Doctor Mama Amon
JF-Expert Member
- Mar 30, 2018
- 2,089
- 2,725
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Mwanza anatafakari kuhusu Ramani ya Kimkakati (Strategy Map) iliyo muhtasari wa ukurasa mmoja wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2021/22 hadi 2025/26 (uk. 70)
Tangu serikali ya wamu ya sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ilipoanza kazi nimekuwa najiuliza maswali yafuatayo, kama sehemu ya kazi yangu ya utafiti wa kawaida kuhusu ujasiriadola nchini Tanzania:
- Serikali ya awamu ya sita inasema kwamba sisi kama nchi tunao utambulisho gani wa kijiografia, kihistoria na kikatiba?
- Serikali ya awamu ya sita inasema kwamba kwa sasa mwaka 2021 sisi kama Taifa tuko wapi?
- Serikali ya awamu ya sita inataka tuwe tumefika wapi ifikapo mwaka 2025?
- Serikali ya awamu ya sita inataka kuchukua hatua gani ili sisi kama Taifa tuweze kufika huko?
- Serikali ya awamu ya sita inataka kutekeleza kazi gani ndani ya kila hatua ya safari yetu?
- Serikali ya awamu ya sita inataka nani achukue hatua gani na lini?
- Serikali ya awamu ya sita inasema kuwa safari yetu ya miaka 5 inahitaji fedha kiasi gani?
- Serikali ya awamu ya sita inafikiri kwamba tutajuaje kuwa tumefika mwisho wa safari yetu ya miaka 5?
Lakini, kabla mpango huo haujakamilishwa wala kuzinduliwa, naona maswali haya yameanza kujibiwa kwa kina kupitia hotuba za Rais.
Tayari Rais Samia amemaliza ziara ya kikazi mkoani mwanza alikokaa kwa siku tatu. Alisema kuwa Kanda ya Ziwa ni Ukanda wa Kiuchumi utakaoitumia Mwanza kama kituo kikubwa cha biashara katika nchi za Maziwa Makuu.
Akiwa huko alizindua miradi na mikakati kadhaa inayoakisi hatua za kimkakati zilizotajwa kwenye Rasimu ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (21/22-25/26). Miradi na mikakati husika iliyozinduliwa ni pamoja na:
- Mradi wa maji wa Misungwi;
- Mradi wa reli ya kimataifa katika ukanda wa Ziwa Viktoria;
- Mradi wa chelezo ya kukarabati meli;
- Mradi wa ujenzi wa daraja la Ziwa Viktoria;
- Mkakati wa kuwawezesha vijana kunufaika na fursa za ajira 8,000,000 zinazotengenezwa na serikali kwa ajili yao;
- Mkakati wa kufuta pengo la kidijitali kati ya wanaume na wanawake (gender digital divide) kwa kujenga shule moja ya kuendeleza Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Sayansi, Ubunifu, Tekinolojia, na Hisabati (SUTH) katika kila mkoa; na
- Mkakati wa kuzalisha ajira kwa vijana wa kike na kiume kupitia miradi mbalimbali ya kitaifa.
Kuhusu ajira, Rais alitaja sekta zifuatazo kama vyanzo vya ajira za vijana hawa: mradi wa umeme wa mwalimu Nyerere, Miradi ya Ujenzi wa Barabara, na Mradi wa bomba la mafuta. Pia alitaja miradi ya kilimo, miradi ya ufugaji, miradi ya uvuvi, na miradi ya TEHAMA inayotekelezwa kupitia ubia wa serikali na sekta.
Aidha, kuhusu suala la ajira, RC David Kafulira alimwahidi Rais Samia kwamba mkoa wake wa Simiyu unakusudia kuchangia 2.5% ya ajira zote, yaani ajira 200,000, kutokana na kuzalisha ajira kupitia minyororo ya ongezeko la thamani ya huduma na bidhaa zilizoko katika sekta mbalimbali mkoani humo.
Kwa mujibu wa hotuba ya jana ya Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwalimu, asilimia baki ya ajira itazalishwa nchini kote katika maeneo yafuatayo: wilaya 126, halmashauri 184, kata 3,956, vijiji 12,319, vitongoji 64,384, na mitaa 4,263.
Na kwa mujibu wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga, katika mwaka 2019, pato la Kanda ya Ziwa lilikuwa TZS bilioni 34, sawa na 25.9% ya Pato la Taifa.
Aidha, Luoga anasema kuwa Kanda ya Ziwa huzalisha zaidi ya 90% ya dhahabu yote nchini, 50% ya pamba na kahawa na zaidi ya 95% ya mauzo ya samaki ndani na nje ya nchi.
Ziara ya Rais Samia huko Kanda ya Ziwa Viktoria ni mwendelezo wa pilika zake za kujipambanua kama mjasiriadola wa kike kwa kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii ili kuwaeleza ndoto aliyo nayo kuhusu Tanzania mpya chini ya serikali ya awamu ya sita.
Kwanza alikutana na wazee kupitia wazee wa Dar es Salaam, kisha akakutana na kina mama kupitia kina mama wa Dodoma, na leo amekutana na vijana kupitia vijana wa Mwanza.
Nimesikiliza hotuba zake zote tangu Dar es Salaam, Dodoma hadi Mwanza. Ni hotuba nzuri kwa ajili ya kueleza ndoto aliyo nayo juu ya Tanzania mpya.
Kutokana na kauli zake nilizozisikia mpaka sasa, Rais anayo majawabu yafuatayo, kwa maswali yaliyotajwa hapo juu:
- Serikali ya awamu ya sita inasema kwamba sisi kama nchi utambuliko wetu wa Kikatiba na Kihistoria ni upi? Serikali inakiri kwamba sisi ni:
- Nchi moja iliyotokana na muungano wa nchi mbili,
- ambayo haifungamani na dini yoyote,
- inayoongozwa kwa mujibu wa kanuni za Jamhuri
- yenye kuhesimu misingi ya demokrasia,
- na yenye kuongozwa na serikali inayopata madaraka kutoka kwa watu.
