Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

fungate.jpeg

144

Mtu aliyekuwepo getini aliendelea kubonyeza kengele. Na hapo nikasimama na kuwasha runinga ndogo ya kuona aliyeko getini huku nikipiga miayo ya uchovu. Runinga ilipowaka nikamwona Olivia akiwa amesimama nje ya geti akiwa ameegemea mbele ya gari lake lililokuwa likiunguruma taratibu huku akiangalia kwa umakini sehemu ya kengele ambako kulikuwa na kamera ya ulinzi. Nilishangaa sana kumwona Olivia nyumbani kwangu muda huo.

Alikuwa amevaa suruali ya bluu ya dengrizi, blauzi ya rangi ya maruni na kofia ya bluu ya kapelo. Nguo zake zilikuwa zimembana kiasi zikilichora vyema umbo lake refu lenye kiuno chembamba lakini imara kilichoshikilia minofu ya mapaja yake. Begani alikuwa amening’iniza mkoba mzuri wa rangi ya maruni wa thamani kubwa.

Nilichukua rimoti ya kufungulia geti kisha nikabofya kitufe cha kuruhusu geti lifunguke taratibu na kitendo hicho kikamfanya Olivia kuingia ndani ya gari lake na kisha akaliingiza gari lake ndani ya uzio wa nyumba yangu na kuliegesha sehemu maalumu ya kuegesha magari.

Aliposhuka toka ndani ya gari alinikuta nikiwa nimesimama kwenye mlango mkubwa wa kuingilia sebuleni kwangu huku macho yangu yakiwa yametia nanga kwenye umbo lake zuri, Olivia alinitazama kwa utulivu huku akitabasamu kabla ya tabasamu lake halijageuka kicheko cha kirafiki.

“Karibu ndani, rafiki,” nilimkaribisha Olivia huku nikiendelea kumtazama kwa utulivu.

Olivia hakunijibu badala yake aliachia tabasamu kisha akaingia ndani huku harufu nzuri ya manukato aliyojipulizia ikitamalaki pale sebuleni na kuongeza uhai wa pua yangu. Alipiga hatua za taratibu mpaka kwenye sofa dogo kisha akakaa huku akinitazama kwa jicho la udadisi, nami nikamtazama, tukawa tunatazamana kabla sijafungua kinywa changu na kusema, “Habari za huko utokako?”

“Nzuri tu, hofu ni kwako,” Olivia alisema huku akinitazama kwa jicho pembe.

“Niko poa… sijui utapendelea kunywa nini?” nilimuuliza huku nikimtazama kwa tuo.

“Maji ya uvuguvugu yatanifaa,” Olivia alisema kwa sauti tulivu na ya kirafiki huku akiitazama chupa tupu ya whisky iliyokuwa mezani.

Nilimtazama kwa muda kidogo kisha nikageuza shingo yangu kutazama jikoni kabla sijayahamishia macho yangu kwenye kaunta ya baa, “Vipi kama nitakuletea glasi ya mvinyo badala ya maji vuguvugu uyatakayo?”

Kwanza Olivia hakujibu kitu, alikaa kimya huku akiitazama picha kubwa ya Rehema iliyokuwa ukutani kana kwamba hakusikia nilichosema. Kisha alishusha pumzi na kusema, “Hapana, maji vuguvugu ni nzuri zaidi.”

“Sawa,” nilisema huku nikianza kupiga hatua kuelekea jikoni.

“Itapendeza zaidi kama utaleta jagi la maji pamoja na glasi mbili,” Olivia alisema kabla sijafika mbali.

Baada ya dakika chache nilirudi pale sebuleni nikiwa na jagi la maji na bilauri mbili na kuyafikisha alipokaa Olivia, nikammiminia maji kwenye bilauri moja na kumpa.

“Karibu,” nilimkaribisha huku nikijitahidi kuufanya uso wangu uwe na tabasamu muda wote.

Olivia aliachia tabasamu na kuipokea ile bilauli ya maji kisha akapiga funda moja kubwa la maji na kuirudisha bilauli yake chini na kunitazama kwa utulivu.

“Vipi, ulibahatika kusoma hiki kitabu?” aliniuliza huku akikitupia macho kitabu cha Sigmund Freud alichokuwa amenipa siku iliyotangulia.

Yeah, nimekisoma usiku kucha. Nadhani kitanisaidia kuyasahu maisha yangu ya nyuma na kuanza maisha mapya,” nilisema huku nikiketi kwenye sofa.

Olivia alinitazama kwa muda kama aliyekuwa anatafuta neno la kuniambia kisha alichukua jagi la maji na kumimina maji kwenye ile bilauri ya pili na kunipa, “Drink some water please…” alisema huku akiniangala kwa utulivu.

Niliichukua ile bilauri lakini sikuyanywa yale maji kama alivyoniambia. Niliishia kuyatazama huku nikilihisi tumbo langu likikoroga kidogo kwa sababu ya njaa na pombe kali niliyokunywa usiku.

“Ni kweli unahitaji kuyasahau maisha yako ya nyuma na kuanza upya?” Olivia aliniuliza huku akinitazama kwa umakini.

“Ndiyo maana yake,” nilimjibu.

“Kama kweli unahitaji kuanza upya basi kunywa hayo maji,” Olivia aliniambia. Sauti yake iliendelea kuwa tulivu na ya kirafiki.

Sikutaka kubishana naye, nilishusha pumzi kisha nikayanywa yale maji haraka haraka hadi yalipoisha na kuitua ile bilauri chini, Olivia akanimiminia maji mengine na kunitaka niyanywe. Nikayanywa yote.

“Sasa funga macho yako kwa utulivu na ujilegeze mwili wako huku ukivuta pumzi ndefu. halafu baadaye utaniambia umeona nini!” Olivia aliniambia. Nami sikufanya ubishi, niliyafunga macho yangu. Na wakati nikiwa nimeyafunga macho nilimsikia Olivia akinielekeza nini cha kufanya.

“Endelea kuvuta pumzi hadi utakapohisi misuli ya mwili wako inalegea…” Olivia alisema na kuendelea, “…kisha anza kwa kutafakari kwanza kinachokusukuma kubadilika. Je, ni kipi kinakusukuma zaidi?”

Nikiwa nimefunga macho huku nikivuta pumzi akili yangu ilianza kujenga taswira fulani iliyonistaajabisha sana, taswira ambayo ilikuwa vigumu sana kuielezea nikaeleweka.

Taswira hiyo iliambatana na sauti fulani tulivu sana na ya kirafiki lakini iliyoonya. Haikuwa sauti ya mwanamume wala ya mwanamke na ilipenya vyema masikioni mwangu, ikaujaza ganzi mwili wangu wote. Sauti hiyo ilinitaka nitafakari kama nilihisi furaha, huzuni au upweke?

Sikujua niliyafunga macho yangu kwa muda gani lakini nilipoyafungua nilishangaa kutomwona Olivia pale sebuleni, nilichokishuhudia ni jagi la maji pamoja na zile bilauri mbili ambazo, moja ilitumiwa na Olivia na nyingine nilikuwa nimeitumia.

“Olivia!” niliita kwa sauti lakini sikupata jibu lolote na hivyo nikanyanyuka kutoka pale kwenye sofa na kuelekea mlangoni, nikaufungua mlango kwa lengo la kumwangalia huko nje ili nimweleze nilichokiona. Sikukuta gari lake, alikuwa ameshaondoka!

* * *

Endelea...
 
fungate.jpeg

145

Saa 10:30 jioni.

Zilikuwa zimepita siku mbili tangu Olivia alipokuja nyumbani kwangu na kuniambia nifumbe macho yangu kisha akatoweka katika mazingira ya kutatanisha, sikumtafuta wala kumpigia simu, yeye pia hakunitafuta wala kunipigia simu. Tangu siku hiyo sikutoka kwenda kokote, niliamua kutulia nyumbani huku nikitafakari kuhusu mustakabari wa maisha yangu.

Muda huo nilikuwa nimevaa bukta nyeusi ya kitambaa cha kadeti iliyoishia juu kidogo ya magoti yangu na shati jepesi jekundu huku nikibaki kifua wazi bila kufunga vifungo, kisha nilikaa kwenye bustani ndogo nyumbani kwangu nikitafakari kuhusu hali yangu, mkononi nikiwa na bilauri ya mvinyo mwekundu aina ya Dompo kutoka Dodoma Wine.

Nilikuwa buheri wa afya, kimwili na kiakili, nikiwa nimerejea kwenye hali yangu ya kawaida kutoka kwenye msongo mkali wa mawazo ambao almanusra unisababishie kulazwa kwenye wadi ya wagonjwa wenye matatizo ya akili.

Nikiwa nimeketi pale bustanini nilianza kuwaza juu ya Rehema, kwanza; nilimhurumia sana kwa sababu ya matatizo ya kiafya yaliyokuwa yanamkabili, matatizo ambayo mimi ndiye niliyeyasababisha. Huruma niliyokuwa nayo kwa Rehema ilisababisha kuibuka kwa jambo la pili; mapenzi!

Kwa mara nyingine tena nilitamani kuwa karibu zaidi na Rehema, ili kumfariji katika kipindi chake kigumu alichokuwa anapigania uhai wake kitandani. Niliamini kuwa, pamoja na mambo yote yaliyotokea kati yetu, bado Rehema alikuwa ananihitaji.

Nikiwa mawazoni, nilishtuliwa na sauti ya muungurumo wa gari lililosimama mbele ya geti la nyumba yangu. Wakati nikijaribu kusikiliza kwa umakini mlango wa gari ulifunguliwa kisha mtu akasogea getini na kubonyeza kengele ya getini. Nikanyanyuka haraka pale nilipoketi na kwenda kufungua geti dogo huku nikichungulia nje.

Macho yangu yakajikuta yakitia nanga kwenye umbo zuri la mwanadada mrembo, mchangamfu na ambaye uzuri wake ulitosha kuudhihirisha utukufu wa Mungu kwenye sanaa ya uumbaji. Alikuwa amevalia gauni zuri la kitenge cha wax lililoshonwa kwa mtindo wa ‘ankara midi tube dress’ likiishia sentimita chache juu ya magoti yake, likiwa limehifadhi vyema umbile lake. Miguuni alivaa sendozi ngumu za kike zilizotengenezwa kwa ngozi imara.

“Karibu ndani, rafiki yangu,” nilimkaribisha Olivia, muda huo alikuwa anazuga kwa kuitazama saa yake ya mkononi akipambana na aibu ya kiutu uzima huku akikitazama kifua changu kilichokuwa wazi kwa jicho la wizi. Alipogundua kuwa nilikuwa namkazia macho aliachia tabasamu la aibu kisha akaingia ndani.

“Leo huingizi gari?” nilimuuliza kwa mshangao baada ya kuona akiliacha gari lake pale pale nje ya uzio wa nyumba.

“Sikai sana, nimekuja mara moja tu kukujulia hali,” Olivia alisema huku akipiga hatua taratibu huku akiendelea kukitazama kifua changu kwa wizi. Nikamsogelea na kumshika mkono.

“Kama hutojali,” nilisema huku nikimkokota taratibu kuelekea sebuleni.

Olivia hakusema neno bali aliangua kicheko hafifu huku akiendelea kukitupia jicho la wizi kifua changu. Tuliingia ndani na kuketi kwenye masofa kisha ukimya kidogo ukapita huku kila mmoja akionekana kuzama kwenye tafakuri yake. Olivia akawa wa kwanza kuutowesha ukimya ule. “Vipi, siku ile ulipofunga macho uliona nini?”

Swali la Olivia liliyarudisha tena mawazo yangu pale sebuleni, na mara hii nikakumbuka kila kitu kilichonitokea siku ile, nikaikumbuka taswira nzima kana kwamba nilikuwa naiona muda huo.

You were right, I saw my future with her,” nilimwambia Olivia kwa sauti tulivu huku nikishusha pumzi ndefu.

Olivia alinitazama kwa kitambo kisha akashusha pumzi za ndani kwa ndani. “Safi, lakini unadhani hiyo future itakukuta ukiwa hapa hapa nyumbani kwako?”

Swali lake lilinitafakarisha sana kwani sikuwa nimetegemea swali la aina hiyo katika muda huo. Ni kama nilikuwa nimezinduka kutoka kwenye usingizi mzito, na kabla sijajua nini cha kujibu sauti ya kengele ya getini ilianza kuita kwa fujo na kutushtua. Tukatazamana katika namna ya kuulizana, “Nani?”

Haraka nikawasha runinga ndogo ya kuona aliyeko getini na hapo nikashtushwa sana na ugeni uliofika nyumbani kwangu asubuhi hiyo, ulikuwa ni ugeni ambao sikuutarajia kabisa. Nilimwona Dk. Camila Mpogoro, dada wa Rehema akiwa amesimama mbele ya geti la nyumba yangu.

