Kinachosikitisha ni kwamba kila anayepanda jukwaa kuelezea kinachoitwa umaskini wa Mkoa wa Kagera anakuja na ngonjera za wingi wa maprofesa na ma-PhD holders kutoka mkoani mwetu. Lawama zote zinarundikwa kwa watu hao na Wanakagera kwa jumla.
Huo ndio ukasuku na unafiki wa watawala wetu ambao tumezoea kwa miaka mingi sasa. Watawala wanajifanya kama hawajui chanzo halisi cha kile wanachokiita umasikini uliokithiri mkoani humo. Bila tafakuri yoyote ya "tafiti" zinazodaiwa kufanywa na Serikali, wanakuja tu na porojo za jumlajumla kuhusu "umasikini" huo. Tafiti hizo za kimangumashi hazielezei chanzo cha tatizo la mkoa wa Kagera.
Haziangalii matokeo ya vita vya Kagera na uharibifu wa usalama na miundombinu uliosababishwa na ugomvi wa Serikali na Iddi Amin. Kwamba shughuli za uzalishaji na kiuchumi zilikufa kabisa kutokana na vita hiyo.
Hawaoni kwamba serikali ilikosea (kwa makusudi) kutotangazwa kwa hali ya hatari mkoani humo, kwa maana ya kujenga miundombinu upya na kuwasaidia wanakagera kurudia maisha yao ya kabla ya vita. Hawasemi Serikali ilifunga mpaka na Uganda, hivyo kusitisha shughuli zote za kiuchumi, ambapo soko kuu la mkoa wa Kagera lilikuwa Uganda. Baada ya vita Ukimwi uliotokea Uganda ulimaliza nguvukazi kubwa ya mkoa huo kwa kupuputisha maisha ya maelfu ya nguvukazi wa Kagera.
Wanajifanya hawajui kwamba MV. Bukoba ilizama na kuua mamia ya watu, wengi wao wakiwa Wanakagera. Hapohapo, MV. Victoria "iliharibika" na kufanya Wanakagera kukosa kabisa usafiri wa kuwaunganisha na nchi yao, huku mazao yao ya kiuchumi yakishindwa kusafirishwa kwenda kwenye masoko makubwa ya kibiashara ya hapa nchini kama Mwanza na Dar es Salaam. Serikali haikuona umuhimu wa kuwapa Wanakagera vyombo vingine vya usafiri ili wajimudu kiuchumi.
Ndipo pia ulipoingia "Ugonjwa wa Mnyauko" wa migomba uliopigilia msumari wa mateso na umasikini wa wanakagera. Yapata sasa zaidi ya miaka 15. Je, Serikali ilichukua hatua gani kuwasaidia wakulima wa kilimo cha migomba mkoani Kagera? Hakuna! Wakati huohuo Wanakagera walikatazwa kuuza kahawa yao nchini Uganda ambako walikuwa wanapata bei nzuri kulingana na gharama za uzalishaji. Waliopatikana na uvushaji wa zao hilo waliadhibiwa, ikiwemo vifungo au kufilisiwa, huko kahawa ikilimbikiziwa "tozo" lukuki bila kutilia maanani gharama za wakulima za uzalishaji.
Hiyo ni mifano michache tu ya hujuma ya serikali dhidi ya mkoa wa Kagera kwa miongo mingi sasa. Matokeo yake ni nini, Wananchi wa mkoa wa wa Kagera waliona serikali ilikuwa haiwataki, haiwapendi. Wakasema isiwe taabu, wakaamua kuhamia mikoa nyingine nchini na kuwekeza huko. Je, serikali inajifanya haioni uwekezaji wao mkubwa na uliotukuka katika mikoa mingine nchini, ikiwemo Dar Es Salaam, Mwanza, Arusha na kwingineko?
Serikali imekuwa ikipiga kelele nyingi eti wahaya wameshindwa kujenga soko na kituo cha mabasi mjini Bukoba, ikijifanya haijui kwamba jukumu hilo ni lake na vyombo vyake, ikiwemo TAMISEMI. Kwani vituo vya mabasi na masoko ya Dodoma, Morogoro, Dar Es Salaam, Mwanza na kwingineko vimejengwa na nani kama sio Serikali? Nimalizie kwa kuishauri Serikali kwamba iwekeze mkoani Kagera kama ambavyo imekuwa ikiwekeza sehemu nyingine nchini.
