348
“Samson Dadi amefikishwa hospitali mchana huu baada ya kukutwa amezirai ofisini kwake. Maofisa wa usalama walipofika ofisini kwake wakamkuta akiwa sakafuni kalala kimya, povu likimtoka mdomoni na hivyo wakamuwahisha hapa,” Daktari Mashaka alitueleza. Kisha akaongeza, “Uchunguzi wa awali umetuonesha kuwa alipandwa na presha.”
“Hakuna kingine?” nilimuuliza Daktari Mashaka huku nikimkazia macho.
“Hakuna. Bado tunaendelea na uchunguzi,” Daktari Mashaka alijibu na kututaka twende wodini kumtazama. Aliinuka kisha tukatoka na kuelekea wodi aliyolazwa mtu huyo.
Mlangoni mwa wodi ile tulikuta askari wawili waliokuwa wamesimama wakilinda usalama, wote walikuwa wameshika bunduki aina ya SMG. Tukawasalimia huku tukitaka kuingia mle wodini. Kwa kuwa wote watatu tulikuwa tumevaa nguo za kawaida, hata Daktari Mashaka hakuwa amevaa koti la kidaktari wala kubeba kifaa chochote cha kupimia, hivyo wale askari wakatuzuia kuingia.
“Kuna daktari, hamruhusiwi kuingia,” askari mmoja alitwambia huku akitutunishia kifua.
Wakati Daktari Mashaka akitaka kujieleza kwa wale askari nikahisi tulikuwa tunachelewa maana kengele ya hatari ililia kichwani kwangu, nikampiga kikumbo yule askari aliyenitunishia kifua na kuzama ndani ya ile wodi
fasta huku nikifuatwa nyuma na Daniella na kuwaacha wale askari wakishangaa.
Hata hivyo ilionesha kuwa kitendo kile kiliwaudhi wale askari, wakaingia ndani kwa hasira kutufuata wakiwa wameshika vyema bunduki zao mkononi na kutuelekezea. Muda huo nilikuwa nimesimama karibu na kitanda nikishangaa baada ya kutomwona daktari yeyote isipokuwa mgonjwa peke yake akiwa amelalia dimbwi la damu mbichi iliyokuwa ikichuruzika sakafuni.
Wale askari nao wakajikuta wakishangaa kuona damu mbichi ikitambaa taratibu ndani ya chumba kile na kushindwa kufanya kile walichokusudia. Niligeuza shingo yangu kuwatazama wale askari kwa macho yaliyotoa ujumbe wa lawama kwa uzembe walioufanya, kisha nikamsogelea yule mgonjwa pale kitandani na kumtazama vizuri, na hapo nikagundua kuwa uhai ulishamtoka na mwili wake ulikuwa na majeraha matatu ya risasi.
“
Shit! Wametuwahi!” niling’aka kwa hasira huku nikikimbilia dirishani na kutazama, nikagundua kuwa kioo cha dirisha kilikuwa wazi jambo lililomaanisha kuwa muuaji baada ya kutekeleza azma yake alipitia hapo, nami nikapita pale dirishani na kutimua mbio kuelekea kule nyuma ya lile jengo la wodi.
Kule nyuma niliangaza huku na kule bila mafanikio. Nikaangalia kila sehemu lakini sikumwona yeyote wa kumtilia shaka.
“Dah! Sijui ni nani aliyewashtua kuwa tunakuja hapa hospitali!” nilijiuliza kwa mshangao huku nikianza kuzunguka lile jengo ili niende nikatokee upande wa pili wa lile jengo, lakini kabla sijapiga hatua zaidi nikasita baada ya kuona koti la kidaktari likiwa limetupwa kando ya tenki lililojengwa ili kukinga maji ya mvua.
Sikusubiri, nikatoka kasi na kutokea upande wa pili wa lile jengo na hapo nikaliona lile gari jeusi aina ya Toyota Rav 4L likiondoka kwa kasi toka eneo lile la maegesho ya magari. Machale yakanicheza, nikachomoa bastola yangu huku nikikimbia upande wa pili ambako niliamini lazima lile gari lizunguke kabla ya kutoka. Nilipofika usawa mzuri nikajificha nyuma ya mti mkubwa wa kivuli, mara nikaona kioo cha nyuma cha lile gari kikishuka haraka na mtutu wa bunduki ukachungulia.
Niliruka na kutua eneo lingine nikiziacha risasi zilizotoka kwenye ile bunduki zikiusulubu ule mti mkubwa wa kivuli na kuchubua magome yake. Nikiwa pale chini nilipoangukia bastola yangu ikabanja mara mbili kwa shabaha maridhawa (kumbuka nilikuwa bingwa wa shabaha chuoni kama ilivyowahi kusimuliwa kwenye mkasa unaoitwa ‘Ufukweni Mombasa’), risasi ya kwanza ilikisambaratisha kioo cha mbele cha gari lile na risasi ya pili ilimpata dereva shingoni, akapoteza mwelekeo na gari likaanza kuyumba.
Na hapo nikashuhudia mlango wa nyuma wa lile gari ukifunguliwa na jamaa wawili wenye bunduki za maana, aina ya US Barrett M82, wakaruka kwa ufundi wa aina yake na kutua kwa kuviringika huku lile gari likienda kugonga kwenye majengo ya damu salama na kufumuka sehemu ya mbele, kwenye boneti, mara moshi ukaanza kutoka. Wale jamaa walikuwa wepesi sana, walipoanguka wakawahi kuinua na kutawanyika haraka eneo lile huku mmoja akinikabili.