Ujio wa Dk. Camila nyumbani kwangu haukunishtua sana kwa sababu haikuwa jambo la ajabu kwa yeye kufika kwangu. Alishawahi kufika mara kadhaa wakati Rehema akiwepo na hata baada ya matatizo kutokea. Kilichonishtua mno ni mgeni aliyeongozana na Dk. Camila, mgeni ambaye alisababisha umakini wangu upotee kwa sekunde kadhaa kabla haujarejea tena.

Mgeni huyo alikuwa ni Mama mdogo wa Rehema ambaye sura yake ilikuwa ya majonzi na macho yake yalikuwa mekundu, bila shaka kwa sababu ya kulia. Hapo hapo hofu ikaanza kuniingia kutokana na hali hiyo. Wasiwasi wa kupokea taarifa za kifo cha Rehema. Nilikuwa tayari kupokea taarifa yoyote ile lakini si taarifa hiyo. Niliamini kuwa ningekatishwa tamaa mno kulisikia jambo kama hilo kwa masikio yangu.

Olivia aliugundua mshtuko na hofu yangu, akanikazia macho kwa udadisi. “Who are they?” aliniuliza huku akiyatuliza macho yake usoni kwangu kwa udadisi.

“Ni jamaa zake Rehema, sijui kuna tatizo gani tena?” niliuliza kwa wasiwasi huku nikiikodolea macho ile runinga iliyowaonesha.

Mapigo ya moyo wangu yalianza kwenda mbio huku nikijiuliza sana nini kiliwaleta nyumbani kwangu? Je, Rehema alikuwa amekufa? Kwa jinsi nyuso zao zilivyoonekana ilinifanya nipatwe na wasiwasi mwingi, nikihisi jambo baya zaidi lilikuwa limemtokea Rehema.

“Kwa nini uwazie matatizo muda wote? Naamini hakuna baya lililotokea,” Olivia aliniambia huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.

Niliinuka na kuelekea getini kisha nikafungua geti dogo na kutoa kichwa changu kuchungulia nje, na hapo nikajikuta nikitazamana na wale wanawake. Walinitazama kwa wasiwasi kisha wakatazamana wakionekana kusita, nyuso zao zilionesha kukata tamaa. Nami nikiwa na wasiwasi niliwasalimia kisha nikawakaribisha ndani huku nikiwapisha waingie, wakaingia na kusimama ndani ya uzio kwa wasiwasi.

Nililifunga geti kisha niliwaongoza hadi sebuleni ambako tulimkuta Olivia akiwa ameketi kwa utulivu kwenye sofa huku akiwatazama wageni wangu kwa wasiwasi.

Walishtuka sana walipomwona Olivia nyumbani kwangu, walitazamana katika hali ya kukata tamaa zaidi kisha waliyarudisha macho yao kwa Olivia kabla hawajayahamishia kwangu. Walikuwa wamechanganyikiwa kumwona Olivia nyumbani kwangu na kwa kupitia mtazamo wao nilihisi walikuwa wanainuliza, “Huyu ni nani? Mbona anafanana na Rehema?”

Niliigundua hali hiyo na hivyo nikaamua kufanya utambulisho wa haraka haraka. “Kutateni na Dk. Olivia Mkuro, rafiki yangu, mnasihi wangu na daktari wa afya ya akili. Ndiye aliyenisaidia kurudi katika hali yangu ya kawaida…” nilimtambulisha Olivia kwa Dk. Camila na mama yake mdogo. Na hivyo utambulisho wangu ukawafanya washushe pumzi za ahueni.

Endelea...
 
fungate.jpeg

146

“Tunashukuru kukufahamu Dk. Mkuro,” Dk. Camila alisema huku akimpa mkono Olivia kumsalimia. Hata hivyo bado hakuwa na ule uchangamfu wake niliouzowea.

Wakati wakipeana mikono nikaendelea na utambulisho wangu, “Kutana na Dk. Camila Mpogoro, daktari wa mifugo wa wilaya, ni dada yake Rehema,” nilimwambia Olivia na kuendelea huku nikielekeza kidole changu kwa mama mdogo, “Na huyu ni Mama yao mdogo.”

Olivia alibetua kichwa chake huku akiuachia mkono wa Dk. Camila na kumpa mkono Mama mdogo wa Rehema, tabasamu likiwa limeutawala uso wake. Wakasalimiana.

Kisha kikazuka kitambo kifupi cha ukimya huku nikiwashuhudia Dk. Camila na Mama mdogo wakitazama kwa wizi, nyuso zao zilionesha hali ya kukata tamaa. Na kabla sijajua sababu ya ugeni ule wa ghafla nikashtuliwa na sauti ya Dk. Camila.

“Jason, Rehema anakuhitaji,” Dk. Camila alisema huku machozi yakianza kumlengalenga.

“Rehema! Anaendeleaje?” niliuliza kwa shauku lakini uso wangu ukiwa na wasiwasi japo sasa wasiwasi ulipungua kidogo, lakini bado nilikuwa na maswali kichwani.

“Hali yake bado ni mbaya sana… wamerudi wiki iliyopita toka India, madaktari wamegundua kuwa kuna ufa katika fuvu la kichwa chake na seli zake za ubongo zimeachana sana. Tafadhali Jason, fanya juu chini ukamwone huenda ikasaidia kumrejesha katika hali yake,” Dk. Camila alisema kwa huzuni huku machozi yakizidi kumlengalenga.

“Ufa kwenye fuvu la kichwa? How possible?” nilimaka kwa mshangao mkubwa huku nikimtazama Olivia.

It’s possible! Na kuna uwezekano hali hiyo imesababishwa na msongo mkali wa mawazo,” Olivia alisema na kushusha pumzi, kisha akaongeza, “tatizo hilo linaweza hata kumsababishia upofu wa maisha.”

Nilihisi kama mwili wangu ulikuwa unaingiwa na ubaridi na kufa ganzi. Nilihisi machozi yakinilengalenga. Mawazo yalianza kuzunguka akilini kwangu, nilikumbuka toka siku ya kwanza niliyokutana na Rehema, tukaanzisha urafiki na hatimaye tukawa wapenzi kabla ya kuwa wachumba. Sura yake ilinijia akilini kwangu. Nilimwona akiwa katika tabasamu na kicheko chake kidogo.

Nilijikuta nikiumia sana kwani tayari nilikuwa na ndoto nyingi na Rehema aliyeingia moyoni mwangu kuliko mwanamke yeyote niliyewahi kukutana naye chini ya jua. Nilijiona mtu mkosaji sana nisiyestahili kusamehewa kutokana na namna nilivyomtendea ingawa yeye alionesha kunipenda kwa dhati. Nilihisi kama moyo wangu ulikuwa unakatwa vipande vipande na kisu kikali sana.

Rehema alikuwa maisha yangu. Alikuwa kila kitu kwangu. Alikuwa amenifanya niyafurahie maisha japo kwa muda mfupi niliokaa naye. Rehema alikuwa mwanamke wa tofauti sana. Alikuwa na moyo wa ajabu na wa kipekee kabisa. Mwenye upendo wa dhati na wa kweli. Upendo wake ulitoka ndani kabisa ya moyo wake. Alikuwa kama malaika anayeishi duniani na hakustahili mateso hayo.

“Unawaza nini, Jason? Basi fanya uamuzi…” sauti ya Olivia ilinizindua toka kwenye lindi la mawazo.

“Masikini Rehema!” nilitamka bila kutarajia na kutoa kitambaa nikayafuta machozi yaliyoanza kunitoka huku nikishindwa kuyazuia.

It’s okay, Jason… usihuzunike sana. Kwa uwezo wa Mungu Rehema atapona tu. Cha muhimu usiache kumwombea kwa Mungu ili aweze kupona haraka,” Olivia aliniambia huku akinipapasa mgongoni katika hali ya kunitia moyo.

Dk. Camila na Mama mdogo walibaki kimya wakinitazama kwa majonzi huku machozi yakiwatoka.

“Sasa nitamwonaje ikiwa baba yenu hataki hata kuniona?” nilimuuliza Dk. Camila kwa huzuni.

“Hilo wala usijali… tumewasiliana na Mama anasema wewe nenda, yeye ataongea na baba, bila shaka ataelewa,” alisema Dk. Camila.

“Dah!” nilimaka huku nikijaribu kufikiria juu ya ugumu wa kumkabili baba yake Rehema kutokana na misimamo yake, nilihisi kukata tamaa. Olivia aliligundua hilo.

“Usijali, Jason… mimi nipo na wewe hadi mwisho, nitakusindikiza ukamwone. Kuanzia sasa ninasitisha shughuli zangu zote na sitarudi Botswana hadi nijue hatma yako na Rehema,” Olivia alisema huku akinipapasa kwenye bega.

Siwezi kuelezea ni jinsi gani nilivyopatwa na furaha ya ghafla kiasi kwamba sikuhisi hata hofu tena.

“Dah… nakushukuru sana Olivia kwa upendo wako wa pekee wa kusitisha shughuli zako zote na kuwa pamoja nami hasa katika kipindi hiki kigumu. Umekuwa mfariji wangu na mshauri wangu mkubwa, na bado unaacha shughuli zako kwa ajili yangu! Itanichukua miaka mingi kulisahau hili. Nina deni kubwa kwako ambalo sijui nitalilipa vipi!” nilimwambia Olivia na kumfanya atabasamu.

“Wewe ni rafiki yangu, una thamani kubwa kupita mali, biashara na kila nilichonacho…” Olivia aliniambia kwa sauti ya kirafiki na kuwafanya Dk. Camila na Mama mdogo watazamane kwa namna ambayo sikuweza kuelewa mara moja.

* * *

Endelea...
 
fungate.jpeg

147

Naomba niwe mkweli…


Saa 5:30 asubuhi.

UAMUZI ni jambo ambalo huamua kesho yetu wanadamu. Kuna uamuzi ambao huwa tunafanya huku tukiamini kuwa ni sahihi lakini kesho yake tunajikuta katika wakati mgumu wa kujutia. Lakini pia wakati mwingine tunafanya uamuzi ulio sahihi na baadaye tunajisifia kuwa tunaweza.

Zilikuwa zimepita siku mbili tangu Dk. Camila na Mama yake mdogo walipofika nyumbani kwangu na kuniomba nikamwone Rehema. Nilifunga safari, nikiwa nimesindikizwa na Olivia, hadi Morogoro Mjini nyumbani kwa akina Rehema, katika jumba kubwa la kifahari lililojengwa eneo la Forest Hill, yalipo makazi ya kisasa ya watu wenye uwezo mkubwa kifedha katika mji wa Morogoro.

Ilikuwa nyumba kubwa na nzuri ya kifahari iliyozungukwa na miti mizuri ya vivuli na sehemu za wazi zenye bustani nzuri ya maua na nyasi za kijani kibichi zilizokatwa vizuri. Ukuta wake kuizunguka ile nyumba ulikuwa mrefu uliofungwa mfumo maalumu wa umeme wa kuzuia wezi na kulikuwa na vibao vidogo vyenye maandishi mekundu ya tahadhari yaliyoandikwa: ‘Nyumba hii inalindwa na mitambo maalumu ya kuzuia wezi’.

Eneo la Forest Hill lilikuwa na majumba ya kifahari yaliyozungukwa na miti mirefu na kuta zenye usalama wa uhakika huku ustaarabu wa kisomi ukionekana kuzingatiwa kwa asilimia zote katika Manispaa hiyo ya Morogoro. Na mitaa yake ilikuwa imeunganishwa kwa barabara nzuri zenye taa za barabarani.

Kwa dakika tano nzima tangu nilipoingia chumbani kwa Rehema sikuweza kusema chochote, nilikuwa nimesimama mbele ya Rehema, miguu yangu haikuwa na nguvu ingawa sikuweza kukaa chini. Mama yake Rehema alikuwa amenipa nafasi ya pekee ya kuonana na binti yake. Muda huo Baba yake Rehema hakuwepo nyumbani.

Rehema alikuwa amelala kitandani katika chumba chake, chumba kikubwa chenye kitanda kikubwa cha samadari cha futi sita kwa sita, hali yake haikuonekana kuwa nzuri. Mwili wake ulikuwa umedhoofu na haukuwa hata ukitikisika. Ilikuwa ni kama nilikuwa natazama sinema ya kusikitisha na ilikuwa vigumu sana kuamini kilichotokea.

Nilijaribu kuvuta picha ya Rehema wa zamani, yule binti mrembo ambaye uzuri wake ulitosha kabisa kuudhihirisha utukufu wa Mungu kwenye sanaa ya uumbaji, lakini sasa alionekana kama kituko fulani kwa jinsi alivyodhoofika!

Nilikumbuka wakati nilipokutana naye mara ya kwanza nikiwa na miaka 19 na yeye akiwa na miaka 16 tu, tukawa marafiki na baadaye kufungua ukurasa mpya wa mapenzi, ingawa ni katika mizania isiyolingana kwa kuwa Rehema alinipenda sana lakini mimi sikujua mapenzi ni kitu gani!

