Nina rafiki yangu ambaye mtoto wake anasoma Shule ya Sekondari Kisungu iliyopo Kinyerezi Dar es salaam. Alikuja kwangu kuniuliza iwapo kwenye saiti yangu nimebakiza walau tofali 20. Nilimuuliza tofali hizo anazihitaji kwa ajili ya nini, ndipo akaniambia kuwa mtoto wake alichelewa kufika shuleni, na adhabu iliyotolewa ni kupeleka tofali 20.
Nilimsaidia, lakini nilibaki nikiwa na mshangao mkubwa kuhusu utaratibu huo. Wakati bado nikiwaza juu ya jambo hilo, haikupita hata wiki moja nikakutana na jirani yangu eneo la saiti nikiwa nakagua mafundi. Alinifuata kuniomba tofali, akisema kuwa mwanae anatakiwa kupeleka tofali 15 kwa sababu ya kukosa kwenda shule siku moja.
Baada ya kutafakari na kuona kuwa utaratibu huo si rafiki, nilimshauri mzazi huyo asipeleke tofali hizo. Hata hivyo, mama huyo aliniambia kuwa endapo hatapeleka tofali hizo, anaambiwa arudi nyumbani na mtoto wake au afike shuleni awe anamfundisha mwenyewe.
Nilipoona mzazi huyo amejawa na hofu ya kupinga maamuzi hayo, niliamua kuuliza kwa watu wengine kuhusu utaratibu huo. Kati ya niliowasiliana nao, nilikutana na wazazi kadhaa waliokumbana na changamoto hiyo hiyo. Baadhi yao walilazimika kulipia fedha shuleni kwa ajili ya ununuzi wa tofali pale waliposhindwa kuyaleta.
Nilipouliza tofali hizo zinatumika kwa ajili ya nini, niliambiwa kuwa zinatumika kujenga uzio wa shule hiyo, ambayo ipo pembezoni mwa barabara inayotokea Kinyerezi kuelekea Mbezi.
Kwa upande wangu, siwezi kulikalia kimya suala hili. Huu si utaratibu rafiki wa utoaji wa adhabu, na sidhani kama kuna mwongozo wowote wa elimu unaotambua adhabu za aina hii.
Natoa wito kwa mamlaka husika, ikiwemo TAMISEMI na Wizara ya Elimu, kupiga marufuku adhabu za aina hii ambazo zinaongeza mzigo kwa wazazi. Ikiwa kuna umuhimu wa kujenga uzio, ni vyema Serikali ikatenga bajeti kwa ajili ya ujenzi huo, au iandaliwe utaratibu mbadala ulio rafiki, shirikishi, na unaohusisha wananchi kwa hiari, badala ya mtindo wa sasa unaotumika.
Zamani nikisoma shule (bweni) kulikuwa na tabia ya wanafunzi wengi kuchelewa kufika shule hasa ikifunguliwa kwa hadi wiki mbili hivi ILA tukaja kuletewa Headmaster mmoja Jemedari nafikiri alitolewa Jeshini yule kwa kuwa shule yetu ilikuwa kubwa na ya Boys tu. Alikomesha kabisa hiyo tabia; wanafunzi walilima robo heka, nusu heka nk kwa mikono kulingana na siku unazochelewa na adhabu ya fimbo kibao.... huwezi kuamini UFAULU uliongezeka mara mbili.
Kuhusu Matofali nafikiri kuna malengo mawili
1. Mojawapo ni mzazi ashiriki kwenye hiyo adhabu ili aone umuhimu wa mtoto kufuata taratibu za shule kwani wakati amechelewa shule, wana amini alikuwa nyumbani.
2. Ni kweli shule inahitaji uzio hivyo akaona waanzie hapo
Mwisho; naamini sio wanafunzi wote wanaochelewa kuripoti shuleni wanapeleka matofali ILA wanaopewa hiyo adhabu ni wale ambao hawana sababu za kutosha kuwafanya wachelewe kuripoti shuleni....