Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Kweli huu ni utata big up bishop..tupo pamoja Hadi mwisho wa harakati kuanzia ufukweni Mombasa mpaka hapa ni kazi kazi tu
 
utata.JPG

347

Saa 9:45 mchana…

Nilitumia takriban dakika ishirini na tano tu kumaliza kile kilichokuwa kimenipeleka pale Benki ya CRDB kisha nikatoka na kuanza kutembea haraka nikiwa sina hili wala lile, nikashika njia kurudi ofisini kwa RSO wa Mtwara, nilipoifikia Barabara ya Tanu nilisimama kwanza nikaangaza macho yangu kulia na kushoto ili nipate kuvuka barabara.

Kwa kufanya vile nikaliona gari moja dogo aina ya Toyota Mark X jeusi lililokuwa na vioo vyeusi visivyoonesha waliokuwemo ndani likija kwa mwendo wa kasi likitokea upande wangu wa kushoto katika barabara ile ya Tanu, lilipokuwa takriban mita mia moja kabla halijafika eneo nililokuwa nimesimama likahamia upande wa kulia ambao nilikuwepo nikisubiri nivuke barabara.

Baada ya kuona lile gari likihamia upande wangu nikaamua kupiga hatua za haraka haraka ili nivuke ile barabara. Cha kushangaza lile gari nalo likahama tena kutoka upande niliotoka na kurudi upande ambao sasa nilikuwepo huku likiongeza kasi maradufu!

Sasa lilikuwa takriban mita tano tu mbele yangu na lilikuwa linakuja kwa kasi kubwa. Kwa mahesabu ya haraka ni kwamba nisingeweza kumaliza barabara kwa kasi ya hatua zangu bila kugongwa. Nikaamua kurusha hatua zangu kukimbia lakini sikuweza kumaliza kuvuka ile barabara, lile gari likawa tayari limeshanifikia karibu mno, sasa nilikuwa nashuhudia kwa macho yangu jinsi ambavyo lile gari lilikuwa linakwenda kunigonga na kunivunja vunja!

Hapo sasa akili yangu ikafanya kazi haraka, ilibidi nitumie ujuzi wangu wote kujiokoa na ajali ile ambayo kwa namna ilivyoonekana dereva wa lile gari alikusudia kuniua. Kwa kutumia mguu wangu mmoja nilijirusha juu huku nikiviringika kwa samasoti, kufumba na kufumbua mgongo wangu ukatua juu ya bodi la gari, nikaviringika mara mbili kabla sijatua upande wa pili huku gari likipita!

Kule nilipoangukia nilitua kwa kuweka mkono wangu wa kushoto chini, mguu wa kulia ukinyookea nyuma na wa kushoto ukiwa umejisimika kwa kuukunja. Kilikuwa kitendo cha haraka sana na cha kustaajabisha kilichomwacha kila mtu aliyeshuhudia tukio hilo kwenye bumbuwazi. Kwa namna watu walivyokuwa wakiniangalia niliamini kabisa kuwa kitu hicho walizoea kukiona kwenye sinema tu lakini siku hii walikiona ‘mbashara’ mbele ya macho yao, tena kamera zikiwa hazipo.

Kisha nilisimama haraka kana kwamba hakuna lolote lililotokea, nikaondoka kuelekea zilipo ofisi za RSO wa Mtwara. Mjini hakuna dogo, muda huo watu walikuwa wanajaa na kunitazama kwa namna ambayo walishindwa kuamini, wapo walioniambia niende hospitali nikacheki huenda nilikuwa nimeumia pasipo mwenyewe kujua. Niliwaambia kuwa nilikuwa salama, halafu nikazidisha hatua zangu ili nipotee eneo lile.

Wakati nikitembea mawazo yalianza kupita akilini kwangu, nilijiuliza, ni akina nani waliotaka kunigonga na gari? Walijuaje kuwa ningetokea njia ile na hivyo kuja na gari lao katika Barabara ile ya Tanu? Hii ilionesha kuwa watu hawa walikuwa ndani au karibu na ofisi ya RSO na walikuwa tayari wamekwisha fahamu kuhusu uwepo wetu pale Mtwara.

Kingine kilichonishtua ni kuwa huenda walikuwa wamefuatilia nyendo zangu wakati naelekea Benki ya CRDB pasipo mwenyewe kujua! Na hapo nikaanza kujilaumu kwa kutokuwa makini zaidi.