Sasa nilikuwa namtazama jinsi alivyodhoofu na hata rangi ya ngozi yake ilikuwa imebadilika, ujasiri wangu wote niliokuwa nao uliniisha, nilijikuta nikitetemeka mwili wote kila nilipomtazama Rehema. Yeye alikuwa ananitazama lakini hakuweza kusema chochote. Macho yangu yalianza kutoa machozi. Na muda huo huo niliiona michirizi ya machozi machoni pake pia.

Hali hiyo ilinifanya nitaabike sana moyoni kila nilipowaza kuwa matatizo yote yaliyokuwa yakimtokea Rehema yalisababishwa na ukware wangu wa kumtamani kila msichana mrembo niliyekutana naye, moyo wangu ulipandwa na hasira kupita kawaida na hapo nikaanza kujichukia mwenyewe, sikuwa radhi kumwona Rehema akiwa katika hali ile.

Niliinama na kumkumbatia pale kitandani. Nilishindwa kujizuia, nilianza kulia kwa sauti, nililia sana kwani sikuwa na matumaini kama angeweza kuinuka na kurudi katika hali yake ya zamani. Nililia sana kwa uchungu. Nilisikia uchungu mkubwa ambao sijawahi kuupata na moyo wangu ulikuwa kama unavutwa kutokana na uchungu mkubwa. Ulikuwa uchungu ambao sikuweza hata kuelezea maumivu yake.

Kilio changu kilipozidi Mama yake Rehema na Olivia waliingia mle chumbani. Mama yake Rehema alikuwa mwanamke nadhifu sana na mrefu. Mtu yeyote asingehitaji kuambiwa kuwa yule mama alikuwa mzazi wa Rehema kwa namna walivyofanana sana. Muda huo alikuwa amevaa gauni zuri la kitenge na alijifunga kilemba kichwani.

Olivia alinitoa pale kitandani kisha akanikumbatia kwa upendo kama mama amkumbatiaye mwanawe wa pekee. Yeye pia alishindwa kuyazuia machozi. Alichukua kitambaa laini na kunifuta machozi, kisha akamfuta na Rehema.

“Usilie, Jason… jipe moyo, naamini kwa uwezo wa Mungu Rehema atapona tu,” Olivia alisema kwa sauti ya kirafiki huku akinipiga piga mgongoni.

Hakikuwa kitu cha kawaida kwa mwanamke kumbembeleza mwanamume asilie kwa sababu imezoeleka kwamba wanaume ni watu majasiri na huwa wanaumia kwa ndani, lakini siku hiyo mambo yalikuwa tofauti kabisa. Nilishindwa kuwa na ule ujasiri wa kiuanaume. Nilishindwa kujizuia kulia mbele ya wale wanawake mle chumbani.

“Rehema, nasikitika sana, sikupaswa kukutenda yale niliyokutenda kwani ulipokuja katika maisha yangu uliyafanya yawe ya furaha kubwa. Sijawahi kupata furaha na sitapata furaha tena katika maisha yangu kama niliyoipata nikiwa nawe. Siwezi kuzisahau zile nyakati nzuri za furaha tulizokuwa pamoja. Hizo zitabaki kuwa kumbukumbu pekee kwangu. Ninakupenda sana Rehema ingawa nimepata wakati mgumu sana wa kukuona kwa kuwa baba yako hataki mimi na wewe tuonane, lakini sitaacha kukupenda…” nilimwambia Rehema kwa uchungu na kisha nikainama pale kitandani na kumbusu kwenye paji la uso.

“Nitakupenda siku zote za maisha yangu na sitakuwa na mwanamke mwingine katika maisha yangu zaidi yako. Ninakuombea upone haraka Rehema,” niliongeza huku nikizidi kutokwa na machozi na kuwafanya Olivia na Mama yake Rehema nao watokwe na machozi.

Sikuwa na hakika kama Rehema aliyasikia maneno yangu lakini nilishuhudia macho yake yakifunikwa na machozi. Nikatoa kitambaa laini toka mfukoni mwangu na kumfuta machozi kwa upendo. Kwa kweli kilikuwa kipindi kigumu mno kwangu. Niliumia sana. Hata hivyo Olivia alikuwa karibu yangu akinitia moyo.

Niliinamisha sura yangu chini nikiwa na mawazo mengi sana. Sikuwa naongea chochote kile kwa kuwa nilikuwa katika maumivu makali sana ya moyo. Nilizama kwenye tafakari ya kina juu ya hatima ya Rehema na maisha yangu bila mwanamke huyo hadi pale sauti ya Mzee Benard Mpogoro, Baba wa Rehema iliponishtua wakati alipoita kutokea sebuleni.

Wote tulishtuka, na hapo mimi na Olivia tukaangaliana na kushusha pumzi. Mama wa Rehema akatoka haraka kuelekea sebuleni akiwa na wasiwasi. Na baada ya muda mfupi alirudi tena chumbani na kuniambia kuwa ‘Mzee’ alikuwa ananiita sebuleni.

I'm sorry, Ray, for what happened. Kwa sasa mimi si yule Jason asiyejua thamani ya pendo lako, nimebadilika sana. Naapa sitakuacha, nitaendelea kukupenda hadi mwisho wa uhai wangu,” nilisema kwa uchungu kisha nikainamia tena pale kitandani nikambusu Rehema kwenye paji la uso wake halafu nikatoka mle chumbani huku nikifuta machozi na kuelekea sebuleni.

Endelea...
 
fungate.jpeg

148

Nilipotokea pale sebuleni nilishangazwa na hali ya ukimya mzito ulionifanya nisikie sauti hafifu ya hatua zangu mwenyewe wakati nilipokuwa nikitembea taratibu kukatisha ile sebule kubwa nikielekea kule alikokuwa ameketi mzee Benard Mpogoro.

Sebule hiyo ilisheheni samani zote muhimu za kisasa; kulikuwa na seti mbili za makochi ya sofa ya kifahari yaliyopangwa katika mtindo wa kuizunguka ile sebule. Katikati ya sebule kulikuwa na meza nzuri ya kioo yenye umbo la yai iliyozungukwa na stuli ndogo nne za sofa.

Upande wa kulia wa sebule hiyo kulikuwa na runinga pana iliyofungwa ukutani na chini yake kulikuwa na meza fupi nyeusi yenye sistimu ya muziki na visimbuzi viwili vya DStv na StarTimes.

Ukutani kulikuwa na picha kubwa nne zilizowekwa ndani ya fremu nzuri za kioo na kuzifanya zionekane vizuri; ya kwanza ilikuwa ya wazazi wa Rehema, nyingine ilikuwa picha kubwa ya Rehema aliyoipiga siku ya mahafali ya kumaliza Chuo Kikuu na alikuwa amevalia joho maalumu na kofia yake. Picha zingine mbili zilikuwa za kuchorwa zenye kuvutia sana, za wanyama pori.

Upande wa kushoto wa sebule kwenye kona kulikuwa na meza fupi ya mapambo na pembeni ya meza hiyo kulikuwa na rafu kubwa iliyopangwa vitabu na majarida mengi na juu ya rafu hiyo kulikuwa na vinyago vya Kimakonde vilivyopangwa kwa ustadi wa hali ya juu.

Upande huohuo kulikuwa na ukumbi mdogo wa chakula wenye meza kubwa ya chakula yenye umbo la yai iliyozungukwa na viti sita nadhifu vyenye foronya laini.

Mzee Benard Mpogoro alikuwa ameketi kwenye sofa kwa utulivu mkubwa huku akionekana mwenye fikra nzito. Uso wake ulikuwa umesawajika kidogo na macho yake yalitazama nje kupitia kioo cha dirisha pana la sebuleni pasipo kuniangalia hata baada ya kujua kuwa nilikuwa nimeingia pale sebuleni.

Alikuwa mrefu, maji ya kunde na mwenye sura mviringo iliyoonesha utulivu, na macho yake yalikuwa makubwa yenye uchovu lakini yaliyokuwa na kila dalili ya kuonya. Kichwani alikuwa amenyoa upara uliokuwa unawaka na alikuwa na ndevu nyingi zilizokizunguka kidevu chake.

Alivaa shati zuri la kitenge na suruali ya kadeti, usoni alivaa miwani mikubwa ya macho na alikuwa ameshika bakora yake ya heshima mkononi.

Nilisimama nikimtazama yule mzee kwa wasiwasi kidogo, nilijua kabisa mambo hayakuwa sawa, huenda alikuwa bado ana kinyongo na mimi!

“Shikamoo, Baba!” nilimsalimia kwa adabu huku nikiendelea kumtazama kwa wasiwasi kidogo.

Yule mzee hakuitikia salamu yangu na wala hakunitazama usoni, ni kama hakuwa amenisikia, aliendelea kutazama nje huku uso wake ukiwa hauoneshi tashwishwi yoyote na mawazo yake yakionekana kuwa mbali na eneo lile.

“Mzee, nakusalimia au kuna tatizo lolote!” nilimuuliza huku nikizidi kushangaa.

Kama mtu aliyezinduka toka kwenye lindi la mawazo, aligeuza shingo yake kunitazama, na alitaka kunijibu lakini nikaona akisita na kuyaelekeza macho yake kutazama nyuma yangu huku akiachia mdomo wake na kubaki wazi kwa mshangao.

Haraka niligeuza shingo yangu kutazama kule ambako macho ya yule mzee yalielekea na hapo nikamwona Olivia akitokea chumbani kwa Rehema akija pale sebuleni tulipokuwa kwa mwendo wa taratibu huku akiwa na wasiwasi kidogo. Nyuma ya Olivia Mama Rehema alifuatia.

Kwa mwonekano wa haraka ungeweza kudhani ni Rehema na mama yake kwa jinsi walivyorandana. Nikagundua kuwa yule mzee alikuwa anamshangaa Olivia hasa kwa namna alivyofanana sana na Rehema.

Sikuona sababu ya kuendelea kusimama, nililiendea sofa moja kubwa nikaketi. Olivia alifika na kuketi juu ya lile sofa kubwa pembeni yangu kisha alimsalimia Mzee Mpogoro kwa adabu. Yule mzee aliitikia salamu hiyo huku macho yake yakiwa yanamtazama Olivia kwa tuo na uso wake ukiwa bado umepambwa na mshangao mkubwa.

Ni kama aliyekuwa amechanganyikiwa au akijiuliza maswali magumu ambayo hakuwa na majibu yake. Kisha aliyahamisha macho yake kutoka kwa Olivia na kunitazama na hapo nikawahi kufanya utambulisho haraka haraka.

“Olivia, kutana na Mzee Benard Mpogoro, ndiye Baba wa Rehema…” nilimwambia Olivia kisha nikaongeza, “Baba, huyu ni rafiki yangu, Dk. Olivia Mkuro, daktari wa masuala ya afya ya akili. Kwa sasa anafanya shughuli zake nchini Botswana.”

Na hapo nikamwona Olivia akinyanyuka na kwenda kumpa mkono yule mzee kwa adabu.

“Ninafurahi sana kukufahamu mzee wangu. Poleni sana kwa matatizo,” Olivia alisema kwa huzuni.

“Hata mimi nafurahi kukufahamu, Dk. Mkuro. Karibu kwetu Morogoro,” Baba yake Rehema alisema kwa sauti tulivu lakini iliyojaa huzuni.

“Ahsante, Baba. Tumekwisha karibia,” Olivia alisema huku akinitupia jicho la wizi kisha akarudi kuketi pale kwenye sofa pembeni yangu.

“Hivi hili jina la Mkuro, si la wenyeji wa Kilosa kweli?” Mzee Mpogoro alimuuliza Olivia huku akimtazama kwa umakini.

“Ndiyo, Baba, mimi ni mzaliwa wa Kilosa. Japo naishi Botswana lakini wazazi wangu bado wanaishi Kilosa eneo la Mazinyungu,” Olivia alisema.

Okay!” Mzee Mpogoro alisema huku akibetua kichwa chake. “Umenishtua sana wakati unaingia hapa, umefanana sana na binti yangu Rehema, mtu akiwaona anaweza kudhani ninyi ni mapacha!”

“Kila mtu ananiambia hivyo… ni kweli tumefanana sana. Unajua duniani wawili wawili,” Olivia alisema na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Uko sahihi ingawa itabidi tufanye uchunguzi isije kuwa tuna undugu!” yule mzee alisema kisha akaendelea, “Sasa Jason, naomba niwe mkweli… sijafurahishwa na ujio wako hapa nyumbani. Kama unakumbuka nilikuomba, kistaarabu kabisa, uachane kabisa na Rehema kwa kuwa wewe ndiye chanzo cha binti yangu kupatwa na matatizo haya.”

Maneno ya Baba yake Rehema yalitufanya mimi na Olivia tutazamane, niliuhisi mwili wangu ukiingiwa na ubaridi mkali. Nilidhani kuwa kutokana na hali aliyokuwa nayo Rehema yule mzee angeweza kulegeza msimamo wake ili tuangalie namna ya kumsaidia aweze kupata nafuu.

