Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
- Thread starter
- #221
144
Mtu aliyekuwepo getini aliendelea kubonyeza kengele. Na hapo nikasimama na kuwasha runinga ndogo ya kuona aliyeko getini huku nikipiga miayo ya uchovu. Runinga ilipowaka nikamwona Olivia akiwa amesimama nje ya geti akiwa ameegemea mbele ya gari lake lililokuwa likiunguruma taratibu huku akiangalia kwa umakini sehemu ya kengele ambako kulikuwa na kamera ya ulinzi. Nilishangaa sana kumwona Olivia nyumbani kwangu muda huo.
Alikuwa amevaa suruali ya bluu ya dengrizi, blauzi ya rangi ya maruni na kofia ya bluu ya kapelo. Nguo zake zilikuwa zimembana kiasi zikilichora vyema umbo lake refu lenye kiuno chembamba lakini imara kilichoshikilia minofu ya mapaja yake. Begani alikuwa amening’iniza mkoba mzuri wa rangi ya maruni wa thamani kubwa.
Nilichukua rimoti ya kufungulia geti kisha nikabofya kitufe cha kuruhusu geti lifunguke taratibu na kitendo hicho kikamfanya Olivia kuingia ndani ya gari lake na kisha akaliingiza gari lake ndani ya uzio wa nyumba yangu na kuliegesha sehemu maalumu ya kuegesha magari.
Aliposhuka toka ndani ya gari alinikuta nikiwa nimesimama kwenye mlango mkubwa wa kuingilia sebuleni kwangu huku macho yangu yakiwa yametia nanga kwenye umbo lake zuri, Olivia alinitazama kwa utulivu huku akitabasamu kabla ya tabasamu lake halijageuka kicheko cha kirafiki.
“Karibu ndani, rafiki,” nilimkaribisha Olivia huku nikiendelea kumtazama kwa utulivu.
Olivia hakunijibu badala yake aliachia tabasamu kisha akaingia ndani huku harufu nzuri ya manukato aliyojipulizia ikitamalaki pale sebuleni na kuongeza uhai wa pua yangu. Alipiga hatua za taratibu mpaka kwenye sofa dogo kisha akakaa huku akinitazama kwa jicho la udadisi, nami nikamtazama, tukawa tunatazamana kabla sijafungua kinywa changu na kusema, “Habari za huko utokako?”
“Nzuri tu, hofu ni kwako,” Olivia alisema huku akinitazama kwa jicho pembe.
“Niko poa… sijui utapendelea kunywa nini?” nilimuuliza huku nikimtazama kwa tuo.
“Maji ya uvuguvugu yatanifaa,” Olivia alisema kwa sauti tulivu na ya kirafiki huku akiitazama chupa tupu ya whisky iliyokuwa mezani.
Nilimtazama kwa muda kidogo kisha nikageuza shingo yangu kutazama jikoni kabla sijayahamishia macho yangu kwenye kaunta ya baa, “Vipi kama nitakuletea glasi ya mvinyo badala ya maji vuguvugu uyatakayo?”
Kwanza Olivia hakujibu kitu, alikaa kimya huku akiitazama picha kubwa ya Rehema iliyokuwa ukutani kana kwamba hakusikia nilichosema. Kisha alishusha pumzi na kusema, “Hapana, maji vuguvugu ni nzuri zaidi.”
“Sawa,” nilisema huku nikianza kupiga hatua kuelekea jikoni.
“Itapendeza zaidi kama utaleta jagi la maji pamoja na glasi mbili,” Olivia alisema kabla sijafika mbali.
Baada ya dakika chache nilirudi pale sebuleni nikiwa na jagi la maji na bilauri mbili na kuyafikisha alipokaa Olivia, nikammiminia maji kwenye bilauri moja na kumpa.
“Karibu,” nilimkaribisha huku nikijitahidi kuufanya uso wangu uwe na tabasamu muda wote.
Olivia aliachia tabasamu na kuipokea ile bilauli ya maji kisha akapiga funda moja kubwa la maji na kuirudisha bilauli yake chini na kunitazama kwa utulivu.
“Vipi, ulibahatika kusoma hiki kitabu?” aliniuliza huku akikitupia macho kitabu cha Sigmund Freud alichokuwa amenipa siku iliyotangulia.
“Yeah, nimekisoma usiku kucha. Nadhani kitanisaidia kuyasahu maisha yangu ya nyuma na kuanza maisha mapya,” nilisema huku nikiketi kwenye sofa.
Olivia alinitazama kwa muda kama aliyekuwa anatafuta neno la kuniambia kisha alichukua jagi la maji na kumimina maji kwenye ile bilauri ya pili na kunipa, “Drink some water please…” alisema huku akiniangala kwa utulivu.
Niliichukua ile bilauri lakini sikuyanywa yale maji kama alivyoniambia. Niliishia kuyatazama huku nikilihisi tumbo langu likikoroga kidogo kwa sababu ya njaa na pombe kali niliyokunywa usiku.
“Ni kweli unahitaji kuyasahau maisha yako ya nyuma na kuanza upya?” Olivia aliniuliza huku akinitazama kwa umakini.
“Ndiyo maana yake,” nilimjibu.
“Kama kweli unahitaji kuanza upya basi kunywa hayo maji,” Olivia aliniambia. Sauti yake iliendelea kuwa tulivu na ya kirafiki.
Sikutaka kubishana naye, nilishusha pumzi kisha nikayanywa yale maji haraka haraka hadi yalipoisha na kuitua ile bilauri chini, Olivia akanimiminia maji mengine na kunitaka niyanywe. Nikayanywa yote.
“Sasa funga macho yako kwa utulivu na ujilegeze mwili wako huku ukivuta pumzi ndefu. halafu baadaye utaniambia umeona nini!” Olivia aliniambia. Nami sikufanya ubishi, niliyafunga macho yangu. Na wakati nikiwa nimeyafunga macho nilimsikia Olivia akinielekeza nini cha kufanya.
“Endelea kuvuta pumzi hadi utakapohisi misuli ya mwili wako inalegea…” Olivia alisema na kuendelea, “…kisha anza kwa kutafakari kwanza kinachokusukuma kubadilika. Je, ni kipi kinakusukuma zaidi?”
Nikiwa nimefunga macho huku nikivuta pumzi akili yangu ilianza kujenga taswira fulani iliyonistaajabisha sana, taswira ambayo ilikuwa vigumu sana kuielezea nikaeleweka.
Taswira hiyo iliambatana na sauti fulani tulivu sana na ya kirafiki lakini iliyoonya. Haikuwa sauti ya mwanamume wala ya mwanamke na ilipenya vyema masikioni mwangu, ikaujaza ganzi mwili wangu wote. Sauti hiyo ilinitaka nitafakari kama nilihisi furaha, huzuni au upweke?
Sikujua niliyafunga macho yangu kwa muda gani lakini nilipoyafungua nilishangaa kutomwona Olivia pale sebuleni, nilichokishuhudia ni jagi la maji pamoja na zile bilauri mbili ambazo, moja ilitumiwa na Olivia na nyingine nilikuwa nimeitumia.
“Olivia!” niliita kwa sauti lakini sikupata jibu lolote na hivyo nikanyanyuka kutoka pale kwenye sofa na kuelekea mlangoni, nikaufungua mlango kwa lengo la kumwangalia huko nje ili nimweleze nilichokiona. Sikukuta gari lake, alikuwa ameshaondoka!
* * *
Endelea...