Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Nashukuru Mungu tatizo limegundulika na nimeshaanza tiba. Kwa sasa nipo sawa kisaikolojia kwani ilikuwa inaniumiza mno kuona naumwa lakini ugonjwa haujulikani, tiba napata lakini sipati nafuu!

Mungu akipenda kesho naubwaga mzigo wote humu ndani. Tusameheane maana season hii ya UTATA pia imekuwa na utata kwenye afya yangu...
Polee sana baba Askofu
 
Kesho tunaimaliza simulizi ya Utata, nimeshamaliza kuipitia upya sehemu yote iliyobakia japo ilikuwa kazi ngumu kidogo...

Tuvumiliane tu wakuuu maana haya mabo yalikuwa nje ya uwezo wangu...
 
Kesho tunaimaliza simulizi ya Utata, nimeshamaliza kuipitia upya sehemu yote iliyobakia japo ilikuwa kazi ngumu kidogo...

Tuvumiliane tu wakuuu maana haya mabo yalikuwa nje ya uwezo wangu...
Ndio nilikuja kuchungulia tena! Haya kila la kheri mkuu tunakuombe afya njema tuamke salama tujue mwisho wa utata
 
Kesho hii apa imefka mkuu Bishop, hopefully ugali njema eroo tufanye wepesi tumalize huu utata man
 
utata.JPG

378

Kinyonga!




Saa 11:15 alfajiri…

AKILI yangu tu ndiyo ilihisi ule ujumbe kwenye karatasi ulikusudiwa kutuonesha kitu cha muhimu sana, ama pengine kutukutanisha na mtu ambaye tulimhitaji sana ili kukamilisha jambo lenye kuendana na mkasa ambao hadi muda huu sikujua niupe jina gani zaidi ya kuuita; ‘utata’. Ndiyo, ilikuwa ni operesheni utata!

Nilidhani jina hili la utata lilistahili kwani hali ilianza kama masihara tu… kama tamthilia, tena tamthilia yenyewe ya mapenzi. Na waigizaji katika tamthilia hii, mimi na Almasi kwa upande mmoja; na Sofia na Amanda, kwa upande wa pili.

Sikupata kabisa kuhisi kuwa mwanzo wa tamthilia hii iliyoanzia kule Capital Social Club jijini Dodoma ulikuwa sawa na kuanza kwa mkasa mzito ulioibuka katikati ya sherehe kama mkondo wa mto unaopita katika majanga ya nchi yenye kila aina ya ukatili na unyama usiomithilika!

Mkasa ambao hatimaye ulinifikisha katika Mji wa Mtwara, ambako yaliibuka mambo makubwa ya kushangaza. Na katikati ya mkasa huu wenye utata uliojaa mapambano makali ya kufa ama kupona, ndipo nilipokutana na kipande hiki cha karatasi yenye ujumbe ambao kwa vyovyote ulikuwa muhimu sana na uliokusudiwa kutuonesha jambo lenye kuendana na mkasa huu…

Ilikuwa ni ile karatasi niliyoikuta chini ya mlango wa gari upande wa dereva, karibu na gurudumu la mbele, ikiwa imekunjwa vizuri na kuwekwa kwa namna ambayo ilikusudiwa ionwe na dereva wa gari hilo tu. Karatasi hiyo ilikuwa imechanwa kutoka kwenye ukurasa fulani wa kitabu cha shule ya msingi, ukurasa uliokuwa na michoro, na katikati ya michoro ile kulikuwa na maandishi yaliyoandikwa kwa kalamu ya wino wa kijani kwa namna fulani ya uficho yakikusudiwa kuonwa na yule aliyekusudiwa tu.

Ujumbe wake ulikuwa wa kuchanganya herufi na tarakimu, ujumbe wa mafumbo (codes). Hata hivyo, uwepo wa Daniella ulizifanya codes hizo zionekane kama hesabu rahisi za shule ya awali. Uliandikwa: LN917-FN910-CN8370.

Ilimchukua Daniella si zaidi ya nusu saa kutambua kuwa herufi na tarakimu zile zilikuwa ni namba za simu zilizoandikwa kinyume. Ilikuwa: LN917 ilimaanisha last number 917; FN910 – first number 910; halafu CN – code number 8370.

Hata hivyo mwanzoni haikuingia akilini baada ya kuzinakiri vizuri zile namba na hivyo kuwa 8370910917 lakini baada ya kuchekecha ubongo na kuziandika kinyume nyume namba zote ndipo tulipokuja kuipata namba hii; 0738019719.

Bila kujiuliza mara mbili niliziingiza zile namba kwenye simu yangu kisha nikazipiga na kuweka spika ya nje, simu ile iliita mara moja tu na kupokewa lakini hakuna aliyeanza kuzungumza kati yetu. Katikati ya kitambo kile kifupi cha ukimya, yule mtu upande wa pili wa simu akauliza kwa sauti iliyojaa wasiwasi; “Nani mwenzangu?”

Ilikuwa sauti nzito ya mwanamume na iliuliza kwa namna iliyoonesha mzungumzaji alikuwa amekerwa kidogo na tabia ya mpigaji kukaa kimya akimtegea yeye awe mzungumzaji wa kwanza. Daniella akaonesha shauku ya kutaka kuongea baada ya kuhisi ile sauti alikuwa ameisikia kabla…

“Daniella,” Daniella alijibu haraka pasipo shaka yoyote kisha akasubiri kusikia yule mtu upande wa pili wa simu angesema nini.

Hata hivyo tulishanganzwa na kicheko chake kilichoibuka ghafla, kilikuwa kicheko kilichobeba kitu ndani yake… na kilipokatika akasema; “Nilijua tu kuwa ungeweza kulifumbua fumbo na kutambua kuwa ni namba za simu! Una akili sana, dada!”

Mimi na Daniella tukaangaliana pasipo kusema neno huku tukijaribu kuitafakari sauti ile ili kubaini alikuwa mtu gani, na wakati tukiwa bado katikati ya tafakari ile, mawazo yetu yakakatizwa na sauti ya mzungumzaji yule aliyekuwa upande wa pili wa simu; “Kwanza, ningeomba unielewe kuwa kwa kuzungumza nawe navunja amri zote za kazi yangu. Jambo ambalo natarajia kuzungumza ni siri kubwa sana ambayo haikutakiwa kuyafikia masikio ya mtu yeyote yule asiyehusika. Kinyonga akinigundua ataninyonga. Natumaini unanielewa.”

“Vizuri sana,” Daniella alimjibu kwa kifupi.

“Hata hivyo, kama nilivyoeleza awali, sioni umuhimu wa kutokukuhusisha. Hakuna binadamu yeyote mwenye mapenzi mema kwa nchi yake atakayefurahia kuiona nchi ikitumbukia kwenye mambo ya ovyo… mambo ambayo yamesababisha utekaji na mauaji yasiyokoma, sioni kwa nini watu wasio na hatia waendelee kuuawa kinyama wakati mtu huyu na kundi lake dogo wanastarehe. Natumaini utanielewa na tutakuwa bega kwa bega kupambana. Sawa?” yule mzungumzaji upande wa pili wa simu alisema.

Hata hivyo katika maneno yote aliyoyaongea bado sikuelewa alikusudia kufikisha ujumbe gani hasa. Vivyo hivyo kwa Daniella, hakuwa amemwelewa. Tulihisi kama tuliokuwa tukipotezewa muda kwa maelezo mengi yasiyo ya msingi. Tulichohitaji ilikuwa ni kitu kidogo sana. Kuelewa nini lilikuwa lengo la ujumbe ule ili tuingie kazini kuendeleza harakati na hatimaye tumpate Rais.

“Unaonaje ukikata mahubiri na kunieleza kile ulichopanga kunieleza. Huoni kama tunapoteza muda?” Daniella alimuuliza yule mzungumzaji aliyekuwa upande wa pili wa simu.

“Usijali…” yule mzungumzaji alisema huku akiangua kicheko hafifu, halafu akaendelea, “…yote ambayo naweza kukwambia ni kwamba, ukihitaji kumjua Kinyonga utampata katika nyumba namba 14 iliyopo Mtaa wa Skoya, kabla ya mapambazuko.”

“Kinyonga?” Daniella aliuliza kwa mshangao.

“Ndiyo. Kwani jana ulitaka kuzungumza na nani? Kinyonga, sivyo?” mzungumzaji huyo upande wa pili wa simu aliuliza. “Kama ulimhitaji awe shahidi basi tambua huyo ndiye mbaya mwenyewe. Anaweza kuwa ni mtu hatari zaidi ya nyati aliyejeruhiwa. Anaagiza watu watekwe na kuuawa huku yeye ametulia kwenye kiti cha kimalkia akinywa sharubati. Wewe na mwenzio mnatakiwa kumpata mtu huyu kwenye nyumba hiyo kabla jua halijachomoza, mkichelewa tu imekula kwenu maana huyu ndiye mwenye majibu yote ya maswali yenu na ndiye anajua wapi alipo mheshimiwa Rais…” yule mzungumzaji upande wa pili wa simu alimaliza maelezo yake.

Mimi na Daniella tuliangaliana huku Daniella akishusha pumzi ndefu, nilijaribu kuyapima maelezo ya mzungumzaji yule aliyekuwa upande wa pili wa simu, kuona kama yalikuwa na chembe yoyote ya ukweli au ulikuwa mtego!

