SURA YA PILI MALENGO MUHIMU, MISINGI YA MWELEKEO WA SHUGHULI ZA SERIKALI NA SERA ZA TAIFA SEHEMU YA KWANZA MALENGO MAKUU
Malengo Makuu
11.-(1) Lengo la Katiba hii ni kulinda, kuimarisha na kudumisha, haki, usawa, udugu, amani, umoja na utangamano wa wananchi wa Jamhuri ya Muungano kwa kuzingatia ustawi wa wananchi na kujenga Taifa huru lenye demokrasia, utawala bora, maendeleo endelevu na kujitegemea.
(2) Bila kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (1), lengo hilo kuu litaendelezwa na kuimarishwa katika nyanja zote kuu, ikijumuisha nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kimazingira.
(3) Bunge litatunga sheria itakayofafanua juu ya utekelezaji wa malengo muhimu kwa mujibu wa Katiba hii.
SEHEMU YA PILI MALENGO YA KISIASA
Lengo la Taifa Kisiasa
12.-(1) Lengo la Katiba hii kisiasa ni kudumisha demokrasia na kuondoa ubaguzi wa aina zote.
(2) Katika kuhakikisha utekelezaji wa lengo hilo, Serikali itachukua hatua zinazofaa ili: (a) kuhakikisha kuwa inazuia na kuondoa dhuluma, vitisho, ubaguzi, unyanyasaji, rushwa, uonevu na upendeleo miongoni mwa wananchi kwa misingi ya itikadi, asili ya mtu, sehemu anayotoka, nasaba, kabila, jinsi, dini au imani yake;
(b) kuhakikisha kuwepo kwa amani na utulivu na kujenga utamaduni wa kuenzi, kuheshimu na kudumisha uzalendo, amani, umoja, utangamano, ushirikiano na uvumilivu wa kisiasa kwa madhumuni ya kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi; na (c) kuhakikisha kuwepo kwa usalama na ustawi wa watu na mali zao. SEHEMU YA
TATU MALENGO YA KIUCHUMI, KIJAMII NA KIUTAMADUNI Lengo la Taifa Kiuchumi
13.-(1) Lengo la Katiba hii kiuchumi ni kujenga uchumi wa kisasa utakaowezesha wananchi na Taifa kujitegemea kwa kuzingatia matumizi ya elimu ya sayansi na teknolojia katika nyanja zote za uzalishaji mali kwa kuhimiza mapinduzi ya kilimo, ufugaji na uvuvi, mapinduzi ya viwanda na kujenga sekta muhimu ya nishati, mawasiliano na miundo mbinu.
(2) Katika kuhakikisha utekelezaji wa lengo hilo, Serikali itachukua hatua zifuatazo:
(a) kuweka na kutekeleza mpango mkakati wa kutoa elimu ya kisasa yenye kusisitiza ubunifu, sayansi na teknolojia kuanzia ngazi ya msingi, sekondari, ufundi na amali hadi vyuo vikuu na katika shughuli za uchumi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla;
(b) kuimarisha na kujenga uwezo wa vyama vya ushirika ili viwe vyombo madhubuti vya kueneza maarifa, mbinu na zana bora za kisasa katika kilimo, ufugaji na uvuvi ili kuongeza tija katika uzalishaji, kutoa mikopo, kutafuta na kuendeleza masoko ya mazao yao;
(c) kuweka utaratibu wa kujenga viwanda vya kati na viwanda vidogo vitakavyosindika na kuchakata bidhaa za kilimo, ufugaji, uvuvi, na madini ili kuziongezea thamani kwa ajili ya mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi;
(d) kuhakikisha kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi wanakuwa na ardhi na nyenzo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao katika kukuza mazingira yaliyo bora kwa ajili ya kuhamasisha sekta binafsi katika uchumi, upangaji na usimamizi wa mizania ya bei za mazao na pembejeo;
(e) kuhamasisha uwekezaji wa pamoja baina ya raia na wasio raia katika miundombinu ya uchumi, uvunaji wa rasilimali na maliasili za Taifa;
(f) kuhakikisha kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo utajiri wa Taifa unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote na kuweka mazingira yatakayochochea maendeleo linganifu na kuwawezesha wananchi kuondokana na umaskini; na
(g) kuweka utaratibu wa usimamizi na udhibiti wa huduma za kijamii ili kuwezesha ushindani wenye haki na ubora wa viwango vya huduma zinazotolewa ili kuwalinda wananchi.
14.-(1) Lengo la Katiba hii kijamii ni kujenga jamii yenye ustawi na uwezo wa kushiriki katika shughuli za kimaendeleo katika nyanja mbalimbali.