_____



Saa 10:05 alasiri…

“Vipi, Jason, katika taarifa ile kuna jambo lolote umelishuku?” Daniella aliniuliza kwa sauti ya chini wakati tukielekea kwenye eneo la maegesho ya magari.

Japo nilikuwa nimefahamiana na Daniella kwa muda mfupi lakini katika muda huo niliweza kumfahamu Daniella kama mwanausalama makini sana na aliyekuwa akiipenda sana nchi yake, lakini hata hivyo sikuona kama kulikuwa na haja ya kumwelezea juu ya hisia zangu hadi kwanza nisikie yeye alishuku nini.

Katika maisha yangu ya kijasusi nilikuwa nimejifunza mengi… nilijifunza kuwa kuumbwa na masikio mawili na mdomo mmoja kulikuwa na maana ya kuweka wazi masikio yako kusikiliza zaidi ya vile ambavyo unatakiwa kuongea. Nami nilifanya hivyo nikiweka maanani kitu kimoja tu; kumruhusu mtu anieleze lolote analoweza, anishauri lolote analoona linafaa kunishauri lakini aidha kuchukua ushauri wake na kuufanyia kazi ilibaki kuwa juu yangu na akili zangu.

“Mh! Kwa sasa ni mapema sana kuzungumza lolote…” niliongea kwa utulivu huku nikimshika Daniella begani ingawa fikra zangu zilikuwa mbali kabisa na eneo lile. Hata hivyo macho yangu yalikuwa makini zaidi kuzichunguza sura za watu eneo lile na mijongeo yao.

“Kutekwa kwa Rais imekuwa pigo kubwa la kiusalama na udhalilishaji kwa taifa letu. Kamwe kitendo hiki hakiwezi kuvumilika hata kidogo,” Daniella aliongea kwa ghadhabu.

Nikaafikiana naye, muda huo tulikuwa tunafika kwenye kona ya lile jengo tukiongozwa na Mama Komba kisha tukaingia upande wa kulia tukielekea eneo la nyuma la ofisi zile sehemu kulipokuwa na maegesho ya magari ya wafanyakazi huku tukiyatembeza macho yetu kwa utulivu huku na kule.

Mama Komba alituonesha gari moja aina ya Toyota Land Cruiser 70 series hardtop la rangi la samawati lenye vioo vyeusi na kutukabidhi funguo. Mama Komba alikuwa ameliandaa gari lile kwa ajili yetu, kwa maelekezo kutoka makao makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa, tangu ilipofahamika kuwa tungefika pale Mtwara.

Lilikuwa bado jipya lenye magurudumu mapya na madhubuti yanayoweza kuhimili vizuri mikikimikiki na rabsha za aina yeyote katika barabara korofi. Pia lilikuwa limesajiliwa kwa namba za binafsi.

Muda mfupi uliofuata tulikuwa ndani ya gari, mimi nikiwa kwenye usukani na injini ya gari lilikuwa linanguruma taratibu. Hapakuwa na muda wa kupoteza zaidi hivyo dakika chache zilizofuata nikalitoa ile gari kwenye maegesho na kuzunguka nikielekea kule upande wa mbele wa lile jengo la ofisi za RSO wa Mtwara kwenye geti la kutokea.

Muda mfupi uliofuata tukawa tayari tumetoka kwenye lile eneo la ofisi za RSO Mtwara na kuingia kulia tukiifuata Barabara ya Tanu. Mshale wa mafuta kwenye dashibodi ya lile gari ulionesha kuwa lile gari lilikuwa na mafuta ya kutosha kiasi cha kufanikiwa kututoa wasiwasi kuwa mizunguko yetu isingekwamia njiani jambo ambalo lilinifurahisha sana.

Tuliifuata Barabara ya Tanu na muda mfupi uliofuata tuliufikia mzunguko wa barabara na kuiacha barabara ya Tanu, tukaingia kulia kuifuata Barabara ya Jamhuri na baada ya mwendo wa ndani ya dakika moja tukajikuta tukiwa nje ya geti la Hospitali ya Ligula. Tukatafuta maegesho na kuliegesha gari letu kando ya gari moja jeusi moja aina Toyota Rav 4L lililokuwa na vioo vyeusi visivyomruhusu mtu kuona ndani.

