UJENZI wa mfereji wa Suez nchini Misri ulioanza mwaka 1859 jadi 1869 ni mradi ambao awali wengi waliona kama mradi kichaa na wa kupoteza muda.
Ujenzi ulihitaji nguvu kazi kubwa na pesa nyingi kufikia malengo ambayo utawala wa Misri wa wakati huo usingeweza kufanikisha.
Ndio maana mradi ulipoanza, serikali ya Misri (na kampuni ya Suez) ilitumia nguvu za ziada kuwalazimisha raia wake kufanya kazi kwa ujira usiolingana na ukubwa wa kazi zilizofanyika. Walioshiriki katika kuchimba mrefeji huo walijihisi kama watumwa ndani ya nchi yao wenyewe.
Kazi zote za uchimbaji wa mfereji wa Suez zilifanyika kwa kutumia zana za mkono na zilizokuwa duni. Katika hatua za awali majembe, mashoka, sururu na zana nyingine ndizo zilizotumika.
Lakini wazalendo hawa waliendela kubeba jukumu la kukamilisha uchimbaji na uondoaji wa kifusi cha mfereji huo wenye urefu wa kilomita 193.30, sawa na umbali wa kutoka Dar mpaka Morogoro.
Shughuli iliyolalamikiwa na wengi sasa inailetea faida kubwa Misri, vizazi kwa vizazi. Huu ni mradi ambao kiuchumi ulikuwa ni lazima utekelezwe kutokana na uhakika wa kuzalisha faida.
Ni mradi ambao umerahisisha meli kutoka Ulaya, Asia, Afrika na Amerika zitumie mfereji huo kurahisisha ‘maisha’ huku serikali ikitengeneza faida.
Uchumi wa Misri kwa sasa unabebwa kwa kiasi kikubwa na mapato yatokanayo na ushuru wa kupitisha meli za mizigo katika mfereji huo.
Kama vijanawa Misri wa wakati huo wangepinga ujenzi wa mradi huo, kiasi cha zaidi ya Dola bilioni 5.3 (kwa mujibu wa Reuters), zinazoingia kama sehemu ya mapato ya Misri kwa mwaka, zingekuwa ni ndoto.
Taswira inayofanana na hii ya Misri ndio inayoonekana nchini Tanzania. Rais John Magufuli anatengeneza mfereji mpya wa kupitisha mizigo kutoka Bara la Asia kwenda nchi zote za Ukanda wa Kati na kusini maghaibi mwa Afrika.
Ikumbukwe kwamba ripoti mbalimbali za biashara duniani zinaonesha ya kuwa asilimia 90 ya bidhaa zote husafirishwa kwa njia ya maji. Ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ni taswira halisi ya mfereji wa Suez kama wa Misri.
Utakuwa mfereji mpya katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Licha ya mfereji wa Misri kutatua changamoto kubwa ya uchumi wa dunia, bado nchi kama Angola, Congo DRC, Afrika ya Kati, Cameroon, Gabon, Congo, Equatorial Guinea na nyingine nyingi, ni waathirika wa safari za umbali mrefu kusafirisha bidhaa kwenda katika nchi zao.
Suluhisho la urefu na gharama kubwa ya kusafirisha mizigo kupitia Cape Town au mfereji wa Suez nchini Misri kwenda katika nchi hizi ni kutengeneza mfereji mpya wa SUEZ kupitia Tanzania.
Kwenye hoja hii ndipo maudhui makuu ya makala haya yamejikita na hatimaye kupata wazo la kuibatiza reli ya kisasa ya Tanzania kama ‘mfereji mpya wa Suez ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.’
Reli hii itakapokuwa imefika Mwanza, Kigoma, na kwenye mpaka wa Rusumo, Tanzania itakuwa na kazi nyingine muhimu ya kufanya ili lengo la kuwa na mfereji huu mpya wa Suez likamilike.
Kazi muhimu katika hatua hii itakuwa ni kupeleka timu maalumu ya ushawishi, kwenye nchi zote za Afrika Mashariki na Kati, yenye uwezo mkubwa wa kuionesha kivitendo diplomasia ya uchumi.
