Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

najua deep down u knew huyu hana ubavu huo.......ila Bishop samahani wewe mtunzi mbona kuna mambo unayajua deep sana kama hii historia umeandika ya kitengo...
Mmh! Hata mimi nashangaa[emoji849]...
 
ufukweni mombasa.JPG

215

‘Shamba’…




Saa 10:30 jioni…

“JASON!” sauti laini ya mwanadada Leyla Slim Abdullas ilinizindua toka kwenye lindi la mawazo. Alinikuta nikiwa nimesimama peke yangu kwenye eneo la uwanja wa shabaha nikiwa nimechoka huku nikiwa na mawazo mengi, wakati wenzangu wakiwa darasani. Mkononi nilikuwa nimeshika bastola aina ya FNX 45 Tactical nikiwa nimetoka kwenye mazoezi ya kulenga shabaha ambayo yalifanyika baada ya kufanya mazoezi binafsi ya kuuweka mwili wangu sawa.

Pale kambini nilisifika kama mkali wa mapigano na wa kulenga shabaha. Ile kambi wengi waliifahamu kama Chuo cha Teknolojia cha Zawyet Sidi Abd el-Ati ingawa kimsingi ilikuwa kambi rasmi ya mafunzo ya siri ya kijasusi, iliyokuwa mpakani mwa maeneo ya kiutawala ya Alexandria na Matrough.

Kambi hii ilikuwa eneo la Kusini Magharibi mwa Jiji la Alexandria, jiji ambalo lipo kando ya delta ya Nile, Kaskazini mwa nchi ya Misri, takriban kilomita 225 kutoka Jiji la Cairo.

Umahiri wangu katika mapigano na kulenga shabaha ulikuwa umewavutia watu wengi, hata walimu wetu wa mazoezi walinihusudu sana na kunifanya kuwa mfano wa kuigwa kwa wanafunzi wezangu ambao hawakuweza kulenga shabaha.

Siku na miezi ilikuwa imesonga mbele na sasa nilikuwa nimeshatimiza miezi sita tangu niwepo pale chuoni. Chuo kile kilikuwa na wanafunzi mchanganyiko, wake kwa waume waliotoka mataifa mbalimbali duniani hasa mataifa ya Kiafrika na yale ya Mashariki ya Kati.

Kila siku kwangu ilikuwa mpya na nilijikuta nikiyapenda mno mafunzo ya kijasusi, hasa masomo ya criminal investigation, crime scene investigation, na Law of evidence kuliko hata masomo ya information and communication technology (ICT) ambayo ndiyo nilikuwa nimebobea.

Sasa akili ya kufikiria nyumbani sikuwa nayo tena na wala sikujua kitu gani kilikuwa kinaendelea nchini kwangu Tanzania kwa maana pale kambini hatukuruhusiwa kabisa kumiliki simu, kusoma magazeti na wala kutazama runinga, labda kwa kusudi maalumu la kimafunzo.

Katika mafunzo yetu ambayo kwa asilimia mia moja yalikuwa ya kijeshi, tulifundishwa mambo yote yanayojumuisha matumizi ya silaha za moto; mbinu za kujilinda kwa mikono mitupu (unarmed combat); ujasiri na ukusanyaji wa taarifa za kiitelijensia katika mazingira magumu; kuajiri watoa habari (recruitment of sources); kufanya upelelezi wa kipolisi (criminal investigation); uchunguzi wa maeneo ya tukio (crime scene investigation); na sheria ya ushahidi (Law of evidence).

Hadi wakati huo nikiwa bado nina miezi mitatu ya kukamilisha programu ile ya mafunzo tayari nilishakamilika kwa kiasi kikubwa.

Sasa, wakati Leyla anafika mahala pale nilipokuwa nimesimama, nilikuwa nimezama kwenye mawazo juu ya kazi maalumu (special task) iliyokuwa ikinikabili, kazi ya uundaji wa programu niliyoipa jina la TracerMark nikishirikiana na wanafunzi wenzangu watatu akiwemo Leyla. Hii ilikuwa programu maalumu ya ufuatiliaji ambayo ingeweza kutumikisha vifaa vya sauti vya tarakilishi yoyote kwenye tarakilishi kuu kupitia njia ya setelaiti.

Hadi wakati huo programu hiyo ilikuwa imefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 90 na tayari ilikuwa imeoneshwa kwenye kampuni ya Dell wakati wa maonesho ya vyuo vikuu na Dell wakaonesha kuvutiwa sana.

Leyla aliponiita sikuitika bali niligeuka tu kumtazama huku nikiachia tabasamu. Leyla alikuwa mwembamba na mrefu lakini akiwa na umbile lililovutia mno. Alikuwa raia wa Kenya akiwa chotara aliyechanganya damu ya Mbantu na Mmanga, nywele zake nyeusi fii zilikuwa ndefu na laini na sura yake ilikuwa ndefu kiasi yenye macho makubwa legevu.

Kwa yeyote awaye mwanaume rijali hapana shaka kama angemuona angekiri kuwa mwanadada huyo alikuwa ni moto wa kuotea mbali na hakuwa na mfano wake. Kwa mlingano wa macho tu, Leyla alitoa tafsiri ya kuwa na ule uzuri usiomithilika, uzuri uwezao kumliwaza, kumpumbaza na hata kumlaza kitandani mtu yeyote aliye timamu na buheri wa afya.

Alikuwa amevaa suruali ya jampsuit ya rangi ya maruni iliyolionesha vyema umbo lake refu maridadi lenye kiuno chembamba lakini imara kikiwa kimebeba minofu ya mapaja iliyokaza kwa sababu ya mazoezi ya nguvu ya kila siku. Miguuni alikuwa amevaa buti ngumu za ngozi za rangi ya hudhurungi.

