View attachment 2280500
194
Nilizidi kumsogelea taratibu hadi karibu yake, nikasimama huku nikimtazama kwa tabasamu. Yeye aliendelea kusimama kama sanamu pasipo kupepesa macho jambo lililoanza kumshtua kila mtu aliyekuwemo pale sebuleni. Tulitazamana. Nilikuwa namtazama kwa umakini nikiwa siamini kama niliyekuwa namwona kasimama mbele yangu alikuwa mke wangu mpenzi, Rehema. Nilisimama pale nikiyashuhudia machozi yakiendelea kumtiririka mashavuni utadhani milizamu iliyopasuka.
Kwa sekunde kadhaa watu wote pale sebuleni walibaki katika taharuki wakitutazamana bila kusema neno, kisha kama aliyegutuka, Rehema alikweza khanga yake na kufuta machozi kwa kutumia pembe ya khanga na kisha akapenga kamasi zilizoanza kumtoka. Halafu akashusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani.
Na hapo nikapata nguvu na kuinua mikono yangu, nikamkumbatia. Yeye pia alinyanyua mikono yake akanikumbatia. Tulikumbatiana kwa furaha kwa muda tusioweza kuukumbuka, mioyo yetu ilikuwa inadunda kwa kasi na jasho jepesi lilikuwa linatutoka.
Wakati tukiwa bado tumekumbatiana nilimsikia Rehema akivuta pumzi ndefu kisha akazishusha taratibu huku akiwa amekilaza kichwa chake kwenye kifua changu. Hadi muda huo hakuweza kuongea neno lolote. Nilijikuta nikizama katika kuuajabia mwili wa Rehema, nikauhusudu urembo wake usiochujuka japo alikuwa ametoka kujifungua lakini bado aliweza kuonekana mrembo.
Kisha Rehema aliinua uso wake kunitazama na hapo akalihisi joto la pumzi zangu jambo nililoamini kuwa lilimfanya kuamini kuwa nilikuwa mtu hai na si mzimu.
Kwa muda wote huo hali ilikuwa ya taharuki kidogo ndani ya ile sebule, watu wote walikuwa kimya wakishuhudia kilichokuwa kikiendelea kati ya wanandoa tuliokuwa tumepotezana kwa takriban miezi kumi, huku mimi nikidhaniwa kuwa nimekufa.
“Rehema!” hatimaye nilimwita Rehema kwa sauti ndogo.
“Abee!” Rehema aliitika kwa sauti ya chini huku akinitazama usoni, uso wake ulikuwa na michirizi ya machozi yaliyolilowesha shati langu eneo la kifuani.
“Ni mimi Jason mumeo, niko hai… usilie mimi ni mzima kama unionavyo,” nilisema huku nikimpapasa nywele zake.
Maneno hayo yalionesha kumwingia sana Rehema, alinitazama kwa haya, alinitazama tangu unyayoni hadi utosini, kisha macho yetu yaligongana na kumfanya aachie tabasamu laini. Mashavu yake yakaonesha vishimo vidogo, pembe za midomo yake zikafinya na macho yake yakafanya kuelea. Midomo yake yenye maki ikafunguka na sauti iliyotoka humo ilitosha kabisa kumtoa nyoka pangoni mwake.
“Hata sijui niseme nini, mume wangu! Ila namshukuru sana Mungu kwa kukurejesha nyumbani ukiwa mwenye afya, karibu tena maisha kwangu,” Rehema alisema na kushusha pumzi ndefu kama aliyetoka kumaliza mbio ndefu za marathoni.
Kwa maneno hayo, mkondo wa umeme ulikuwa umepitishwa katika mwili wangu. Nilishusha pumzi na kumwachia Rehema kisha nikamsogelea Grace na kusimama nikimtazama Jason Junior aliyepakatwa mikononi. Kuona hivyo Grace akanyoosha mikono yake kunipa mtoto.
Nilimchukua mtoto na kumtazama kwa umakini, nikashusha pumzi za ndani kwa ndani na kumbusu kwenye paji la uso wake, kisha nikamkumbatia kifuani kwangu huku nikijitahidi kuyazuia machozi yaliyokuwa yakinilengalenga machoni.
Grace alinyanyuka toka pale alipokuwa ameketi na kunipisha, akaketi kwenye kochi jingine lililokuwa kando kabisa ya sebule. Niliketi huku nikiendelea kumtazama Jason Junior kwa umakini. Kitambo kirefu cha ukimya kikapita huku kila mmoja akiwaza lake na ukimya ule ulipokuwa mbioni kushika hatamu nikanyanyua uso wangu kuwatazama watu walioketi pale sebuleni.
“Habari za hapa?” niliwasalimia mle ndani huku nikivunja ukimya ulioanza kutawala pale sebuleni.
“Za hapa nzuri,” wote walijibu. Mama Mchungaji akaongeza, “Sisi hatujambo kama unavyotuona. Pole sana.”
“Nimekwisha poa,” nilijibu kisha nikamtazama Rehema, “Pole sana kwa maisha ya upweke na yote yaliyotokea wakati mimi sipo.”
“Hivi sasa sina tena upweke,” Rehema alisema huku akiangua kicheko hafifu cha kimahaba.
“Hata hivyo akili yangu inashindwa kukubali, ni kama vile mambo haya yametendeka ndani ya wiki moja tu tangu ile ajali itokee,” nilisema huku nikiutazama mkono wangu wa kushoto uliofungwa plasta ngumu.
