Wabara tuko imara, kumbukumbu na mantiki,
Siyo siasa uchwara, kwenye haki hatutoki,
Wala huu si mkwara, janja janja hatutaki,
Tujadili ya nchini, siasa huchangamsha!
Mengi yamekwishapita, jahazi lasonga mbele,
Kwa staha tumepita, kimya pasipo kelele,
Ya nini kusita sita, enyi malenga wa kale,
Tujadili ya nchini, siasa huchangamsha!
Siasa huchangamsha, tujadili ya nchini,
Wepesi watachemsha, wabaki wale makini,
Hii siyo kujichosha, na matusi ya wahuni,
Tujadili ya nchini, siasa huchangamsha!
Pana chaguzi zimepita, na mazagazaga yake,
Pana hata za ukuta, vuguvugu za makeke,
Pana waliojikita, ni hadi kieleweke,
Tujadili ya nchini, siasa huchangamsha!
Mheshimiwa
missile,usitue peni chini,
Senzige wa zenji kule, uongezee watani,
Ukomavu ule ule, haki iwepo nchini,
Tujadili ya nchini, siasa huchangamsha!
Tunao magwiji wengi, wakiwamo wenda kimya,
Yupo
Makanyaga Kingi, mfalme wa kule mbeya,
Yupo binti yake mangi,
Lowassa bingwa wa kaya,
Tujadili ya nchini, siasa huchangamsha!
Hapa niongeze nini, Senzige kumuuitika?
Hata bila kalimani, wamwelewa huyu kaka,
Ya siasa tuyaghani, tukisaka miafaka,
Nimefikisha ujumbe, na mjumbe hauwawi!