Hata hivyo, Daniella alinifanyia ishara fulani ya dole gumba iliyomaanisha kuwa ile sauti ilimfanya kuyaamini maneno ya mtu yule. Alikuwa ameitambua sauti ile japo mzungumzaji alijaribu kuibadili kidogo.

“Nimekusoma, daktari…” hatimaye Daniella alimwambia mtu huyo aliyekuwa upande wa pili wa simu.

“Hunijui, sikujui. Sawa?” yule mzungumzaji aliyekuwa upande wa pili wa simu alisema kwa msisitizo.

“Sawa,” Daniella alijibu akitabasamu. Simu ikakatwa.

“Ni nani? Mbona umemwita daktari!” nilimuuliza Daniella kwa mshangao.

“Ni daktari wa mke wa Rais! Japokuwa amejitahidi kubadilisha sauti yake lakini sikushindwa kumtambua, jana alinikatalia katakata kuonana na mke wa Rais, nadhani sasa ana hoja muhimu na anataka kutuonesha kitu tusichokijua,” Daniella alisema na kushusha tena pumzi ndefu.

Endelea....
 
utata.JPG

379

Kisha kwa dakika chache sana tulijadiliana kuhusiana na ujumbe ule tulioupata toka kwa yule daktari kabla hatujainuka kwenda kwenye harakati ambazo pengine zingetuingiza kwenye mtego mbaya ulio sawa na kujipeleka wenyewe kwenye mdomo wa chatu mwenye njaa.

Cha kwanza tulichojiuliza ni iwapo jina alilolitumia la ‘Kinyonga’ lilikusudiwa kututambulisha juu ya mtu tuliyemfahamu kwa jina la ‘Chameleon’ au la!

Na kama ndivyo, je, Chameleon alikuwa nani? Maana taarifa tulizokuwa nazo zilibainisha kuwa ni mkuu wa kikosi cha siri cha ulinzi wa Rais, Yusuf Assad Taifa! Kama yeye ndiye Chameleon kwa nini sasa tuambiwe kuwa Kinyonga alikuwa ametulia kwenye kiti cha kimalkia akinywa sharubati? Kiti cha kimalkia ilimaanisha kuwa Chameleon ni mwanamke…

Na kama ni mwanamke, je, alikuwa ni Juliana Masinde, mke wa Rais Albert Masinde? Dah! jambo hili lilianza kuchanganya na kuibua maswali kibao, maswali ambayo, hata hivyo, hatukuwa na muda wa kuyatafutia majibu kwani majibu yake tungeyapata baada ya kufika kwenye eneo husika kabla hakujapambazuka kama tulivyoshauriwa.

* * *



Saa 11:35 alfajiri…

Dakika ishirini baadaye ilitukuta katika Mtaa wa Labamba, na muda huo Daniella alikuwa akiligesha gari letu mwanzoni mwa mtaa ule wa Labamba, uliokuwa nyuma ya Mtaa Skoya tuliloamini ilikuwepo ile nyumba namba 14 tuliyoikusudia. Gari tulilotumia safari hii lilikuwa aina ya Toyota Prado TX la rangi ya fedha tuliloazimwa na Askofu Masinde.

Kama kawaida yetu, nilitangulia kushuka na kuanza kutembea taratibu kuufuata Mtaa wa Labamba kwa tahadhari, na baada ya muda mfupi nikatokea katika mtaa mrefu kiasi wa Skoya, mtaa ambao hata kama ingekuwa mchana isingekuwa rahisi kuona nyumba za mwanzo au hata za mwisho wa mtaa huu, achilia mbali mida hii ya usiku wenye giza nene, giza totoro.

Pamoja na giza lililokuwa limetamalaki katika mtaa huu lakini niligundua kuwa ulikuwa ni mtaa wenye nyumba za kisasa na zilizojengwa katika mpangilio unaovutia. Mtaa huu ulikuwa na miti mingi mikubwa ya kivuli iliyosababisha kuwe na giza ambalo lilimudu kufifisha mwanga uliothubutu kutoka katika baadhi ya nyumba zile za kisasa zilizokuwa zimejengwa ndani ya uzio wa kuta ndefu, na kufanya mwanga huo wa umeme kuonekana kama chemli zisizo na mafuta ya kutosha.

Nilizidi kuambaa na giza lile huku macho yangu yakijaribu kuzipitia namba za majengo yaliyokuwa katika mtaa ule wa Skoya, na hatimaye nikawa nimeifikia nyumba namba 8, ni wakati huo ambapo niliona harakati fulani zikiendelea kwenye nyumba fulani iliyokuwa upande wa kulia kwangu, takriban mita hamsini mbele yangu, nyumba ambayo niliamini ndiyo tuliyoihitaji.

Ilikuwa nyumba kubwa ya ghorofa moja kwenda juu iliyozungushiwa uzio mrefu wa ukuta wenye mfumo maalumu wa kuzuia wezi. Na wakati nilipokuwa nikisogea niliona taa za vyumba vya juu zikiwaka lakini ghafla tu zilizimwa, hadi taa za nje. Hata hivyo jambo lile halikunifanya nisite kuendelea kusogea mbele.

Na nikiwa nimebakisha hatua chache tu kuifikia ile nyumba nikashtuka kuyaona magari mawili ya kijeshi yakiwa yameegeshwa mbele ya nyumba ile chini ya vivuli vya miti mikubwa yenye giza nene, iliyokuwa ndani ya uzio wa nyumba ile ingawa matawi yake makubwa yalitokezea kwa nje. Gari moja likiwa ni aina ya Jeep Wrangler na lingine lilikuwa aina ya Van likiwa na kimwerumweru juu na alama ya msalaba na mwezi mwekundu, ikimaanisha kuwa lilitumika kubeba wagonjwa.

Haraka nilichepuka na kujibanza nyuma ya mti mwingine mkubwa wa mwembe wenye giza nene uliokuwa kwenye nyumba ya jirani na nyumba ile tuliyoikusudia.

Niliendelea kujibanza pale nyuma ya mwembe huku nikiendelea kutazama kwenye ile nyumba na wakati nikifanya hivyo niligundua kuwa kulikuwa na wanajeshi wakakamavu wawili waliokuwa wamevaa mavazi ya kivita (combat gear) na kubeba bunduki za kivita na muda ule walikuwa wakiranda randa mbele ya ile nyumba.

Nikiwa nimejibanza nyuma ya ule mwembe akili yangu ilianza kufanya kazi nikifikiria namna ya kuingia ndani ya nyumba ile. Haukupita muda mrefu mara nililiona geti kubwa la mbele katika nyumba ile likifunguliwa, na hapo nikaliona lile gari la kubebea wagonjwa likisogea hadi pale getini pasipo kuwashwa taa na kisha wanajeshi wengine wawili wakatoka ndani ya uzio wa ile nyumba wakiwa wamebeba machela iliyoonesha ilikuwa na mtu aliyelazwa juu yake. Sikuweza kumtambua mtu yule ingawa niliamini alikuwa mwanamume.

Hali hiyo ikanifanya niyaache yale maficho yangu nyuma ya ule mwembe mkubwa na kisha nikanyata nikivuka barabara ile ya mtaa na kuhamia upande wa pili kwenye maficho ya mti mwingine uliyokuwa jirani zaidi na lile geti kubwa la mbele ya nyumba ile, mahali ambapo ningeweza kuwaona vizuri wale watu.

Kwa kujibanza pale nilipata nafasi nzuri ya kuthibitisha idadi yao. Walikuwa askari wa kijeshi wanne, wote walionekana kuwa makomando waliofuzu kwenye medani za kivita, watu wa kazi, na miongoni mwao hapakuwa na hata mmoja niliyeweza kumtambua. Sura zote zilikuwa ngeni kwangu!

Wale wanajeshi wawili waliotoka na machela walimwingiza yule mtu aliyelala juu ya machela ndani ya lile gari la kubebea wagonjwa ambalo injini yake iliunguruma taratibu pasipo kuzimwa, huku wale wanajeshi wengine wawili waliokutwa pale nje wakiendelea kulinda eneo lile.

Baada ya kumwingiza yule mtu, wale wanajeshi nao wakajipakia kwenye lile gari la kubebea wagonjwa na mara mlango wa lile gari ukaanza kujifunga.

Ni wakati huo niliposhuhudia jambo lingine tena. Niliona kivuli kikijitokeza kizani na kwa wepesi wa hali ya juu kikaenda hewani na kilipotua kilikuwa juu ya gari lile la kubebea wagonjwa kisha kikashuka na kwa aina nyingine ya ajabu, wanajeshi wale wawili waliokuwa wakilinda eneo lile wakajikuta wakichezea kipigo huku wakijaribu kujibu lakini hawakuweza kuzuia nguvu ya kile kivuli.

Kivuli kile kilikuwa na wepesi wa ajabu kiasi cha kuwashangaza wale makomando. Mara moja nilitambua kuwa yule alikuwa Daniella na muda ule alionekana kama kivuli kutokana na mavazi meusi aliyoyavaa. Kumbe wakati mimi nikisubiri kuona nini kingejiri yeye hakutaka kuwa na subira, alijitoa kimasomaso na kulianzisha. Hivyo na mimi sikutakiwa kuzubaa.

