Ridhiwani: Familia ilitikisika nilipohojiwa dawa za kulevya
Julieth Kulangwa, Mwananchi 22/03/2017
jkulangwa@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete amesema taarifa za kuitwa kuhojiwa kuhusu tuhuma za kuhusika na biashara ya dawa za kulevya ilitingisha famiilia yake, lakini baba yake Jakaya Kikwete alimtia moyo.
Tofauti na watuhumiwa wengine waliohojiwa kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya, Ridhiwani hakutangazwa hadharani badala yake aliitwa kimyakimya na kuhojiwa na baadaye kuruhusiwa aendelee na shughuli zake baada ya kuonekana hana hatia.
Hata hivyo, katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Ridhiwani alisema JK hakushtushwa na badala yake alimpa nguvu ya kwenda kueleza ukweli .
“Pengine aliamua kuficha hofu yake ili kunitia nguvu,” alisema Ridhiwani.
Ridhiwani alisema alimpigia simu baba yake ambaye wakati huo alikuwa Abidjan nchini Ivory Coast na tofauti na matarajio yake, hakuonekana kushtushwa na badala yake alimtia nguvu.
“Nenda ukawasikilize, wape ushirikiano na uwaambie ukweli. Usiwe na wasiwasi, nakuamini mwanangu na kama ningekuwa na wasiwasi wowote kuhusu wewe, ningekwambia,” alisema Ridhiwani akimkariri baba yake, ambaye aliondoka Ikulu miezi 16 iliyopita.
Pamoja na kupewa moyo na baba yake, Ridhiwani anasema mama yake, Salma Kikwete hakulipokea vizuri suala hilo.
Lakini anasema alijitahidi kumtoa wasiwasi kwa kumhakikishia kuwa hahusiki na hivyo hapaswi kuwa na wasiwasi kwa kuwa ukweli ungejulikana.
“Hata wadogo zangu niliwaambia kuhusu jambo hili ili isije ikatokea wakaliona kwenye magazeti. Walipata mshtuko,” alisema mbunge huyo wa Chalinze.
“Wadogo zangu walighadhibika na walitaka kujua kwanini nimehusishwa, lakini niliwaambia hapa mjini tunaishi kwa namna ambayo huwezi kujua nani rafiki wa kweli.”
Si mama wala wadogo zake tu waliotikiswa na jambo hilo, kwani Ridhiwani anasema hali haikuwa nzuri kwa mkewe. “Mke wangu alitikisika sana, ikawa kazi yangu sasa kumtoa wasiwasi.”
Akizungumzia kutajwa katika orodha hiyo, Ridhiwani aliiambia Mwananchi alishangazwa na kitendo cha mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuweka jina lake kwenye orodha ya watu 97 wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
Alisema kilichomuudhi zaidi ni kuitwa na kuhojiwa kwa zaidi ya saa mbili kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga na baadaye kuambiwa hakuwa na hatia.
Wakati akitangaza majina hayo, Makonda hakumtaja Ridhiwani kama mmoja wa watu waliotakiwa kuhojiwa kuhusu biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
Lakini alisema orodha hiyo pia inajumuisha “watoto wa vigogo” ambao hakuwataja. Makonda alikabidhi majina hayo kwa Kamishna Sianga Februari 13 katika mkutano wake wa tatu kwa waandishi wa habari wa kampeni ya kupambana na dawa za kulevya.
“Sina ugomvi na Makonda, tumekua naye katika chama,” alisema Ridhiwani.
“Sielewi kwanini aliamua kuliweka jina langu. Angeweza hata kuniita na kuniuliza kwa kuwa jambo lenyewe lilikuwa ni tuhuma tu.
“Huwezi kuwaita watu ilimradi kuwaita tu wakati hakuna jambo lolote. Mbaya zaidi naitwa halafu naambiwa hakuna jambo lolote kwangu, (hivyo) naweza kwenda.
“Kama hakuna jambo lolote kwanini nimeitwa, kwanini hawakufanya uchunguzi wa kina kwanza? Sikupenda kuitwa na kuhojiwa kwa zaidi ya saa mbili halafu naambiwa hakuna jambo lolote. Sidhani kama ilikuwa busara.”