Nilijikuta nikizoeana sana na Leyla wiki chache tu tangu tulipojiunga pale chuoni. Nilimpenda sana Leyla kwa kuwa alikuwa na uwezo mkubwa wa kiakili katika kupambanua mambo kwa uharaka. Urafiki wetu ulishamiri siku hadi siku na hatimaye tukajikuta tumetumbukia kwenye ukaribu zaidi uliotafsiriwa kuwa ni mapenzi mazito kiasi cha kuanza kuonewa wivu na wanafunzi wengine.

Hata hivyo, ukaribu huo ulisababisha kuwepo na ushindani mkali kati yangu na Romeo Kwame, raia wa Ghana, ambaye pia alikuwa mshindani wangu mkubwa darasani.

Tulikutana karibu kila siku usiku hata kama tulikuwa tumechoka sana na suluba za mchana, na siku za mwisho wa wiki tulikwenda kwenye matembezi pamoja, na hapo nikajikuta niko karibu yake zaidi na zaidi. Hatimaye, kila nilipomwona moyo wangu ulipapatika na nilipokuwa mbali naye tumbo langu liliniuma kwa upweke. Ila bado tulikuwa na katika urafiki wa kawaida, hadi wakati huo sikuwa nimemtamkia kama nampenda wala kufanya chochote zaidi ya kumbusu.

Kupitia ukaribu wangu na Leyla sikuchelewa kugundua kuwa mimi na yeye tulikuwa tunafanana kwa mambo mengi mno. Lakini mara nyingi nilikuwa makini, nikijionya kwa kujikumbusha kauli ya mkufunzi wangu wa somo la Surveillance, Luteni Kanali Abdel Salah, kwamba, “vitu vingi haviko kama vinavyoonekana kwa macho.”

“Jason, mbona unanitazama hivyo?” Leyla aliniuliza swali na kunizindua kutoka kwenye mawazo yangu. Na hapo nikakumbuka kuwa hadi muda huo sikuwa nimesema lolote zaidi ya kumkodolea macho tu.

“Ah, usijali!” nilisema huku nikishusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Leo naomba unifundishe mbinu za kulenga shabaha, haiwezekani kila siku niwe wa mwisho katika kulenga shabaha,” Leyla aliniambia huku akiwa amesimama pembeni yangu na bastola yake aina ya Glock 19M.

“Kwenye kulenga shabaha ni wapi huwa unashindwa?” nilimuuliza Leyla huku nikimtazama kwa umakini.

“Kwa kweli sifahamu ni wapi?” Leyla aliniambia katika hali ya kukata tamaa.

“Hebu lenga ile target,” nilimwonesha Leyla picha ya mtu iliyokuwa mita mia moja kutoka sehemu tuliyokuwa tumesimama.

“Sawa,” Leyla alisema na kusimama akitanguliza mguu wa kulia mbele ule wa kushoto ukiwa nyuma.

Bastola yake aliiweka usawa wa kifua chake na jicho moja akalifumba. Kisha aliikoki bastola na risasi moja ikaingia kwenye chemba halafu akapiga risasi moja, ikapita sentimita chache kutoka ilipo ile picha.

“Dah, unaona nimekosa!” Leyla alisema kwa unyonge huku akiwa katika hali ya huzuni. Nikatabasamu na kumsogelea.

“Shika bastola yako kama ulivyokuwa umeshika awali,” nilimwambia Leyla, naye akatii.

“Unajua kitu ambacho unakosea wewe ni katika suala la kubana pumzi. Unapolenga sehemu huku ukiwa umeachia pumzi yako ni lazima mkono wako utayumba na kukosa target ambayo ulihitaji kupiga. Bana pumzi kisha piga risasi,” nilimpa maelekezo huku nikimweka sawa kifua chake.

Leyla akabana pumzi yake na kupiga risasi. Ikatua katikati ya ile target, kwenye alama ndogo nyeusi.

Inaendelea...
 
ufukweni mombasa.JPG

216

Yap! I won it!” Leyla alisema kwa furaha huku akinikumbatia.

You see! Very simple…” nilimwambia huku nami nikimkumbatia.

“Yaani tangu nianze kulenga shabaha leo ndiyo nimepata kwa usahihi kabisa!” Leyla alisema kwa furaha.

“Sasa rudia mara mbili zaidi tuone kama somo limekuingia,” nilimwambia. Akarudia mara mbili zaidi na zote alifanikiwa kulenga kwenye target.

“Asante sana, Jason… that’s why I love you,” Leyla alisema huku akizidi kunikumbatia kwa nguvu.

Kisha tuliachana, mimi nikaelekea chumbani kwangu kwenye chumba namba 20 kilichokuwa kwenye ghorofa ya kwanza ya jengo la hosteli ya wanafunzi wa mafunzo maalumu ya kijasusi liitwalo Block E. wakati huo Leyla alielekea darasani.

Niliingia kwenye chumba changu na kujitupa kitandani huku nikiwa na mawazo mengi juu ya kazi iliyonikabili hasa namna ya kuikamilisha programu ile ya TracerMark. Nikiwa katikati ya mawazo hayo mara nikashtushwa na sauti ya mtu aliyeanza kugonga mlango wa chumba changu.

Niliyapeleka macho yangu hadi pale mlangoni huku akili yangu ikisumbuka kujiuliza mgongaji angekuwa nani. Lakini kwa kuwa nilikuwa mtu wa watu sikujihangaisha sana kuwaza. Nikapaza sauti yangu kumwambia mgongaji kuwa afungue ule mlango na kuingia ndani kwa kuwa sikuwa nimeufunga kwa funguo.