Kwa haraka sana nilichupa toka pale kwenye maficho yangu huku mkono wangu ukiwa umeshika vyema bastola tayari kwa lolote, nia yangu ilikuwa kuliwahi lile gari la kubebea wagonjwa na kuwazuia wale watu waliokuwa ndani ya lile gari la wagonjwa wasiweze kuondoka.

Hata hivyo, nilikwisha chelewa kwani wakati natua eneo lile, gari hilo nalo lilikuwa linaondoka kwa mwendo wa kasi, hivyo nikasimama na kupiga hesabu zingine tena.

Endelea...
 
utata.JPG

380

Ni wakati huo huo nilipowashuhudia wale wanajeshi waliokuwa wakipambana na Daniella wakiruka kwa namna ya ajabu na kurukia kwenye lile gari lingine aina ya Jeep Wrangler ambalo nalo lilikuwa linaondoka kwa kasi toka eneo lile.

Daniella alinipa ishara kuwa mimi niendelee na harakati za kuingia ndani ya ile nyumba wakati yeye akiwafuatilia wale jamaa, halafu akatoka mbio akiyafukuza yale magari. Bastola yake ikiwa mkononi.

Sikuwa na muda wa kupoteza, nilizungusha haraka macho yangu kutazama huku na huko katika namna ya kulikagua eneo lile na sikuchelewa kujihakikishia kuwa hapakuwa na mtu mwingine aliyesalia eneo lile, na hapo ndiyo nikaanza kunyata kwa tahadhari nikielekea kwenye geti la mbele la ile nyumba.

Lile geti lilikuwa bado halijafungwa sawa sawa, lilikuwa limerudishiwa tu. Dakika iliyofuata ilinikuta nikiwa ndani ya uzio wa nyumba ile, nyumba namba 14 ambayo sikubahatika kumjua mmliki wake, kwa jina, ila nilihisi ilihusiana na Chameleon na genge lake.

Mle ndani ya uzio wa nyumba niliyaona magari mawili ya kifahari, moja lilikuwa aina ya Mercedes Benz la rangi nyeusi na lingine lilikuwa Nissan Patrol la rangi nyekundu, yalikuwa yameegeshwa kwenye banda maalumu la kuegesha magari chini ya mti mmoja mkubwa, nikawa natembea kwa tahadhari kubwa nikiingia ndani zaidi huku nikiwa sina hakika na usalama wangu hadi muda huo.

Eneo lile lilikuwa giza kabisa. Niliufuata mlango wa nyuma wa kuingia ndani ya nyumba ile ambao nao ulikuwa wazi, hivyo nilifanya jitihada kidogo kuusukuma kisha nikaingia ndani huku bastola yangu ikiwa mkononi kutuliza ukorofi wa namna yoyote ambao ungejitokeza.

Mara baada ya kuingia mle ndani niligundua kuwa nilikuwa sehemu ya jikoni, na hapo nikasimama kimya nikijibanza pembeni kidogo ya mlango na kutulia huku nikiupima utulivu wa mle ndani na kujaribu kunasa mjongeo wa kitu chochote ndani ya giza la pale jikoni.

Zilipita takriban dakika kumi bila kusikia chochote na hapo hisia zangu zikaniambia kuwa hapakuwa na dalili za uwepo wa kiumbe hai yeyote mle ndani ingawaje hali hiyo haikunifanya nijiamini, kisha nilianza kunyata taratibu huku bastola yangu ikiwa mkononi.

Nikaanza kupita kwenye ukumbi mdogo wa kulia chakula wenye meza ya umbo duara iliyozungukwa na viti sita, nilikuwa makini ili nisigonge kitu ambacho kingemshtua adui endapo alikuwa ametega mtego mle ndani, nikaelekea sebuleni na halafu nikawa naambaa ambaa na ukuta nikitafuta swichi ya umeme ili niwashe taa.

Nilikuwa mbioni kuifikia swichi ile ya umeme pale nilipohisi kitu kama chuma cha baridi kikikigusa kisogo changu na kwa sekunde kadhaa nikasimama huku viungo vya mwili wangu vikikosa mawasiliano mazuri. Moyo wangu uliyasahau ghafla mapigo yake kabla ya kuanza kwenda mbio huku jasho jepesi likifanya ziara katika sehemu mbalimbali mwilini mwangu.

Nilianza kupanga namna ya kumuwahi yule mtu aliyekuwa amesimama nyuma yangu lakini sikufanikiwa kwani wakati nikitaka kuunyanyua mkono wangu ulioshika bastola nilishtukia nikipigwa pigo ambalo sikuweza kulielewa kwa haraka lilipigwa kwa mtindo gani kiasi cha kuweza kuipokonya bastola yangu mkononi.

Ile bastola yangu iliangukia sehemu fulani sakafuni na sikuweza kuiona kutokana na giza zito lililokuwa mle ndani, yule mtu nyuma yangu hakunisemesha neno lolote hali iliyozidi kunitia hofu na kunichanganya.

Sasa nilipanga kuchomoa kisu toka kiunoni kwangu, nikaupeleka taratibu mkono wangu kiunoni na kukipapasa kile kisu lakini ilionekana kuwa yule mtu alikuwa akifahamu kila kilichokuwa kikiendelea kwenye mawazo yangu kabla sijatenda, kwani kabla sijafanikisha zoezi hilo sauti ya kilimi cha bastola kilichovutwa nyuma yangu ilipenya masikioni mwangu na kunionya.

Dah! Jasho likazidi kunitoka. Ilibidi nisitishe kile nilichokuwa nikitaka kukifanya na sikuwa na namna nyingine ya kufanya zaidi ya kuanzisha mapambano ya ana kwa ana katikati ya giza lile.

Niliona ningezubaa ningekufa kikondoo, hivyo nilizunguka kwa kasi ya ajabu nikitupa pigo la ngumi usawa wa shingo ya yule mtu aliyekuwa nyuma yangu lakini ilikuwa kazi bure kwani yule mtu alikuwa mwepesi kuishtukia hila yangu, hivyo pigo langu lilikata hewa bila kutoa majibu, nikapepesuka na kupoteza mhimili, na wakati huo huo nilijikuta nikipokea kipigo cha ngumi mbili kavu za haraka haraka tumboni kwangu zilizonifanya nijihisi kutapika.

Kuona vile nikakusanya nguvu kisha nikafanya tukio hatari la kushtukiza, kufumba na kufumbua nilijitupa ukutani na kukita miguu yangu kisha nikarudi nikijitupa kunyume nyume na kumvamia yule mtu nyuma yangu. Kwa nguvu ile niliyoitumia sote tukapiga mweleka na kuanguka chini huku bastola yake ikimponyoka mkononi na kuangukia kusikojulikanana.

Haraka nilijiviringisha kuelekea kando. Yule mtu naye kuona vile alijiviringisha sakafuni kunifuata huku akinitupia mapigo hatari ya mateke katika kunishambulia. Hata hivyo aliambulia patupu kwani mchezo ule wa gizani niliupenda kwa vile ulimpunguzia adui umakini. Niliendelea kujiviringisha hadi kwenye kona ya sebule ile, hapo nikaukita mguu wangu kisha nikajibetua samasoti na kusimama.

Dah! Sekunde ile ile, kabla hata sijapata mhimili vizuri, nilijikuta nikichapwa teke hatari la tumbo lililonivuruga zaidi tumbo langu na kunitupa nyuma. Nikaangukia kwenye kochi moja la sofa pale sebuleni na kulivunja. Maumivu niliyoyahisi muda huo yalikuwa makali sana na yalisambaa haraka mwilini.

Niliwahi kujizoazoa pale chini na kusimama na wakati huo yule mtu alinifikia tena, akatupa ngumi tatu makini kichwani lakini nilizikwepa kama nipo kwenye mchezo wa rede na hivyo zikakata upepo na kumpunguza nguvu. Kuona vile yule mtu alibadili mtindo na kunitupia pigo la kareti lililokuwa litue shingoni, hata hivyo likaishia kunipunyua kidogo huku nikifanikiwa kulikwepa.

Kisha nilikusanya nguvu na kumtandika kichwa kilichotua katikati ya macho na pua yake na kuupasua mwamba wa pua yake, akapiga mweleka. Nikamuwahi pale pale chini na kumchapa teke kali la kwenye korodani na hapo nikamsikia akibweka kama mbwa koko, lakini aliwahi kusimama na kunijia kwa kasi ya ajabu.

Kitu kimoja kilinishangaza kidogo, sauti niliyoisikia haikuwa ngeni kabisa masikioni kwangu. Ilikuwa sauti niliyoifahamu vyema lakini muda huo sikukumbuka ni ya nani.

Wakati nikiitafakari sauti ile nikajikuta nikichapwa pigo hatari mbavuni na maumivu yake yakanifanya niachie mguno mkali wa maumivu. Nikayumba na kurudi nyuma, na kabla sijakaa sawa yule mtu alinichapa teke la kifua lililonitupa chini. Pigo lile la kifuani lilinifanya nihisi maumivu makali sana kifuani kama niliyerushiwa na mfuko wa sementi wa kilo hamsini.

Endelea...
 
utata.JPG

381

Hata hivyo niliwahi kuinuka lakini yule mtu hakutaka kuniacha na mara hii aliongeza kasi zaidi akinijia kwa mapigo ya mateke ya haraka ambayo nilijitahidi kwa kila namna kuyapangua kwa mikono yangu huku mengine nikiyakwepa na kuyaacha yakate hewa.