Alipoulizwa anahisi ni kwanini alitajwa katika orodha hiyo, Ridhiwani alisema: “Hata mimi sijui, naomba labda nyinyi mkamuulize (Makonda) kwanini alinitaja katika orodha ya watu 97.”
Ridhiwani alisema tangu alipoitwa na kuhojiwa, hajawahi kumuuliza wala kuonana na Makonda, ila kuna marafiki zake walikwenda kwa mkuu huyo wa mkoa kumuuliza na akawaambia si kweli kwamba aliweka jina la mbunge huyo.
Juhudi za Mwananchi kumpata makonda kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa na hata alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi, haikupokelewa na jana ilikuwa imefungwa kwa muda mrefu.
Ahojiwa kwa saa mbili
Makonda, ambaye alianza kwa kutangaza majina ya wasanii akitaka waripoti polisi kwa mahojiano na baadaye kutangaza wanasiasa, wafanyabiashara na viongozi wa dini, alisema awamu ya tatu ingetingisha nchi kwa kuwa ilikuwa na majina ya watoto wa vigogo. Lakini tofauti na awamu mbili za mwanzo, watuhumiwa wa awamu hiyo hawakutangazwa hadharani.
Ridhiwani anaamini kuwa alikuwamo katika orodha ya watu 97 ambayo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda aliikabidhi kwa Sianga, Februari 13.
“Nilipigiwa simu nafikiri ni wiki moja tangu Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda amkabidhi Kamishna Sianga zile document (nyaraka) zilizoonyesha zina majina ya watuhumiwa wa dawa za kulevya,” alisema.
“Nilipigiwa simu Jumapili, nikaambiwa natakiwa kufika kwa mahojiano siku inayofuata yaani Jumatatu.”
Baada ya kufika ofisi za mamlaka hayo, aliambiwa ameitwa kwa sababu yumo katika orodha ya majina waliyonayo ya watu wanaoshukiwa kujihusisha na biashara hiyo.
“Waliniambia tunataka kukusikiliza na sisi tuna yetu ya kukueleza. Niliwaambia mimi nimekuja kusikia kutoka kwenu. Waliniambia ‘sisi tunataka utuambie unafanyafanya vipi?’ Niliwaambia sijawahi hata kuyaona, kushiriki au kumsaidia mtu zaidi ya kuona katika sinema na unajua kwenye sinema huwa vinakuja vikete vya rangi tofauti,” alieleza.
Ridhiwani alisema aliulizwa kuhusu mahali anapopenda kutembelea pamoja na marafiki zake.
“Wakaniuliza kuhusu marafiki zangu, nikawaambia mmeniita mimi kwa hiyo ya wengine siyajui. Bahati nzuri wamekiri kuwa walipopata jina langu na kufanya uchunguzi wao, walijiridhisha kuwa si mimi wala rafiki zangu wanaohusika na biashara hiyo,” alisema.
“Isipokuwa walisema katika maeneo ambayo huwa ninatembelea hawa watu wanaofanya biashara za dawa za kulevya wanakwenda na mimi nikawajibu kuwa maeneo hayo ni ya public (umma) kwa hiyo siwezi kujua. Sikuwa na wasiwasi wowote kwa kuwa sikuwa na jambo la kuficha. Sihusiki kabisa.
“Sikupenda ushauri wao, na maeneo hayo si kwamba nimeanza kwenda jana. Maana yake wananiambia nini kwa sababu hizo hatari wanazoziona sasa huenda zingeweza kutokea zamani kwa kuwa nilikuwa mtoto wa Rais ndio maana walikuwa hawasemi siku zote. Ina maana ningeweza kukamatwa siku za nyuma, heshima ya Rais ingeweza kuharibika au ya mzee.
“Nilihojiwa na watu watatu. Nilikuwa comfortable kwa kuwa sijawahi kushiriki na nilikuwa na majibu sahihi ya chochote ambacho wangeniuliza, hata kama wangeniambia uliingia nyumba ya muuza dawa za kulevya, ningekuwa na jibu kuwa nilifuata hiki au kile. Sikuwa na jambo la kuficha au kutengeneza.
Alipoulizwa ni kipindi gani alianza kutajwa sana katika tuhuma hizo, alisema ni jambo ambalo limekuwa katika miaka mitano ya mwisho wa uongozi wa baba yake na kwamba wakati linatajwa alikuwa analichukulia katika sura tofauti.