Mlango ulipofunguliwa akaingia James Sipho, raia wa Afrika Kusini na mwanafunzi mwenzangu wa programu ya mafunzo maalumu ya kijasusi.

“Mr. Sizya, unaitwa na Mkuu wa Chuo,” James aliniambia huku akinitazama kwa umakini usoni kama aliyekuwa akijaribu kuyasoma mawazo yangu.

Okay! Yupo wapi?” nilimuuliza James huku nami nikimkazia macho usoni.

“Yupo kwenye ofisi yake,” James alisema huku akiyakwepa macho yangu na kutazama kando.

“Sawa,” nilisema huku nikiinuka na kuanza kutoka. James akatoka na kuelekea darasani wakati huo mimi nikiharakisha kuelekea kwenye jengo la utawala ilipokuwa ofisi ya Mkuu wa Chuo, Meja Jenerali Nasser Tariq, huku nikiwa na wasiwasi kidogo moyoni mwangu, kwani yule mzee alijulikana kuwa na roho mbaya. Aliogopwa sana na wanachuo pamoja na walimu wote.

Ofisi ya Meja Jenerali Nasser Tariq ilikuwa mkono wa kushoto mara baada ya kuingia kwenye lile jengo la utawala lenye ghorofa nne, hatua chache kabla ya kuifikia ofisi ya mkuu wa sera na mipango.

Nilipofika mlangoni nilisimama kwanza ili kuupimia utulivu wa mle ndani. sikusikia sauti yoyote ya maongezi na hivyo nikahisi kuwa Meja Jenerali Nasser Tariq alikuwa peke yake. Bila kupoteza muda nikagonga hodi pale mlangoni. Ukimya kidogo ukapita kisha kutoka mle ndani ya ofisi nikasikia sauti nzito ya Meja Jenerali Nasser Tariq yenye mamlaka ikiniambia, “Ingia ndani, Jason.”

Ruhusa ile ilinifanya niufungue ule mlango haraka na kuingia ndani huku nikipiga hatua zangu za kijeshi. Hii ilikuwa mara yangu ya pili kuingia kwenye ofisi ya Meja Jenerali Nasser Tariq. Mara ya kwanza ni pale aliponiita kunipa kazi maalumu ya siri ya kuhakikisha nambaini jasusi pandikizi (double agent) aliyekuwemo ndani ya programu yetu ya mafunzo akiwa na kazi ya kuvujisha taarifa za siri za kijasusi ili kuleta uchonganishi.

Kazi ile ilinichukua mwezi mzima, na jambo ambalo sikulijua ni kwamba nilikuwa naingia kwenye mlolongo wa matukio ya hatari na somo kubwa nililokuja kulipata hapo ni kwamba ndani ya kazi ya ujasusi kila mtu kwako ni adui na hutakiwi kumwamini yeyote.

Ofisi ya Meja Jenerali Nasser Tariq ilikuwa pana yenye hadhi ikiwa na meza ndefu ya ofisini yenye viti ishirini na mbili. Viti kumi na mbili upande wa kushoto na viti vingine kumi na mbili upande wa kulia. Nilipoyatembeza macho yangu mle ndani nikahisi kuwa kulikuwa na kikao kizito kilichokuwa kimefanyika muda mfupi uliokuwa umepita.

Meja Jenerali Nasser Tariq aliyekuwa na umri wa miaka 56, alikuwa mrefu kiasi mwenye mwili mkakamavu. Alikuwa amevaa suti nzuri ya kijivu ya pande tatu brand ya Brioni Vanquish ambayo bila shaka ilimgharimu fedha nyingi, ambazo zingetosha kabisa kujenga nyumba ya maana Uswahilini. Pia alikuwa amevaa miwani ya macho na mkononi alivaa saa ya thamani kubwa aina ya Rolex Submariner.

Wakati naingia yeye alikuwa ameketi nyuma ya meza yake kubwa ya ofisini mwisho wa ofisi akiwa mtulivu sana huku ameegemea kiti chake kikubwa cha ofisi. Alinitazama moja kwa moja machoni mwangu kwa umakini kana kwamba mwalimu wa usafi aliyekuwa akitafuta kasoro kwenye sare ya mwanafunzi, wakati nilipokuwa napiga hatu zangu kikakamavu kuisogelea meza yake.

Na macho yetu yalipokutana nikafunga mguu na kupiga saluti moja ya nguvu. Huku akinitazama moja kwa moja machoni mwangu aliitikia salamu yangu ya kijeshi kwa utulivu kisha akanikaribisha niketi kwenye kochi moja la sofa lililokuwa likitazamana na ile meza yake mle ndani.

“Karibu, keti hapo,” Meja Jenerali Nasser Tariq aliniambia kwa sauti yake nzito lakini tulivu huku akiendelea kunitazama moja kwa moja machoni mwangu. Kisha alikohoa kidogo kusafisha koo lake.

“Jason, nina kazi muhimu sana ya kukupatia. Najua hutaniangusha tena,” Meja Jenerali Nasser Tariq aliniambia huku akiwa bado ananitazama moja kwa moja machoni.

Mara moja akili yangu ikaanza kuwaza ni kazi gani hiyo? Ndivyo tulivyokuwa tumefundishwa, kwamba yakupasa kuwaza ya mbele, hata kubashiri kwa mantiki pale unapoona kuna haja ya kufanya hivyo. Halikuwa kosa. Ila sikuweza kuwaza sana kwa maana nilipaswa pia kuweka akili na masikio yangu kwenye kinywa cha mkuu wangu wa chuo.

“Kwanza nikwambie tu kuwa umefaulu vizuri sana katika mtihani wako wa kwanza wa uchunguzi, kwa kweli uko makini sana na ni mwepesi wa kujifunza mbinu mbalimbali za kijasusi…” Meja Jenerali Nasser Tariq alisema na kunyamaza kidogo huku akiwa bado ananitazama moja kwa moja machoni.