Niligundua kuwa yule mtu alikuwa anatumia nguvu kubwa sana kurusha mapigo yake akitaraji kumaliza pambano katika dakika za mwanzo tu, na hivyo sasa alikuwa mbioni kuishiwa nguvu. Hivyo nilijitupa sakafuni kumfuata na kabla hajaishtukia hila yangu nikawa nimezungusha mguu wangu sakafuni na kumchota mtama uliompaisha hewani kimo cha mbuzi na kumtupa chini, akatua juu ya meza fupi ya kioo iliyokuwa pale sebuleni na kuivunja vipande vipande.

Yule mtu alikuwa sugu kwani nilimsikia akiishia kuguna tu badala ya kupiga yowe. Ni wakati huo huo nilihisi kuwa alikuwa ameshika kisu alichokichomoa toka kiunoni kwake, nikawahi kujirusha chini na kujiviringisha huku kisu kile kikinikosa na kwenda kukita kwenye mlango.

Hata hivyo kama nisingewahi kujirusha basi kisu alichonirushia kingenipata kifuani. Halafu nilijiviringisha kumfuata katika mtindo wa zigizaga jambo lililomchanganya. Nikamfikia na kumchapa teke la tumbo, akaanguka chini, nikamrukia na kumkaba kabari ya nguvu.

Yule mtu alijitahidi sana kufurukuta huku akinipiga ngumi za tumboni kwa kutumia mkono wake mmoja lakini sikumwachia. Niliendelea kumkaba japokuwa alionekana kuwa na nguvu nyingi sana, hivyo alipoona ngumi zake zimeshindwa kunifanya nimwachie tukaanza kupelekana huku na kule, hata hivyo sikumwachia.

Sikutaka kumpa nafasi ya kuomba poo, niliikaza mikono yangu kisawasawa. Jicho lilimtoka kama mjusi aliyebanwa na mlango, mishipa ya kichwa nayo ilimtuna na jasho likamtiririka. Nilikuwa nimemdhibiti vizuri hivyo akaanza kutupa tupa mikono na miguu yake huku na kule kujitetea lakini sikumwachia.

Alipoona hali imezidi kuwa mbaya alijitutumua na kusimama na mimi huku nimemng’ang’ania shingoni kisha akanibwaga chini. Sote tukaanguka chini lakini bado sikumwachia.

Muda mfupi baadaye nilimwona akianza kuishiwa nguvu na kupunguza kutapa tapa pale sakafuni na hatimaye akatulia kabisa. Sikulegeza ile kabari, niliendelea kumkaba kwa dakika kadhaa na nilipomwachia nilijiviringisha kando huku nikihema kwa nguvu kutafuta pumzi iliyokuwa mbioni kuniishia, hata hivyo nilikuwa makini kumtazama kama alikuwa hai na kama bado alikuwa na nguvu za kupambana, nikauona mwili wake ukiwa umelegea pale sakafuni.

Nilisimama kwa kujikongoja kueleka kwenye swichi ya taa iliyokuwa ukutani, nikaiwasha lakini taa hazikuwaka. Nikatambua kuwa mzimaji wa taa zile alikuwa amezima kwenye swichi kubwa iliyokuwa ikipokea umeme wa nyumba nzima (main switch). Nikarudi kwa yule mtu pale chini alipolala nikimsogelea kwa tahadhari.

Nilimpekua mifukoni lakini sikumkuta na kitu chochote, hata hivyo nilishawishika kutaka kuiona sura yake huenda ningeweza kumfahamu. Nikaanza kuitafuta swichi kubwa iliyokuwa ikipokea umeme wa nyumba nzima na kuikuta kwenye ukumbi mdogo wa chakula. Nikaiwasha, na hapo taa za chini za nyumba ile zikawaka.

Sikuamini macho yangu pale nilipomwona Yusuf Assad Taifa, mkuu wa kikosi cha siri cha ulinzi wa Rais, akiwa amelala sakafuni. Kwa kumtazama tu nilitambua kuwa hakuwa na uhai. Jicho lilikuwa limemtoka kama mjusi aliyebanwa na mlango na ulimi ulikuwa nje.

Halafu nilizifuata zile bastola pale sakafuni, ya kwangu na ile ya Yusuf Taifa, nikaziokota na kuzichomeka kiunoni, kisha nikaanza kupanda ngazi za kuelekea juu kwenye ile ghorofa ya kwanza, huku nikiongeza umakini kwa kuzifuata kanuni zote nilizofundishwa kambini na zile nilizojifunza kulingana na matukio niliyokuwa nimeyapitia.

Nilipofika juu nilijikuta nikitokea kwenye ukumbi (corridor) uliokuwa unatazamana na milango minne. Milango miwili ilikuwa upande wa kushoto na mingine miwili katika upande wa kulia, lakini mlango mmoja ukiwa mwisho kabisa wa ule ukumbi. Katika eneo lile kulikuwa na kiza chepesi kwa sababu taa hazikuwa zimewashwa. Nilitulia pale kwa dakika moja nzima bila kutikisika mwili lakini macho yangu yakifanya kazi kwa kasi mno.

Nilitazama kama kulikuwa na dalili yoyote ya uwepo wa kiumbe hai eneo lile. Kwa ile dakika nzima sikusikia chembe ya uhai eneo lile, lakini kabla sijapiga hatua yoyote, nikiwa bado katika kufikiria nini cha kufanya, nikahisi kuona kivuli kikisogea taratibu. Nikatulia tuli bila kujitikisa hadi nilipohakikisha kuwa uelekeo wa kivuli kile ulikuwa ni katika mlango mmojawapo uliokuwa mwisho wa ukumbi ule.

Nikahesabu hatua hadi ziliposimama, nikainama na kuvua kiatu kimoja cha mguu wa kushoto, nikakitupa pembeni yangu, kikaanguka na kutoa kishindo hafifu mithili ya mtu kutua pale.

Nilifanya vile makusudi, na hapo yule mtu akajitokeza haraka huku akiachia risasi kwenda sehemu ile. Kwangu huu ulikuwa ushindi wala sikutaka kupoteza muda, nikajirusha upesi na kuipiga teke ile bastola yake, na kabla hajapiga kelele nikamdhibiti kikamilifu, akatulia tuli.

Kisha nilimsukuma tukauendea mlango ule wa mwisho, mlango ulikuwa haujafungwa maana nilipousukuma tu ukafunguka na hapo nikamsukumia ndani ya chumba kile huku nami nikijirusha na kutua katikati ya chumba kwa namna ya kumchanganya adui, endapo kungekuwa na adui mwingine amenitegema mtego.

Kilikuwa chumba kikubwa chenye nafasi ya kutosha, kwa haraka haraka niligundua kulikuwa na madirisha mapana mawili ya vioo yaliyokuwa yamefunikwa kwa mapazia marefu na mepesi. Dirisha moja lilikuwa limeungana na mlango uliokuwa unatokea kwenye kibaraza cha ghorofani (terrace).

Upande wa kushoto ukutani kulikuwa na kabati kubwa la nguo la ukutani na kando ya kabati lile kulikuwa na meza nzuri nyeusi ya kioo. Juu ya meza hiyo kulikuwa na seti moja ya runinga bapa katikati ya spika mbili za mfumo wa kisasa wa muziki (music system).

Katikati ya chumba kulikuwa na kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita chenye nakshi nzuri za kupendeza na kilitandikwa shuka nyekundu yenye maua meupe na alama za kopa. Upande huo wa kulia kulikuwa na mlango mwingine ambao niliutambua kuwa ulikuwa mlango wa kuingilia bafuni.

Pia kulikuwa na kochi moja kubwa la sofa la kisasa juu ya zulia zuri lenye rangi za ngozi ya Pundamilia. Mbele ya kochi hilo kulikuwa na meza ndogo ya mbao iliyokuwa na umbo la nusu duara. Juu ya ile meza kulikuwa na kibakuli kidogo cha majivu ya sigara, kibiriti kimoja cha gesi, kasha tupu la miwani ya macho na simu ya mezani.

“Rais yupo wapi? Jibu moja tu sihitaji maelezo,” niliunguruma huku sauti yangu ikiwa si ile ya kubembeleza, huku nikimkwida. Nilimtambua yule mtu, alikuwa mwanadada mmoja wa walinzi wa mke wa Rais na aliitwa Monica. Mwanadada ambaye kuna wakati aliwahi kutumwa na mke wa Rais anifikishie ujumbe fulani.

“Sijui, kama umeshindwa kumtafuta huko unakuja kuniuliza mimi!” Monica alinijibu kwa jeuri.

Endelea...
 
utata.JPG

382

Nilimchapa kibao kikali usoni, akaachia kilio kilichoambatana na maneno ya kujitetea kuwa yeye hajui lolote.

“Aliyekufundisha kuwa sugu hata mimi alinifundisha hivyo hivyo kwamba nisiseme ukweli mpaka nikione kifo sekunde moja kutoka katika uhai wangu… sasa…” nilisema na kusita kidogo nilipohisi kulikuwa na mtu mwingine mle chumbani, mara nikasikia sauti ikiniamuru.

“Tulia hivyo hivyo, ukitikisika tu napasua kichwa chako!” ilikuwa sauti ya ukakamavu ya kike ikiunguruma nyuma yangu. Ilikuwa ni sauti niliyoifahamu vyema.

