216
“
Yap! I won it!” Leyla alisema kwa furaha huku akinikumbatia.
“
You see! Very simple…” nilimwambia huku nami nikimkumbatia.
“Yaani tangu nianze kulenga shabaha leo ndiyo nimepata kwa usahihi kabisa!” Leyla alisema kwa furaha.
“Sasa rudia mara mbili zaidi tuone kama somo limekuingia,” nilimwambia. Akarudia mara mbili zaidi na zote alifanikiwa kulenga kwenye
target.
“Asante sana, Jason…
that’s why I love you,” Leyla alisema huku akizidi kunikumbatia kwa nguvu.
Kisha tuliachana, mimi nikaelekea chumbani kwangu kwenye chumba namba 20 kilichokuwa kwenye ghorofa ya kwanza ya jengo la hosteli ya wanafunzi wa mafunzo maalumu ya kijasusi liitwalo Block E. wakati huo Leyla alielekea darasani.
Niliingia kwenye chumba changu na kujitupa kitandani huku nikiwa na mawazo mengi juu ya kazi iliyonikabili hasa namna ya kuikamilisha programu ile ya
TracerMark. Nikiwa katikati ya mawazo hayo mara nikashtushwa na sauti ya mtu aliyeanza kugonga mlango wa chumba changu.
Niliyapeleka macho yangu hadi pale mlangoni huku akili yangu ikisumbuka kujiuliza mgongaji angekuwa nani. Lakini kwa kuwa nilikuwa mtu wa watu sikujihangaisha sana kuwaza. Nikapaza sauti yangu kumwambia mgongaji kuwa afungue ule mlango na kuingia ndani kwa kuwa sikuwa nimeufunga kwa funguo.
Mlango ulipofunguliwa akaingia James Sipho, raia wa Afrika Kusini na mwanafunzi mwenzangu wa programu ya mafunzo maalumu ya kijasusi.
“Mr. Sizya, unaitwa na Mkuu wa Chuo,” James aliniambia huku akinitazama kwa umakini usoni kama aliyekuwa akijaribu kuyasoma mawazo yangu.
“
Okay! Yupo wapi?” nilimuuliza James huku nami nikimkazia macho usoni.
“Yupo kwenye ofisi yake,” James alisema huku akiyakwepa macho yangu na kutazama kando.
“Sawa,” nilisema huku nikiinuka na kuanza kutoka. James akatoka na kuelekea darasani wakati huo mimi nikiharakisha kuelekea kwenye jengo la utawala ilipokuwa ofisi ya Mkuu wa Chuo, Meja Jenerali Nasser Tariq, huku nikiwa na wasiwasi kidogo moyoni mwangu, kwani yule mzee alijulikana kuwa na roho mbaya. Aliogopwa sana na wanachuo pamoja na walimu wote.
Ofisi ya Meja Jenerali Nasser Tariq ilikuwa mkono wa kushoto mara baada ya kuingia kwenye lile jengo la utawala lenye ghorofa nne, hatua chache kabla ya kuifikia ofisi ya mkuu wa sera na mipango.
Nilipofika mlangoni nilisimama kwanza ili kuupimia utulivu wa mle ndani. sikusikia sauti yoyote ya maongezi na hivyo nikahisi kuwa Meja Jenerali Nasser Tariq alikuwa peke yake. Bila kupoteza muda nikagonga hodi pale mlangoni. Ukimya kidogo ukapita kisha kutoka mle ndani ya ofisi nikasikia sauti nzito ya Meja Jenerali Nasser Tariq yenye mamlaka ikiniambia, “Ingia ndani, Jason.”
Ruhusa ile ilinifanya niufungue ule mlango haraka na kuingia ndani huku nikipiga hatua zangu za kijeshi. Hii ilikuwa mara yangu ya pili kuingia kwenye ofisi ya Meja Jenerali Nasser Tariq. Mara ya kwanza ni pale aliponiita kunipa kazi maalumu ya siri ya kuhakikisha nambaini jasusi pandikizi (
double agent) aliyekuwemo ndani ya programu yetu ya mafunzo akiwa na kazi ya kuvujisha taarifa za siri za kijasusi ili kuleta uchonganishi.
Kazi ile ilinichukua mwezi mzima, na jambo ambalo sikulijua ni kwamba nilikuwa naingia kwenye mlolongo wa matukio ya hatari na somo kubwa nililokuja kulipata hapo ni kwamba ndani ya kazi ya ujasusi kila mtu kwako ni adui na hutakiwi kumwamini yeyote.
Ofisi ya Meja Jenerali Nasser Tariq ilikuwa pana yenye hadhi ikiwa na meza ndefu ya ofisini yenye viti ishirini na mbili. Viti kumi na mbili upande wa kushoto na viti vingine kumi na mbili upande wa kulia. Nilipoyatembeza macho yangu mle ndani nikahisi kuwa kulikuwa na kikao kizito kilichokuwa kimefanyika muda mfupi uliokuwa umepita.