“Dk. Mkuro… naomba usinielewe vibaya, binti yangu. Najua rafiki yako ni kijana mzuri mwenye moyo wa upendo, jasiri, mtu makini na mwenye nidhamu lakini hafai kabisa kuwa na binti yangu. Labda asubiri hadi nitakapokuwa nimekufa,” Baba yake Rehema alisema kwa msisitizo.

“Kwa nini tusiangalie kwanza namna ya kumsaidia Rehema hasa kwa wakati huu? Mimi nadhani mpe Jason nafasi ya kuwa karibu na Rehema japo kwa wakati huu tu na Rehema atakapopata nafuu…” Olivia alisema kwa huzuni lakini yule mzee akamkata kauli.

Endelea...
 
fungate.jpeg

149

“Hapana!” Baba yake Rehema alisema huku akitingisha kichwa chake, sauti yake ilionesha wazi kuwa alikuwa na hasira. “Tayari nilikwisha fanya uamuzi na siwezi kuubadili tena. Nashangaa kwa nini Jason hajakwambia!”

“Lakini, Baba, kama unataka Rehema apate nafuu haraka ni vyema ukamruhusu Jason kuwa karibu naye, kwa taaluma yangu najua kuwa kinachomsumbua zaidi Rehema ni msongo mkali wa mawazo na kwa hali hiyo anahitaji zaidi faraja ya mtu anayempenda,” Olivia alisema kwa sauti tulivu lakini iliyosisitiza, na hata sura yake ilimaanisha kile alichokisema.

Baba wa Rehema alikaa kimya kwa muda kama aliyekuwa anafikiria jambo kisha alitingisha kichwa chake akionesha kutoafikiana na maneno ya Olivia.

“Kwa sasa hataiwezekana… hata hivyo naomba niwashukuru sana kwa namna mlivyoonesha kuguswa na kutaka kumsaidia Rehema. Mungu awajalie afya na…” yule mzee alisema na kusita kidogo kisha alinikazia macho akanitazama kwa umakini.

“Nakuombea umpate mwanamke mwingine utakayempenda kama unavyompenda Rehema,” alisema kwa namna ambayo nilihisi alikuwa akinisimanga.

Nilibaki kimya huku machozi yakinilenga lenga. Moyoni niliumia sana. Mama wa Rehema alionekana kunionea huruma sana lakini hakuwa na uamuzi japo alionekana kutaka kusema jambo. Niliinamisha uso wangu kwa zaidi ya dakika tano nikiwaza.

Kwa mara nyingine tena nilihisi kuadhibiwa na dunia. Nilisikia maumivu makali sana ndani ya moyo wangu, maumivu ambayo hayaelezeki kwani ilikuwa ni zaidi ya maumivu. Niliwaza sana kuhusu mustakabari wa maisha yangu, nikajiona mtu mwenye mkosi mkubwa na laana.

Jason, it’s time to go,” sauti ya Olivia ilinizindua toka kwenye lindi la mawazo. Niliinua uso wangu uliokuwa umejaa machozi nikamtazama Olivia na kisha Mama wa Rehema ambaye alionekana kunionea huruma sana. wakati huo Mzee Mpogoro alikwisha ondoka pale sebuleni na sikujua alielekea wapi!

Niliinuka kwa unyonge kisha tukaondoka huku tukisindikizwa na Mama wa Rehema. Sikuweza kutamka chochote kwa sababu nilihisi fundo kubwa la hasira likinikaba kooni.

“Jason, usikate tamaa mwanangu. Siku zote mtegemee Mungu naye atakusaida katika kila jambo. Endelea kumwombea mwenzako na Mungu akipenda siku moja mtakuwa pamoja tena. Nitakuwa nakupigia simu mara kwa mara kukujulisha maendeleo yake,” Mama wa Rehema aliniambia wakati tulipofika kwenye gari letu na kunipa mkono wa kuniaga. Macho yake yalionesha kulengwa lengwa na machozi.

“Nashukuru sana, Mama. Naomba nikiri kwamba Rehema ndiye mwanamke ninayempenda sana hapa duniani na kuumwa kwake ni pigo kubwa kwangu na katika maisha yangu. Lakini sina namna maana napaswa kuuheshimu uamuzi wa Baba, ila nitaendelea kumwombea kwa Mungu aweze kupona,” nilisema huku nikimpa mkono yule mama kumuaga.

Kisha tuliingia kwenye gari letu na kurejea Msamvu hotelini tulikofikia. Sasa nilikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa kiakili. Sikujua nifanye nini kwa wakati huo.

“Olivia, kwa nini maisha yangu yamekuwa ya namna hii? Sidhani kama ninastahili adhabu ya kiwango hiki!” nilimwambia Olivia wakati tukiwa tumeketi hotelini baada ya kutoka nyumbani kwa akina Rehema.

“Usiwaze sana, Jason, ni wakati mwafaka sasa wa kufanya uamuzi katika maisha yako na kuitafuta amani ya moyo,” Olivia aliniambia kwa sauti ya upole.

“Sina hakika kama nitaipata hiyo unayoiita amani ya moyo. Nimeumizwa sana na moyo wangu umejaa huzuni…” nilisema kwa huzuni huku nikihisi machozi yanataka kunitoka.

“Amani ya moyo inapatikana pale tu unapomwachia Mungu fadhaa zako zote. Ni Mungu pekee atayekupa amani ukimwomba, atakupa pia mke mwema, atakupa familia na atakupa kila unachokihitaji,” Olivia alisema kwa sauti ya upole lakini iliyobeba msisitizo.

Nilishusha pumzi za ndani kwa ndani nikimshukuru Mungu kwa kumleta Olivia kwenye maisha yangu maana bila yeye huenda ningekuwa nimeshachanganyikiwa.

* * *



Saa 1:30 usiku.

“Umekula?” Olivia aliniuliza baada ya kuingia chumbani kwangu na kunikuta nikiwa nimejilaza chali kitandani nikitafakari, macho yangu yakitazama juu darini.

“Hapana! Unafikiri nitaweza kula wakati Siijui hatma yangu na Rehema yupo katika hali ile!” nilimjibu Olivia pasipo hata kumtazama.

“Unatakiwa kula, Jason, tangu asubuhi hujala kitu chochote au unataka na wewe ulale kitandani kama Rehema?” Olivia aliniuliza kwa sauti ya upole. “Nikuletee nini?”

“Usijali niko sawa, wala usisumbuke,” nilimjibu huku macho yangu yakiendelea kutazama juu.

“Lakini Jason, una…” Olivia alitaka kusema lakini nikamkatiza.

“Niko sawa, husikii!” nilimjibu kwa sauti ya juu ya ukali kidogo. Kisha nikajishtukia kwa kuwa Olivia hakupaswa kujibiwa hivyo. Yeye alikuwa anatimiza wajibu wake kama rafiki mwema na mnasihi wangu aliyependa kuniona nikifurahi na kuwa na amani ya moyo.

“Usijali… niko sawa, mpenzi. Wewe nenda ukale mimi nimeamua kuanza mfungo na maombi ya siku tatu,” niliongea kwa sauti ya chini ya kirafiki.

Olivia alinitazama kwa muda kama aliyekuwa akijaribu kuyasoma mawazo yangu kisha akaachia tabasamu pana na kutoka akiniacha peke yangu. Ni kweli niliamua kutokula kwa siku tatu na kuomba kwa Mungu japo sikujua hata namna ya kuomba, lakini niliamini kuwa Mungu alifahamu kuhusu dhamira yangu.

* * *

Endelea...
 
fungate.jpeg

150

Haraka ya nini!


Saa 1:00 jioni.

ILIKUWA jioni tulivu mno yenye manyunyu hafifu ya mvua yaliyokuwa yanaanguka juu ya paa la mgahawa wa kisasa wa La Costa uliokuwa jirani na jengo moja la biashara la Zongomera Plaza, barabara ya Zongomera. Ulikuwa mgahawa mzuri wa kisasa wenye huduma zote muhimu, utulivu wa kutosha na aina mbalimbali ya vyakula vya watu wa mataifa tofauti.

Mimi na Olivia tulikuwa ndani ya mgahawa huo. Tulikuwa tumeketi kwenye meza moja iliyojitenga kwenye kona moja ya mgahawa. Sehemu ile tuliyoketi ilituwezesha sote kuona nje ya mgahawa ule kupitia kuta safi za vioo zilizokuwa zikitazamana na barabara pana ya lami.

Mimi nilikuwa napata supu nzito ya ng’ombe yenye saladi na chapati mbili, Olivia yeye alikuwa ameagiza kuku nusu wa kienyeji na saladi ya mboga za majani.

Jioni hiyo uzuri wa Olivia ulikuwa umeongezeka maradufu. Alikuwa amevaa gauni refu la kumeremeta lililochanganywa rangi nyeupe na maruni na lilikuwa na ‘lace’ za kuvutia huku zikiwa na mwonekano wa kupendeza sana, kichwani alivaa kofia nyeupe yenye ‘lace’ mfano wa kofia ya kimalkia na miguuni alivaa viatu vya rangi nyeupe vyenye visigino virefu.

Gauni hilo lilimpendeza sana kiasi cha kuzitaabisha vibaya nafsi za wanaume wasiokuwa na msimamo na mkono wa kushoto alivaa saa ghali aina ya Cartier yenye nakshi ya madini ya dhahabu.

Nami nilivaa suti nzuri nzuri ya kitambaa cha kodrai ya rangi ya samawati na ndani ya suti hiyo nilivaa shati zuri la mikono mirefu la rangi ya maruni. Miguuni nilivaa viatu vya ngozi vya rangi ya maruni.

Ndani ya mgahawa huo kulikuwa na watu wengi, wengi wao wakionesha kuwa wageni wa kutoka nje ya nchi ambao niliwatambua haraka baada ya kuwasikia vizuri wakizungumza Kiswahili chenye lafudhi ya mataifa kama DR Congo, Burundi, Uganda na wengine waliongea lugha za mataifa mengine, na muda mwingi walikuwa wakitutazama kwa jicho la wivu. Hakika tulipendeza sana na kuonekana kama wapenzi tulioshibana na kuendana vizuri sana.

Muda mwingi macho ya Olivia yalikuwa yakinitazama kiwiziwizi na akili yake haikuonekana kuzama kwenye kile chakula alichokuwa anakula badala yake alikuwa akinitazama kila mara na kutabasamu. Aina ya utazamaji wake siku hiyo iliniacha njia panda. Nilihisi alikuwa na jambo ambalo alitaka kunifanyia surprise. Nilichofanya ni kusubiri tu nione mwisho wake.

Ilikuwa imeshapita miezi mitatu tangu tulipokwenda Morogoro kumwangalia Rehema kabla hatujafukuzwa na Baba yake. Sasa nilikuwa nimekubaliana na hali halisi na kuanza maisha mapya kabisa kwa msaada wa Olivia, maisha bila ya Rehema.

Olivia alikuwa amenisaidia kukubaliana na hali halisi kuwa Rehema hakuwa wangu tena na kama tuliandikiwa kuwa pamoja, kwa kuwa ndoa huandikwa mbinguni, basi hakuna binadamu yeyote angezuia, na kwamba siku moja Rehema angerejea kwenye maisha yangu.

Wiki moja baada ya kutoka Morogoro Olivia aliniaga na kurudi nchini Botswana kuendelea na shughuli zake, na alipokuwa huko hatukuacha kuwasiliana. Pia sikuacha kuwasiliana na Mama yake Rehema au wakati mwingine kwenda nyumbani kwa Dk. Camilla ili kutaka kujua maendeleo ya afya ya Rehema.

Hata hivyo mara zote majibu niliyopewa yalikuwa kwamba, “hali ya Rehema bado si nzuri” na yalionekana kunivunja moyo kabisa.

Muda mwingi nikaanza kushughulikia masuala ya kampuni yangu ya teknolojia kwa kuwa nilikuwa nimeacha kazi katika mgodi wa dhahabu wa Buzwagi.

Sasa miezi mitatu ilikuwa imepita na siku moja Olivia alirejea ghafla Kahama bila hata kunijulisha kama angekuja na alinikuta nikiwa nimelala kwenye sofa sebuleni kwangu kutokana na uchovu mwingi niliokuwa nao baada ya pilika pilika za hapa na pale.

Sikukumbuka nilikuwa nimelala kwa muda gani hadi niliposhtuliwa na mtu aliyekuwa ameingia ndani kwangu na kunitingisha taratibu. Nilipofumbua macho yangu nikagundua kuwa alikuwa ni Olivia. Nikashangaa sana! Sikujua aliingia saa ngapi na aliingiaje!

“Hey, Olivia!” nilimaka kwa mshangao huku nikiyafikicha macho yangu.

“Jason, samahani kwa kukukatiza usingizi wako…” Olivia alisema kwa sauti tulivu huku akiketi pale kwenye sofa nililolalia.

“Mbona umekuja bila hata taarifa?” nilimuuliza Olivia huku nikimtazama kwa mshangao.