Sikuwa na muda wa kubashiri alikuwa ni mwanamke gani isipokuwa kwa haraka nilijaribu kuupima umbali uliokuwepo kati yangu na mzungumzaji huyo, nikagundua kuwa alikuwa nyuma yangu kwa umbali wa takriban mita mbili na nusu tu hivi. Niligundua kuwa wakati tunaingia mwanamke huyo alikuwa amejificha bafuni na sasa alikuwa amesimama kwenye mlango wa kuingilia bafuni.

Nilikuwa makini sana kumtazama Monica aliyekuwa mbele yangu kuliko kumzingatia yule mwanamke aliyekuwa amesimama nyuma yangu. Sasa sikuwa nikiogopa kifo katika harakati zangu kwani kama ni vifo nilikuwa nimeviona vingi vya ajabu ajabu tena vingine vikipitia mikononi mwangu. Hivyo kifo hakikuniogopesha tena, nilijua kuwa ipo siku moja ningekufa tu, lakini kifo cha kizembe nilipingana nacho na hivyo nilitulia kimwili lakini si kiakili.

Nilijua kuwa yule mtu nyuma yangu alikuwa amenielekezea bunduki, na siku zote muuaji anayemaanisha huwa haelekezei bunduki miguuni, bali kichwani ama maeneo ya moyo. Nikiwa nimetulia lakini akili yangu ikiwa makini nilikuwa nikisubiri amri, na kama yule mtu nyuma yangu angeitoa ingekuwa ndiyo nafuu yangu. Wala haikuchukua sekunde tatu ikawa kama nilivyowaza!

“Tupa bastola yako chini na usithubutu kufanya hila yoyote… kisha nyanyua mikono yako uiweke kisogoni!” ile sauti kakamavu ya kike iliniamuru. Safari hii ilikuwa imesogea karibu zaidi, nyuma yangu.

Kwa mwanadamu wa kawaida hii amri ilikuwa nzito na huwezi kuwa na ujanja tena lakini si kwangu na watu wa kariba yangu. Niliidondosha bastola yangu mguuni huku nikijifanya kama nanyanyua mikono yangu na sekunde ile ile nikachomoa kisu toka kiunoni na kugeuka kwa kasi huku nikikirusha kumwelekea yule mwanamke, na wakati huo huo nikiinama.

Yule mwanamke alikuwa mwepesi kukikwepa kile kisu na wakati huo huo alifyatua bastola yake kwa papara, risasi zikatoka na kukisambaratisha kifua cha Monica aliyekuwa mbele yangu.

Bila kuchelewa teke langu matata lilitua kwenye mkono wa kushoto wa yule mwanamke ulioshika bastola na kufanikiwa kumpokonya ile bastola, ikadondoka sakafuni. Tukabaki tunatazamana. Alikuwa mrefu aliyekuwa amevaa tracksuit nyeusi na kofia nyeusi ya pama kichwani. Nilipomwona tu nikathibitisha kuwa ni kweli alikuwa mwanamke… si mwanamke tu bali mke wa Rais… Mama Juliana Isidory Masinde!

Alikuwa na umbo refu lililovutia sana. Alikuwa mweupe kwa rangi ya ngozi yake, rangi ambayo ilikuwa na mng’aro wa aina yake na ilipendeza sana, ikiwa na weupe wa asili na wenye mvuto wa pekee kiasi cha kumfanya aonekane bado msichana mbichi tofauti na umri wake.

Macho yake, dah… yalikuwa ni yale macho yanayoita kwa mng’aro sadifu lakini yaliyoonya kama simba jike mwenye watoto, yakiambatana na kope nyingi nyeusi ambazo ziliachia nafasi kwa nyusi ili zipate kujidai. Pua yake ilikuwa ndogo na ndefu, ya Kitutsi, na midomo yake ilikuwa minene yenye kingo nyepesi na mikunjo midogo midogo.

Mara nyingi sauti yake ilikuwa ya upole kila alipoongea. Lakini sasa nilitambua kuwa mwanamke huyu alikuwa mpole sana na mkarimu kwa kumtazama tu lakini alikuwa na roho saba. Roho ngumu kama ya paka…

Japo nilishafahamu nini kilikuwa kinaendelea kuhusu jamii ya siri ya Triangle lakini hiyo haikunifanya nisistaajabu kumwona mke wa Rais pale na muda ule, nikiwa bado katika mshangao nilishtukia nikitandikwa teke la tumbo na kurushwa ukutani. Nilipotaka kunyanyuka Mama Masinde alinitandika tena teke la tumbo na kunifanya nijisikie kutaka kutapika.

Na hapo nilijikuta nikizidi kushangazwa sana, sikushangazwa kwa namna alivyoweza kunipiga mateke ya ufundi bali sikuamini kama mwanamke huyo alikuwa na uwezo wa kupambana na mtu kama mimi niliyepitia shuluba ngumu, achilia mbali kumpiga kijana wa mtaani.

Kitu kingine kilichonishangaza ni namna akili yangu ilivyoanza kuwa nzito ghafla katika kufanya maamuzi tangu nilipomtambua, muda mwingi nilijikuta nikimfikiria yule mama badala ya kupambana. Ndiyo maana pigo lingine la teke lilipokuja lilitua kifuani likanirusha tena hadi ukutani.

Sasa akili yangu ikazinduka ghafla toka kwenye mduwao uliokuwa umenishika tangu nigundue kuwa nilikuwa napambana na mke wa Rais. Nilikusanya nguvu na kumrukia yule mama mtata lakini kumbe alikuwa tayari ameishtukia hila yangu hivyo akawahi kuniepa kwa kujisogeza kando.

Kisha alinisindikiza na teke la mgongoni lakini nami nilimshtukia mapema na kulikwepa teke lake huku nikiudaka mguu wake, akagundua kuwa sekunde iliyokuwa ikifuata nilikuwa naenda kuuvunja mguu huo.

Upesi akajipinda na kurusha mguu mwingine uliobaki chini na kunipiga teke la mbavuni, sote tukapiga mweleka. Kisha yule mwanamke aliwahi kujiinua kwa samasoti, nami nikajiinua na kujitanua na kuchana msamba halafu nikajizungusha na kumchota miguu yake, nikamsomba hadi chini. Yule mama alitokwa na yowe la maumivu, lakini upesi alisimama na hatimaye tukawa tunatazamana ana kwa ana.

Haikuwa mara ya kwanza kutazamana na mwanamke yule kwa namna tulivyotazamana. Mara ya kwanza ilikuwa ni pale katika viwanja vya Ikulu ya Dar es Salaam siku nilipoitwa na Rais Albert Masinde ili kupewa tuzo maalumu ya ushujaa uliotukuka, nikiwa na wenzangu wawili, Luteni Lister na Pamela Mkosamali.

Hii ilitokana na kukamilisha operesheni hatari iliyofanikisha kuufichua mtandao hatari wa kigaidi katika mkasa uliopewa jina la ‘Taharuki’. Siku hiyo tulipogonganisha macho yetu, japokuwa ilikuwa ni kwa sekunde moja tu ya kutazamana, nilijikuta nikisisimkwa sana mwili wangu kwa sababu nilitambua kuwa nilikuwa natazamana na mwanamke ambaye si wa kawaida kabisa!

Nilihisi moyo wangu ukipiga kite kwa nguvu maana nilikuwa naangaliana na macho ambayo sikuwaza kuyaona kwa mtu wa aina yake. Yalikuwa kama ya simba jike mwenye watoto aliyeghadhabika na yalikuwa yanatoa cheche!

Hata hivyo siku hiyo sikupoteza muda wangu kumfikiria mwanamke yule na badala yake nilirudi kwenye kiti changu kuketi. Nilikuja kushangazwa baadaye wakati tukiondoka pale Ikulu mara Monica, mlinzi aliyekuwa amepewa jukumu la kumlinda mama huyo, aliponifuata na kuniambia; “Mama anasema nikwambie amependa macho yako ulivyomwangalia…”

Maneno yale yaliniweka katika bumbuwazi, sikutarajia kusikia maneno ya aina ile kutoka kwa mke wa Rais, tena yakitamkwa na mlinzi wake!

Endelea...
 
utata.JPG

383

Hata hivyo, kwa Monica aliyetumwa, ujumbe huu ulikuwa na maana ya kawaida ya kuwa mama yule alikuwa amenitamani kimapenzi ndiyo maana akatuma ujumbe ule, na mwanadamu yeyote yule wa kawaida angeweza kuutafsiri ujumbe huu moja kwa moja vile vile, lakini kwa mwanadamu asiyekuwa wa kawaida huu ulikuwa ujumbe mzito sana.

Naam! Nami sikuwa mwanadamu wa kawaida! Niliielewa maana ya mtu wa kariba yangu kusema ameyapenda macho yangu nilipomtazama, hii ilimaanisha kuwa mtu huyo aliutambua uwezo mkubwa niliokuwa nao ndani yangu wa kumsoma mtu na hivyo alitamani kuwa karibu nami kwa ajili ya kupata ulinzi, au kama ni adui basi alitamani tukabiliane!

Wakati huo sikuwa nimemchukulia mama huyo kama adui, nilimwona ni first lady anayempenda na kumheshimu mumewe, na zaidi ya yote akiipenda sana nchi yake. Sasa leo tukiwa ana kwa ana, nilipata tena nafasi ya kuyaona macho yake yaliyokuwa kama ya simba jike anayewinda na ambaye alikuwa tayari kunirarua. Yalikuwa yanatoa cheche!