“Hapa tuongeapo, kuna safari ya ‘Shamba’ ambako kuna special task tofauti kabisa na hizi mnazofanya hapa na wewe ndiye unayepaswa kuwaongoza wanafunzi wenzako kwenye safari hiyo. Kama ujuavyo, ninakuamini sana hivyo nakupatia task nyingine ya siri na nitahitaji uniletee ripoti. Tuko pamoja?”

“Ndiyo, mkuu!” niliitikia kwa sauti ya ukakamavu ingawa sikujua huko Shamba ni wapi.

Kauli yake kuwa alitaka kunipatia task nyingine ilitosha kuifanya akili yangu iwe makini zaidi kumsikiliza kuliko wakati mwingine wowote. Nilijitengeneza vyema kitini na kumtazama yule mkuu wa chuo wakati akijiandaa kuniambia.

Kilipita kitambo fulani cha ukimya, Meja Jenerali Nasser Tariq alinitazama kwa kitambo fulani kama aliyekuwa anatafuta neno la kuniambia, kisha aliniambia jambo lililoufanya moyo wangu upoteze utulivu kabisa. Na hapo kikafuatia kitambo kingine cha ukimya baina yetu huku kila mmoja akionekana kuzama kwenye tafakuri nzito kichwani mwake.

“Jason!” Meja Jenerali Nasser Tariq aliniita kwa sauti tulivu na kuvunja ukimya.

“Naam, Mkuu!” niliitikia kwa sauti ya ukakamavu huku nikimtazama usoni.

“Hii ni siri… ni wewe tu ambaye umekuwa wa kwanza kufahamu kuhusu lengo la safari hii, wanafunzi wenzako unaoondoka nao bado hawafahamu lolote. Naomba usiniangushe, Jason,” Meja Jenerali Nasser Tariq alisema kisha akaniruhusu nitoke huku akinyanyua simu iliyokuwa juu ya meza yake na kubonyeza namba kadhaa.

Niliinuka, na hapo nikafunga mguu wangu na kupiga saluti ya heshima mbele ya mkuu wa chuo. Na kabla sijatoka kabisa ofisini kwake nikamsikia Meja Jenerali Nasser Tariq akimwagiza mtu wa upande wa pili aliyepokea simu kufanya utaratibu wa haraka wa kugonga kengele ya kuwaita watu wote kwenye viwanja vya makutano.

Dah! Sikujua Meja Jenerali Nasser Tariq alikuwa na nini na mimi kwa kunipa kazi za hatari kama sehemu ya mafunzo hasa kama kazi yenyewe ilihusu kumchunguza jasusi mbobevu! Hisia zangu ziliniambia kuwa safari hii nilikuwa nimepatikana, nilikuwa naelekea kukabiliana na jambo kubwa la hatari sana ingawa picha kamili ya hatari hiyo ilikataa kuumbika kichwani. Nikiwa nimezama kwenye tafakuri ile, akili yangu ikaenda mbele zaidi katika kuunda hoja kichwani.

Kama isingekuwa kiapo nilichoapa wakati najiunga rasmi na mafunzo hayo maalumu ya ujasusi ningeweza kabisa kuikataa kazi ya Meja Jenerali Nasser Tariq kisha ningeandika barua ya kuomba kuacha chuo ili nirudi kuendelea na shughuli zangu za teknolojia ya habari na mawasiliano. Lakini jambo hilo lilikuwa haliwezekani kabisa kwani woga ulikuwa ni kinyume kabisa na taratibu za taaluma ya ujasusi.

Wakati nikiwa katika tafakari huku nikielekea kwenye chumba changu niliisikia kengele ya kutuita kwenye viwanja vya makutano. Haraka nikakimbilia katika eneo hilo. Na ndani ya dakika tano tu watu wote tulikuwa tumeshakusanyika pale uwanjani na kujipanga kwenye mistari iliyonyooka. Meja Jenerali Nasser Tariq alifika na kusimama sehemu ambayo alihakikisha kila mtu aliweza kumwona.

“Kuna safari maalumu ya mafunzo, sasa kila atakayesikia jina lake likitajwa atatakiwa kusimama upande ule,” Meja Jenerali Nasser Tariq alizungumza kwa sauti ya mamlaka huku akituonesha eneo ambalo watu ambao wangesomwa majina yao walipaswa kwenda kusimama.

Msemaji wa chuo alisoma majina kumi na nane ya wanafunzi, likiwemo jina langu. Kila ambaye jina lake lilitajwa alijitoa kutoka kwenye mstari na kutembea kwa ukakamavu kuelekea upande tuliooneshwa. Miongoni mwa wanafunzi ambao majina yao yalisomwa ni Leyla Slim Abdullas, James Sipho na Romeo Kwame.

Nilipomtazama Leyla akaninyooshea kidole gumba huku akitabasamu. Meja Jenerali Nasser Tariq akatufuata pale tuliposimama, alitutazama kwa sekunde kadhaa pasipo kuzungumza kitu chochote.

“Jason, ingawa mtaondoka na walimu sita lakini wewe ndiye utakuwa kiongozi wa wanafunzi wenzako kwenye safari hii… kwenye safari yenu mkumbuke kwamba nyinyi ni watu muhimu sana, hivyo hakikisheni mnafanya mtakachoagizwa kwa uwezo wenu wote. Sijui nimeeleweka?” Meja Jenerali Nasser Tariq alituambia huku akitutazama machoni kwa namna ya kutukagua.

“Ndiyo, mkuu!” tuliitikia kwa pamoja kwa sauti ya ukakamavu.