Meja Jenerali Nasser Tariq aliyekuwa na umri wa miaka 56, alikuwa mrefu kiasi mwenye mwili mkakamavu. Alikuwa amevaa suti nzuri ya kijivu ya pande tatu
brand ya
Brioni Vanquish ambayo bila shaka ilimgharimu fedha nyingi, ambazo zingetosha kabisa kujenga nyumba ya maana Uswahilini. Pia alikuwa amevaa miwani ya macho na mkononi alivaa saa ya thamani kubwa aina ya
Rolex Submariner.
Wakati naingia yeye alikuwa ameketi nyuma ya meza yake kubwa ya ofisini mwisho wa ofisi akiwa mtulivu sana huku ameegemea kiti chake kikubwa cha ofisi. Alinitazama moja kwa moja machoni mwangu kwa umakini kana kwamba mwalimu wa usafi aliyekuwa akitafuta kasoro kwenye sare ya mwanafunzi, wakati nilipokuwa napiga hatu zangu kikakamavu kuisogelea meza yake.
Na macho yetu yalipokutana nikafunga mguu na kupiga saluti moja ya nguvu. Huku akinitazama moja kwa moja machoni mwangu aliitikia salamu yangu ya kijeshi kwa utulivu kisha akanikaribisha niketi kwenye kochi moja la sofa lililokuwa likitazamana na ile meza yake mle ndani.
“Karibu, keti hapo,” Meja Jenerali Nasser Tariq aliniambia kwa sauti yake nzito lakini tulivu huku akiendelea kunitazama moja kwa moja machoni mwangu. Kisha alikohoa kidogo kusafisha koo lake.
“Jason, nina kazi muhimu sana ya kukupatia. Najua hutaniangusha tena,” Meja Jenerali Nasser Tariq aliniambia huku akiwa bado ananitazama moja kwa moja machoni.
Mara moja akili yangu ikaanza kuwaza ni kazi gani hiyo? Ndivyo tulivyokuwa tumefundishwa, kwamba yakupasa kuwaza ya mbele, hata kubashiri kwa mantiki pale unapoona kuna haja ya kufanya hivyo. Halikuwa kosa. Ila sikuweza kuwaza sana kwa maana nilipaswa pia kuweka akili na masikio yangu kwenye kinywa cha mkuu wangu wa chuo.
“Kwanza nikwambie tu kuwa umefaulu vizuri sana katika mtihani wako wa kwanza wa uchunguzi, kwa kweli uko makini sana na ni mwepesi wa kujifunza mbinu mbalimbali za kijasusi…” Meja Jenerali Nasser Tariq alisema na kunyamaza kidogo huku akiwa bado ananitazama moja kwa moja machoni.
“Hapa tuongeapo, kuna safari ya ‘Shamba’ ambako kuna
special task tofauti kabisa na hizi mnazofanya hapa na wewe ndiye unayepaswa kuwaongoza wanafunzi wenzako kwenye safari hiyo. Kama ujuavyo, ninakuamini sana hivyo nakupatia
task nyingine ya siri na nitahitaji uniletee ripoti. Tuko pamoja?”
“Ndiyo, mkuu!” niliitikia kwa sauti ya ukakamavu ingawa sikujua huko Shamba ni wapi.
Kauli yake kuwa alitaka kunipatia task nyingine ilitosha kuifanya akili yangu iwe makini zaidi kumsikiliza kuliko wakati mwingine wowote. Nilijitengeneza vyema kitini na kumtazama yule mkuu wa chuo wakati akijiandaa kuniambia.
Kilipita kitambo fulani cha ukimya, Meja Jenerali Nasser Tariq alinitazama kwa kitambo fulani kama aliyekuwa anatafuta neno la kuniambia, kisha aliniambia jambo lililoufanya moyo wangu upoteze utulivu kabisa. Na hapo kikafuatia kitambo kingine cha ukimya baina yetu huku kila mmoja akionekana kuzama kwenye tafakuri nzito kichwani mwake.
“Jason!” Meja Jenerali Nasser Tariq aliniita kwa sauti tulivu na kuvunja ukimya.
“Naam, Mkuu!” niliitikia kwa sauti ya ukakamavu huku nikimtazama usoni.
“Hii ni siri… ni wewe tu ambaye umekuwa wa kwanza kufahamu kuhusu lengo la safari hii, wanafunzi wenzako unaoondoka nao bado hawafahamu lolote. Naomba usiniangushe, Jason,” Meja Jenerali Nasser Tariq alisema kisha akaniruhusu nitoke huku akinyanyua simu iliyokuwa juu ya meza yake na kubonyeza namba kadhaa.
