Hivi kwa nini hadi sasa serikali bado inafumbia macho ukweli kwamba Tanzania imefikia hali mbaya sana ya maambukizi, kuugua na vifo vinavyotokana na Covid-19? Ni kwa kuwa raisi na voingozi wengine wanaona aibu kukubali ukweli kwa kuwa huko nyuma walitoa kauli zilizoonyesha kwamba Tanzania hatuna Covid-19?
Mtu mwenye busara, kukubali kwamba tulikosea na hali ni mbaya kuliko tulivyofikiria ni jambo la kawaida. Na pia kuna uwezekano kwamba ni kweli huko nyuma tatizo la Covid-19 Tanzania lilikuwa dogo sana, lakini sasa hali zimebadilika, na huenda hata tumeingilia na strain mpya za Covid-19 ambazo huko nyuma hazikuwepo.
Inashangaza sana kwamba hadi sasa taasisi zimeamua kuchukua maamuzi za kutoa matamko yao bila kuwapo tamko rasmi la serikali. Hili ni jambo lisilokubalika hata kidogo, lazima serikali ichukue nafasi ya kwanza katika kuwaongoza watanzania katika janga hili, sio kuachia watu mmoja mmoja, familia au taasisi huku serikali inakaa kimya.
Tunasubiri nini hasa, kwamba tumpoteze raisi, au makamu wa raisi, au spika au mawaziri kadhaa kwa Covid-19 ndio tukiri kwamba tuna tatizo la Corona nchini? Hawa wananchi, wataalamu wetu, wazee wetu, watoto wetu, waume zetu, wake zetu, marafiki zetu nk wanaokufa kila siku wao si muhimu kwa serikali kuona kuna uharaka mno wa kuweka mkakati maalumu?
Labda ni vema kwa wenye utaalamu wa sheria kuanza kufikiria kuwafikisha viongozi wetu Mahakama ya Kimataifa ICC kwa kosa la kuwanyima kimakusudi wananchi haki ya kuendelea kuishi kwa kuacha waambukizwe na kufa kwa Covid-19, ikiwa ni pamoja na kuzuia chanjo. Organization zinazopigania haki za binadamu mnapaswa kuanza kufikiria hili.
Serikali inatakiwa sio tu kutoa maelekezo ya kujilinda kama kuzuia mikusanyiko na kuvaa barakoa, bali pia kuwa na mkakati wa matibabu unaoelweka kwa wanaougua Covid-19. Imefikia mahali ambapo wengi wa wanaogua wanapelekwa hospitali kwa ajili ya kufia huko, kwa kuwa serikali haina mkakati maalumu wa kushughulikia wagonjwa wa Covid-19.
Na pia serikali sasa inabidi ijikite kwenye kupima na kutoa takwimu za wenye virusi, wanaoumwa na wanaokufa kwa Covid-19. Tutakaa kimya hadi lini?
Serikai inapaswa kukumbuka kile wahenga walisema - mficha maradhi mauti humuumbua!