- Serikali ya awamu ya sita inasema kwamba kwa sasa mwaka 2021 sisi kama Taifa tuko wapi? Serikali inasema kuwa hapa tulipo kuna
- magonjwa,
- ujinga,
- ikolojia duni,
- ofisi za utawala zinazosuasua katika kutoa huduma kwa watu,
- na uchumi usiojali maslahi ya pamoja kwa ajili ya makundi yote ya watu.
- Serikali ya awamu ya sita inataka tuwe tumefika wapi ifikapo mwaka 2025? Serikali inataka kuona kila Mtanzania akiwa na maisha yanayoendana na kipato cha uchumi wa kati , kwa maana ya kipato kinachoweza kuchochea upatikanaji wa
- afya bora,
- elimu bora,
- ikolojia bora,
- ofisi zinazotoa huduma kwa kasi, kwa usawa na kwa wote, katika namna inayoendana na imani ya jamii ya kitaifa ambayo ni msingi wa ujenzi wa jamii ya amani.
- na uchumi unaojali maslahi ya pamoja kwa ajiliya makundi yote ya watu.
- Serikali ya awamu ya sita inataka kuchukua hatua gani ili tuweze kufika huko? Serikali inasema kuwa hatua zifuatazo lazima zichukuliwe:
- Kuchochea maendeleo ya rasilimali watu, usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa makundi yote ya watu wakiwemo vijana, wanawake, wazee, watoto, wajane, yatima na walemavu;
- Kuchochea utajiri wa Taifa kupitia uvunaji wa maliasili, uzalishaji mali, kubuni na kukuza kanda za kiuchumi;
- Ujenzi wa taasisi za kiuchumi, kisiasa na kijamii zinazotoa huduma bora kwa kasi, kwa usawa na kwa wote ;
- Kuimarisha usalama wa nchi na mahusiano ya kimataifa yaliyo bora zaidi;
- Kutunza mazingira na kufanya menejimenti ya mabadiliko ya tabianchi;
- Kujenga imani ya jamii na jamii ya amani kwa kukuza na kuhami mila, maadili na tunu za Taifa;
- Kuweka mipango ya maendeleo yenye kuonyesga bayana vigezo vya ufanisi, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wake.
- Serikali ya awamu ya sita inataka kutekeleza kazi na majukumu gani ndani ya kila hatua ya safari yetu? Serikali inataka kuchukua hatua hizi kwa
- kusimika uongozi bora,
- kujenga mfumo wa sheria unaoruhusu utoaji wa haki,
- kujihusisha na ujenzi wa miundo mbinu wezeshi kama vile upatikanaji wa nishati na maji,
- kukusanya rasilimali fedha,
- kuchochea ushirikishwaji wa makundi yote ya kijamii, na
- kusimamia uwajibika wenye tija na kasi.
- Serikali ya awamu ya sita inataka nani achukue hatua gani na lini? Kwa kuzingatia kalenda ya kazi za serikali, watekelezaji ni:
- Mawaziri na makatibu wakuu,
- Wakurugenzi wa Idara na wakala za serikali,
- Ma-RC na ma-RAS,
- Ma-DC na ma-DAS,
- Ma-DED na wafanyakazi wa halmashauri,
- Ma-DEO, ma-WEO, ma-VEO, ma-MEO, na ma-KEO,
- Wadau wa sekta binafsi yakiwemo makampuni, NGOs, FBO, na Vyombo vya habari,
- Mahakimu, majaji, wasajili wa mahakama, na wanasheria,
- Spika, Katibu wa Bunge, na wabunge,
- Na wadau wa maendeleo wa kimataifa.
- Serikali ya awamu ya sita inasema kuwa safari yetu ya miaka 5 inahitaji fedha kiasi gani? Kiasi cha rasilimali zinazohitajika ni Shilingi trilioni 115 ambazo ni
- bajeti za miaka 5,
- Bajeti za wizara zote,
- Bajeti za Halmashauri zote,
- na bajeti za mawakala wote wa serikali.
- Serikali ya awamu ya sita inafikiri kwamba hatimaye tutajuaje kwamba tumefika mwisho wa safari yetu? Kuna vipimo vya ufanisi vinaandaliwa kwa ajili ya kupima kasi na ufanisi wa
- kila wizara,
- kila Halmashauri,
- kila wakala wa serikali,
- na kwa kila mwaka.
Mpango huu ndio andiko pekee linaloweza kujibu maswali yote hapo juu kwa kina. Hivyo, kwa sasa ni muhimu zaidi kuliko Ilani ya Uchaguzi kwani utafafanua mambo haya kwa kina katika njia inayoruhusu usimamizi na ufuatiliaji. Ilani ya chama ni muhimu, lakini inapaswa kubaki kama "kiambatanisho" kwenye andiko hili muhimu.
Kwako Waziri Mwigulu Lameck Nchemba: Kasi ya Rais Samia ni kubwa kuliko kasi ya Ofisi yako. Kuna kitendeakazi muhimu kinakosekana mikononi mwa Rais--Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (21/22-25/26). Huu ndio waraka pekee unaopaswa kujibu maswali yote hapo juu kwa urefu na upana wake.
Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango
Kwa hiyo basi, changamka kuziba pengo hili ambalo ni kinyume cha mazoea bora ya kiutendaji yanayotutaka kuanza utekelezaji baada ya kukamilisha mipango.
Mnyumbulisho wa Mchoro Unaoonyesha Nadharia ya Mabadiliko katika FYDP III, uk. 70