Sasa eneo lile la hospitali lilianza kunuka harufu ya damu, ilikuwa ni patashika kati yangu na yule jamaa mmoja huku yule wa pili nikiwa sijui ameelekea wapi!
Watu walianza kutoka na kushangaa kabla hawajasambaratika kila mmoja akikimbilia anakokujua baada ya bunduki ya yule jamaa kubanja risasi kadhaa wakati akijaribu kunilenga, bahati nzuri nilikwisha baini nini ambacho angefanya na hivyo niliwahi kujitupa chini kwa kasi ya aina yake na kujibanza pembeni ya gari moja aina ya
Toyota Hiace, risasi zikanikosa, na wakati huo huo niliviringika chini na kupenya katika uvungu wa gari lile na kutokea upande mwingine.
Nikiwa nimejilaza pale chini risasi ziliendelea kuvuma kule kwenye gari nilikojificha na kuliharibu vibaya lile gari na wakati huo huo wale watu waliokuwa maeneo ya karibu wakipatwa na taharuki ya aina yake na kuanza kukimbia ovyo.
Nikiwa makini na nyendo za yule jamaa mara nikaiona miguu yake ikija eneo lile huku akiendelea kumimina risasi, nikaiweka sawa bastola yangu na kufyatu risasi mbili nikiilenga miguu yake, risasi zile zikavunja mifupa ya ugoko kwenye miguu yake yote, akapiga yowe kali la maumivu huku akianguka chini, bunduki ikamtoka mikononi na kuanguka kando.
Nikajitokeza haraka toka pale mafichoni na kumfuata huku nikimwelekeza bastola. Sikuwa na lengo la kummaliza kwa risasi bali nilitaka tumpate akiwa hai ili tukamhoji kujua ni nani aliyewatuma kuja kumuua Samson Dadi.
Wakati nikimfuata, muda huo huo nikaliona gari moja aina ya
Toyota Mark X jeusi lililokuwa na vioo vyeusi visivyoonesha waliokuwemo ndani likija kwa mwendo wa kasi toka katika lango la kuingilia hospitalini hapo. Mara moja nikalitambua, lilikuwa ni lile gari lililokosa kunigonga kule Barabara ya Tanu. Lilikuwa likija kwa kasi ya ajabu kuelekea kule nilikokuwa, na lilipokuwa umbali wa takriban mita ishirini kabla halijafika eneo nililokuwepo sauti ya kishindo kikubwa cha mlipuko ikazizima eneo lile ikifuatiwa na moto mkubwa ulioruka hewani.
Nilipotazama vizuri nikaliona lile gari likinyanyuliwa juu zima zima na kurushwa hewani kama kiberiti huku likisambaratika vipande vipande. Hali ile ikaniogopesha sana. Nikajitupa chini huku nikimkumba yule jamaa niliyemvunja ugoko kwa risasi na kumkandamiza chini asiweze kutoroka.
Wakati huo nilikuwa najaribu kuwaza ni nini kilichosababisha lile gari likalipuka, na hapo nikahisi kuwa lile gari huenda lililipuliwa au lilikuwa limebeba mlipuko mkubwa. Kwa dakika chache mahala hapo pakageuka kama sehemu ya kuchezea sinema. Kilizuka kizaazaa cha aina yake kilichomtia hofu kila mtu aliyekuwepo eneo lile.
Tukio lile la kulipuliwa kwa gari likafanya kumbukumbu ya tukio la usiku wa kuamkia siku ile kule Dodoma irudi tena kichwani mwangu na kuwakumbuka jamaa zangu Almasi, Sofia na Amanda. Roho ikaniuma sana kwani sikuwa na uhakika kama walikuwa wamesalimika na dhahama ile.
Baada ya kitambo fulani hivi nikiwa bado nipo pale chini nimemkandamiza yule jamaa nikasikia nimeguswa na kitu cha baridi shingoni ambacho moja kwa moja nilitambua kuwa ulikuwa ni mtutu wa bunduki. Mwili ukaingiwa na baridi.
“
Put your gun down and get up slowly,” nilisikia sauti kavu ya mwanamume ikiniamuru. Lafudhi ya Kiingereza chake iliniashiria kuwa mtu yule hakuwa Mtanzania.
Mwili wote ulikuwa umekufa ganzi maana nilijua kuwa sikuwa na ujanja tena na kupona ilikuwa ni muujiza, sikujua Daniella alikuwa wapi muda huo. Mara nikasikia mlio hatari wa risasi, nikajirusha na kuviringika kando huku nikigeuka kumkabili yule mtu aliyeniwekea mtutu wa bunduki shingoni, nikamwona yule jamaa akinyanyuliwa juu na kubwagwa chini kama mzigo. Risasi ilikuwa imefumua kichwa chake.
Dah, nikashangaa na kugeuka kutazama kule nilikohisi risasi hiyo ilitokea. Nikamwona Daniella akija haraka mbele yangu akiwa na bunduki aina ya US Barrett M82, kama ambazo walikuwa nazo wale jamaa. Nikachoka kabisa.
Nikakumbuka kuangalia saa yangu ya mkononi, ilikwishatimia saa kumi na dakika therathini na tano alasiri.
Endelea kufuatilia hadi mwisho wa utata huu...