Date::11/16/2009Rostam: Nataka uchunguzi mpya, si lazima wawe majaji
Na Ramadhan Semtawa
Mwananchi
MBUNGE wa Igunga, Rostam Aziz amemwambia Spika Samuel Sitta kuwa bado kuna umuhimu wa kuchunguza upya kashfa ya Richmond na kwamba namna au njia ya uchunguzi huo ni jambo jingine.
Rostam, ambaye alitakiwa na kamati teule ya Bunge kujitokeza ili aeleze sababu za Richmond kutumia anuani ya kampuni yake ya Caspian na sababu za kuitafutia kampuni ya ushauri wa mambo ya habari, pia amemwambia Sitta kuwa kama mtu anaweza kuhukumiwa kwa tuhuma, basi hata mbunge huyo wa Urambo Mashariki asingeweza kuwa hapo alipo.
Rostam aliipigia simu Mwananchi mwishoni mwa wiki kutaka kutoa ufafanuzi wa maelezo ya Sitta ya kupinga ushauri wake kuwa liundwe jopo la majaji watatu kuchunguza suala hilo kwa kuwa ana uhakika kuwa kamati teule ya Bunge, ambayo iliongozwa na mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe ilitoa ripoti ya uongo na haikumtendea haki.
Sitta alipinga pendekezo hilo la Rostam akisema kuwa maamuzi ya Bunge hayawezi kuchunguzwa upya na mhimili mwingine wa nchi na akamshangaa Rostam kwa kutaka kujitetea sasa wakati alipewa nafasi hiyo lakini hakuitumia.
Lakini Rostam alisema kama njia ya kutumia majaji ni ngumu, basi hata kuwe na usikilizwaji wa umma pamoja lakini akasisitiza: "Ninachotaka ni haki itendeke... suala la njia ipi itatumika ni jingine kama ya majaji ni ngumu."
Mbunge huyo wa Igunga ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM alizidi kujitetea kuwa hajawahi kupewa haki ya kujitetea bungeni kwani alipotaka kufanya hivyo, Spika alimzuia.
Rostam alisema uamuzi wa kutaka uchunguzi mpya unatokana na ukweli kwamba, kuna nyaraka nyingi za msingi ambazo hazikutumiwa na kamati hiyo teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza utoaji wa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura kwa Kampuni ya Richmond Development LLC mwaka 2006.
Alifafanua kwamba mbali ya kutotumika nyaraka nyingi za msingi, kamati hiyo pia haikutoa haki na muda wa kutosha kwa baadhi ya watu kujieleza (akiwemo yeye) na kuhoji kama watu wanaweza kuhukumiwa bila kujitetea nani atasalimika.
Rostam alitakiwa kwenda kujitetea mbele ya kamati hiyo Desemba 24 mwaka 2007, lakini hakutokea na alijieleza baadaye kuwa kamati ilimwita wakati ikijua kwamba siku hiyo ilikuwa ni siku kuu na hivyo asingeweza kutokea. Hata hivyo, Mwakyembe alisema watu wengine walioitwa siku hiyo, akiwemo mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah walitokea na kuhojiwa.
Akijenga hoja zake kuhusu hukumu ya mtuhumiwa, Rostam alisema hata Spika Sitta aliwahi kukumbana na kashfa mwaka 2001 katika wilaya yake ya Urambo, lakini kamati ya CCM ya mkoa ilikataa kumwajibisha.
"Kama watu wangekuwa wanahukumiwa kwa tuhuma basi Sitta leo hii angekuwa siyo Spika wala mwanachama wa CCM," alidai Rostam.
"Zilikuja tuhuma tena za..., lakini mimi nikauliza kama alipewa haki ya kujitetea, tukaambiwa bado, basi nikasema uamuzi huo ungekuwa batili hivyo isingefaa kumhukumu."
Kuhusu tuhuma za kuhusika kwa kampuni yake ya Caspian, Rostam alisema suala la mawasiliano na Dowans alikwishaweka bayana kwamba linatokana na shughuli za kibiashara na akasema tuhuma kwamba aliwahi kuratibu mawasiliano na Richmond ni uongo na upotoshaji umma.
"Mbona Caspian ilijenga Mwananchi (jengo la Mwananchi Communications linalochapisha gazeti hili), hapa tatizo la mawasiliano linatoka wapi? Lakini pia sijawahi kuwa na mawasiliano na Richmond hata siku moja wala kampuni yangu," alijitetea.
"Kama barua pepe ni ushahidi wa kuhusika na kampuni, je tusemeje kuhusu yeye (Sitta) aliyekuwa na mawasiliano na hata kupendekeza kudhamini utambulisho wa Richmond?"
Spika Sitta alikiri kuileta Richmond kama mwekezaji wakati akiwa mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), lakini baada ya kubainika kuwa kampuni hiyo haina uwezo, ilinyimwa mradi wa bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza mwaka 2004.
Rostam alihoji kwanini Spika hakuwahi kulieleza bunge hata siku moja kuitambua Richmond iwe kwa uzuri au ubaya kwani ndiye aliyewahi kuileta.
"Kwa kuongoza bunge lililoambiwa Richmond ilikuwa kampuni hewa na ya kitapeli ya akina Rostam wakati yeye akijua kuwa hayo hayakuwa ya kweli kwa maana, ni mtu aliye karibu nao (wamiliki wa Richmond) na kutosema kuwa hayo si kweli, hakuwatendea haki wananchi," alisema mfanyabiashara huyo. "Hakutendea haki wananchi, Bunge na wamiliki wa Richmond ambayo aliwahi kuileta akiwa TIC na kudiriki kuwaombea udhamini."