Thursday, 29 April 2010 21:38 0diggsdigg
Clara Alphonce - Mwananchi
KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, imetangaza matokeo ya pingamizi kwa wagombea mbalimbali wa uongozi katika klabu ya Simba ya Dar es Salaam.
Simba itafanya uchaguzi wa wagombea wake, Mei 9 kwenye Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam. Nafasi zinazowaniwa ni mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wa kamati ya utendaji. Mweka hazina na katibu mkuu watakuwa wa kuajiriwa.
Awali wagombea 57 waliomba nafasi mbalimbali katika klabu hiyo, kabla ya baadhi yao kuwekewa mapingamizi ambayo jana yalifikia tamati yake kwa Kamati hiyo ya TFF kuwaweka bayana watakaoingia kwenye uchaguzi.
Katika nafasi ya mwenyekiti, mgombea wa kwanza kuwekewa pingamizi alikuwa ni mwenyekiti anayemaliza muda wake Hassan Dalali ambaye aliondolewa kutokana na vyeti vyake kuwa na matatizo.
Wengine waliowania nafasi hiyo ni Michael Wambura, Aden Rage, Mohamed Nyangamala, Andrew Tupa, Hassan Hassanoor na Zacharia Hanspope. Kati ya hao, Tupa aliondolewa jina lake kwa kukosa sifa wakati waliowekewa pingamizi ni wote isipokuwa Hassan Hassanor.
Akitangaza jana mbele ya wanahabari, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Deo Lyatu alisema baada ya mahojiano na wote waliowekewa pingamizi, ni Aden Rage pekee ndiye aliyesalimika hivyo atasimama na Hassanoor katika uchaguzi kwa nafasi ya mwenyekiti.
Lyatu alisema, Wambura ameondolewa kutokana na ibara ya tisa ya kanuni za uchaguzi wa wanachama wa TFF na Kamati ya rufaa ya TFF ya 2008 ndiyo iliyotumika kumwondoa Wambura wakati alipoomba kuwania nafasi ya makamu wa rais wa TFF. Rufani hiyo ilikatwa na mwanachama wa Simba, Daniel Kamna,.
Kwa upande wa Hanspope, Kamati imebaini kuwa rufani iliyokatwa dhidi yake na Issa Said, ilisema mgombea aliwahi kufungwa kwa kosa la uhaini ibara ya 26 (5) ya Katiba ya Simba, inamuondolea sifa za kuwania uongozi na hastahili kuwania uongozi wa klabu ya Simba.
Katika nafasi ya Makamu, katibu mkuu wa zamani wa klabu hiyo, Mwina Kaduguda, ameondolewa kutokana na kutotimiza majukumu ya kikatiba ya Simba, ibara ya 19 kifungu namba 2 hadi 8, ibara ya 21 kifungu C, D, F, G, H, I ibara ya 38 na matakwa ya ibara ya tisa ya kanuni za uchaguzi wa TFF.
Kwa upande wa Chano Almasi, ameshindwa kukidhi haja kutokana na kutotimiza majukumu ya kikatiba ya klabu ya Simba kifungu namba 2 hadi 8, ibara ya 21 kifungu C hadi I, ibara ya tisa ya sheria za uchaguzi kwa wanachama wa TFF.
Akizungumza baada ya majibu ya Kamati ya TFF, Wambura ambaye alihojiwa kwa zaidi ya saa mbili, alisema atakutana na mwanasheria wake kuweka pingamizi la uchaguzi kwa kile anachoamini kuwa jina lake liliondolewa kwa 'fitna' ilhali alikuwa na sifa zote.
"Nilikwishayajua majibu siku tatu kabla na nitahakikisha napata haki yangu na pia nitataka ushauri wa kisheria juu ya hili neno uadilifu...kila kitu uadilifu sasa nataka kumaliza fitna zote," alisema.
Naye Almasi alisema hajafanya maamuzi yoyote kwa kuwa alikuwa akifahamu.