Sasa hapakuwa na muda wa maongezi bali shughuli kwa kwenda mbele, tulipaswa kuoneshana nani zaidi, kati yangu ambaye nilikuwa na jukumu la kumkomboa Rais wa Nchi au mwanamama yule aliyefanya kila liwezekanalo kuhakikisha anatimiza haja ya mabwana zake wa jamii ya siri ya Triangle.

Wakati nikiamini kuwa nilikuwa mpelelezi mashuhuri niliyepitia mafunzo makali ya kijasusi nchini Misri na kuanza kazi zangu kivitendo kule ufukweni Mombasa, nchini Kenya, nikiwa na umakini wa hali ya juu huku nikizifuata kanuni zote nilizofundishwa kambini na zile nilizojifunza kulingana na matukio niliyoyapitia, sikujua mwanamke yule alipatia wapi mafunzo yake!

Hata hivyo, macho yake tu yalidhihirisha kuwa alikuwa ni mtu hatari sana zaidi ya vile nilivyomfikiria. Kama ni ujasusi basi alikuwa amefunzwa akafunzika!

Wakati mawazo hayo yakipita haraka kichwani kwangu, kwa kasi ya ajabu nilishtukia nikipigwa teke la kichwa na pigo hilo likanifanya nisiweze kuona vizuri mbele yangu. Hofu ikaniingia na kuhisi kuwa dakika zangu za kubaki duniani zilikuwa zikihesabika.

Nikiwa bado najihisi kuchanganyikiwa nilikusanya nguvu na pigo jingine la teke lilipokuja niliwahi kulidaka kabla halijanifikia tumboni kisha nikauzungusha mguu wa yule mama kwa nguvu na kwa kasi ya ajabu na bila upinzani nikafanikiwa kuutengua mfupa wake wa goti na hapo yule mama akapiga yowe kali la maumivu.

Alipoanguka chini mfupa wa goti lake ulikuwa tayari umevunjika, nikawahi kunyanyuka kwa kupiga samasoti ya chini na kumfuata lakini wakati nikifanya hivyo nilisita pale nilipojikuta nikitazamana na mtutu wa bastola yake mkononi. Alikuwa ameshika bastola yenye kiwambo cha kuzuia sauti.

“Ulidhani utashinda kirahisi! Unajidanganya bure, kijana…” mwanamama yule alizungumza huku akicheka.

Niliipima sauti yake nikagundua kuwa ilikuwa mbali na mzaha. Sasa jasho jepesi la hofu likaanza kunitoka maana nilikuwa nimeingia kwenye mtego ambao kwa akili za kibinadamu nisingeweza kujinasua kirahisi, hivyo akili yangu ilianza kufikiria haraka namna ya kujinasua.

“Kama ni vita umeshinda, lakini niambie kwa nini umeamua kuisaliti nchi yako?” nikamuuliza yule mama huku nikitabasamu.

That’s non of your business!” yule mama alifoka kwa hasira huku akinitazama kwa umakini usoni. Macho yalikuwa bado yanatoa cheche.

So, what kind of a business are you doing?” nilimuuliza kwa utulivu.

Yule mama akaangua kicheko kilichonishangaza, lakini ghafla kicheko chake kilikoma huku sura yake ikiwa mbali na mzaha. Tabia yake hii ikaanza kunichanganya.

“Mbona hutaki kunijibu swali langu, mama?” nilimuuliza, akanitazama kwa utulivu na uso wake haukuonesha tashwishwi yoyote.

“Tayari umechelewa kwani hata nikikujibu hutofanikiwa kufika na majibu hayo kokote,” yule mama aliniambia huku akibinua midomo yake kwa dharau.

“Una maanisha nini?” nilimuuliza kwa utulivu.

“Umefanya makosa sana kukubali kazi hii, na mbaya zaidi kuja hadi humu ndani,” yule mama alisema. Nikazidisha tabasamu usoni kwangu. Na hapo akaongeza, “Na kama unadhani nakuongopea umekosea sana kwani huu ndiyo mwisho wako na habari zako zitaishia humu ndani.”

Nilimtazama yule mama kwa umakini huku nikijaribu kumpigia hesabu kali namna ya kumpokonya ile bastola. Hata hivyo alikuwa makini sana kuchunguza kila hatua niliyotaka kuchukua.

“Nilikutumia ujumbe siku unapewa tuzo pale Ikulu nikadhani labda una akili ya kuupambanua… kama ungekuwa umeniomba ushauri huenda ningekushauri usijiingize kwenye harakati hizi ila kwa sasa nafasi hiyo huna. Huu ni mtandao mkubwa sana usioweza kuvunjwa kwa urahisi na hivyo vijiharakati vyenu,” yule mama alisema kwa nyodo.

“Najua wewe ndiye Chameleon, sasa niambie Tiger ni nani?” nilimuuliza yule mama huku nikianza kupiga hatua kumfuata.

Shut up your mouth, you bastard!” yule mama alifoka huku akipeleka kidole chake cha shahaada kwenye kifyatulio tayari kufyatua risasi.

Hisia zangu ziliniambia kuwa sasa hakutaka tena masihara, alidhamiria kuniua, nikajirusha haraka pembeni na wakati huo huo risasi mbili alizozifyatua moja ilipita karibu kabisa na sikio langu ikapasua kioo cha dirisha na risasi nyingine ikachimba ukuta na hapo nikajua kuwa kweli yule mama alikuwa amedhamiria kuniua.

Nilijirusha tena nikadondokea nyuma ya kitanda wakati yule mama akiendelea kufyatua risasi ovyo mle ndani akinilenga, lakini nilikuwa mwepesi wa kujirusha upande huu na ule na hapo risasi moja ikanipunyua begani.

Sasa nilikuwa nakabiliwa na hatari kuliko wakati mwingine wowote. Sikuwa na namna, nikainua kitanda ili kujikinga na mashambulizi yale huku nikiupeleka mkono wangu haraka kuichomoa ile bastola ya Yusuf Taifa niliyoiokota kule sebuleni. Nikaikamata sawa sawa na kuanza kutafuta upenyo mzuri wa kucheza naye.

Mara mlango wa kile chumba ukafunguliwa kwa kasi ya ajabu, na sote tukashtushwa na tukio lile. Ni wakati huo nilimwona mwanamume mrefu mwenye mwili wa kimazoezi akiwa amevaa mavazi ya kimchezo, tracksuit ya bluu ya timu ya taifa pamoja na viatu vyepesi vya mazoezi akiruka kwa namna ya kininja na kutua kando kabisa ya chumba huku akielekeza bastola yake kwa yule mwanamama.

“Weka silaha yako chini!” yule mwanamume alimwamuru yule mama. Mara moja nikaitambua sauti yake. Alikuwa ni Askofu Masinde. Hata yule mama pia alimtambua Askofu Masinde.

“Bishop!” yule mama alimaka kwa mshangao. Alitoa macho ya woga na mashaka.

“Weka silaha yako chini sasa hivi!” Askofu Masinde alisisitiza huku uso wake ukionesha kuwa hakuwa na mzaha hata chembe.

“Bishop, kwani na wewe u…?” yule mama alitaka kuuliza swali lakini akasita. Hata hivyo hakutaka kutii amri, na wala hakutaka kushindwa.

Kwa kuyatazama macho yake tu nilitambua kuwa sasa alipanga kuhamishia mkono wake wenye silaha kwa Askofu Masinde lakini asiwe mwepesi vya kutosha. Askofu Masinde alimuwahi na kumshindilia risasi moja ya bega!

Asiridhike, akataka kufurukuta tena, sasa ikamlazimu Askofu Masinde atumie risasi nyingine kumnyamazisha kabisa. Risasi hiyo ilitoboa shingo ya mama yule na kumlaza akiwa hoi bin taaban chini. Alikuwa anavuja damu kupita kiasi. Mkono wake wa kushoto uliokuwa umeshika bastola sasa ulishikilia jeraha lake.

Japokuwa alikuwa ni mtu mdhalimu aliyekaribia kuligharimu taifa lakini alitia huruma. Kinywa chake kilikuwa kinatema damu nyingi kwa mtindo wa kwikwi! Mara akakata pumzi.

“Jason, umesalimika?” Askofu Masinde aliniuliza kwa wasiwasi huku akigeuka kunitazama.

“Nipo salama kabisa, mjomba… umejuaje kuwa nipo hapa?” nilimuuliza Askofu Masinde swali la kijinga huku nikimkazia macho. Akacheka kidogo.

“Umesahau kuwa mimi pia ni mwanausalama mwenye mbinu zote za kijasusi? Anyway, hatuna muda… Daniella anakuhitaji haraka, ameshagundua mahali alipofichwa Rais,” Askofu Masinde alinisihi.

I see! Lakini hapa pia panatakiwa kufanyiwa ukaguzi na kuwekewa ulinzi kabla hatujaondoka…” nilisema lakini Askofu masinde alinikatisha.

“Twende nikupeleke ukamsaidie Daniella, wanausalama watafika hapa wakati wowote. So, the whole thing here is under control from now on,” Askofu Masinde alisema na kuanza kuondoka. Kisha alinihimiza, “Upesi! Upesi, Jason! Tunachelewa…”

Niliitazama saa yangu ya mkononi, nikagundua kuwa ilishatimia saa kumi na mbili kasoro dakika moja za asubuhi. Nikautazama mwili wa Mama Juliana Masinde kwa uchungu mkubwa, kisha nikaziokota bastola na kutoka nikimfuata Askofu Masinde kule nje.

