Rais S. S. H na Mange Kimambi pichani.
Nimeona watu wametoa maelezo yenye hisia tofauti kufuatia Mange Kimambi kuonekana katika picha na Mhe. Rais huko nchini Marekani.
Mimi nlifuatilia video inayoonesha namna Watanzania waishio nchini Marekani walivyojitokeza kumpokea Mhe. Rais kwa mahaba makubwa sana akiwamo huyo dada Mange Kimambi. ( Maarufu mtandaoni). Aidha, nimeona katika video, Watanzania mbalimbali wakihangaika kutaka kupata kumbukumbu ya picha na Rais wao mara baada ya kukutana naye. Mmoja kati yao ni huyo Mange Kimambi ambaye anaoneka akitoa simu yake ili apigwe picha na Mhe. Rais wetu.
Inaeleweka dhahiri kuwa, Rais ni Mkuu wa nchi , Amiri jeshi Mkuu, Mfariji Mkuu wa taifa. Vilevile Rais wetu ni mzazi, mama na ni Mlezi. Sisi Wazaramo tuna msemo usemao ' Bozi jako' yaani ukizaa mtoto asiye akili ( bozi) huyo naye ni wa kwako pia. Mama/ mzazi anaweza kuzaa Imamu au Padri, anaweza kuzaa mchumi, mhandisi, mwalimu, daktari, nk hii ikawa furaha sana kwa mzazi. Kwa mkosi tu, mzazi anaweza kuzaa jambazi , kahaba, gaidi, dikteta hata mkwepakodi, hii ikawa huzuni na fedheha. Hata hivyo, mama/ mzazi aliyetimamu kichwani na moyoni hatamkana mwanawe kwa sababu yoyote ile. Na kwamba akipata majanga mtoto huyo mama ataumia na kusikitika sana. Hii ndiyo imekuwa silka na hulka ya kimama siku zote kwa miaka na mikaka . ( Asiye mama anaweza asiilewe vizuri hali hii). Kwa hiyo, kwa maoni yangu, mama ameitumia ile nadharia ya Kiswahili ya 'kiganja kilichonyewa na mtoto akikatwi' au ile ya Wazaramo ya 'Bozi jako'.
Nadharia nyingine huenda imetumika hata kukubali kupiga picha na Mange Kimambi ni ile ya msemo wa Kiswahili ' Mwiba unapoingilia ndipo unapotokea' Mange Kimambi huko nyuma kidogo alionekana akisema vibaya nchi na baadhi ya viongozi wetu kupitia mtandao. Alifanya vibaya sana. ( Bila kujali sababu gani, alikosea), kwa hiyo, kwa kiasi fulani aliichafua taswira ya nchi yetu. Kwa hiyo, huenda mama alitaka yuleyule aliyeichafua taswira ya nchi yetu ndiye huyohuyo aisafishe. 'Mwiba unapoingilia ndipo unapotokea'.
Aidha, tangu dahari, watu wamekuwa wakifanya makosa makubwa na madogo usoni mwa wanadamu na kujisahihisha, kutubu, kuungama, na kujutia makosa yao. Nani anajua, huenda Mange Kimambi naye ameamua kujirudi, kujisahisha, kuungama na kutubu dhidi ya ujinga wake. Kwa mintarafu hii na kwa kanuni ile ya 'kiganja alichonyea mtoto akikatwi', ndiyo maana kwa maoni yangu mama ameamua kukisafisha kiganja chake na kuendelea na maisha.
Hii pia imekuwa ni Falsafa ya mzee Jakaya Kikwete ya kutorithi maadui bali ni busara kutengeneza rafiki wengi zaidi iwezekanavyo. Jamani, ' Bozi jako, mwiba ulipoingilia ndipo utokepo na kiganya alichonyea mtoto akikatwi! Bila shaka picha ile inasema zaidi kuliko maneno yetu. Tuupe muda wakati uwakatike.