Ikiwekeza Kagera, kama ambavyo Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imepanga kufanya kwa kujenga kitengo cha Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM), mkoani humo, basi itarajie kwamba maprofesa na PhD holders kutoka mkoani Kagera watarudi nyumbani kufaidi fursa za uwekezaji wa serikali. Ni matumaini ya wengi mkoani Kagera kwamba Mkuu mpya wa mkoa wa Kagera, Mhe. Chalamila ataelewa chanzo cha "umasikini wa mkoa wa Kagera."
Changamoto zifuatazo, zinafanya Kagera tuwe nyuma. Tuache visingizio.
1. Ardhi ni ndogo
Kupata mkulima mwenye acre 2 au zaidi ni shida. Maeneo mengi yaliyotumika na jamii kwa kuchungia, kulima nafaka kama karanga n.k. yalichukuliwa na watu wachache wakapanda miti ya mbao, na kuacha watu wengi wakabaki wanahangaika.
2. Utamaduni wa kilimo cha migomba.
Migomba ni utamaduni wa Mhaya. Migomba hii haizalishi tena kwa wingi. Mashamba mengi ni yamechoja. Siyo rahisi kuwashauri watu kung'oa na kupanda mazao yenye tija. Hii ni crop rotation ambayo ingesaidia kurudisha rutuba na kutokomeza mnyauko.
3. Matumizi ya mbolea
Watu wengi wanaamini kwamba, mbolea inaharibu ardhi. Kwa hiyo, mapinduzi ya kilimo kwa kutumia ardhi iliyochoka ni ngumu.
4. Kaitu kaila
Acceptance ya aina mpya ya mazao ni ngumu. Tukubaliane, Mhaya anapenda sana migomba.
Pia, Takwimu zinaonyesha Kagera unaoongoza uzalishaji wa maharage kitaifa. Tatizo kubwa ni kwamba hawalengi soko. Maharage yanalimwa kwa wingi, lakini ni local na mchanganyiko. Yaani kila variety kidogo kidogo kiasi kwamba ukiyachambua na kukusanya, kiasi kinachopatikana hakikidhi soko individually.
5. Vijana na akina baba kutoshiriki kilimo
Mathalani, vijana wengi wilaya ya Missenyi hasa Kiziba na Kibumbilo, wamejikita sana kwenye kunywa
karadarugo ambayo ni starehe ya vijana wengi. Hii inua nguvukazi.
Fursa za masoko
Masoko siyo shida. Kuna kipindi nimeshuhudia mihogo inatoka Lindi na Kigoma kupita Mutukula kwenda South Sudan. Vivyo hivyo, maharage na mahindi kutoka Rukwa na Mbeya. Halafu, wakati wa vita ya Rwanda, Kulikuwa na soko kubwa la WFP. Waliofaidi ni watu wa mbali.
Kuna mashule ya bweni pamoja na majeshini. Maharage yanayotumika huko ni ROZIKOKO. Soko siyo shida.
Kwa hiyo, swala la Stendi au Soko Kuu, havitaongeza chochote kwenye mfuko wa mwananchi. Vitabadili mandhari tu na kuongeza mapato ya serikali. Ni sawa na kuvaa suti huku una njaa.
Ili kubadili wananchi, inatakiwa nguvu kiasi, hasa ya kisiasa. RC ameanza vizuri japo tunataka zaidi action.
Nashauri kampeni kubwa iwe ni kubadili mindset za watu. Mfano, badala ya radio nyingi(Kasibante, Fadeco n.k) kushinda wanajadili mpira na miiziki, wajikite kutoa elimu ya kilimo na uchumi muda mwingi.
Ianzishwe TV station ya Kagera. Hii itakuwa na muda mwingi wa kutoa elimu kwa vitendo. Mpaka sasa kuna watu hawajui hata namna ya kupanda mahindi na maharage kitaalamu!. Watu hawajui kama kuna aina mpya za migomba na kahawa inayogawiwa bure.
Nashauri vikundi vya kilimo, vilivyo na uwezo wa kuunganisha wakulima pamoja, kama kule Kenyana Kilimilile, vipewe elimu na misaada ili kuleta chachu kwa wakulima wengine.
Nashauri pia, Maafisa ugani wapewe mafunzo ambayo ni 'tailor made' kwa ajili ya kupeleka elimu sahihi kwa wakulima.
Inawezekana. Hapo chini ni shamba la maharage katika kijiji cha Kenyana, 2021