Reli ya kisasa inayojengwa nchini itakuwa sawa kabisa na kazi ya mfereji wa Suez kwa Tanzania, Afrika Mashariki na Kati, na hata kwa dunia nzima.
Nimewahi kuandika kwamba diplomasia ya uchumi hutegemea mambo kadhaa; uwezo wa nchi kiuchumi, ushawishi wa nchi katika hoja za kimataifa, na nafasi ya nchi katika makundi mbalimbali ya kimataifa.
Katika mambo yote hayo, Tanzania inaweza kuwa na ushawishi mkubwa kutokana na nafasi yake katika ukanda wetu huu.
Tanzania ni miongoni mwa nchi katika ukanda huu inayomiliki eneo kubwa la Pwani ya Bahari ya Hindi na ndio nchi pekee katika ukanda huu inayopakana na nchi nyingi zisizo na bandari (land locked).
Tanzania ndio nchi pekee yenye bandari kubwa bahari ya Hindi inayopakana moja kwa moja na nchi yenye bandari kwenye bahari ya Atlantiki, yaani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Congo DRC).
Tanzania ndio nchi ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na wakati huo huo ni mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Ndio nchi yenye mradi mkubwa wa reli ya kisasa inayotoka bahari ya Hindi na yenye uwezo wa moja kwa moja wa kuziunganisha nchi zaidi ya tano. Hivyo haijawahi kutokea katika historia ya nchi ya Tanzania ambapo diplomasia ya uchumi inahitajika kufanyiwa kazi kivitendo kama wakati huu.
Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati pamoja na viongozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mikutano ya kikanda wanapaswa kufanya kazi ya ziada ili diplomasia hii ya uchumi itamalaki katika kukuza uchumi kupitia mradi wa SGR.
Baada ya SGR kufika Bandari ya Mwanza, mizigo ya Uganda na Sudan Kusini itasafirishwa kwa uharaka na kwa gharama nafuu kutoka bandari ya Dar es Salaam mpaka Mwanza na baadae mabehewa 22 kuingizwa moja kwa moja ndani ya meli za mizigo na kuvushwa mpaka Bandari ya Portbell, Kampala au Jinja.
Kutokea Uganda mzigo wa Sudan Kusini utasafirishwa kwa umbali mfupi na kuwafikia walaji. Ushawishi kwa nchi za Uganda na Sudan Kusini utahitajika ili kuonesha faida kubwa za kiuchumi kwa nchi hizo kwa kusafirisha mizigo kwa SGR kutoka Tanzania.
Reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam ikifika Rusumo, Tanzania itahitaji kushawishi Wanyarwanda na Warundi kuhusu unafuu wa gharama na uharaka wa kusafirisha mizigo kutoka nje ya nchi kwa kutumia reli ya kisasa kutoka Tanzania.
Bidhaa za China, India na hata tende za Uarabuni husafiri kwa umbali mrefu na kwa gharama kubwa kufika Congo DRC, Afrika ya Kati, Angola na baadhi ya nchi nyingine nyingi.
Kama ujenzi wa mfereji huu mpya wa Suez na hasa kutoka mpaka wa Rwanda au Burundi kuelekea bandari ya Matadi nchini Congo DRC kwenye bahari ya Atlantiki ukifanikiwa, soko la Asia na lile la Magharibi mwa Afrika, na lile la bara la Amerika na Mashariki na Kati mwa Afrika yataunganishwa na kuwa mkombozi wa ukanda huu kama mfereji wa Suez wa Misri ulivyoleta unafuu kwa Ulaya na Amerika kuunganishwa na Asia.
Ujenzi wa miradi pacha ya SGR na umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ilipoanza kutekelezwa ilikuwa ndio mwanzo wa ndoto mpya ya Dk John Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi tajiri na yenye uwezo wa kuanza kutoa misaada kwa nchi nyingine.
