Kwa upande wangu sitokuja kushiriki hilo zoezi kwa sababu kuu zifuatazo:-
1) Tume ya uchaguzi haina uhuru kwa sababu inateuliwa na Mwenyekiti wa chama tawala.
2) Wakurugenzi wa Halmashauri/Miji/ Manispaa, nk wote ni Makada wa CCM na wanayeuliwa na Mwenyekiti wa CCM! Halafu wamepewa jukumu la kuwa wasimamizi ngazi ya Wilaya.
3) Matokeo ya Rais yakishatangazwa, hata yawe feki au yawe na dosari! Bado hayawezi kupingwa mahali popote pale mfano Mahakamani, nk.
4) Vyombo vya dola mfano polisi na usalama wa Taifa wamekuwa wakitumiwa waziwazi kwenye kukinufaisha chama tawala kwa kuwatisha wapiga kura na wagombea wake, kuwalinda Wakurugenzi wanaowatangaza wagombea ambao hawakushinda kihalali, nk.
5) Mara nyingi mshindi wa uchaguzi amekuwa akijulikana hata kabla ya matokeo. Kwa mfano mgombea wa Urais kupitia CCM akishapitishwa na chama chake; tayari huyo anatambulika kuwa Rais mtarajiwa hata kabla ya zoezi la uchaguzi kufanyika.
Kutokana na hizi sababu zangu hapo juu; aisee kupiga kura ni majaliwa. Ni mpaka hapo nitakapo jiridhisha kura yangu itaheshimiwa.
Umejieleza vizuri sana; hata mimi katika mazingira hayo siwezi kupiga kura.
Sasa ngoja nami nikueleze ni wakati gani ni muhimu kabisa kuhimizana kwenda kupiga kura; tena kwa wingi kabisa, na kama ingewezekana hata iwe kwa asili mia ya waTanzania wote wenye sifa ya kupiga kura; ikiwa ni pamoja na kujiandikisha kufanya hivyo.
Nitakwenda kupiga kura na kuhimiza wenzangu wote wakapige kura; hata kama CCM watakuwa wameng'ang'ania yote uliyo yaorodhesha hapo juu, iwapo kutakuwepo na vuguvugu la wananchi (kundi), lililopania kupambana na CCM katika uhalifu wao katika zoezi la upigaji kura.
Kundi hili linaweza kuwa linaongozwa na chama cha siasa, au hata asasi maalum itakayokuwa imejitoa kusimamia uongozi na utekelezaji wa mikakati ya kupambana na CCM.
Kujitokeza kwa wingi kwa waTanzania kupiga kura katika mazingira kama hayo kutawafanya hata CCM wenyewe waogope kufanya uhalifu.
Pia kujitokeza kwa wingi na kupiga kura za kuwakataa CCM hata wizi wa kuziba pengo la kura zilizowakataa litakuwa haliwezekani.
Kujitokeza kwa wingi na kupiga kura kuwakataa CCM, hata hao wateule wanaotumika kuharibu kura za wananchi wataogopa kufanya kazi hiyo.
Kujitokeza kwa wingi na kupiga kura kuwakataa CCM, ni ushahidi utakaokuwa wazi hata kwa mataifa mengine na washiriki wa kutoa misaada wataiona hali hiyo bila kujificha.
Kwa hiyo ni muhimu, kujitokeza kwa wingi wetu kupiga kura nyingi sana kuwakataa CCM, na kujipanga vizuri kukabiliana nao endapo watataka kuendeleza uhalifu katika mazigira hayo.
Jambo la muhimu sana hapa, ni huko kujipanga kwa wananchi, kuwa tayari kulinda kura zao zisiharibiwe.
Ukweli ni huu: pakiwepo na kundi la watu kama laki tano tu, watakaokuwa tayari kujitoa na kusimamia HAKI za waTanzania wenzao katika zoezi hilo la uchaguzi nchi nzima, CCM watakuwa hawana uwezo wa kufanya uhalifu juu ya uchaguzi huo.
Nisisitize tena. Nitahimiza watu wajitokeze kwa wingi sana kwenda kupiga kura iwapo kutakuwepo na chama, au kundi lililo tayari kusimamia haki za wananchi wa nchi hii.
Kutokwenda kupiga kura kukiwa na matumaini hayo, ni kuisaliti nchi yetu; na kuwafanya CCM wazidi kutamba.