“Nilitaka kuja kufumania, si unajua tena wivu sina ila roho inauma!” Olivia alisema kwa utani na kuangua kicheko. Nami nikacheka huku nikiinuka kwa uchovu na kuketi pale kwenye sofa huku nikimkabili Olivia.

“Duh! It’s realy a surprise visit! Karibu sana, Olivia, nimefurahi kukuona tena,” nilisema kwa furaha. Olivia alitabasamu tu pasipo kusema chochote.

“Enhe! Lete habari rafiki yangu, kulikoni kuja kimya kimya!” nilimuuliza Olivia huku nikimtazama kwa tuo usoni.

“Samahani, Jason, nina ombi moja tu kwako tafadhali,” Olivia alisema kwa sauti tulivu huku akinitazama kwa namna ya mashaka kidogo.

“Sema tu, Olivia, hata kama ni maombi kumi, tena bila ya tafadhali,” nilimwambia Olivia kumtoa shaka.

“Nimekushtukiza lakini naomba jiandae nataka tutoke twende sehemu kuna kitu kizuri nataka nikuoneshe, naamini utafurahia sana,” Olivia aliniambia kwa sauti ya kirafiki huku akinitazama kwa namna ambayo sikuweza kuelewa maana yake.

Niliwaza haraka haraka ni kitu gani hicho ambacho Olivia alitaka kunionesha? Uso wangu hakuficha shauku yangu na hapo nikamuuliza,
“Ni kitu gani unachotaka kunionesha!”

“Ni mpaka hapo tutakapofika sehemu hiyo ndiyo utakijua, tusiandikie mate wakati wino upo!” Olivia alisema na kuzidi kunipa shauku.

Sikuwa na namna yoyote ya kufanya wala kubisha kwa sababu nilimwamini sana Olivia, sikutegemea kama angeweza kunifanyia uhuni maana tangu nifahamiane naye amekuwa msaada mkubwa sana kwangu, amekuwa mshauri na rafiki yangu mkubwa, hivyo nikajiandaa na saa moja baadaye tulikuwa ndani ya mgahawa huo wa kisasa wa La Costa.

Tulipoingia ndani ya mgahawa huo tulitafuta meza moja iliyojitenga kwenye kona moja ya mgahawa tukaketi.

Wakati tukiendelea kupata mlo niligundua kuwa Olivia alikuwa akinitazama kwa jicho la wizi. Sikutaka kumnyima nafasi ya kunitazama na hivyo mara kwa mara nikawa nikizuga kutazama nje ya mgahawa ule. Pamoja na yote macho ya Olivia hayakuhama kwangu na badala yake yalikuwa makini kunitazama na kufuatilia kwa karibu kila tukio nililokuwa nikilifanya.

Sikujua alikuwa na nini mwanamke huyo! Hadi muda huo hakuwa amenionesha kile alichoahidi kunionesha, na wakati wote tukiendelea kula akili yangu ikawa ikiendelea kusumbuka katika namna ya kuwaza kuwa ni kitu gani alichopanga kunionesha! Hata hivyo, niliendelea kusubiri hadi nione mwisho wake.

Kuna wakati nilipoacha kutazama nje ya mgahawa ule niliyatembeza macho yangu kuzitazama sura za watu waliokuwa mle ndani. Bado Olivia hakuacha kunitazama kwa kuibaiba na kuna wakati akikaribia kuniambia jambo lakini akasita, hata hivyo sikumtilia maanani. Kuna wakati macho yetu yaligongana na hapo kila mmoja akajikuta akiachia tabasamu maridhawa.

“Chakula cha hapa kina ladha nzuri sana,” Olivia alizuga kwa kusifia kile chakula huku akitabasamu.

“Ni kweli,” nilimjibu huku nikimtazama kwa umakini.

Endelea...
 
fungate.jpeg

151

Niligundua kuwa mara kwa mara Olivia alikuwa ‘busy’ na simu yake, alikuwa akisiliana na mtu au watu, walikuwa wakichati kwa jumbe fupi fupi za maandishi kwenye simu na hakutaka kabisa nijue alikuwa akiwasiliana na nani, kila alipotuma ujumbe aliyahamisha macho yake toka kwenye simu yake na kunitazama kidogo kabla ya kuyahamishia pembeni.

Hatimaye nilishindwa kuvumilia nikamuuliza, “Vipi, kuna shida yoyote?”

“Hapana,” Olivia alinijibu huku akiendelea kupata mlo taratibu.

“Ulisema kuna kitu kizuri unataka unioneshe, mbona hadi sasa upo kimya tu na sioni dalili za kuoneshwa?” nilimuuliza Olivia huku nikiwa nimemkazia macho.

Olivia aliyakwepa macho yangu akatazama kando huku akibabaika kidogo, “Haraka ya nini! Wewe subiri muda ukifika utaoneshwa.”

“Ngoja ngoja yaumiza matumbo ati,” nilimwambia Olivia huku nikiwa na shauku kubwa.

“Na haraka haraka haina baraka ati,” Olivia alinijibu na kisha alinyanyua na kunitaka radhi kisha akaelekea maliwato.

Aliniacha nikiwa na shauku ya kutaka kujua nini kilikuwa kinaendelea maana siku hiyo Olivia alikuwa amenishangaza sana kwa tabia aliyoionesha kwangu, alikuwa akinitazama kila mara na kutabasamu kiasi cha kuniacha njia panda. Sasa nilianza kuhisi kuwa huenda aliamua kujikabidhi kwangu.

Ilimchukua takriban dakika kumi huko maliwato na aliporudi aliniomba tuondoke, muda huo ilikuwa imetimu saa 1:30 usiku. Sikuwa na namna yoyote ya kupinga, niliinuka nikamfuata hadi kwenye gari, safari hii alikuja na gari jingine la kifahari aina ya Toyota Landcruiser GX V8 la rangi nyeusi.

Mvua hafifu ilikuwa bado inanyesha na hali ya hewa ilikuwa ya ubaridi ikiambatana na upepo wa wastani. Olivia aliliondoa lile gari kwa mwendo wa kasi na kuyafanya magurudumu yachimbe ardhi, akaingia katika barabarani. Muda huo niliamua kuwa mtulivu sana huku nikitafakari hili na lile kuhusu tabia mpya ya Olivia.

Mara kwa mara Olivia alikuwa akinitupia jicho la wizi wakati lile gari lake likichanja mbuga kukatiza mitaa na baadaye nilishangaa kuona safari yetu ilikuwa ya kurudi nyumbani kwangu Mwime. Na sasa nikashindwa kuvumilia dhihaka ya Olivia.

“Olivia, tangu lini mimi na wewe tumeanza utani?” nilimuuliza Olivia huku nikiwa nimekereka kidogo.

“Ki vipi? Mbona sikuelewi?” Olivia aliniuliza huku akionesha mshangao kidogo.

“Naona umeamua kunifanyia dhihaka, uliniambia unanipeleka sehemu kunionesha kitu lakini…” nilisema kwa hasira lakini Olivia akanikatisha kwa kuangua kicheko kikubwa.

“Kwani wewe tatizo lako nini? Sasa ndo nakwenda kukuonesha unachopaswa kukiona, natumaini utafurahi mno,” Olivia aliniambia baada ya kile kicheko kukoma.

Nilitaka kusema neno lakini nikaamua kukaa kimya maana kwa vyovyote neno hilo lingenifanya nigombane na Olivia na pengine urafiki wetu ungeishia hapo.

Ilitukuchukua dakika ishirini na tano kutoka La Costa hadi kufika nyumbani kwangu, muda huo nyumba ilikuwa kimya sana na kulikuwa na giza nene lililotawala. Nililifungua geti kubwa kwa kubonyeza kitufe kwenye rimoti, geti likafunguka taratibu na kumruhusu Olivia kuliingiza gari lake ndani ya uzio wa nyumba yangu kisha aliliegesha sehemu maalumu ya maegesho ya magari.

Baada ya kuunguruma kwa kitambo kifupi alilizima gari lake na kuteremka, wakati huo nilikuwa nimeshashuka na kumsubiri kisha tuliongozana kuelekea barazani, nikajipapasa na kutoa funguo za nyumba nikafungua mlango wa mbele na kusimama nikiupima utulivu wa mle ndani.

Nilibonyeza swichi ya umeme iliyokuwa pembeni ya mlango ili kuleta nuru ndani ya nyumba na hapo nikakutana na kitu cha ajabu kilichonishtua mno. Mwili wangu wote ukanisisimka na moyo wangu ulipiga kite kwa nguvu. Nilibaki nimepigwa na butwaa kwa sekunde kadhaa nisiamini nilichokiona.

Macho yangu yalikuwa yakakishuhudia kitu ambacho sikukitarajia mahali hapo na kunifanya nitokwe na sauti ya mshango kama vile nisiyeamini kile nilichokiona. Niligeuka kumtazama Olivia aliyekuwa amesimama nyuma yangu kwa utulivu nikamwona akitabasamu kwa bashasha.

Kisha nikayarudisha macho yangu kwenye kitu ambacho sikuwa nimekitarajia kabisa, “Rehema!” nilijikuta nikilitamka jina hilo kwa mshangao mkubwa.

Hakika alikuwa ni yeye, mwanamke ambaye nilimhitaji kuliko uhai wangu alikuwa amesimama mbele yangu huku afya yake ikiwa imeimarika, uso wake ulikuwa umepambwa na tabasamu na macho yake mazuri na malegevu yalikuwa yakilengwa lengwa na machozi huku yakinitazama kwa upendo. Bado alikuwa na ule uzuri usiomithilika uwezao kumliwaza, kumpumbaza na hata kumlaza kitandani mwanamume yeyote aliye buheri wa afya.

Alikuwa amevaa gauni refu lililochanganywa rangi nyeupe na maruni likiwa na ‘lace’ za kuvutia huku zikiwa na mwonekano wa kupendeza sana na nyuma lilijitandaza kama mkia wa ndege mrembo mwenye maringo anayevutia, Tausi!

Kichwani alikuwa amevaa kofia nzuri ya kimalkia iliyozifunika nywele zake ndefu na laini na miguuni alivaa viatu vya rangi ya maruni vya mchuchumio vyenye visigino virefu. Ukichanganya na urefu wake alionekana kama malkia haswa!

“Jason wangu!” sauti ilimtoka Rehema, sauti ambayo ilisikika sawia masikioni mwangu.

Ilikuwa kama ndoto! Nilikuwa kama nisiyeamini, kabla sijajua nini cha kusema, Rehema alinitaka nifunge macho yangu. Niligeuza shingo yangu kumtazama Olivia, akaonesha kunisisitiza nifunge macho. Kwa kuwa kauli ile ilitoka kwa mwanamke niliyempenda sana, sikuwa na jinsi ilibidi kutii kile nilichoambiwa na mwanamke nimpendaye. Nikayafunga macho yangu huku mapigo ya moyo wangu yakinienda kasi.

Sekunde chache baadaye Rehema aliniambia nifungue macho, na hapo ndipo mapigo ya moyo wangu yalipoongeza kasi na kwenda mbio isivyo kawaida. Sebule ilikuwa imefurika watu ambao mwanzo sikujua walitoka wapi lakini baadaye niligundua kuwa wakati naingia walikuwa wamejificha nyuma ya masofa.

Niliwashuhudia wazazi wangu, wazazi wa Rehema, kaka Eddy na mkewe, Swedi na mkewe, mjomba Japheti, Dk. Camila na mumewe, mwanasheria wa Olivia, Fadhil Mbezi na jamaa wengine waliokuwa wakinitazama kwa tabasamu. Mwili ukanisisimka.

Happy birthday to you, happy birthday to you, happy birthday dear Jason… happy birthday to you!” wote walikuwa wanaimba wimbo huo ambao ulinikumbusha kuwa siku hiyo ilikuwa tarehe 26 Machi, siku ambayo nilipaswa kuazimisha siku yangu ya kuzaliwa.

Dah! kweli Olivia alikuwa ameniweza! Alikuwa amefanyia surprise ya nguvu! Nilishindwa kuvumilia, machozi yalinitoka, machozi ya furaha ambayo yalinifanya kwanza nigeuke kumtazama Olivia nikiwa siamini kisha nikamtazama Rehema usoni kabla sauti haijanitoka, “On my birthday!” Lilikuwa swali zaidi ya mshangao.

Endelea...
 
fungate.jpeg

152

Licha ya kumuuliza Rehema swali hilo, bado nilikuwa na maswali mengine kichwani. Niliendelea kumtazama kwa mshangao nisiamini nilichokiona. Mtu ambaye miezi mitatu iliyokuwa imepita alikuwa hoi kitandani akiwa hawezi kufanya kitu chochote sasa alikuwa mzima wa afya!

Yes, my dear, it’s on your birthday!” Rehema alinijibu na kisha akanikumbatia kwa huba. Sauti za makofi na vigelegele kutoka kwa mashuhuda waliokuwepo zilisikika zikisindikiza kumbato hilo. Sikuamini nilihisi kama vile bado niko ndotoni.