Utajiri wa Tanzania utaongezeka pia pale njia ya umeme wa ziada utasafirishwa sambamba na mfereji huu mpya wa Suez kuelekea nchi zote ambazo mfereji unaweza kufika, na kuwauzia umeme wale wenye uhitaji.
Ifahamike kuwa juhudi kubwa ya kuifanya reli ya kisasa kuwa mfereji mpya wa Suez iko mikononi mwa Tanzania. Bandari kavu ya Isaka ilipoanzishwa ilikuwa na lengo linalofanana na hili la ujenzi wa mfereji mpya wa Suez ambayo kwa hakika ilifanya kazi kwa ufanisi.
Isaka kwa muda ikawa ni muarobaini wa changamoto za mrundikano wa malori kwenye barabara zetu kutoka nchi nyingi zinazoizunguka Tanzania. Mizigo mingi ya nchi hizo ilichukuliwa kutokea bandarini hapo.
Majasusi wa kiuchumi kutoka ndani na nje ya nchi walifanya kila linalowezekana ili umaarufu wa bandari ya nchi kavu ya Isaka ufutike na hivyo kudhoofisha uchumi wa Tanzania.
Kimantiki, ni jambo lisiloeleweka kwa namna nchi inavyoingia gharama ya ujenzi na ukarabati wa barabara kutokana na uharibifu unaofanywa na wingi wa malori yenye uzito mkubwa yanayokwenda bandari ya Dar es Salaam kuchukua mizigo badala ya mizigo hiyo kuchukuliwa bandari kavu ya Isaka au bandari ya Mwanza.
Mashindano makubwa ya wafanyabiashara duniani ni kuzalisha na kusafirisha bidhaa kwa gharama ya chini kwa kadiri inavyowezekana ili zinapowafikia watumiaji ziuzwe kwa bei ndogo kwa lengo la kuwapa watumiaji nguvu au uwezo wa kununua bidhaa husika.
Ni kampuni au mfanyabiashara yupi asiyehitaji kusafirisha bidhaa kwa bei ya chini ili mzunguko wa bidhaa zake uwe mkubwa? Ni nani asingependa kusafirisha mizigo yake kwa kwa haraka?
Taarifa za kiuchumi na hata zile za wataalamu wanaojenga SGR duniani zinaonesha kuwa usafirishaji kwa kutumia reli ya kisasa hupunguza gharama kwa kiasi kikubwa.
Ninapoandika makala haya, bandari ya Kigoma katika ripoti zake inaonesha kuwa baadhi ya wafanyabiashara kutoka Kaskazini Mashariki mwa nchi ya Congo hunufaika kwa kusafirisha mizigo yao kwa reli ya kati kupitia Bandari ya Kigoma.
Kutoka Kigoma mizigo husafirishwa kwa meli mpaka Burundi na kisha DRC. Amani na usalama wa Tanzania ndio kivutio na mtaji wa kufanya biashara na mataifa yote yanayotuzunguka katika Ukanda wa Kati na Mashariki mwa Afrika.
Ukamilishwaji wa ujenzi wa SGR ya Tanzania inayobeba taswira ya mfereji mpya wa Suez katika ukanda huu utarahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka Mashariki ya mbali na hata kutoka bara la Amerika.
Mizigo kutoka Amerika, India, Uchina, Japan na kutoka nchi nyingine nyingi kwenda Sudan Kusini, Uganda, Zambia, Malawi na nchi zote za ukanda huu itasafirishwa kupitia SGR ya Tanzania na hivyo kukuza uchumi kama ilivyo kwa mfereji wa Suez kule Misri.
Mabilioni ya dola yanayopatikana Misri, yanaweza kupatikana nchini Tanzania kama tutaendelea kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli ili mfereji huu mpya wa Suez ujengwe na kukamilika.
Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili.
Chanzo: Reli ya Kisasa; mfereji mpya wa ‘Suez’ EAC
=======
MY TAKE: Ukijumlisha na bomba la gesi kwenda Uganda na Kenya, na Umeme wa bwawa la Nyerere na uzalishaji wa Chakula unavyoongezeka kwa Nani[emoji23][emoji23][emoji23][emoji23][emoji23]