(2) Katika utekelezaji wa lengo hilo, Serikali itachukua hatua zinazofaa ili:
(a) kuhakikisha kwamba heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata mila, desturi na Kanuni za Tangazo la Dunia kuhusu Haki za Binadamu na mikataba mingine ya kimataifa iliyoridhiwa na Tanzania;
(b) kuhakikisha kwamba Serikali na vyombo vyake vyote vya umma vinatoa nafasi na fursa sawa kwa raia wote, bila ubaguzi;
(c) kuhakikisha kuwa huduma na hifadhi ya jamii inatolewa kwa watu wasiojiweza, wazee, watoto na watu wenye ulemavu;
(d) kuwezesha upatikanaji na utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za mawakili;
(e) kuweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa haki ya mtu kujipatia elimu na kuwa huru kupata fursa sawa ya kutafuta elimu katika fani anayoipenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na uwezo wake; na
(f) kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora ya afya kwa watu wote ikiwa ni pamoja na afya ya uzazi salama.
Lengo la Taifa Kiutamaduni
15.-(1) Lengo la Katiba hii kiutamaduni ni kukuza, kudumisha na kuhifadhi lugha ya Kiswahili, urithi wa asili na utamaduni wa wananchi.
(2) Katika kuhakikisha utekelezaji wa lengo hilo, Serikali itachukua hatua zinazofaa ili: (a) kulinda na kuendeleza lugha ya Kiswahili;
(b) kulinda na kuhifadhi urithi wa asili, malikale na sehemu zenye umuhimu wa kihistoria ili kuepuka uharibifu, wizi au utoroshaji nje ya nchi;
(c) kulinda, kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wa jamii mbalimbali;
(d) kujenga utamaduni wa kuwepo ushirikiano, maelewano, maridhiano, uvumilivu na kuheshimu mila, desturi na imani ya dini ya kila mtu; na
(e) kuweka mazingira yatakayowezesha wasanii kutumia fursa zilizopo na vipaji vyao katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na mabadiliko katika jamii.
SEHEMU YA NNE
UTAFITI, DIRA YA MAENDELEO, MIPANGO NA UTEKELEZAJI WA MALENGO YA TAIFA Utafiti na Maendeleo
16. Katika kuweka mipango ya Taifa, Serikali itatoa kipaumbele kwenye shughuli za utafiti na maendeleo kwa lengo la kupata taarifa zitakazowezesha upatikanaji wa maendeleo ya kiuchumi nchini.
17.-(1) Kutakuwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo katika nyanja mbalimbali kwa kuzingatia haki na wajibu wa kila raia kupata maendeleo.
(2) Katika kutekeleza ibara ndogo ya
(1), Mamlaka za Serikali zitaweka mipango ya kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo. Tume ya Mipango ya Jamhuri ya Muungano
18.-(1) Kutakuwa na Tume ya Mipango ya Jamhuri ya Muungano itakayoitwa Tume ya Mipango ambayo itakuwa ndicho chombo cha juu cha kupanga na kusimamia utekelezaji wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Taifa.
(2) Bunge litatunga sheria kwa ajili ya utekelezaji wa Ibara hii. Utekelezaji wa Malengo ya Taifa
19.-(1) Malengo ya Taifa yaliyoainishwa ndani ya Katiba hii yatakuwa ni mwongozo kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kwa wananchi katika matumizi au kutafsiri masharti ya Katiba hii au sheria nyingine yoyote au katika utekelezaji wa maamuzi ya kisera kwa madhumuni ya kujenga jamii iliyo bora, huru na makini.
(2) Serikali ya Jamhuri ya Muungano itawasilisha katika Bunge mara moja kwa mwaka, taarifa ya hatua ilizozichukua katika utekelezaji wa malengo ya Taifa. Matumizi ya masharti ya Sura ya Pili
20.-(1) Bila kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (2), Serikali, vyombo vyake vyote na watu au mamlaka yoyote yenye kutekeleza madaraka ya utawala, kutunga sheria au ya utoaji haki, vitakuwa na jukumu na wajibu wa kuzingatia na kutekeleza masharti yote ya Sura hii.
(2) Masharti ya Sura hii hayatatiliwa nguvu ya kisheria na Mahakama yoyote. Mahakama yoyote nchini haitakuwa na uwezo wa kuamua juu ya suala kama kutenda au kukosa kutenda jambo kwa mtu au mahakama yoyote au kama sheria au hukumu yoyote inaambatana na masharti ya Sura hii.
Soma ibara ya 20(2) hapo , hakuna haki za wavujishwa,wafugaji,Wazee, wanawake, uzazi salama, vijana , etc ....ni kuzuiwa Mbuzi kwenye gunia .