Nilishuhudia watu wote waliokuwepo hapo sebuleni wakifurahi, na wakati huo huo Olivia na Mama wakikumbatiana kwa furaha huku machozi yakiwatoka. Nikajiuliza urafiki wa Mama na Olivia ulianza lini! Na hapo nikabaki kwenye mshangao zaidi.

“Nashukuru sana kukuona tena, Ray. Ila bado siamini kama ni wewe kweli!” nilisema huku nikimwachia Rehema na kumtazama kwa umakini.

“Ni mimi, Jason, Mungu ametenda muujiza wake hasa baada ya kutambua bado unanipenda sana na unajutia kosa…” Rehema alijibu huku akitokwa na machozi.

Nilijikuta nikinyoosha mikono yangu juu kumshukuru Mungu kwa kumfanya mwanamke niliyempenda kuwa mzima tena. Niliachana na Rehema na kwenda kuwasalimia wazazi wake, sikuamini kuiona sura ya Baba wa Rehema, Mzee Benard Mpogoro ikiwa imepambwa na tabasamu la upendo huku macho yake yakilengwa lengwa na machozi.

“Jason kijana wangu!” mzee huyo aliniita kwa sauti tulivu na ya upole.

“Naam, Baba!” niliitika huku sura yangu ikipambwa na tabasamu la matumaini.

“Tumekuja sisi sote pamoja na Rehema kwa kuwa nataka kuchukua nafasi hii kukuomba samahani kwa maneno yote mabaya niliyokutamkia, maneno ambayo yalikuudhi sana. Naomba tusameheane na tufungue ukurasa mpya kati yetu. Yaliyopita si ndwele tutazame ya mbele…” yule mzee aliniambia kwa sauti ya upole huku akizidi kulengwa lengwa na machozi.

“Niligundua kuwa hata baada ya maneno yale bado ulionesha upendo mkubwa kwa binti yangu. Rafiki yako Dk. Mkuro amekuwa msaada mkubwa sana na amenieleza mengi sana uliyokuwa unayapitia, pia binti yangu mkubwa Dk. Camila amenieleza mengi na nimeelewa. Sisi kama wazazi wa Rehema hatutakuwa na kipingamizi tena kuhusiana na hatima ya maisha yake, ni yeye mwenyewe ndiye atakayemchagua nani anataka kuwa naye maishani mwake,” yule mzee aliongeza huku akinikumbatia kwa upendo.

“Nawashukuru sana wazazi wangu kwa kufika kwenu. Kwa ufupi mimi sina tatizo lolote nawe. Maneno yote uliyoyasema nilikwisha yasahau kwa sababu Dk. Olivia amekuwa msaada mkubwa kwangu kiroho na kisaikolojia, na siku zote amenisisitiza sana kumkabidhi Mungu fadhaa zangu,” nilisema huku nikipangusa machozi yaliyokuwa yakinilenga lenga.

Kisha watu wote tuliketi kwenye masofa kwa utulivu kwenye masofa huku tukiwatazama Rehema na Olivia waliokuwa wakisaidiana kuleta keki kubwa ya ‘Birthday’ iliyokuwa imepambwa vizuri sana huku ikiwa imeandikwa jina langu juu yake, chupa kubwa mbili za Champaigne (Shampeni) bilauri kadhaa ndefu, sahani na kisu maalumu cha kukatia keki na kuviweka juu ya meza.

Kwa kweli walionekana kama mapacha kwa jinsi walivyofanana. Hadi muda huo bado nilionekana kushangaa sana nikidhani labda nilikuwa ndotoni. Nikashusha pumzi.

“Siamini kabisa, Rehema, umeamua kunifanyia surprise hii katika siku yangu ya kuzaliwa?” nilimuuliza Rehema kwa mshangao kama punguwani.

“Ndiyo Jason… Hongera sana!” Rehema alisema huku akigeuka kumtazama Olivia kwa tabasamu. “Hata hivyo yote haya ameyaandaa rafiki yako Olivia, ukweli mimi sikukumbuka kabisa!”

“Ahsante sana rafiki yangu,” nilimwambia Olivia huku nikifuta machozi ya furaha yaliyoendelea kunilenga lenga.

“Usijali, Jason, imenipasa nifanye hivi kwa kuwa nakujali kama rafiki wa dhati na ninapenda kukuona ukifurahi, lakini pia si mimi niliyeandaa yote haya…” Olivia alisema kwa sauti laini na kusita kidogo, kisha akageuka kumtazama Mama. “Ni mama… mama yako, Jason…”

Niligeuka kumtazama Mama, alikuwa anatabasamu huku machozi ya furaha yakimlenga lenga machoni. Nilishindwa kujizuia nilimsogelea Mama nikamkumbatia na kumpiga busu kwenye paji la uso.

“Ahsante, Mama!” ndilo neno pekee nililomudu kulitamka kwa wakati huo. Mama hakusema neno aliendelea kunitazama kwa upendo huku machozi yakimtoka. Nikatoa kitamba na kuyafuta.

Kisha Olivia aliwasha mishumaa midogo midogo iliyowekwa juu ya keki halafu niliambiwa ninuie jambo ninalotaka kisha niizime mishumaa hiyo kwa kuipuliza, nikafanya kama nilivyoambia na baada ya hapo Olivia alichukua kisu na kukata vipande kadhaa vidogovidogo vya keki na kuviweka kwenye sahani kisha akampa Rehema.

Rehema alichukua uma akachoma kwenye kipande kimoja kidogo cha keki na kunilisha kisha alimpa Olivia, naye akachukua kipande kidogo cha keki na kunilisha. Halafu wakanipa ule uma, nami nikachoma vipande vidogo vya keki na kuwalisha.

Baada ya hapo nilichukua vimbaka vya kuchokolea meno na kuwalisha vipande vya keki watu wengine waliokuwepo hapo sebuleni, na muda huo Rehema na Olivia walichukua zile chupa za Shampeni, wakazitikisha kidogo na kuzifungua kwa ustadi mkubwa, povu liliruka juu na kunilowanisha pale nilipokuwa nimesimama.

Kisha Rehema alimimina Shampeni kwenye bilauri mbili, moja akanipa mimi na nyingine akabaki nayo mkononi, wakati huo huo Olivia akimimina kwenye bilauri zilizobaki na kuwagawia watu wengine, baada ya hapo tukatakiana maisha mema na kunywa kwa furaha.

“Rehema Benard Mpogoro!” nilimwita Rehema kwa sauti tulivu huku nikilitaja jina lake kwa ukamilifu, nikamwona akishtuka sana na kunitazama usoni maana alijua nilikuwa na jambo. Watu wote walikuwa kimya.

“Rehema Mpogoro!” niliita tena huku nikimtazama kwa tuo. Safari hii sikulitaja jina lake la katikati.

“Rabeka! Nakusikiliza,” Rehema alisema kwa sauti laini yenye kitetemeshi kidogo.

After all that happened do you still love me?” nilimuuliza Rehema huku nikiwa bado namtazama usoni.

Rehema alinitazama kwa muda pasipo kusema chochote kisha aliiweka bilauri yake juu ya meza na kunisogelea zaidi, akanishika mikono yangu yote miwili huku akinitazama usoni.

“Jason Sizya!” aliita na kutulia huku akinitazama.

“Naam!” niliitika huku nikiendelea kumtazama kwa tuo.

“Kwa nini umeniuliza hivyo?” Rehema aliniuliza kwa sauti ya upole huku akinitazama machoni.

“Samahani kwa swali langu, maana yangu ni…” nilipotaka kujieleza Rehema akanikata kauli.

World and everything do change but Rehema will never change… I’m the same Ray the MP you knew… bado una nafasi katika moyo wangu,” Rehema aliniambia kwa sauti laini ya upendo kisha akaongeza.

“Umekuwa mwanamume pekee hadi sasa katika maisha yangu. Ulikuwa mwanamume wa kwanza kuingia moyoni mwangu, nikakupa moyo wangu, mwili wangu na kila kitu changu. Pamoja na yote yaliyotokea, I still love you more and more…”

“Rehema, mwenzio nina haya na wala sina hidaya, ninakiri kwa moyo wangu wote kwamba maisha yangu yote yanasubiri kauli yako tu. Je, uko tayari nikutolee posa ili nikuoe?” nilimuuliza Rehema na hapo nikahisi maneno yangu yalimwingia vyema.

Rehema alimwemwesa macho yake na kutabasamu kwa aibu kisha aliinamisha uso wake chini na kuanza kuvunjavunja vidole vyake vya mikono yake.

Kisha aliinua uso wake akinitazama kwa haya na macho yake mazuri, aliniangalia tangu unyayoni hadi usoni, na macho yetu yalipogongana akaachia tabasamu laini. Mashavu yake yalionesha wazi vishimo vidogo, na pembe za midomo yake zikafinya na macho yake yalifanya kuelea. Midomo yake yenye maki ilifunguka na sauti iliyotoka humo ilitosha kabisa kumtoa nyoka pangoni mwake.

“Jason, kwani wataka niseme nini tena? Yote uliyoyataka kwangu ndiyo hayo nimekukabidhi. Mimi ni mali yako peke yako na tayari wazazi wako wameshatoa posa nyumbani kwetu, kilichobaki ni wewe tu kunipokea niwe mkeo…”

Kwa maneno hayo, mkondo wa umeme ulikuwa umepitishwa katika mwili wangu, vita vilikuwa vimekwisha na mimi nikiwa nimesalimu amri! Niliduwaa kwa muda nikiwa sijimudu huku nikiiajabia sauti iliyovunjika, na macho yaliyolegea. Vyote pamoja vilitoa haiba ya kike ndani mwa Rehema na kunimwaia.

Niligeuka kuwatazama wazazi wangu, wakakubali kwa kubetua kichwa. Kisha nilimtazama Rehema, tukatazana na kujikuta tukiachia tabasamu ambalo lilizaa kicheko. Kilikuwa ni kicheko cha furaha isiyopimika!

Tukajikuta tukikumbatiana kwa furaha, Rehema akaipitisha mikono yake nyuma ya shingo yangu na kufanya chuchu za matiti yake kukitekenya kifua changu, na hapo nikajikuta nikiwa na wakati mgumu sana wa kupambana na joto kali la mwili wake.

Nami nikambana zaidi hadi akawa kama sehemu ya mwili wangu. Kisha nilisogeza midomo yangu karibu na midomo ya Rehema, tukaikutanisha. Tulibaki hivyo kwa muda nisioweza kuukumbuka, mioyo yetu ilidunda kwa kasi na muda huo nikihisi kijasho chembamba kikinitoka mwilini, na tulipotaka kubadilishana ndimi zetu mara tukasikia sauti ya kaka Eddy akikohoa.

Tulishtuka sana na kuachiana huku tukiona haya maana tulikuwa tumesahau kuwa pale sebuleni kulikuwa na watu wengine zaidi yetu!

* * *

Endelea...
 
fungate.jpeg

153

Mwisho wa tamthiliya…


Saa 3:00 usiku.

MIMI na Rehema tulikuwa ndani ya mavazi ghali ya harusi. Rehema alikuwa amesimama upande wangu wa kushoto akiwa mtulivu sana, alionekana kuwa na wasiwasi na muda wote macho yake yalikuwa yakitazama chini.

Alikuwa amevalia gauni refu jeupe lililomeremeta likiwa na ‘hollie 2.0’ ya kifahari nyuma na mkono wa ‘applique’d’ ya Kifaransa, pia lilikuwa na lace za kuvutia huku zikiwa na mwonekano wa kupendeza sana. Gauni hilo lilikuwa linaburuzika chini wakati alipokuwa akitembea na kutengeneza umbo zuri mfano wa mkia wa ndege tausi.

Mkono wake wa kushoto alivaa saa ghali ndogo ya kike aina ya Cartier La Dona iliyotengenezwa kwa madini ya dhahabu nyeupe ya Karati 18 ikiwa na kesi imara ya milimita 27 kwa 29 na mkanda wake ulitengenezwa kwa dhahabu nyeupe.

Shingoni alikuwa amevaa mkufu mwembamba wa dhahabu uliokuwa umeizunguka shingo yake nyembamba na kidani cha madini ya tanzanite kilichopotelea katikati ya uchochoro wa matiti yake mazuri.

Kichwani Rehema alikuwa amevaa taji zuri la kimalkia lenye kito cha madini ya tanzanite. Taji hilo lilimfanya aonekane ni mrembo kupindukia! Na alikuwa amejipulizia manukato ghali aina ya Clive yenye harufu nzuri ya kuhamasisha ngono.

Mimi nilikuwa nimevaa suti ghali ya vipande vitatu ya rangi ya kijivu ya single button, brandi ya Dunhill, kwa ndani nilivaa shati zuri la rangi ya samawati la mikono mirefu brandi ya Maria Santangelo kutoka Italy, tai nyekundu shingoni brandi ya Massimo dutti kutoka Spain na viatu ghali vyeusi vya ngozi halisi kutoka nchini Switzerland.