Niliinuka, na hapo nikafunga mguu wangu na kupiga saluti ya heshima mbele ya mkuu wa chuo. Na kabla sijatoka kabisa ofisini kwake nikamsikia Meja Jenerali Nasser Tariq akimwagiza mtu wa upande wa pili aliyepokea simu kufanya utaratibu wa haraka wa kugonga kengele ya kuwaita watu wote kwenye viwanja vya makutano.
Dah! Sikujua Meja Jenerali Nasser Tariq alikuwa na nini na mimi kwa kunipa kazi za hatari kama sehemu ya mafunzo hasa kama kazi yenyewe ilihusu kumchunguza jasusi mbobevu! Hisia zangu ziliniambia kuwa safari hii nilikuwa nimepatikana, nilikuwa naelekea kukabiliana na jambo kubwa la hatari sana ingawa picha kamili ya hatari hiyo ilikataa kuumbika kichwani. Nikiwa nimezama kwenye tafakuri ile, akili yangu ikaenda mbele zaidi katika kuunda hoja kichwani.
Kama isingekuwa kiapo nilichoapa wakati najiunga rasmi na mafunzo hayo maalumu ya ujasusi ningeweza kabisa kuikataa kazi ya Meja Jenerali Nasser Tariq kisha ningeandika barua ya kuomba kuacha chuo ili nirudi kuendelea na shughuli zangu za teknolojia ya habari na mawasiliano. Lakini jambo hilo lilikuwa haliwezekani kabisa kwani woga ulikuwa ni kinyume kabisa na taratibu za taaluma ya ujasusi.
Wakati nikiwa katika tafakari huku nikielekea kwenye chumba changu niliisikia kengele ya kutuita kwenye viwanja vya makutano. Haraka nikakimbilia katika eneo hilo. Na ndani ya dakika tano tu watu wote tulikuwa tumeshakusanyika pale uwanjani na kujipanga kwenye mistari iliyonyooka. Meja Jenerali Nasser Tariq alifika na kusimama sehemu ambayo alihakikisha kila mtu aliweza kumwona.
“Kuna safari maalumu ya mafunzo, sasa kila atakayesikia jina lake likitajwa atatakiwa kusimama upande ule,” Meja Jenerali Nasser Tariq alizungumza kwa sauti ya mamlaka huku akituonesha eneo ambalo watu ambao wangesomwa majina yao walipaswa kwenda kusimama.
Msemaji wa chuo alisoma majina kumi na nane ya wanafunzi, likiwemo jina langu. Kila ambaye jina lake lilitajwa alijitoa kutoka kwenye mstari na kutembea kwa ukakamavu kuelekea upande tuliooneshwa. Miongoni mwa wanafunzi ambao majina yao yalisomwa ni Leyla Slim Abdullas, James Sipho na Romeo Kwame.
Nilipomtazama Leyla akaninyooshea kidole gumba huku akitabasamu. Meja Jenerali Nasser Tariq akatufuata pale tuliposimama, alitutazama kwa sekunde kadhaa pasipo kuzungumza kitu chochote.
“Jason, ingawa mtaondoka na walimu sita lakini wewe ndiye utakuwa kiongozi wa wanafunzi wenzako kwenye safari hii… kwenye safari yenu mkumbuke kwamba nyinyi ni watu muhimu sana, hivyo hakikisheni mnafanya mtakachoagizwa kwa uwezo wenu wote. Sijui nimeeleweka?” Meja Jenerali Nasser Tariq alituambia huku akitutazama machoni kwa namna ya kutukagua.
“Ndiyo, mkuu!” tuliitikia kwa pamoja kwa sauti ya ukakamavu.
“Mna dakika ishirini tu za kwenda kujiandaa, mtaondoka na ndege maalumu ya mapambano na hakuna atakayeruhusiwa kuondoka na bastola, silaha zote zirudishwe kwa mwalimu wa mazoezi, sawa?” Meja Jenerali Nasser Tariq alisema tena kwa sauti ya mamlaka huku akiendelea kututazama machoni.
“Ndiyo, mkuu!” tuliitikia tena kwa pamoja.
“Haya, tawanyikeni,” Meja Jenerali Nasser Tariq alisema.
Nikaondoka haraka kuelekea chumbani kwangu ambako nilitumia muda mfupi tu kujiandaa, nilivua nguo zangu kisha nikajifunga taulo na kuelekea bafuni ambako nilioga haraka haraka, kisha nilivaa suti maalumu ya chuo halafu nikatoka na kuelekea katika kiwanja kidogo cha ndege pale chuoni.
Muda wa kuondoka ulipowadia tuliingia kwenye ndege maalumu ya mapambano, tulikaa kwa kutazamana, na safari ya kuelekea ‘Shamba’ ikaanza. Katika msafara huo tulikuwa wanafunzi kumi na nane, walimu sita na marubani wawili.
* * *
Inaendelea...