“Niliamini watu wanataka kumuumiza mzee wangu na ndivyo nilivyoamini siku zote. Nimeishi kwa kujiamini kwa kuwa nilijua watu walifanya hivyo kwa sababu gani. Nilijua si kitu kinachonigusa moja kwa moja,” alisema Ridhiwani.
“Wakati mwingine watu wanataka kumharibia mzee. Sasa juzi nilipoitwa nikajua kumbe hili jambo linaweza kuwa langu. Waliponiita sikuwa na wasiwasi kwa sababu nilijua ni maneno wanayotoka mtaani tu. ”
Haki itendeke
Ridhiwani alishauri vita hiyo iwe ya haki ili watu wasionewe na kusababisha waanze kuangaliana kwa usoni badala ya jambo husika.
“Jambo linalosumbua ni kujua kweli vita hii inalenga kukomesha dawa za kulevya au kukomoa baadhi ya watu? Tupige vita dawa za kulevya, lakini tuwe na huruma siyo kurudisha watu nyuma kwa kuwanufaisha wachache na wengine wakionekana vituko. Nchi ni yetu sote lazima tuilee vizuri, tufanye haki,” alisema.
Alisema watu wasio na hatia wanaweza kuumizwa kutokana na wanasiasa kuanzisha vita hiyo.
“Unajua mimi pia ni mwanasiasa lakini napenda kujiona mwanasheria zaidi. Wanasiasa wanapotumia nafasi zao kuumiza watu na hadhi zao, kwa mfano mimi sitaki kuamini kama Serikali haijui kama sifanyi biashara hiyo,” alisema.
“Mimi kuandikwa kwenye orodha hizo inaamsha maswali je, unacholenga ni kukomesha dawa za kulevya au kukomesha watu?”
Alisema kama yeye ni mbunge ambaye hadhi yake imejengwa na vizazi vitano vya ukoo wa Kikwete, hali itakuwaje kwa watu wasio na sifa kama zake.
Nini kifanyike?
Ridhiwani alisema ili vita dhidi ya dawa za kulevya ifanikiwe, ni lazima misingi ya haki ifuatwe kwa kila mtu kufanya kazi yake ili kuondoa mkanganyiko unaojitokeza.
“Kuna matatizo katika approach (mbinu iliyotumika). Unajua katika sheria kuna kitu kinaitwa three ways pillars yaani katika jambo lolote lazima kuwe na law makers (watunga sheria), interpreters (wanaotasfiri) na enforcers (wanaosimamia),” alisema.
“Approach iliyotumika inagongana. Sasa hapa unakuta enforcer ndiye yeye anayetengeneza sheria na kushtaki, jambo linaloonekana kuwa la ovyo. La msingi Serikali inatakiwa iliweke vizuri ili tulishinde janga hili. Watu tunaowategemea wangekuwa wajenzi wa nchi hii tunawapoteza. Hali ni mbaya.”
Alisema katika vita hiyo watu wamejigeuza kuwa wakamataji na wanaoshtaki hivyo alimuomba Rais asimamie hilo.
Alisema pia lazima ijulikane nani anafanya nini tofauti na sasa ambako kumekuwa na mwingiliano wa vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi kwa njia tofauti.
“Sirro anakamata, kamishna anakamata. Sasa nani ni nani na anafanya nini? Sirro anatangaza, Sianga kimyakimya. Sianga anafanya uchunguzi, ila kwa Sirro unaitwa Jumanne ufike kituoni Ijumaa baada ya hapo unapelekwa kwa mkemia halafu mahakamani. Hii inachanganya sana na lazima Serikali iharmonise (iweke mwongozo kwa) vyombo hivyo.
Uhusiano na Makonda
Kuhusu uhusiano wake na Makonda alisema haujabadilika baada ya jina lake kuwamo katika orodha yake, lakini anamwachia Mungu kama alitajwa kwa hila.
Alisema pamoja na kuhojiwa kuhusu kashfa hiyo, amefurahi kuwa angalau sasa ukweli umejulikana.
Kwenye orodha ya Makonda Ridhiwani hakuwepo. Sasa hapo Makonda anaingiaje?