.
Serikali imekuwa mstari wa mbele, kuwahudumia, kuchukua hatua za chapuchapu kwa wale wote watakao shukiwa kuwa na maambukizi na kuwapa ushirikiano, ni sawa kabisa.
Serikali imekuwa mstari wa mbele kuwafariji na kuwapa matumaini wananchi kuwa wasiingiwe na hofu, waendelee kuchapa kazi ila wachukue tahadhari, ni sawa kabisa.
Serikali imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na mataifa mengine, iwe kwa kupata maelekezo, ushauri, elimu, msaada au hata mkopo ili kupambana na Corona, ni sawa kabisa.
Licha ya mambo yote hayo lakini kuna jambo serikali sijasikia ikilizungumzia. Binafsi ningelisikia ningefarajika mno. Ingekuwa kama sehemu ya "SISI NI TANZANIA MPYA, TUNAWEZA"
Jambo hili lipo pia kwa magonjw mengine, unaweza sikia kauli zote lakini sio rahisi kulisikia jambo hili.
Serikali sijaisikia ikisema kuwa imeshaandaa wataalamu wa masuala ya afya ambao ndani ya muda miezi mitatu au sita watakuja na chanjo, au dawa, au tiba ya Corona.
Ningefurahi siku moja nikiwa naangalia habari, namuona Ummy Mwalimu, au Waziri Mkuu, Au Mhe Rais au kiongozi yeyote atakayepewa nafasi ya kusema.
Aseme hivi: Ndugu zangu Watanzania, serikali yenu imeandaa wataalamu ambao wamepewa jukumu la kutafuta chanjo, au tiba ya Corona. Tuendelee kuchukua tahadhari, tunauhakika wataalamu wetu watatuletea suluhu, na huyu adui tutammudu. Ahsante"
Watu woyooo!
Tungeshangilia, ni sehemu ya kujiamini kama taifa. Ni sehemu ya kujiona sisi tunaweza kukabiliana na adui yeyote bila kumtegemea yeyote.
Ingekuwa ni kauli ambayo ingetoa muelekeo mpya katika fikra za kizazi kichanga kinachokua. Ni kauli ya kujitegemea, yenye ishara za utawala na mamlaka kamili kama taifa.
Ingefaa, serikali pia ingetangaza donge nono, kwa atakayekuja na tiba ya Corona. Ni sehemu ya kuwaamsha Watanzania na kuitangazia dunia kuwa taifa letu linawatu muhimu kwa dunia ya leo.
Hata matajiri wa Tanzania wangepaswa watangaze dau nono kuwa atakayegundua dawa ya Corona hapa nchini atapewa dau hilo. Ni sehemu ya kuamsha kizazi hiki, kuwa kuna uwezekano wa sisi wenyewe kujitengenezea tiba kwa magonjwa makubwa ya mlipuko kama hili.
Serikali jambo hili ndio limeniuma mno. Sijasikia mkilisema. Hata kama nchi ni haina hela ya kufanya utafiti wa kuvumbua tiba hizo hiyo haizuii matangazo kama hayo. Sio kila dawa inapatikana kwa njia ya kanuni za kitafiti.
Serikali lazima ijenge mazingira ya kufanya jamii ijitegemee hata kwenye mambo makubwa kama haya.
Tusingesikia nchi za wenzetu wakitaka kutufanyia majaribio. Kwani kwa kauli ya kuwa muda wa miezi mitatu tutakuwa tumekuja na tiba ya Corona ingewafanya waone kwamba kumbe hata sisi tunajiamini. Kitendo cha kusema tuu ni dalili ya ujasiri ambao kinachofuata ni vitendo.
Ningefurahi kusikia sauti kutoka kwa wataalamu wa tiba mbadala wakisema wapewe muda wa miezi mitatu watakuja na suluhu. Hiyo ni kujiamini na kuonyesha uwezo. Hata kama hawatakuja na suluhu ya moja kwa moja ila ninauhakika watakuwa wamepiga hatua kwa sehemu kubwa kupitia kuhangaika kwao.
Madaktari waliokosa ajira waliokuwa mtaani, ingependeza kama wangeiambia serikali bila ya woga kuwa, tupewe sehemu na muda wa kutafuta suluhu ya Corona.
Lakini kusubiri wenzetu wazungu wahangaike alafu sisi tusubiri kupewa madawa, sijui chanjo kwa kweli sio wazo la busara hata kidogo. Binafsi siamini kwa nchi yetu yenye watu zaidi ya milion 50 ati hakuna wenye uwezo wa kutatua tatizo la Corona. Kinachotukwamisha ni baadhi ya viongozi wetu wenye kasumba ya kumuona Mtanzania kama mtu ambaye hawezi, viongozi wanaowaamini zaidi wazungu, hawa ndio sumu kwa nchi yetu.
Wakati mkiwaweka washukiwa Karantini, wawekeni pia watu ambao watajitolea kutafuta tiba ya Corona Karantini huko wakatafute dawa.
Msiishie kukariri kuwa tiba ni mpaka sijui utafiti sijui kulingana na kanuni walizoandika watu fulani. Na sisi tunaweza kuandika kanuni zetu za kiutafiti.
Hicho ndicho kitu ambacho serikali haikisemi kuhusu Corona. Kwamba imejipangaje na wataalamu wa Afya kugundua dawa, au tiba ya Corona.
Wasalamu katika kujenga nchi.
Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300 au 0711345431