Haikutuwia vigumu, kwani dakika tano baadaye tulikuwa ndani ya Ofisi ya Daktari Mfawidhi wa Hospitali ya Ligula, mzee wa makamo mrefu mwembamba na kichwani alikuwa na upara na nywele fupi zilizoanza kutawaliwa na mvi. Alikuwa amevaa shati jeusi lenye mistari myeupe la mikono mirefu na suruali ya kadeti ya rangi ya maruni.

Tulijitambulisha kwa kumwonesha vitambulisho vyetu. Yeye pia alijitambulisha kwetu kuwa aliitwa Swedy Mashaka… Daktari Swedy Mashaka. Kisha tulimweleza lengo letu la kutaka kujua hali ya Samson Dadi, meneja wa bandari ya Mtwara aliyekuwa amelazwa pale Ligula na kisha tulihitaji kumwona.

Endelea...
 
utata.JPG

348

“Samson Dadi amefikishwa hospitali mchana huu baada ya kukutwa amezirai ofisini kwake. Maofisa wa usalama walipofika ofisini kwake wakamkuta akiwa sakafuni kalala kimya, povu likimtoka mdomoni na hivyo wakamuwahisha hapa,” Daktari Mashaka alitueleza. Kisha akaongeza, “Uchunguzi wa awali umetuonesha kuwa alipandwa na presha.”

“Hakuna kingine?” nilimuuliza Daktari Mashaka huku nikimkazia macho.

“Hakuna. Bado tunaendelea na uchunguzi,” Daktari Mashaka alijibu na kututaka twende wodini kumtazama. Aliinuka kisha tukatoka na kuelekea wodi aliyolazwa mtu huyo.

Mlangoni mwa wodi ile tulikuta askari wawili waliokuwa wamesimama wakilinda usalama, wote walikuwa wameshika bunduki aina ya SMG. Tukawasalimia huku tukitaka kuingia mle wodini. Kwa kuwa wote watatu tulikuwa tumevaa nguo za kawaida, hata Daktari Mashaka hakuwa amevaa koti la kidaktari wala kubeba kifaa chochote cha kupimia, hivyo wale askari wakatuzuia kuingia.

“Kuna daktari, hamruhusiwi kuingia,” askari mmoja alitwambia huku akitutunishia kifua.

Wakati Daktari Mashaka akitaka kujieleza kwa wale askari nikahisi tulikuwa tunachelewa maana kengele ya hatari ililia kichwani kwangu, nikampiga kikumbo yule askari aliyenitunishia kifua na kuzama ndani ya ile wodi fasta huku nikifuatwa nyuma na Daniella na kuwaacha wale askari wakishangaa.

Hata hivyo ilionesha kuwa kitendo kile kiliwaudhi wale askari, wakaingia ndani kwa hasira kutufuata wakiwa wameshika vyema bunduki zao mkononi na kutuelekezea. Muda huo nilikuwa nimesimama karibu na kitanda nikishangaa baada ya kutomwona daktari yeyote isipokuwa mgonjwa peke yake akiwa amelalia dimbwi la damu mbichi iliyokuwa ikichuruzika sakafuni.

Wale askari nao wakajikuta wakishangaa kuona damu mbichi ikitambaa taratibu ndani ya chumba kile na kushindwa kufanya kile walichokusudia. Niligeuza shingo yangu kuwatazama wale askari kwa macho yaliyotoa ujumbe wa lawama kwa uzembe walioufanya, kisha nikamsogelea yule mgonjwa pale kitandani na kumtazama vizuri, na hapo nikagundua kuwa uhai ulishamtoka na mwili wake ulikuwa na majeraha matatu ya risasi.

Shit! Wametuwahi!” niling’aka kwa hasira huku nikikimbilia dirishani na kutazama, nikagundua kuwa kioo cha dirisha kilikuwa wazi jambo lililomaanisha kuwa muuaji baada ya kutekeleza azma yake alipitia hapo, nami nikapita pale dirishani na kutimua mbio kuelekea kule nyuma ya lile jengo la wodi.

Kule nyuma niliangaza huku na kule bila mafanikio. Nikaangalia kila sehemu lakini sikumwona yeyote wa kumtilia shaka.

