Sehemu ya 18
Wakiwa wamebakiza hatua themanini na tano kulifikia gari, niliachia risasi mfululizo, risasi zikawapiga miguu yao wakadondoka chini wanaolia kwa maumivu. Lakini kumbe hawakuwa peke yao, ilikuja gari ndogo iliyokuwa wazi kwa nyuma, wakashuka wengine watano, kama wenzao, nao wamevaa viremba vyeusi. Wakamimina risasi mfululizo hata nikashindwa kufanya maamuzi, vioo vya basi letu vikapukutika vyote na nikasikia sauti ya vilio. Haraka sana, wale jamaa waliwaokota wale wenzao kisha wakapanda katika gari ambalo liligeuza haraka na kuanza kurudi walikotoka, nikazimimina risasi kadhaa ili kuwasimamisha, lakini sikuwapata.
Baada ya kuona hali ipo shwari, nilirudi ndani ya basi, nikapokelewa kama shujaa, tukashangilia pamoja. Tulikaguana wote ili tuone kama tupo salama, watu wote walikuwa salama isipokuwa dereva bonge ambaye alilala muda wote kutokana na kupoteza fahamu kwa sababu ya ule mshituko wa risasi. Nilibaini mawazo ya watu na hofu waliyokuwa nayo, dereva ndiyo huyo kapoteza fahamu, nani angeendesha basi ile?
Ukiachilia mbali hofu, palitokea jambo moja la kutisha. Abiria walianza kuwasema vibaya wale askari waoga. Palitokea mzozano mkubwa, askari mmoja akapigwa kofi, mwingine akakimbia akachukua ile silaha aliyoitupa chini, akapiga risasi tano juu halafu akaamrisha watu wote wakae chini. ukimya ukatawala. Halafu akaninyooshea bunduki yake, akanitaka nirudishe silaha ile niliyokuwa nayo nimpe yule askari mwingine. Nikakataa, huku nasogea karibu yake, akaniamrisha nisisogee zaidi lakini alishachelewa. Nilishafika karibu yake, nikaishika bunduka na kuielekeza juu halafu nikampiga teke kali la kifua, akadondoka kama furushi la dhambi. Nikazikamata bunduki zote mbili kisha nikaagiza askari wale wafungwe kamba. Abiria waliwafunga kamba huku wakiwapiga makofi, sikuwazuia, lakini jamaa waliumizwa kidogo japo si kwa kiasi cha kutisha, kilikuwa kiasi cha kuadhibu tu.
Kama nilivyosema awali palikuwa na hofu ya nani angeendesha gari, hata nyuso za abiria zilionyesha wasiwasi huo, naye Dereva Bonge hakuwa na dalili yoyote ya kuamka.
Nilikaa katika kiti cha dereva, nikapiga honi, abiria wakashangilia, askari waoga wakanuna. Basi lenyewe lilikuwa ‘automatic’, nikaliwasha, halafu nikakanyaga breki, nikatia gia, nikakanyaga mafuta, gari likaenda.
Abiria aliyegeuka dereva, niliendesha basi lile nikielekezwa njia za kupita na mhudumu wa basi, kijana huyu kabla hayajatufika maafa, alituhudumia kwa soda moja na biskuti, sasa alikuwa akinielekeza kona za kupita hasa tulipokuwa tunafika eneo lenye njia tatu au nne.
“Asante sana, umetuokoa,” sauti ilisikika, hata bila kugeuza shingo, niliitambua, alikuwa Kijana Msomi. “Tuko pamoja,” nilijibu, nikapiga honi kwa mbwembwe, kijana akarudi kukaa katika nafasi yake.
Baada ya kimbiakimbia nyingi humo njiani, hatimaye tulifika Kolkata, askari walishauri kuwa, badala ya kwenda stendi ya mabasi, tupitie kituo cha polisi ili kutoa taarifa za uhalifu. Sikukaidi, na abiria wengine waliunga mkono, basi nikaliendesha mpaka katika kituo cha polisi, ilikuwa yapata saa nne usiku.
Dereva bonge alirudiwa na fahamu tulipofika kituo cha polisi, mhudumu wa basi akamsimulia ilivyokuwa. Tulishuka, askari waoga wakafunguliwa na kuungana na wenzao kituoni pale, kisha kijana msomi akishirikiana na abiria wengine, akasimulia namna ilivyokuwa.
Baadae watu waliruhusiwa kuondoka, kila mmoja na mzigo wake. Nami nikazipiga hatua nikitafuta mahali pa kulala usiku huo, lakini kabla sijazimaliza hatua tatu, niliitwa na askari, akaniomba niingie ndani.
Tulifika ndani ya kituo, nikakuta askari watatu wengine waliokuwa wananisubiri. Wawili kati yao, walikuwa ni wale askari waoga.
“Ndugu, kwa nini ulipora silaha za askari na kuzitumia kushambulia wahalifu?” aliniuliza askari niliyemkuta kakaa tulivu, kwa kuwa nilikuwa sijakaa, ikabidi nikae kwanza.
“Sikupora silaha za askari, askari walitupa silaha kwa uoga wao wenyewe.”
“Vipi kuhusu kuhamasisha abiria wawashambulie askari hawa?”
“Sikufanya hivyo!”
Askari hakuendelea kunihoji, aliamrisha niwekwe rumande, dakika moja iliyofuata, nilikuwa ndani ya chumba cha rumande, chumba kidogo, kichafu tena kilichokuwa na wahalifu saba.
Ndani ya mahabusu hiyo sikutaka kuzungumza na mtu, kwa vyovyote tusingeelewana. Nilifika nikajiweka katika kona moja, kisha nikaanza kuzipiga hesabu, kitendo cha kuwekwa ndani mule kingetosha kunichelewesha kutoka. Vipi kama mahakamani ningeshindwa kesi na kufungwa? Halafu hiyo kesi yenyewe ingetumia siku ngapi? Niliona siwezi kuchomoka katika mtego ule, ushujaa wote niliofanya haukuthaminiwa, nikaishia kuwekwa rumande!
Inaendelea...
Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp,
Gusa Hapa Kujiunga
Tupate Wadhamini:
Kwa Mahitaji ya kuandikiwa CV, Barua ya Maombi ya Kazi na Masomo kwa Wanafunzi wanaorudia mitihani,
Gusa Hapa Tuwasiliane Whatsapp.