“Mna dakika ishirini tu za kwenda kujiandaa, mtaondoka na ndege maalumu ya mapambano na hakuna atakayeruhusiwa kuondoka na bastola, silaha zote zirudishwe kwa mwalimu wa mazoezi, sawa?” Meja Jenerali Nasser Tariq alisema tena kwa sauti ya mamlaka huku akiendelea kututazama machoni.

“Ndiyo, mkuu!” tuliitikia tena kwa pamoja.

“Haya, tawanyikeni,” Meja Jenerali Nasser Tariq alisema.

Nikaondoka haraka kuelekea chumbani kwangu ambako nilitumia muda mfupi tu kujiandaa, nilivua nguo zangu kisha nikajifunga taulo na kuelekea bafuni ambako nilioga haraka haraka, kisha nilivaa suti maalumu ya chuo halafu nikatoka na kuelekea katika kiwanja kidogo cha ndege pale chuoni.

Muda wa kuondoka ulipowadia tuliingia kwenye ndege maalumu ya mapambano, tulikaa kwa kutazamana, na safari ya kuelekea ‘Shamba’ ikaanza. Katika msafara huo tulikuwa wanafunzi kumi na nane, walimu sita na marubani wawili.

* * *

Inaendelea...
 
ufukweni mombasa.JPG

217

Mtegoni…




Saa 3:15 usiku…

ULIKUWA usiku wa saa tatu na robo tukiwa angani ndani ya ile ndege, tulimsika rubani wetu akitangaza kuwa tulikuwa tunaingia eneo la ‘Shamba’ na hivyo basi tuanze kujiandaa kwa ajili ya kuruka na parachuti. Muda huo hatukuwa tunaona kule nje lakini kila mmoja wetu alijiandaa kwa kuweka vitu vyake sawa; begi la parachuti na miwani ya kutusaidia kuona usiku.

Punde tu rubani aliposema tumefika, mkia wa ndege ukafunguka nasi tukarukia nje pasipo kujiuliza mara mbili. Ilikuwa ni kama vile tulikuwa tunaenda kwenye operesheni ngumu ya kijasusi. Baada ya kuelea hewani kwa dakika kadhaa tukibebwa na maparachuti na kusukumwa na upepo tulitua kwenye eneo la msitu, lilikuwa eneo la kisiwani.

Kisha tukaanza kutembea taratibu kuelekea upande wa Mashariki kama ambavyo ramani yetu ilituonesha. Eneo lile lilikuwa na ukimya wa kutisha sana.

Ulikuwa msitu mkubwa sana. Sikuweza kuelewa kabisa hapo tulikuwa eneo gani kwani msitu ule ulimaanisha kuwa hatukuwa katika nchi ya Misri kwa kuwa nchi hiyo ilikuwa jangwa. Sasa tulikuwa wapi? Hilo ni swali ambalo kila mmoja wetu alijiuliza na hakuna hata mmoja wetu aliyeweza kuwa na jibu. Hata hivyo tuliendelea kuita eneo lile ‘Shamba’. Ule msitu ulikuwa umeota mgongoni mwa safu ya milima na kulikuwa kimya kabisa na kwa mtu mwenye woga asingeweza hata kukatiza eneo lile.

Tuliendelea kuzama msituni. Tukatembea mwendo wa takriban kilomita moja na nusu huku milima ikiwa imetuzingira, mbele na nyuma yetu kwa sana. Hapo nikaanza kujiuliza kama tulikuwa tumefuata uelekeo sahihi, niliwauliza walimu wetu kama tulikuwa kwenye uelekeo sahihi walinitaka niendelee tu na safari kwani huko ndiko ramani ilituonesha kuwa kulikuwepo kambi yetu ya mafunzo. Nilianza kukata tamaa kwani hadi hapo sikuwa naona alama yoyote ya kambi.

“Tazama kule!” Leyla ambaye muda wote alikuwa karibu yangu alisema huku akionesha kidole chake mbele yetu upande wa kushoto. Kwa mbali, niliweza kuona nyumba ndogo nyeupe. Ilikuwa ni nyumba pweke kwa maana ilionekana pekee mle msituni.

Tulianza kusonga kuelekea huko alipokuwa amenionesha Leyla, nikiwa siamini kama ile nyumba ndipo mahali tulipotakiwa kufikia. Mbona ilikuwa nyumba ndogo wakati sisi tulikuwa kikosi cha watu ishirini na nne? Lakini kadiri tulivyozidi kusonga mbele nikagundua kuwa haikuwa nyumba ndogo kama ilivyoonekana kwa mbali bali ilikuwa kubwa sana, tena si nyumba moja bali kambi maalumu ya kijeshi ya ‘Shamba’.

Ile kambi ilikuwa inalindwa kwani wakati tunaisogelea tulishtukia tukiwa tumezingirwa na wanajeshi sita waliovalia mavazi ya kivita wakiwa na bunduki za kivita aina ya M4 Carbine kila mmoja tayari kwa mapambano, wale wanajeshi wakatuzunguka. Nilishtuka sana lakini sikutaka kuionesha hofu yangu.

Niliwachunguza vizuri wale askari ili kubaini walikuwa wanatoka nchi gani, hiyo ingenisaidia kuweza kutambua eneo lile lilikuwa nchi gani, lakini sikufanikiwa kwani mavazi yao hayakuwa na bendera ya nchi yoyote wala nembo ambayo ingeashiria nchi. Hata hivyo, nilichoweza kufahamu ni kwamba askari hao walikuwa wa asili mchanganyiko, wawili kati yao walikuwa Waafrika, tena Weusi fii, na waliobakia walikuwa Waarabu.