Wakati natoka kupitia mlango wa jikoni nikajikwaa, nilipotazama chini nikakaiona chombo fulani hivi ambacho ukikitega sehemu hutoa mwanga mithili ya mlipuko wa umeme. Mara nyingi hutumiwa kumchanganya adui. Nikakiokota na kutoka haraka.

Nilimkuta Askofu Masinde nje kabisa, mtaani, akiwa ana-trot, nikamkimbilia mpaka tukafikia mahali alipoegesha gari lake aina ya Toyota Landcruiser GX V8 la rangi nyeusi. Tukajipakia garini, halafu Askofu Masinde akaliondoa gari lake kwa mwendo wa kasi. Magurudumu yalizunguka kwa kasi sana na kuchimba ardhi wakati akiliondoa lile gari.

* * *

Endelea...
 
utata.JPG

384

Siku ya mavuno…




Saa 12:05 alfajiri…

ASKOFU Masinde alilisimamisha gari lake katika eneo la karibu na Bandari ya Mtwara, Barabara ya Bandari. Toka pale aliposimamisha gari lake, alinionesha mtaa uliokuwa na maghala (godowns) ya kuhifadhia mizigo, umbali wa kama mita mia mbili hivi.

“Nenda ghala lililopo katika kitalu namba 164… mimi narudi kule Mtaa wa Skoya kuungana na wanausalama wengine, kisha tukakuja hapa,” Askofu Masinde alisema kisha akaongeza, “Ila kuwa makini.”

Mara moja nikakumbuka ule ujumbe ulioandikwa kwa codes: ‘N-23 - 11:00. G-WH.164. Farmstead is occupied of weeds, wheat must be reaped instantly.’ Wakimaanisha kuwa Shamba liliingia magugu, ngano ilipaswa ivunwe haraka mnamo Novemba 23, saa tano kamili asubuhi, kwenye ghala lililopo katika kitalu namba 164.

Toka umbali wa mita mia mbili lilikosimamishwa gari, niliweza kushuhudia geti likifunguliwa na magari mawili, yote yalikuwa aina ya Jeep Wrangler ya rangi nyeusi yakaingia na geti likafungwa tena. Nilijua ni katika ghala lile ndiko ningeweza kupata majibu ya maswali yangu. Nililiangalia ghala lile kwa hasira wakati nikichukua simu yangu, nikatafuta namba maalumu za Kanali Mjaka na kupiga.

“Hallo! Nipe taarifa za maendeleo!” sauti nzito ya Kanali Mjaka iliita.

“Tumeshagundua mahali alipofichwa Rais, Daniella tayari yuko ndani ingawa sijui kama yupo salama. Mimi ndiyo najiandaa kuingia.” Nilimwambia Kanali Mjaka kisha nikakumbuka kumuuliza. “Vipi tayari timu ya kuja kusaidia imeshaondoka huko?”

“Tayari tupo Mtwara, nipe uelekeo,” Kanali Mjaka alisema.

“Eneo la Bandari ya Mtwara, ghala lililopo kwenye kitalu namba 164. Sina muda mrefu wa kuongea na wewe… nitakujulisha baada ya muda si mrefu, ila ikipita nusu saa sijapiga simu basi ujue hali ni tete,” nilimwambia kisha nikakata simu bila kumpa nafasi ya kuuliza kitu chochote.

Akili yangu ilikuwa imenituma kwamba asubuhi hii ni lazima kuna jambo lingetokea. Nililitazama geti la ghala lile lililokuwa limefungwa, nikawa natembea kuliendea ghala lile kama mpita njia tu. Hali ya mahala pale ilikuwa ya ukimya kabisa.

Nikiwa umbali wa kama mita hamsini hivi, niligundua ugumu uliokuwepo katika kuingia ndani ya ghala lile. Ukuta uliolizunguka ulikuwa mrefu na isitoshe ulizungushiwa nyaya maalumu za usalama. Iwapo ningejaribu kuigusa hata nyaya moja basi ningekuwa nimeharibu kila kitu.

Nilikuna kichwa ili kuangalia ni jinsi gani ningeweza kuingia mle ndani. Wakati nikikuna kichwa ili kupata namna ya kuingia mle ndani, nikasikia muungurumo wa gari. Haraka nikajibanza katika mti mmoja mkubwa ili nisionekane iwapo magari yale yangekuwa yakija upande ule. Kama nilivyotabiri kulikuwa na magari mawili, yote aina ya Jeep Wrangler ya rangi nyeusi yalikuwa yakielekea katika ghala lile.

Hali ile ikanifanya nizidi kupatwa na tashwishwi ya kutaka kujua ni akina nani waliokuwa wakiwasili na nini kilichokuwa kinaendelea ndani ya lile ghala. Lile geti lilifunguliwa na kuyaruhusu magari yale kuingia ndani. Kwa kuwa sikuwa mbali sana na geti niliweza kuona ndani.

Kulikuwa na magari kadhaa, yote ya kifahari yaliyojipanga lakini sikuweza kuona mtu yeyote zaidi ya watu wawili walioonekana kuwa walinzi wa eneo lile, waliobebelea bunduki za kivita wakiwa wamesimama mlangoni. Kwa kuwaona tu nilitambua kuwa walikuwa makomando. Kisha lile geti likafungwa tena.

Mara moja nikapata wazo. Nikaangaza macho yangu huku na huko kutazama kama kulikuwa na kamera yoyote ya ulinzi, nikaziona. Nilichofanya ni kutoa simu yangu ya mkononi iliyokuwa na mfumo maalumu wa TracerMark na kuingiza codes kadhaa, nikibofya hapa na pale nikiwa na wazo moja tu, la kuzidukua zile kamera.

Ilinipa shida kidogo kuweza kuzidukua zile kamera kwani codes zilikuwa ngumu, ilikuwa ni lazima uingize mchanganyiko wa namba kadhaa ndipo uingie kwenye mfumo wa kamera zile. Hata hivyo, nilikuwa mtundu sana wa kucheza na vitu vya aina ile, na baada ya kucheza nazo kwa takriban dakika tano hatimaye nilifanikiwa kuingia kwenye mfumo wa kamera za ulinzi za ghala lile. Nikawa na uwezo wa kuzidhibiti kutokea kwenye simu yangu ya mkononi.

Niliyatazama mandhari ya mle ndani ya uzio wa ghala, nikawaona walinzi watatu na jinsi walivyokuwa wamesimama, kisha nikachagua upande mzuri ambao nilipaswa kuingilia, upande ambao haukuwa na ulinzi isipokuwa kamera za usalama ambazo tayari niliweza kuzidhibiti kwa kutumia simu yangu ya mkononi. Nilichofanya ni kuzisimamisha zile kamera ili zisiendelee kurekodi picha.

Halafu kwa hatua za kunyata niliikaribia nguzo moja ya umeme huku nikiichomoa bastola yangu yenye kiwambo cha kuzuia sauti, nikaachia risasi mbili na kuzikata nyaya zilizokuwa zinapeleka umeme katika ghala lile. Ghafla taa zote katika ghala lile likazimika. Japokuwa kulishapambazuka lakini nilikuwa nikiihitaji hali ya kiza kama kile.

Kama umeme nilikimbia na kuelekea katika ukuta ule mrefu. Ulikuwa ni ukuta mrefu kuupanda, lakini siku zote niliamini kuwa Mungu alikuwa upande wangu kwani hatua chache toka nilipokuwa nimesimama pembeni ya ule ukuta niliona viroba vingi vya mchanga na kokoto vilivyopangwa.

Kwa kasi ya ajabu nilirudi nyuma na kukimbia, kwa kasi ile ile nilisimama juu ya vile viroba na kuuparamia ukuta ule. Sekunde chache zilizofuata nilikuwa juu ya ukuta, nikajirusha kuelekea ndani na kutua pasipo kutoa kishindo, huku macho yangu yakiwa makini kuangaza upande ule niliokuwepo, sikuona mtu yeyote.

Halafu nilijibanza nyuma ya mti mdogo uliokuwa karibu. Mara taa zote zikaanza kuwaka na hapo nikaanza kusikia muungurumo wa jenereta upande wangu wa kulia. Hata hivyo walikwisha chelewa kwani tayari nilikwisha jitoma ndani.

Nikiwa pale chini nilitumia takriban dakika mbili hivi kuisoma hali ya usalama wa mle ndani. Niliweza kumwona komando mmoja akizunguka zunguka eneo lile, alikuwa na bunduki ya kivita akiwa katika jukumu la kuhakikisha ulinzi unaimarishwa. Nilipomtazama vizuri nikagundua kuwa alikuwa ni mmoja wa wale makomando niliowaona pale getini wakati magari yakiingia.

Toka pale nilipokuwa nilitambaa kwa tumbo kuelekea kwenye maegesho ya magari. Kisha nilitambaa chini ya uvungu wa magari nikaelekea mahala ulipokuwapo mlango mkubwa wa kuingilia ndani ya ghala lile. Sikuweza kuonekana kiurahisi kwa sababu magari yalikuwa yamekaribiana sana.

