Ukweli ni kwamba, hizi kelele za baadhi ya watu kutaka Magufuli aongezewe muda, ni kelele tu za watu wachache ambao ama wanafaidika na huu utawala, au wanatumika na huu utawala kuendesha hiyo kampeni na si vinginevyo.
Ni imani yangu, watanzania wengi wanatamani muda wake uishe aondoke apishe wengine kuanzia wafanyakazi, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji, watu walioko katika sekta ya madini, vijana wanaotafuta ajira, n.k kiasi kwamba hata kura ya maoni ikipigwa leo hii kuhusu swala hili la kumuongezea Magufuli muda wa kukaa madarakani, hawezi pata uungwaji mkono hata wa asilimia 30 ya kura zote zitazopigwa.
Hata baadhi ya aliowapa vyeo nao wanaweza kupiga kura ya kukataa jambo hilo kwani hata wao hawana uhakika wa nafasi zao huku wako ambao na wao wanatamani hiyo- nafasi ya uraisi.
Siamini kabisa kama watu wanafurahia namna Magufuli anavyoendesha hii nchi wakiwemo wana-CCM wenyewe kwani ni wazi kauli za Magufuli na vitendo vyake haviwapendezi wengi na mfano mzuri ni kauli ya hivi karibuni kuhusu madakatri walioacha kazi serikalini na ile ya kuhusu kutoa chakula cha msaada wakati wa njaa kwa wananchi kauli hizi zikiwa ni muendelezo wa kauli zake zenye ukakasi tangu aingie madarakani mwaka 2015.
Ukiacha maswala kama ya kutoongeza wafanyakazi mishahara, wafanyabiashara kubambikiziwa kodi kubwa, mazao ya wakulima kukosa soko,kuminya uhuru wa maoni, kukandamiz demokrasia,vitendo vya utekaji, n.k ,jambo lingine linalommaliza vibaya kisiasa ni ili la kuutangazia umma kuwa hakuna Covid na kuonekana ni kosa kusema mtu fulani kafa kwa corona katika nchi hii wakati mitaani hali inaonekana kuwa ni tofauti.
Jambo lingine linalomuweka pabaya kisiasa ni tuhuma za kutumia fedha za umna kuendeleza sehemu anayotoka (Chato), jambo linaloonekana kuwakera watanzania wengi na hivyo kujiuliza iwapo ataongezewa muda hiyo Chato itakuwaje ukilinganisha na maeneo mengine ya nchi na maswali mengine mengi.
Kwa kifupi, kulingana na mtazamo wangu na ambao naamini ni mtazamo wa watu wengi pia, Magufuli amefeli sana katika swala zima la uongozi na alichoweza ni kuendeleza tu sekta ya ujenzi na miundombinu mambo ambayo hayawezi kumfanya aonekane anastahili kuongezewa muda kwani mahitaji ya watanzania ni zaidi ya miundombinu.
Hivyo, kutokana na sababu hizo na zingine ambazo sikuzitaja(amabazo unaweza kuzitaja), Magufuli hawezi pata uungwaji mkono hata wa asilimia 30 litapokuja swala la kura ya maoni juu ya kumuongezea au kutumuongezea muda wa kukaa madarakani.