“Jitambulisheni, ninyi ni akina nani, mnatoka wapi na mnakwenda wapi?” askari mmoja alituuliza kwa sauti ya amri huku katuelekezea bunduki.

Kama kiongozi wa wanafunzi nilisogea mbele mikono yangu ikiwa juu kuomba amani na kujitambulisha kisha nikaeleza kuhusu lengo la safari yetu pale ‘Shamba’.

Okay! Karibuni sana,” yule askari alisema na kuwaashiria wenzake washushe bunduki zao kisha wakatuongoza kuelekea kwenye ile kambi. Wakati tukitembea, mbele kidogo, karibu na lango kuu la kuingilia kambini tulikuta wanajeshi wengine sita wakizunguka zunguka eneo lile kuimalisha ulizni. Wote walikuwa wameshikilia bunduki kubwa za kivita. Tukakaribishwa na kisha taratibu zote zikafanywa.

Siku iliyofuata tuliamka alfajiri sana kama ilivyokuwa kawaida, tukafanyishwa mazoezi ya nguvu ya kijeshi na kisha tukagawanywa kwenye vikosi kazi (task force) sita, kila kikosi kazi kilijumuisha wanafunzi watatu na mwalimu mmoja. Nikajikuta nikipangwa kikosi kazi namba tatu nikiwa pamoja na Leyla na Khalid Nawaz, raia wa Pakistan.

Siku hiyo ilikuwa ya pilika pilika ngumu na mazoezi magumu ya kijeshi na tulifundishwa mbinu mbalimbali za mapambano ikiwemo matumizi ya silaha za moto na namna ya kujilinda kwa mikono mitupu (unarmed combat). Kwa wiki tatu mfululizo hatukuwa tukilala kabisa, ilikuwa ni mshikemshike tukifanyishwa mazoezi magumu sana, mazoezi yaliyosimamiwa na makomando tuliowakuta pale kambini wakishirikiana na walimu wetu.

Tukiwa katika wiki yetu ya tatu, ikaja siku moja, mwisho wa wiki, tulipewa mapumziko na kuruhusiwa kutembea pale kisiwani. Ilikuwa majira ya saa kumi jioni Leyla aliponifuata na kuniomba tutoke twende tukatembelee upande wa Magharibi wa kile kisiwa, kwenye eneo lililokuwa na mwinuko kidogo.

Siku hiyo Leyla alivaa blauzi nyepesi nyeupe na kuzifanya chuchu zake laini zilizosimama kwa utulivu juu ya milima miwili midogo ya matiti yake kutishia kuitoboa, chini alivaa suruali ya dengrizi ya rangi ya bluu mpauko iliyombana na kuushikana vyema mwili wake wenye mapaja yaliyonona na kiuno chembamba mfano wa dondola, na miguuni alikuwa amevaa sendozi ngumu za kike zilizotengenezwa kwa ngozi imara ya mamba. Mkononi alikuwa ameshika mkoba wake mdogo wa kike.

Nilipatwa na hisia kuwa siku kuwa hiyo Leyla alikuwa na kitu maalumu kwa ajili yangu. Macho yake yalikuwa yanacheza cheza kwa msisimuko na yaliniashiria nitarajie kitu fulani kizuri kutoka kwake. Yaani yalikuwa yanapepesa na kuwaka waka kama kioo.

Japokuwa mimi na Leyla tulikuwa tumezoeana sana kiasi cha kuondoa dhana ya mapenzi, na pia alipenda sana utani, lakini hali aliyokuwa nayo siku hiyo ilinifanya nihisi shauku na msisimuko fulani mkubwa ambao uliniashiria kuwa kulikuwa na kitu kizuri kinakuja. Sikuwa na ujasiri wa kupingana zaidi na hisia zangu hivyo ilikuwa lazima nikubali kwenda alikokutaka ili nijue alikuwa amekusudia kunifanyia surprise gani!

Tulikwenda mbali zaidi na ile kambi, takriban kilomita tatu toka kambini, na hapo nikagundua kuwa kile kisiwa kilikuwa kikubwa, huko tulijikuta tukitokea kwenye eneo moja lililokuwa na korongo, basi tukasimama juu ya lile korongo, na huko chini, kama mita mia moja hivi kulikuwa na mto mkubwa wenye maji ya kasi yaliyokuwa yanakwenda baharini! Kisha tukawa tunaambaa ambaa na lile korongo kwenda upande ambao ule mto ulikuwa unaelekea.

Muda wote Leyla hakuwa na haraka, alionekana kusubiri kwa muda mrefu hadi tulipofika kwenye eneo fulani zuri mno lenye chemchem ya maji na lilikuwa limepakana na bonde lililotokana na msimu wa mvua za masika ambazo zilitengeneza mkondo wa maji lakini maji hayo yakakauka baada ya msimu wa mvua kupita.

Leyla aliniambia tusimame hapo kisha alinisogelea zaidi, na hapo nikajikuta nikimshika kiunoni bila ruhusa yake, hata hivyo nilishukuru kwa kuwa sikukutana na upinzani wowote. Leyla alinitazama machoni kisha tabasamu maridhawa likachomoza usoni mwake.

“Jason!” Leyla aliniita akinitazama machoni kwa utulivu kisha aliipitisha mikono yake nyuma ya shingo yangu na kuzifanya chuchu za matiti yake kukitekenya kifua changu.

“Naam!” niliitika huku nami nikimtazama machoni.

Kitendo cha kunikumbatia kilinifanya kusikia kwa ukaribu mno harufu nzuri ya manukato mwilini kwake. Ilikuwa kama vile nimelala katikati ya konde lililojaa maua yenye kunukia vizuri wakati wa majira joto. Leyla alikuwa amejichonya kidogo manukato hayo nyuma ya kila sikio lake na mengine kidogo aliyatonea katikati ya matiti yake yenye kuvutia.

