Rais SSH ni Muislamu, kwa kupitia imani yake hiyo ya kidini hafahamu kwa undani juu ya jina la Simba atokaye katika kabila la Yuda, kuwa ndiye Bwana Yesu Kristo. Wala haamini Kristo alipokuja kwa mara ya kwanza alikuwa ni Mwana wa Mungu yaani mwanakondoo wa Mungu, Masihi, na Mkombozi wa wanadamu dhidi ya mauti, dhambi na kuzimu.
Imani yake haimtambui Bwana Yesu Kristo baada ya kufufuka na kurudi mbinguni sasa ndiye Mungu mwenyewe na Kuhani Mkuu, yaani Mungu na Mwana Kondoo.
Imani yake inamtambua Yesu kuwa ni miongoni mwa mitume, yaani Issa bin Mariam aliyezaliwa chini ya mti wa mtende. Kwa hiyo imani yake wala haitambui kuwa alizaliwa katika zizi la ng'ombe.
Kwa hiyo matumizi ya jina la Simba wa Yuda, na sehemu alipoyatumia yalikuwa hayana ukakasi wowote wenye kuweza kukwaza Wakristo. Ndiyo maana aliweza kuchagiza na maneno mengine kama kujaribu kushika sharubu zake.
Ni vyema tukakumbuka kuwa, serikali yetu haina mfungamano na dini yoyote ile, yaani "secural state" hivyo mwanasiasa awapo jukwaani kama fanani na kutamka maneno ya kisiasa achukuliwe kuwa ana maana ya kufikisha ujumbe wa kisiasa hadhira yake aliyoilenga, na wala si vinginevyo.
Mbona tumewahi kusikia kauli za JK kubatiza watu kwa maji, JPM kubatiza watu kwa moto, na hata sasa SSH kubatiza watu kwa maji na kuwapa faraja na wala hazijasikika lawama za watu kukwazwa kiimani. Ni lazima tuwe na ngozi ngumu na kuweka hoja nzito zenye kubeba "constructive criticisms" ambazo zinaweza kuamsha fikra mpya.