Rehema aliyapeleka macho yake kuutazama mkono wangu wenye plasta ngumu kwa umakini huku akijitahidi kuyazuia machozi yake, kisha alinisogelea na kuketi sakafuni huku akiishika miguu yangu kwa upendo. Akamwagiza Grace alete maji kwenye kikombe kikubwa na beseni dogo.
Grace aliinuka na kuleta maji kwenye kikombe na beseni dogo na kumpa Rehema ambaye alivipokea na kunivua viatu na soksi, kisha akaniosha miguu yangu kwa upendo huku akiyakinga yale maji kwenye beseni, halafu akayanywa yale maji aliyonioshea. Kila mtu alimtazama kwa mshangao lakini yeye hakujali.
“Kwa miezi tisa nimeishi kwa ukiwa, sikujua kama ingetokea siku kama ya leo tukiwa pamoja na mtoto wetu Junior,” Rehema alisema huku akifuta machozi yaliyokuwa yanamlengalenga machoni.
Muda mfupi uliofuata Grace alielekea jikoni na kurudi akiwa amebeba sinia kubwa la mbao safi ambalo lilikuwa na majagi mawili makubwa ya kioo, moja likiwa na sharubati ya mchanganyiko wa embe na
passion na jingine lilikuwa na sharubati ya parachichi. Akayaweka juu ya meza na kuondoka tena, akarejea na bilauri kadhaa. Kisha alimimina sharubati kwenye zile bilauri na kutukaribisha.
Kila mmoja alichukua bilauri ya sharubati kulingana na alivyopenda halafu tukagongesha bilauri zetu kutakiana afya njema na maisha marefu. Tukanywa taratibu huku tukiongea na kufurahi kwa pamoja.
“Haya ni maajabu kabisa! Hiki kilichotokea ni kama ile hadithi ya mwana mpotevu wa kwenye Biblia,” Eddy alisema huku akiachia kicheko hafifu. Watu wote walicheka kwa furaha huku wakionekana kuafikiana na maneno yake.
“Wala hujakosea, mimi pia ni mwana mpotevu, nilipotea na sasa nimepatikana. Nilikufa na sasa nimefufuka,” nilisema kwa furaha huku nikinyanyua bilauri yangu juu kisha nikapiga funda kubwa la sharubati.
“Ni kweli, wewe ni mwana mpotevu ila tofauti yako na yule wa kwenye Biblia ni kwamba, mwenzio aliondoka akiwa na fahamu zake na wewe uliondoka ukiwa huna kumbukumbu zako na ukaishi maisha ya kufikirika,” Grace alisema huku akiangua kicheko. Kisha aliinuka na kunifuata huku akinyoosha mkono wake wenye bilauri, tukagongesha bilauri zetu.
“
Cheers!” tulisema kwa pamoja na kuinua bilauri, tukapiga mafunda mfululizo kana kwamba tulikuwa kwenye mashindano.
“
Long live, my dear brother!” Grace alisema kwa sauti kubwa akiwa na furaha.
“
Long live, my dearest sister!” nilijibu mapigo huku nikiikita ile bilauri tupu juu ya meza kwa furaha.
“Na ninyi mkishakutana basi tabu tupu,” Eddy alisema huku akitabasamu.
“Wacha tufurahi, kaka… mwana mpotevu amefufuka na kurudi nyumbani,” Grace alisema huku akicheka kisha akaongeza huku akinitazama usoni, “Kwanza
juice haipandi kabisa, hapa tungepata
Castle baridi ingependeza zaidi, au vipi
brother?”
“Hiyo pombe yenu mkainywee huko huko si ndani ya nyumba ya Mchungaji,” Eddy alisema kwa utani na hapo tukageuza shingo zetu kumtazama Mchungaji Ngelela aliyeketi kwa utulivu kwenye kochi.
* * *
Saa 11:30 jioni…
Jioni ya siku hiyo ilinikuta nikiwa nimesimama mbele ya kaburi ambalo ulizikwa mwili uliodhaniwa kuwa wangu, nililitazama kaburi hilo kwa huzuni kubwa huku mawazo yangu yakirudi nyuma miezi tisa iliyokuwa imepita siku tuliyopata ajali. Kisha nilijaribu kuwaza kuhusu maisha mapya niliyoishi kama Mgeni lakini sikuwa na kumbukumbu zozote.
Wakati nikilitazama lile kaburi nilishindwa kuyazuia machozi yangu hasa nilipoyaona maandishi makubwa yaliyokuwa yameandikwa juu ya msalaba wa zege, maandishi ambayo yalikuwa yanawakilisha jina langu, tarehe ya kuzaliwa na ya kufa.
Nilikuwa nimeambatana na Mchungaji Ngelela, Eddy na Grace waliosimama kando yangu huku wakinifariji. Nilisimama pale kwa dakika kadhaa nikilitazama lile kaburi kisha nikashusha pumzi ndefu na kufuta machozi yaliyokuwa yakinitoka. Halafu kwa kusaidiana na watu niliofuatana nao tuliuondoa ule msalaba kutoka kwenye lile kaburi.
Baada ya kuhakikisha kuwa sijaacha alama yoyote yenye kuonesha utambulisho wangu kwenye lile kaburi, niliinamisha kichwa changu kwa huzuni mbele ya kaburi lile na kufumba macho. Kisha nilimshukuru Mungu kwa kuniepusha na mauti na nikamwomba anipe nguvu na maisha marefu yenye heri, halafu nilimwombea marehemu aliyezikwa kwenye kaburi hilo ili Mungu ampumzishe mahala pema.
Nilipomaliza nikaondoka taratibu kwa huzuni huku nikifuatwa na jamaa zangu niliokuja nao.
* * *
Endelea kuufuatilia mkasa huu wa kusisimua...