Mkononi nilivaa saa ghali aina ya Cartier yenye nakshi ya madini ya dhahabu na nilikuwa nimejipulizia manukato ghali aina ya Dolce & Gabbana.

Tulishikana mikono na kutembea kwa mwendo wa taratibu huku sauti za hoihoi, nderemo na vifijo zikitusindikiza. Wakati huo nyimbo nzuri za harusi zilisikika eneo lote na kufanya eneo hilo liwe na shangwe za furaha zisizo kifani.

Nyuma yetu tulifuatwa na wapambe wetu, kaka Eddy aliyekuwa ‘bestman’ wangu na Olivia aliyekuwa ‘matron’ wa Rehema ambao pia walikuwa wamependeza sana kwa mavazi yao ghali yaliyowafanya waonekana kama Malkia na Mfalme.

Tulitembea kwa mwendo wa taratibu kuelekea mbele ya madhabahu ambako Kasisi alikuwa amesimama akitusubiri kwa hamu. Tulifika na kusimama mbele ya Kasisi huyo tukiwa kimya kabisa. Muda huo mapigo ya moyo wangu yalikuwa yanakwenda mbio isivyo kawaida.

Kasisi alikuwa kashika Biblia mkononi na aliifungua na kunukuu mistari kadhaa ndani yake kisha alituuliza kama tulikuwa tayari kuishi maisha ya ndoa tukivumiliana katika shida na raha.

Wote tulikubali na kutoa kiapo cha utii katika ndoa tukiahidi kuvumiliana katika shida na raha, kisha tulifungishwa ndoa na kuvishana pete nzuri za dhahabu. Na hapo vigelegele, vifijo na nderemo vikasikika kutoka kila upande…

“Vipi Jason, unawaza nini?” Rehema alinitupia swali lililonizindua kutoka kwenye njozi ya kupendeza.

Niligundua kuwa yote niliyoyashuhudia kuhusu harusi yetu ilikuwa ni njozi tu, nikaachia tabasamu huku nikiwatazama Rehema na Mama kwa kwa aibu.

Wakati huo mimi, Rehema na Mama tulikuwa ndani ya ofisi binafsi iliyokuwa ndani ya nyumba yangu kwa mazungumzo mafupi. Nikakumbuka kuwa ilikuwa ni katikati ya sherehe ya birthday Mama alituomba mimi na Rehema twende chemba kidogo tukazungumze.

Tulipoingia mle ofisini Mama alileta trei kubwa lililokuwa na jagi kubwa la sharubati na bilauri tatu. Akamimina sharubati hiyo ndani ya zile bilauri na kutupa mimi na Rehema huku ile ya tatu akibaki nayo mkononi. Baada ya hapo alituomba tunyanyue bilauri zetu na kuzigongesha ili kutakiana maisha marefu yenye heri.

Muda huo bilauri za sharubati zilikuwa mbele yetu, ni mimi tu nilisubiriwa kunyanyua bilauri yangu ili tugongeshe kwa pamoja na kutakiana maisha marefu yenye heri. Niliinyanyua bilauri yangu haraka kisha tukagongesha huku tukisema kwa Pamoja, “Cheers” halafu nikapiga funda dogo la sharubati na kuirudisha juu ya meza.

Tuliendelea kunywa taratibu huku tukiwa kimya kabisa. Mama alikunywa funda ndefu kisha akaiweka bilauri yake juu ya meza. Alitutazama kwa zamu huku macho yake yakilengwa lengwa na machozi ya furaha na uso wake ukiwa umepambwa na tabasamu.

Tulitazamana katika hali ya kujiuliza maswali yasiyokuwa na majibu, tulionekana kuushangaa ukimya wa Mama, ambaye kwa kawaida alikuwa mtu mcheshi na mwongeaji mzuri.

Hata hivyo kwa mwonekano wake tu niligundua kuwa alikuwa na furaha isiyo kifani iliyomfanya asiamini kile kilichokuwa kinaendelea. Huwenda furaha hiyo ilimfanya apate ububu wa muda huku akidhani labda alikuwa yupo ndotoni na baada ya kuamka kila kitu kingekuwa tofauti kabisa.

Aliendelea kututazama kwa zamu huku akionekana kufurahi sana, kwa mtazamo wa mara moja tu ungeweza kung’amua kuwa alikuwa mwenye furaha isiyo kifani. Nilifahamu kuwa Mama alijivunia sana kuwa na kijana kama mimi.

“Wanangu, msishangae kwa ukimya wangu, hadi sasa siamini kuhusu hiki kinachotokea mbele ya macho yangu, namshukuru sana Mungu hatimaye amesikia kilio changu na vilio vyenu. Ni bayana kuwa kila mmoja wenu sasa amepata tumaini jipya kwa kumpata mwenzi wake wa maisha anayempenda kwa dhati…” Mama alisema huku akifuta machozi. Mimi na Rehema tukaangalia kwa tabasamu. Kisha Mama aliendelea.

“Jason, mwanangu, naifahamu fika tabia yako tangu ukiwa mtoto, natumaini Mungu amekubadilisha, nakuomba sana baada ya ndoa umtunze Rehema kama mkeo uliyechaguliwa na Mungu, na uwe tayari hata kufa kwa ajili yake. Mkaishi maisha mazuri yenye amani, mkisaidiana wakati wa shida na raha, na katika kupata na kukosa. Pia muwe tayari kupokea na kutunza pamoja zawadi mtakayopewa na Mungu.”

Alikaa kimya kidogo huku akinitazama kwa umakini kisha akafungua tena kinywa chake, “Nakuomba sana Jason, umwangalie Rehema kama mboni ya jicho lako na uwe na uwezo wa kuitawala nyumba yako pamoja na moyo mkuu wa kuyashinda majaribu. Pale utakaposhwa jaribu kupata ushauri kutoka kwa watu waliokutangulia.”

Kisha aligeuza shingo yake kumtazama Rehema. Alinyoosha mkono wake kuushika mkono wa Rehema huku akiendelea kutabasamu.

“Rehema, binti yangu, wewe ni fahari ya moyo wangu… sina shaka na nimeridhika kabisa wewe kuolewa na Jason, kijana uliyemchagua mwenyewe na kumpenda kwa dhati ya moyo wako bila kulazimishwa na mtu yeyote,” alisema na kunyamaza kidogo, akafuta machozi yaliyomlenga lenga.

“Sina mengi ya kukwambia kwa kuwa najua kabisa upendo wako ulivyo mwingi kwa Jason… nakuomba endelea kumvumilia mumeo katika taabu na raha na muwe tayari kupokea na kuitunza zawadi mtakayopewa na Mungu…” Mama alisema.

Kisha ndipo Mama alipotueleza kuhusu jambo ambalo liliniacha mdomo wazi. Kwa kweli nilijiona fala! Ilikuwa ni kuhusu siri nzima ya tamthiliya ya kusisimua sana kati yangu kwa upande mmoja na Olivia kwa upande mwingine. Ni Mama ndiye aliyekuwa mwandaaji wa tamthiliya hiyo na iliandikwa kwa namna ambayo isingekuwa rahisi kuujua mwisho wake.

Kwa kweli sikupata angalau kuhisi tu kuwa mwisho wa tamthiliya hiyo ungekuwa ndiyo mwanzo wa safari mpya na ndefu ya matumaini, baada ya kupita kwenye mikasa mizito ya kusisimua.

Mama aliniambia baada kuondoka nyumbani kwangu akiwa pamoja na wajomba zangu wakiniacha nimechanganyikiwa, hakuridhika na hali yangu, kwa kuwa uchungu wa mwana aujuaye mzazi aliamua kutafuta msaada kwa gharama yoyote na ndipo alipokutana na Mama yake Olivia ambaye waliwahi kuwa marafiki enzi za utoto wao miaka mingi nyuma walipokuwa wanasoma shule ya msingi, tena katika darasa moja.

Kwa kujua kuwa Mama yake Olivia alikuwa anaye binti daktari wa afya ya akili ambaye Mama aliamini angeweza kusaidia kunirudisha katika hali yangu ya kawaida, hakusita kumweleza shoga yake huyo kuhusu mapito niliyokuwa nikiyapitia.

Ilikuwa ni bahati kuwa binti huyo alikuwa anafanana kwa asilimia kubwa na Rehema na hivyo ikawa rahisi kuniingia baada ya kupewa taarifa zangu zote na kujifanya mwekezaji, ni Mama aliyekuwa akigharamia kila kitu.

Ukiachia suala la kuwa Olivia alikuwa daktari wa afya ya akili, mambo mengine yote aliyonieleza Olivia ikiwemo habari za ex-boyfriend wake kufanana na mimi na hadithi ya kutendwa havikuwa na ukweli wowote, kwani mchumba wa Olivia ni Fadhil Mbezi ambaye aliwahi kutambulishwa kwangu kama mwanasheria wa kampuni ya Olivia. Kwa kusikia hadithi hiyo nilijikuta nikichoka kabisa!

Kumbe muda wote katika urafiki wangu na Olivia alikuwa akinichora tu kwani mambo yake ya uwekezaji pia yalikuwa ya kutungwa. Si hivyo, hata wale wawakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika tuliokutana nao siku moja kule Krystal Park Hotel walikuwa wameandaliwa, hayo yote yalipangwa ili kuniweka sawa kisaikolojia!

Kwa kweli Olivia alikuwa ameicheza vyema nafasi yake, na kwa kiasi kikubwa ndiye alimsaidia hata Rehema kurudi katika hali yake ya kiafya na hatimaye tukaungana tena. Mimi na Rehema tulitazamana tusijue lipi la kusema.

Nilishangaa kujua kuwa hata kaka Eddy alikuwa anaujua mchezo wote lakini hakuwahi kuniambia chochote!

* * *

Endelea kufuatilia...
 
View attachment 2246623
147

Naomba niwe mkweli…


Saa 5:30 asubuhi.

UAMUZI ni jambo ambalo huamua kesho yetu wanadamu. Kuna uamuzi ambao huwa tunafanya huku tukiamini kuwa ni sahihi lakini kesho yake tunajikuta katika wakati mgumu wa kujutia. Lakini pia wakati mwingine tunafanya uamuzi ulio sahihi na baadaye tunajisifia kuwa tunaweza.

Zilikuwa zimepita siku mbili tangu Dk. Camila na Mama yake mdogo walipofika nyumbani kwangu na kuniomba nikamwone Rehema. Nilifunga safari, nikiwa nimesindikizwa na Olivia, hadi Morogoro Mjini nyumbani kwa akina Rehema, katika jumba kubwa la kifahari lililojengwa eneo la Forest Hill, yalipo makazi ya kisasa ya watu wenye uwezo mkubwa kifedha katika mji wa Morogoro.

Ilikuwa nyumba kubwa na nzuri ya kifahari iliyozungukwa na miti mizuri ya vivuli na sehemu za wazi zenye bustani nzuri ya maua na nyasi za kijani kibichi zilizokatwa vizuri. Ukuta wake kuizunguka ile nyumba ulikuwa mrefu uliofungwa mfumo maalumu wa umeme wa kuzuia wezi na kulikuwa na vibao vidogo vyenye maandishi mekundu ya tahadhari yaliyoandikwa: ‘Nyumba hii inalindwa na mitambo maalumu ya kuzuia wezi’.

Eneo la Forest Hill lilikuwa na majumba ya kifahari yaliyozungukwa na miti mirefu na kuta zenye usalama wa uhakika huku ustaarabu wa kisomi ukionekana kuzingatiwa kwa asilimia zote katika Manispaa hiyo ya Morogoro. Na mitaa yake ilikuwa imeunganishwa kwa barabara nzuri zenye taa za barabarani.

Kwa dakika tano nzima tangu nilipoingia chumbani kwa Rehema sikuweza kusema chochote, nilikuwa nimesimama mbele ya Rehema, miguu yangu haikuwa na nguvu ingawa sikuweza kukaa chini. Mama yake Rehema alikuwa amenipa nafasi ya pekee ya kuonana na binti yake. Muda huo Baba yake Rehema hakuwepo nyumbani.

Rehema alikuwa amelala kitandani katika chumba chake, chumba kikubwa chenye kitanda kikubwa cha samadari cha futi sita kwa sita, hali yake haikuonekana kuwa nzuri. Mwili wake ulikuwa umedhoofu na haukuwa hata ukitikisika. Ilikuwa ni kama nilikuwa natazama sinema ya kusikitisha na ilikuwa vigumu sana kuamini kilichotokea.

Nilijaribu kuvuta picha ya Rehema wa zamani, yule binti mrembo ambaye uzuri wake ulitosha kabisa kuudhihirisha utukufu wa Mungu kwenye sanaa ya uumbaji, lakini sasa alionekana kama kituko fulani kwa jinsi alivyodhoofika!

Nilikumbuka wakati nilipokutana naye mara ya kwanza nikiwa na miaka 19 na yeye akiwa na miaka 16 tu, tukawa marafiki na baadaye kufungua ukurasa mpya wa mapenzi, ingawa ni katika mizania isiyolingana kwa kuwa Rehema alinipenda sana lakini mimi sikujua mapenzi ni kitu gani!