Inaendelea...
 
ufukweni mombasa.JPG

218

Niilipenda mno harufu yake jioni hiyo. Nilijikuta nikimbusu kwenye paji la uso wake na yeye akanirudishia busu mdomoni, kisha alinishika kichwa changu na kukivuta karibu yake na hapo ndimi zetu zikakutana. Tukabadilishana ndimi zetu na kuanza kunyonyanya na baada ya muda kidogo alinitaka nisubiri kwanza, nikamwachia na hapo nikamwona akitoa mkebe mdogo kutoka kwenye mkoba wake.

Alipoufungulia ule mkebe nikaona kitu mfano wa utepe wa dhahabu ukiwa na kito kikubwa cha thamani chenye rangi ya zambarau katikati ya utepe huo. Nilipotazama vizuri nikagundua ilikuwa pete.

Leyla akanivisha kwenye kidole changu cha katikati cha mkono wa kushoto akiniambia kuwa aliamini kukutana kwetu hakukuwa kwa bahati mbaya bali kulikuwepo na nguvu kubwa ya asili katikati yetu tusiyoweza kuitawala, nguvu ambayo hata yeye hakuijua, ndiyo maana aliamua kunipa ile pete akiamini ingeendelea kutuunganisha katika kazi hata kama tungekuwa mbalimbali.

Nilipatwa na mshangao mkubwa. Sikuwa nimetarajia kitu kama hicho kutoka kwake. Hakikuwa kitu cha kawaida sana kwa mwanamke kumvisha mwanaume pete. Hasa katika utamaduni wa nchi yangu, haijawahi kabisa kufanyika.

Jiwe la thamani lenye rangi ya zambarau lilikuwa kubwa juu ya pete lakini halikuwa limechongwa kwa staili ya migongo migongo kama ilivyo kwa vito vingine, badala yake lilikuwa laini. Naam, baada ya kunivisha ile pete, nilimtazama Leyla kwa umakini kwa macho yaliyoonesha maswali kibao.

Ni kama alikuwa akiyasoma mawazo yangu, alicheka, lakini kabla sijajua nifanye nini nikastaajabu nyavu imetusomba na kutukusanya, halafu ikatupeleka juu kabisa ya mti! Nyavu hiyo ilikuwa ngumu hasa na ilitubana mno kiasi cha kuhema kwa tabu. Tulikuwa tumenasa mtegoni! Hatukuwa na ujanja wowote wa kufanya kwani viungo vyote vilikuwa vimebaniwa mwilini.

Nilipotazama chini niliwaona watu watano waliokuwa wamevalia mavazi yaliyoficha sura zao na hivyo ilikuwa ngumu kuwatambua mara moja kuwa walitoka wapi. Kitu cha mwisho kabisa nilichokumbuka ilikuwa ni maumivu ya kitu kama sindano mgongoni kwangu. Nikapoteza fahamu.

_____



Sikufahamu nini kiliendelea baada ya hapo na wala sikujua nilipoteza fahamu kwa muda gani hadi nilipokuja kuamka nikiwa kwenye chumba chenye giza! Nilikuwa kizani sifahamu kinachoendelea na mazingira yalikuwa ya ukimya mno ulionitisha sana, na kadiri muda ulivyokuwa unaenda, nikaanza kujihisi nipo sakafuni, tena sina nguo kwani mwili ulikuwa unapigwa na baridi kali.

Nilijitahidi kukodoa macho yangu lakini haikusaidia. Nilijaribu kukumbuka nini kilitokea mara ya mwisho lakini sikuambulia kitu bali maumivu makali ya kichwa na pia nilihisi maumivu mgongoni. Nikajikakamua ili nisimame lakini sikuweza kabisa!

Viungo vyangu vya mwili havikuwa na nguvu, mdomo ulikuwa umekauka na masikio niliyahisi ya moto! Ulimi nao niliuhisi mchungu sana. Na nilipojaribu kumeza mate nikahisi yananiunguza koo! Na hapo nikagundua kuwa nilikuwa nimechomwa sindano ya sumu. Lakini sikuwa na uhakika.

Nilibaki nimelala pale sakafuni nikisubiri hatma yangu maana sikuwa na na namna yoyote ya kufanya! Nilitamani niite ili kama kulikuwa na mtu yeyote eneo lile basi anisikie lakini koo langu liligoma kabisa. Sauti haikuwa inatoka. Pumzi nazo zilikuwa zinanibana kama vile mapafu yangu yalikuwa yamesinyaa!

Nikiwa bado nasubiria majaliwa yangu mara mlango wa kile chumba ukafunguliwa na kusababisha mwanga mkali kuzama ndani na kunipiga machoni. Haraka nikayafunga macho yangu na kuyaminya kwa nguvu kujitetea na mwanga ule mkali. Kwa kufanya vile sikuweza kumwona mtu aliyeingia. Lakini nilichofanikiwa kugundua ni kuwa muda ule ulikuwa ni mchana.

Mlango ulipofungwa, taa zikawashwa kufukuza kiza. Na hapo nikafanikiwa, japo kwa tabu, kumwona mwanamume mmoja mrefu mwenye mwili mpana. Kwa mwonekano tu nilitambua kuwa alikuwa Mwarabu, macho yake yalikuwa makubwa na makali yaliyoashiria wazi kila aina ya ukatili. Kwa mwonekano wa haraka tu yeyote asingeshindwa kubaini kuwa mtu yule hakuonekana kuogopa kitu chochote hapa duniani zaidi ya kupenda kutoa roho za watu.