“Dah! Sijui ni nani aliyewashtua kuwa tunakuja hapa hospitali!” nilijiuliza kwa mshangao huku nikianza kuzunguka lile jengo ili niende nikatokee upande wa pili wa lile jengo, lakini kabla sijapiga hatua zaidi nikasita baada ya kuona koti la kidaktari likiwa limetupwa kando ya tenki lililojengwa ili kukinga maji ya mvua.

Sikusubiri, nikatoka kasi na kutokea upande wa pili wa lile jengo na hapo nikaliona lile gari jeusi aina ya Toyota Rav 4L likiondoka kwa kasi toka eneo lile la maegesho ya magari. Machale yakanicheza, nikachomoa bastola yangu huku nikikimbia upande wa pili ambako niliamini lazima lile gari lizunguke kabla ya kutoka. Nilipofika usawa mzuri nikajificha nyuma ya mti mkubwa wa kivuli, mara nikaona kioo cha nyuma cha lile gari kikishuka haraka na mtutu wa bunduki ukachungulia.

Niliruka na kutua eneo lingine nikiziacha risasi zilizotoka kwenye ile bunduki zikiusulubu ule mti mkubwa wa kivuli na kuchubua magome yake. Nikiwa pale chini nilipoangukia bastola yangu ikabanja mara mbili kwa shabaha maridhawa (kumbuka nilikuwa bingwa wa shabaha chuoni kama ilivyowahi kusimuliwa kwenye mkasa unaoitwa ‘Ufukweni Mombasa’), risasi ya kwanza ilikisambaratisha kioo cha mbele cha gari lile na risasi ya pili ilimpata dereva shingoni, akapoteza mwelekeo na gari likaanza kuyumba.

Na hapo nikashuhudia mlango wa nyuma wa lile gari ukifunguliwa na jamaa wawili wenye bunduki za maana, aina ya US Barrett M82, wakaruka kwa ufundi wa aina yake na kutua kwa kuviringika huku lile gari likienda kugonga kwenye majengo ya damu salama na kufumuka sehemu ya mbele, kwenye boneti, mara moshi ukaanza kutoka. Wale jamaa walikuwa wepesi sana, walipoanguka wakawahi kuinua na kutawanyika haraka eneo lile huku mmoja akinikabili.

Sasa eneo lile la hospitali lilianza kunuka harufu ya damu, ilikuwa ni patashika kati yangu na yule jamaa mmoja huku yule wa pili nikiwa sijui ameelekea wapi!

Watu walianza kutoka na kushangaa kabla hawajasambaratika kila mmoja akikimbilia anakokujua baada ya bunduki ya yule jamaa kubanja risasi kadhaa wakati akijaribu kunilenga, bahati nzuri nilikwisha baini nini ambacho angefanya na hivyo niliwahi kujitupa chini kwa kasi ya aina yake na kujibanza pembeni ya gari moja aina ya Toyota Hiace, risasi zikanikosa, na wakati huo huo niliviringika chini na kupenya katika uvungu wa gari lile na kutokea upande mwingine.

Nikiwa nimejilaza pale chini risasi ziliendelea kuvuma kule kwenye gari nilikojificha na kuliharibu vibaya lile gari na wakati huo huo wale watu waliokuwa maeneo ya karibu wakipatwa na taharuki ya aina yake na kuanza kukimbia ovyo.

Nikiwa makini na nyendo za yule jamaa mara nikaiona miguu yake ikija eneo lile huku akiendelea kumimina risasi, nikaiweka sawa bastola yangu na kufyatu risasi mbili nikiilenga miguu yake, risasi zile zikavunja mifupa ya ugoko kwenye miguu yake yote, akapiga yowe kali la maumivu huku akianguka chini, bunduki ikamtoka mikononi na kuanguka kando.

Nikajitokeza haraka toka pale mafichoni na kumfuata huku nikimwelekeza bastola. Sikuwa na lengo la kummaliza kwa risasi bali nilitaka tumpate akiwa hai ili tukamhoji kujua ni nani aliyewatuma kuja kumuua Samson Dadi.

Wakati nikimfuata, muda huo huo nikaliona gari moja aina ya Toyota Mark X jeusi lililokuwa na vioo vyeusi visivyoonesha waliokuwemo ndani likija kwa mwendo wa kasi toka katika lango la kuingilia hospitalini hapo. Mara moja nikalitambua, lilikuwa ni lile gari lililokosa kunigonga kule Barabara ya Tanu. Lilikuwa likija kwa kasi ya ajabu kuelekea kule nilikokuwa, na lilipokuwa umbali wa takriban mita ishirini kabla halijafika eneo nililokuwepo sauti ya kishindo kikubwa cha mlipuko ikazizima eneo lile ikifuatiwa na moto mkubwa ulioruka hewani.

