Riwaya: Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta

Riwaya: Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta

Sehemu ya Nane

Sasa ilikatika miezi miwili na wiki moja tangu kumpoteza Asi. Nimefanya juhudi hii na ile kumtafuta lakini sijampata. Likizo yangu pia, ilikuwa imebakiwa na wiki tatu tu. Katika hali ya kukata tamaa, niliamua kwenda kusalimia wagonjwa katika hospitali ya Mwananyamala.

Majira ya saa kumi jioni, mwanamume aliyevalia suti ya kijivu na viatu vyeusi alionekana akipita katika geti la hospitali na kwenda moja kwa moja mpaka katika wodi ya watoto. Hakupata shida kupita getini kwa sababu ya ile suti lakini pia, ule ulikuwa muda wa kuona wagonjwa. Mwanamume huyo, alikuwa mimi Mako. Mtu mwenye jina moja kama mbwa!

Niliingia mpaka ndani ya wodi iliyohudumu watoto wadogo, vitandani walilala watoto na pembeni walikaa wazazi wao. Nilianza kwa kumsalimia mama mmoja aliyekuwa vitanda vya mwanzo karibu na mlango.

“Mama mwanao amepatiwa matibabu,” niliuliza baada ya salamu.

“Hajapatiwa baba, wamesema mpaka helaa!” alijibu Mama wa mtoto, machozi yakimlenga.

“Matibabu ni lazima, pesa italipwa baadae,” nilisema kwa sauti iliyosikika pote mle. Mama mmoja aliyekuwa kitanda cha tatu akadakia, “Mheshimiwa hata mwanangu hajapatiwa matibabu,” kabla sijakaa sawa, bibi mmoja akapaaza sauti, “Mkuu wa mkoa nisaidie mjukuu wangu hajapewa dawa siku ya tatu baba.”

Ama hakika bibi yule sijui aliwaza nini kuniita mkuu wa mkoa! Ni kweli siku tatu zilizopita, mkuu wa mkoa alibadilishwa ama wengine wanasema alitumbuliwa na wananchi hawakumfahamu vyema mkuu wao mpya ambaye hakuwa ameanza kuonekana katika Luninga.

Sasa kitendo cha yeye kuniita mimi mkuu wa mkoa, kiliamsha watu wote wodini mle, macho yao yakawa kwangu hata manesi na madaktari wakanyanyuka katika siti zao wakija mahali niliposimama.

“Nkuu wa Nkoa kaja kwa ku shtukiza… patachimbika humu ndani nakwambia, atatumbuliwa ntu baada ya ntu,” alisema bibi mwingine aliyekuwa anamuuguza mjukuu wake.

“Unapiga simu wapi?” nilimfokea nesi ambaye alionekana kupiga simu kuwaita wakubwa wake. “Usipige simu, usimuite yeyote, hapa nimekuja kwa kushtukiza na nitaingia kila wodi kwa kushtukiza.”

“Sawa mkuu,” walijibu watumishi wale wa afya. Wagonjwa wakatabasamu.

“Sasa sikiliza,” niliendelea. “Wagonjwa watibiwe, pesa italipwa baada ya matibabu, tuhakikishe tunaokoa uhai kwa gharama yoyote. Pesa zipo tu na haziwezi kamwe kufanana na thamani ya uhai wa mwanadamu.”

“Ndiyo mkuu,” walijibu.

“Natoka humu katika ziara yangu hii ya kushtukiza, msipige makelele wala msinifuate, pia msipigiane simu, nakwenda kwenye jengo lile wodi ya wazazi, nawatakia utekelezaji mwema.”

Nilitoka katika wodi ile na kuanza kuelekea wodi ya wazazi. Nilikuwa na hofu kwamba, watu wangeongezeka zaidi, lazima ningegundulika kuwa mimi siyo mkuu wa mkoa. Hii ingekuwa kesi kubwa tena ya aibu. Vilevile sikuwa nimepanga kuwa nitambulike hivyo, ni watu niliowakuta wodini ndiyo walinipachika cheo hicho.

Nilitembea haraka nikazipandisha ngazi za jengo la wodi ya wazazi. Nilikuwa napiga jicho nyuma kwa kuibia, kumbe maelekezo yangu hayakufuatwa, kuna manesi walishapiga simu na nyuma kiasi cha hatua mia mbili, niliona watu wengi wakija nilipo, niliweza kuwatambua watu hao, mmoja wao alikuwa Daktari mkuu wa hospitali hiyo. Alikuwa anakuja nilipo akiongozana na madaktari wengine watano na askari watatu.

Sasa niliiona hatari iliyokuwa inaninyemelea. Daktari mkuu na wenzake wote wasingeshindwa kutambua kuwa mimi sikuwa mkuu wa mkoa hata kama mkuu mpya wa mkoa hakuwa ameanza kuonekana katika Luninga. Wazee hawa wanawafahamu viongozi wote kwani ni jamaa zao.

Nilitembea haraka nikalifikia jengo la wazazi na sasa nilikuwa ndani ya jengo hilo lililo juu kimo cha ghorofa moja. Niliwaacha mbali watu wale lakini nao walikuwa wakija kwa kasi zaidi. Niliingia wodini kama ninayesalimia watu. Jengo hili lina upande wa kushoto na kulia, mimi nilielekea kulia, nikatembea mpaka mwisho na bahati njema, mapokezi hapakuwa na daktari wala nesi na wodi nzima ilikuwa na mgojwa mmoja tu aliyekuwa anaongezwa damu na alilala usingizi.

Nilifungua dirisha kubwa la vioo kisha nikatoka kwa kushuka taratibu, nilipoona kimo cha chini ni kidogo, nilijitupa kikomandoo, kisha kwa kuinama, nikakimbia mpaka ulipo ukuta, nikauparamia kama mjusi na kuukwea mpaka kilele chake, halafu ‘puuu’, nilikuwa nje ya hospitali. Huko nyuma sikujali kama kuna mtu aliniona au hakuniona.

Inaendelea...

Tupate Wadhamini:

Kwa Mahitaji ya kuandikiwa CV, Barua ya Maombi ya Kazi na Masomo kwa Wanafunzi wanaorudia mitihani, Gusa Hapa Tuwasiliane Whatsapp.
Dah, mkuu wa mkoa umeacha taharuki huko
 
Niwatoe hofu wasomaji wangu kuwa, Riwaya hii itaendelea hapa bure, hakuna atakayetozwa hata senti moja. Jumatatu mpaka Ijumaa tutapokea vipande vyetu raha msitarehe. Pengine kusema Whatsapp ni tamaa yangu tu ya kutaka kuwaona wasomaji wangu katika kundi moja.
 
Back
Top Bottom