Alikuwa amevalia suruali nyeusi ya dengrizi, jaketi jeusi la ngozi na fulana nyekundu kwa ndani. Kichwani alivaa kilemba na mkononi alibeba mkoba mweusi wa kiofisi.

Kwa tabu niliweza kuyaona mazingira ya kile chumba, kilikuwa chumba kikubwa ambacho kwa mtazamo wa haraka tu sikuchelewa kutambua kuwa kilikuwa chini ya ardhi kikiwa na kuta imara na hakikuwa na dirisha lolote, na ukutani kulikuwa na kioo kipana.

Kwa mwonekano tu nilifahamu kuwa kilikuwa chumba cha mateso makali, kilionekana kutisha kwa mambo yaliyokuwa yanafanyika humo. Katikati ya kile chumba kulikuwa na bomba refu la chuma lililotoka upande mmoja wa kile chumba hadi upande wa pili ukutani. Juu ya dari kulining’inizwa vyuma vifupi vilivyokunjwa na kuchongwa mbele yake mfano wa vyuma vya kuning’inizia nyama buchani.

Upande wa kulia kulikuwa na tangi kubwa lililokuwa limejengwa kwa vioo ambalo ndani yake lilijazwa maji na kando ya lile tangi kulikuwa na beseni kubwa ambalo pia lilikuwa limejazwa maji.

Upande mwingine wa kile chumba kulikuwa na kitanda chembamba cha chuma chenye mikanda imara, mnyororo mfupi na pingu za miguuni na mikononi za chuma. Kando ya kile kitanda kulikuwa na kiti cha umeme. Mbele ya kile kiti cha umeme kulikuwa na meza ya kioo ambayo juu yake kulikuwa na sinia dogo lenye kisu, waya mwembamba lakini imara, koleo, nyundo na misumali. Pia kulikuwa na mabomba mawili ya sindano ambayo yalikuwa na dawa ndani yake.

Nilipotazama vizuri nikaona pia kitu mfano wa betri kubwa ya gari yenye kufua umeme na vishikizo vyake. Pia kulikuwa na mtungi wenye gesi, kamba imara na vifaa vingine ambavyo sikuvielewa sawasawa.

Hadi wakati huo akili yangu ilikuwa bado haifanyi kazi sawasawa, nilimtazama yule mwanamume ambaye wakati huo alikuwa amesimama mbele yangu akinitazama kwa makini, nikajaribu kutafakari kuhusu mazingira yale ya kile chumba, nikahisi kuwa hayakuwa mageni kabisa kwangu.

Nilijitahidi kuvuta kumbukumbu ya nini kilitokea kabla lakini sikuweza kukumbuka, hata hivyo hisia zangu ziliniambia kuwa mazingira hayo niliyokuwepo yalikuwa hatarishi. Ni mazingira ambayo huambatana na maumivu ya mateso ya kumlazimisha mtu kuongea kitu ambacho aidha anakijua ama hakijui. Kitu ambacho anahusika nacho ama lah!

Mara nikakumbuka matumizi ya kile kioo kikubwa cha ukutani, mara nyingi kilimfanya mtu aliyekuwemo mle ndani asiweze kumwona mtu aliyekuwa nje ya chumba lakini yule mtu wa nje aliweza kumwona vizuri, na hata kumsikia, mtu aliyekuwa mle ndani.

Sasa… mimi ningeeleza nini nilichokijua wakati kumbukumbu zangu zilikuwa zimepotea kichwani? Si hicho tu kilichonipa hofu bali hata ile hali niliyokuwemo ilikuwa ni tishio kwa usalama wangu kwani ningeweza kujikuta natoa taarifa ambazo hazitakiwi kutolewa kwa adui!

Unajua kabla ya kutumia ujuzi wa kudanganya na kulaghai lazima kwanza uwe unaujua ukweli ili ufahamu namna gani ya kuumba katika njia nyingine ya tofauti ambayo inafanana nayo. Mimi sikuwa naujua huo ukweli.

Mara nikamwona yule mtu akifungua mkoba wake wa kiofisi na kutoa sindano kisha aliitazama kwa umakini. Ndani ya ile sindano kulikuwa na kimiminika chenye rangi ya njano iliyokoza. Akauweka mkoba wake chini na kunifuata, nikajua alikuwa anataka kunichoma.

Hey, please!” nilijaribu kumpigia kelele lakini sauti haukutoka na badala yake nilihisi koo likiniuma sana.

Yule mwanaume, pasipo kujali, alinishika, nikajaribu kupambana lakini mwili wangu haukuwa na nguvu kabisa. Sikuwa najiweza kabisa. Nikamshuhudia akitoboa mshipa wa damu kwenye mkono wangu wa kuume na kunizamishia kile kimiminika kilichokuwa ndani ya sindano. Nilijikuta nikikata tamaa kabisa kwa kuwa sikujua kama kile kimiminika kilikuwa ni dawa ama sumu. Muda huo nilijihisi baridi la ajabu mpaka nilikuwa natetemeka.

Kisha kwa mbali nilimsikia yule mtu akiondoka na kufunga mlango nyuma yake. Baada ya dakika mbili au tatu mwili wangu ukaanza kurudi kwenye joto la kawaida lakini bado nilijihisi si mzima. Nikajikunyata na punde nikajiona nikianza kudidimia kwenye shimo refu lenye kiza kizito. Fahamu zikanitoka.

* * *

Tukutane wakati mwingine tena. Endelea kuifuatilia simulizi hii ya kusisimua...
 
Kwa kweli tunashukuru sana kwa simulizi hii nzuri. Yaani naisoma kwa mtiririko, mfululizo na kwa muunganiko bila kupoteza utamu wake. Hujawa na choyo kwenye kuipost hapa jukwaani. Ubarikiwe sana mkuu
 
Back
Top Bottom