Nilipotazama vizuri nikaliona lile gari likinyanyuliwa juu zima zima na kurushwa hewani kama kiberiti huku likisambaratika vipande vipande. Hali ile ikaniogopesha sana. Nikajitupa chini huku nikimkumba yule jamaa niliyemvunja ugoko kwa risasi na kumkandamiza chini asiweze kutoroka.

Wakati huo nilikuwa najaribu kuwaza ni nini kilichosababisha lile gari likalipuka, na hapo nikahisi kuwa lile gari huenda lililipuliwa au lilikuwa limebeba mlipuko mkubwa. Kwa dakika chache mahala hapo pakageuka kama sehemu ya kuchezea sinema. Kilizuka kizaazaa cha aina yake kilichomtia hofu kila mtu aliyekuwepo eneo lile.

Tukio lile la kulipuliwa kwa gari likafanya kumbukumbu ya tukio la usiku wa kuamkia siku ile kule Dodoma irudi tena kichwani mwangu na kuwakumbuka jamaa zangu Almasi, Sofia na Amanda. Roho ikaniuma sana kwani sikuwa na uhakika kama walikuwa wamesalimika na dhahama ile.

Baada ya kitambo fulani hivi nikiwa bado nipo pale chini nimemkandamiza yule jamaa nikasikia nimeguswa na kitu cha baridi shingoni ambacho moja kwa moja nilitambua kuwa ulikuwa ni mtutu wa bunduki. Mwili ukaingiwa na baridi.

Put your gun down and get up slowly,” nilisikia sauti kavu ya mwanamume ikiniamuru. Lafudhi ya Kiingereza chake iliniashiria kuwa mtu yule hakuwa Mtanzania.

Mwili wote ulikuwa umekufa ganzi maana nilijua kuwa sikuwa na ujanja tena na kupona ilikuwa ni muujiza, sikujua Daniella alikuwa wapi muda huo. Mara nikasikia mlio hatari wa risasi, nikajirusha na kuviringika kando huku nikigeuka kumkabili yule mtu aliyeniwekea mtutu wa bunduki shingoni, nikamwona yule jamaa akinyanyuliwa juu na kubwagwa chini kama mzigo. Risasi ilikuwa imefumua kichwa chake.

Dah, nikashangaa na kugeuka kutazama kule nilikohisi risasi hiyo ilitokea. Nikamwona Daniella akija haraka mbele yangu akiwa na bunduki aina ya US Barrett M82, kama ambazo walikuwa nazo wale jamaa. Nikachoka kabisa.

Nikakumbuka kuangalia saa yangu ya mkononi, ilikwishatimia saa kumi na dakika therathini na tano alasiri.


Endelea kufuatilia hadi mwisho wa utata huu...
 
Bishop jumamosi ya leo tutamsoma Mr sizya?kama itakupendeza tuletee utata jamaa yetu!
 
Litro njoo tuandamane bishop atupie leo!
Nitaleta baadaye kidogo, mkuu, naumwa sana na kichwa kiasi kwamba nakwepa kukaa kwenye computer. Halafu Litro hawezi kuja[emoji849], amekasirika kwa kuwa Utata ilichelewa kuanza[emoji17]...
 
Nitaleta baadaye kidogo, mkuu, naumwa sana na kichwa kiasi kwamba nakwepa kukaa kwenye computer. Halafu Litro hawezi kuja[emoji849], amekasirika kwa kuwa Utata ilichelewa kuanza[emoji17]...
Pole sana mwamba,tunakuombea upate nafuu haraka utuletee utata,sidhani kama litro amekasirika anafahamu una majukumu mengine sio kutuletea riwaya tu!
 
Nitaleta baadaye kidogo, mkuu, naumwa sana na kichwa kiasi kwamba nakwepa kukaa kwenye computer. Halafu Litro hawezi kuja[emoji849], amekasirika kwa kuwa Utata ilichelewa kuanza[emoji17]...
Kama ulikuwepo mpz yani nimeget attached addicted na hii kitu till it has broken my heart
 
Back
Top Bottom