Sasa nilikuwa namtazama jinsi alivyodhoofu na hata rangi ya ngozi yake ilikuwa imebadilika, ujasiri wangu wote niliokuwa nao uliniisha, nilijikuta nikitetemeka mwili wote kila nilipomtazama Rehema. Yeye alikuwa ananitazama lakini hakuweza kusema chochote. Macho yangu yalianza kutoa machozi. Na muda huo huo niliiona michirizi ya machozi machoni pake pia.

Hali hiyo ilinifanya nitaabike sana moyoni kila nilipowaza kuwa matatizo yote yaliyokuwa yakimtokea Rehema yalisababishwa na ukware wangu wa kumtamani kila msichana mrembo niliyekutana naye, moyo wangu ulipandwa na hasira kupita kawaida na hapo nikaanza kujichukia mwenyewe, sikuwa radhi kumwona Rehema akiwa katika hali ile.

Niliinama na kumkumbatia pale kitandani. Nilishindwa kujizuia, nilianza kulia kwa sauti, nililia sana kwani sikuwa na matumaini kama angeweza kuinuka na kurudi katika hali yake ya zamani. Nililia sana kwa uchungu. Nilisikia uchungu mkubwa ambao sijawahi kuupata na moyo wangu ulikuwa kama unavutwa kutokana na uchungu mkubwa. Ulikuwa uchungu ambao sikuweza hata kuelezea maumivu yake.

Kilio changu kilipozidi Mama yake Rehema na Olivia waliingia mle chumbani. Mama yake Rehema alikuwa mwanamke nadhifu sana na mrefu. Mtu yeyote asingehitaji kuambiwa kuwa yule mama alikuwa mzazi wa Rehema kwa namna walivyofanana sana. Muda huo alikuwa amevaa gauni zuri la kitenge na alijifunga kilemba kichwani.

Olivia alinitoa pale kitandani kisha akanikumbatia kwa upendo kama mama amkumbatiaye mwanawe wa pekee. Yeye pia alishindwa kuyazuia machozi. Alichukua kitambaa laini na kunifuta machozi, kisha akamfuta na Rehema.

“Usilie, Jason… jipe moyo, naamini kwa uwezo wa Mungu Rehema atapona tu,” Olivia alisema kwa sauti ya kirafiki huku akinipiga piga mgongoni.

Hakikuwa kitu cha kawaida kwa mwanamke kumbembeleza mwanamume asilie kwa sababu imezoeleka kwamba wanaume ni watu majasiri na huwa wanaumia kwa ndani, lakini siku hiyo mambo yalikuwa tofauti kabisa. Nilishindwa kuwa na ule ujasiri wa kiuanaume. Nilishindwa kujizuia kulia mbele ya wale wanawake mle chumbani.

“Rehema, nasikitika sana, sikupaswa kukutenda yale niliyokutenda kwani ulipokuja katika maisha yangu uliyafanya yawe ya furaha kubwa. Sijawahi kupata furaha na sitapata furaha tena katika maisha yangu kama niliyoipata nikiwa nawe. Siwezi kuzisahau zile nyakati nzuri za furaha tulizokuwa pamoja. Hizo zitabaki kuwa kumbukumbu pekee kwangu. Ninakupenda sana Rehema ingawa nimepata wakati mgumu sana wa kukuona kwa kuwa baba yako hataki mimi na wewe tuonane, lakini sitaacha kukupenda…” nilimwambia Rehema kwa uchungu na kisha nikainama pale kitandani na kumbusu kwenye paji la uso.

“Nitakupenda siku zote za maisha yangu na sitakuwa na mwanamke mwingine katika maisha yangu zaidi yako. Ninakuombea upone haraka Rehema,” niliongeza huku nikizidi kutokwa na machozi na kuwafanya Olivia na Mama yake Rehema nao watokwe na machozi.

Sikuwa na hakika kama Rehema aliyasikia maneno yangu lakini nilishuhudia macho yake yakifunikwa na machozi. Nikatoa kitambaa laini toka mfukoni mwangu na kumfuta machozi kwa upendo. Kwa kweli kilikuwa kipindi kigumu mno kwangu. Niliumia sana. Hata hivyo Olivia alikuwa karibu yangu akinitia moyo.

Niliinamisha sura yangu chini nikiwa na mawazo mengi sana. Sikuwa naongea chochote kile kwa kuwa nilikuwa katika maumivu makali sana ya moyo. Nilizama kwenye tafakari ya kina juu ya hatima ya Rehema na maisha yangu bila mwanamke huyo hadi pale sauti ya Mzee Benard Mpogoro, Baba wa Rehema iliponishtua wakati alipoita kutokea sebuleni.

Wote tulishtuka, na hapo mimi na Olivia tukaangaliana na kushusha pumzi. Mama wa Rehema akatoka haraka kuelekea sebuleni akiwa na wasiwasi. Na baada ya muda mfupi alirudi tena chumbani na kuniambia kuwa ‘Mzee’ alikuwa ananiita sebuleni.

I'm sorry, Ray, for what happened. Kwa sasa mimi si yule Jason asiyejua thamani ya pendo lako, nimebadilika sana. Naapa sitakuacha, nitaendelea kukupenda hadi mwisho wa uhai wangu,” nilisema kwa uchungu kisha nikainamia tena pale kitandani nikambusu Rehema kwenye paji la uso wake halafu nikatoka mle chumbani huku nikifuta machozi na kuelekea sebuleni.

Endelea...
daaaaah forest ndo napokaa aseeeee ila kwa sasa ata sisi wa kipato cha chini tupo
 
View attachment 2246626
149

“Hapana!” Baba yake Rehema alisema huku akitingisha kichwa chake, sauti yake ilionesha wazi kuwa alikuwa na hasira. “Tayari nilikwisha fanya uamuzi na siwezi kuubadili tena. Nashangaa kwa nini Jason hajakwambia!”

“Lakini, Baba, kama unataka Rehema apate nafuu haraka ni vyema ukamruhusu Jason kuwa karibu naye, kwa taaluma yangu najua kuwa kinachomsumbua zaidi Rehema ni msongo mkali wa mawazo na kwa hali hiyo anahitaji zaidi faraja ya mtu anayempenda,” Olivia alisema kwa sauti tulivu lakini iliyosisitiza, na hata sura yake ilimaanisha kile alichokisema.

Baba wa Rehema alikaa kimya kwa muda kama aliyekuwa anafikiria jambo kisha alitingisha kichwa chake akionesha kutoafikiana na maneno ya Olivia.

“Kwa sasa hataiwezekana… hata hivyo naomba niwashukuru sana kwa namna mlivyoonesha kuguswa na kutaka kumsaidia Rehema. Mungu awajalie afya na…” yule mzee alisema na kusita kidogo kisha alinikazia macho akanitazama kwa umakini.

“Nakuombea umpate mwanamke mwingine utakayempenda kama unavyompenda Rehema,” alisema kwa namna ambayo nilihisi alikuwa akinisimanga.

Nilibaki kimya huku machozi yakinilenga lenga. Moyoni niliumia sana. Mama wa Rehema alionekana kunionea huruma sana lakini hakuwa na uamuzi japo alionekana kutaka kusema jambo. Niliinamisha uso wangu kwa zaidi ya dakika tano nikiwaza.

Kwa mara nyingine tena nilihisi kuadhibiwa na dunia. Nilisikia maumivu makali sana ndani ya moyo wangu, maumivu ambayo hayaelezeki kwani ilikuwa ni zaidi ya maumivu. Niliwaza sana kuhusu mustakabari wa maisha yangu, nikajiona mtu mwenye mkosi mkubwa na laana.

Jason, it’s time to go,” sauti ya Olivia ilinizindua toka kwenye lindi la mawazo. Niliinua uso wangu uliokuwa umejaa machozi nikamtazama Olivia na kisha Mama wa Rehema ambaye alionekana kunionea huruma sana. wakati huo Mzee Mpogoro alikwisha ondoka pale sebuleni na sikujua alielekea wapi!

Niliinuka kwa unyonge kisha tukaondoka huku tukisindikizwa na Mama wa Rehema. Sikuweza kutamka chochote kwa sababu nilihisi fundo kubwa la hasira likinikaba kooni.

“Jason, usikate tamaa mwanangu. Siku zote mtegemee Mungu naye atakusaida katika kila jambo. Endelea kumwombea mwenzako na Mungu akipenda siku moja mtakuwa pamoja tena. Nitakuwa nakupigia simu mara kwa mara kukujulisha maendeleo yake,” Mama wa Rehema aliniambia wakati tulipofika kwenye gari letu na kunipa mkono wa kuniaga. Macho yake yalionesha kulengwa lengwa na machozi.

“Nashukuru sana, Mama. Naomba nikiri kwamba Rehema ndiye mwanamke ninayempenda sana hapa duniani na kuumwa kwake ni pigo kubwa kwangu na katika maisha yangu. Lakini sina namna maana napaswa kuuheshimu uamuzi wa Baba, ila nitaendelea kumwombea kwa Mungu aweze kupona,” nilisema huku nikimpa mkono yule mama kumuaga.

Kisha tuliingia kwenye gari letu na kurejea Msamvu hotelini tulikofikia. Sasa nilikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa kiakili. Sikujua nifanye nini kwa wakati huo.

“Olivia, kwa nini maisha yangu yamekuwa ya namna hii? Sidhani kama ninastahili adhabu ya kiwango hiki!” nilimwambia Olivia wakati tukiwa tumeketi hotelini baada ya kutoka nyumbani kwa akina Rehema.

“Usiwaze sana, Jason, ni wakati mwafaka sasa wa kufanya uamuzi katika maisha yako na kuitafuta amani ya moyo,” Olivia aliniambia kwa sauti ya upole.

“Sina hakika kama nitaipata hiyo unayoiita amani ya moyo. Nimeumizwa sana na moyo wangu umejaa huzuni…” nilisema kwa huzuni huku nikihisi machozi yanataka kunitoka.

“Amani ya moyo inapatikana pale tu unapomwachia Mungu fadhaa zako zote. Ni Mungu pekee atayekupa amani ukimwomba, atakupa pia mke mwema, atakupa familia na atakupa kila unachokihitaji,” Olivia alisema kwa sauti ya upole lakini iliyobeba msisitizo.

Nilishusha pumzi za ndani kwa ndani nikimshukuru Mungu kwa kumleta Olivia kwenye maisha yangu maana bila yeye huenda ningekuwa nimeshachanganyikiwa.

* * *



Saa 1:30 usiku.

“Umekula?” Olivia aliniuliza baada ya kuingia chumbani kwangu na kunikuta nikiwa nimejilaza chali kitandani nikitafakari, macho yangu yakitazama juu darini.

“Hapana! Unafikiri nitaweza kula wakati Siijui hatma yangu na Rehema yupo katika hali ile!” nilimjibu Olivia pasipo hata kumtazama.

“Unatakiwa kula, Jason, tangu asubuhi hujala kitu chochote au unataka na wewe ulale kitandani kama Rehema?” Olivia aliniuliza kwa sauti ya upole. “Nikuletee nini?”

“Usijali niko sawa, wala usisumbuke,” nilimjibu huku macho yangu yakiendelea kutazama juu.

“Lakini Jason, una…” Olivia alitaka kusema lakini nikamkatiza.

“Niko sawa, husikii!” nilimjibu kwa sauti ya juu ya ukali kidogo. Kisha nikajishtukia kwa kuwa Olivia hakupaswa kujibiwa hivyo. Yeye alikuwa anatimiza wajibu wake kama rafiki mwema na mnasihi wangu aliyependa kuniona nikifurahi na kuwa na amani ya moyo.

“Usijali… niko sawa, mpenzi. Wewe nenda ukale mimi nimeamua kuanza mfungo na maombi ya siku tatu,” niliongea kwa sauti ya chini ya kirafiki.

Olivia alinitazama kwa muda kama aliyekuwa akijaribu kuyasoma mawazo yangu kisha akaachia tabasamu pana na kutoka akiniacha peke yangu. Ni kweli niliamua kutokula kwa siku tatu na kuomba kwa Mungu japo sikujua hata namna ya kuomba, lakini niliamini kuwa Mungu alifahamu kuhusu dhamira yangu.

* * *

Endelea...
Jason una vituko unalalamika why Mungu ameamua kukuadhibu kiasi hicho, yaani umesahau ujinga wote uliokuwa unaufanya, umesahau hata sababu why Rehema amaelala kitandani.....Ni uamuzi mzuri kuamua kufunga na utubu sasa
 
Kaka Bishop Hiluka nimependa mtitiriko wako wa matukio, kikubwa umeijenga vizuri sana TAHARUKI. Nilijua kwa tabia ya "JS" angelianzisha mahusiano na Olivia lakini haikuwa hivyo. Shukrani sana
 
Back
Top Bottom