Hata hivyo shughuli ilikuwa ngumu sana, sikuweza kuvuka eneo lile kiurahisi kwa kuwa nilifahamu kuwa kulikuwa na makomando watatu wenye silaha za kivita. Mmoja akiwa getini na mmoja alikuwa akizunguka eneo lile. Hata hivyo yule komando wa tatu sikumwona!

Nikiwa pale kwenye uvungu wa gari niliutazama mlango wa kuingilia ndani ya ghala lile kwa uchungu, mara nilimwona komando wa tatu akilinda mlangoni. Nilihitaji kuingia ndani ya ghala lile kwa kupitia ule mlango uliokuwa ukilindwa lakini sasa namna ya kuingia mle ndani ndiyo ilikuwa shida. Kwa haraka haraka nilielewa kuwa ili kuingia ndani nilipaswa kupambana na makomando watatu, wote wakiwa na silaha.

Mara nikapata wazo. Nikatambaa tena kwa tumbo kurundi nyuma kisha nilitoa kile chombo ambacho ukikitega kinatoa mwanga mithili ya mlipuko wa umeme, nikakiweka chini ya gari. Lengo lilikuwa ni kuwaondoa wale makomando pale mlangoni.

Endelea...
 
utata.JPG

385

Hata hivyo kabla sijaondoka eneo lile nilijikuta nikipigwa na kitako cha bunduki katika eneo la chini kidogo ya shingo yangu, nikahisi maumivu kwenye uti wa mgongo. Sikuzubaa kwani niligeuka na konde zito lililotua kwenye shavu la yule mtu aliyenipiga. Hakuwa amejiandaa na shambulio lile hivyo konde langu lilimpeleka chini.

Sikutaka matata mengi, niliachia risasi moja yenye shabaha makini kwenye moyo wake, nikampatia usingizi wa milele pasipo hata kuomba maji. Halafu nikauburuta haraka mwili wa yule mtu na kuuficha chini ya uvungu wa gari huku macho yangu yakiwa makini kulikagua eneo lile.

Kama nilivyokuwa nimepanga, muda ule ule chombo kile nilichokitegesha kilianza kutoa mwanga mithili ya ule unaotokea pindi panapokuwa na shoti ya umeme. Hali ile ikawavuta wale makomando wawili, walikuja haraka wakidhani kwamba kulikuwa na hitilafu katika moja ya magari.

Wote wawili waliinama chini ya uvungu ili kuangalia kulikuwa na nini. Hii ndiyo fursa niliyokuwa nikiisubiri. Kwa kutumia bastola yangu yenye kiwambo cha sauti niliwachapa risasi zilizofumua vichwa vyao na kuwapa pumziko la milele.

Haraka haraka nilichukua bunduki moja na kisha nikawasukumia wale jamaa katika uvungu wa magari, halafu nikaondoka na kuelekea mlangoni. Pale mlangoni nilisimama kwa sekunde chache na kuangalia kama kulikuwa na mtu yeyote ambaye angeweza kuzusha udadisi kwangu. Sikuona mtu yeyote aliyenitilia shaka.

Nilipohakikisha mahala pale ni shwari, nikakinyonga kitasa na mlango ukafunguka. Taratibu nikaingia ndani na kuufunga tena mlango bila kutoa ukelele. Na hapo nikajikuta nikitokea katika varanda kubwa iliyojengwa mfano wa sehemu ya mapokezi, lakini hakukuwa na mtu.

Varanda ile ilijengwa kuelekea upande wa kushoto, na kwenye eneo lile la kushoto kulikuwa na mlango mkubwa wa kioo cheusi kisichoonesha mle ndani, nikaufuata mlango ule kwa tahadhari na kuufungua.

Na hapo nikakutana tena na varanda nyingine, ila hii ya pili haikuwa kubwa sana kama ile ya kwanza ila nayo ilijengwa katika mfumo wa mapokezi na ilielekea upande wa kulia. Hatua sita kutoka pale nilipokuwa nimesimama niliona ukumbi mwingine mpana. Nikaufuata ukumbi ule kwa tahadhari na kugundua kulikuwa na milango miwili, huku na huku.

Wakati nikiangaza angaza ili nijue wapi pa kwenda nikasikia sauti za watu wakija eneo lile. Haraka haraka nilirudi nyuma nikajibanza chini ya meza ya mapokezi pale kwenye varanda ndogo. Na hapo nikawaona watu wawili waliovalia suti nzuri za kijivu wakipita haraka jirani na pale nilipojificha na kuelekea kule nilikotokea.

Nikapatwa na wasiwasi nikihisi muda wowote mambo yangeanza kwenda mrama endapo wangegundua kuhusu kile kilichotokea kule nje kwa wenzao na kisha kutoa taarifa kule ndani, hapo kila kitu kingeharibika.

Mapigo ya moyo wangu yalikuwa yanakwenda haraka mno na moyo kudunda kwa nguvu mno huku wasiwasi mwingi ukiwa umenijaa moyoni, maana sikujua Daniella alikuwa wapi na alikuwa na hali gani. Hata hivyo, sikutaka kurudi nyuma. Niliamua kusonga mbele… liwalo na liwe!

Baada ya wale maofisa kupotea kabisa nikaibuka toka pale mafichoni. Na kwa haraka nikaifuata ile njia ambayo wale jamaa walitokea, katika ule mlango wa kushoto uliokuwa na maandishi ‘Official Operatives Only’, yaani ni wafanyakazi walioidhinishwa tu ndio waliotakiwa kuingia humo.

Ule mlango ulikuwa wazi. Nilisimama pale mlangoni huku nikiwa makini, sikusikia sauti ya mtu yeyote mle ndani, nikanyata na kuzama ndani huku nikiurudishia ule mlango nyuma yangu. Hali ya hewa nyepesi ilinifanya niyatembeze macho yangu mle ndani na hapo nikakiona kiyoyozi kimoja ukutani.

Niligundua kuwa nilikuwa ndani ya chumba kipana chenye mitambo kadhaa ya kielektroniki mfano wa studio ya redio. Pia chumba kile kilikuwa kinatumika kuongoza tarakilishi kubwa mbili zilizounganishwa na mfumo wa kamera za usalama na ukutani kulikuwa na runinga tatu pana, zote zilikuwa zikionesha alama ya 'Remote Procedure Error' yaani kulikuwa na hitilafu katika kuingia kwenye mfumo wa mawasiliano.

Mara moja nikatambua kuwa hali ile ilisababishwa na kazi yangu ya udukuzi wa zile kamera za usalama, ambazo sasa niliweza kuziendesha kupitia simu yangu ya mkononi.

Kulikuwa na meza kubwa mbili na viti kadhaa vya kiofisi, na kwenye kiti kimoja mbele ya zile tarakilishi nilimwona mwanamume mmoja aliyevaa suti nadhifu ya rangi nyeusi akiwa ameketi kwa utulivu, sikuwa na hakika kama alikuwa anafanya kazi au alikuwa amesinzia ila alipohisi uwepo wa mtu mle ndani akageuka haraka na kunitazama kwa mshangao. Alikuwa mrefu mweusi na mwenye mwili uliojengeka kwa mazoezi.

“Habari yako?” nilimsalimia yule mtu huku nikiupuuza mshangao wake.

“Nani aliyekuruhusu uingie humu wewe?” yule mtu aliniuliza huku akinitazama kwa wasiwasi.

“Nahitaji msaada wako tafadhali,” niliongea kwa sauti ya utulivu huku nikipiga hatua zangu taratibu kusogea pale alipokuwa ameketi. Kitendo changu kilimfanya yule mtu anikate jicho kama mtu anayetafuta hakika ya maneno yangu na wakati huo huo akiupima utimamu wa akili yangu.

Haraka sana alinyanyuka huku akichomoa bastola yake toka kiunoni. Mara nikajikuta nikitazamana na mdomo wa bastola yake yenye uchu iliyoshikwa vyema mkononi.

“Tulia hapo hapo, hatua moja tu ndiyo utakuwa mwisho wako,” yule mtu alinionya huku akiwa makini na nyendo zangu.

“Nadhani hujui unachotaka kukifanya…” nilianza kuongea kwa utulivu huku akili yangu ikipiga mahesabu namna ya kujinasua kwenye hatari ile.

Yule mtu hakunijibu bali alinitazama kwa umakini usoni kama aliyekuwa akinifananisha, nami nikawa naupima umbali uliokuwepo kati yangu na yeye. Mdomo wa ile bastola yake ulikuwa umbali mfupi mbele yangu. Utayari wa kidole chake kwenye kile kilimi cha bastola ulinitahadharisha kuwa mtikisiko hafifu ungeweza kuruhusu risasi kupenya kifuani kwangu na kuacha tundu linalovuja damu na huo ndiyo ungekuwa mwisho wangu.

Hivyo sikutaka kupuuza amri yake, hata hivyo wakati nikiendelea kufikiria namna ya kukabiliana na tukio lile ghafla mlango wa kile chumba nyuma yangu ukafunguliwa kwa kasi ya ajabu na kabla sijageuka vizuri kutazama nyuma yangu nikazabwa kofi zito la shingoni na kunyang’anywa ile bunduki niliyoichukua kwa wale waliokuwa wakilinda kule nje.

Haraka nikaupeleka mkono wangu mafichoni kuifikia bastola yangu. Bahati mbaya mkono wangu ukaishia njiani kwani mkono ulidakwa njiani kwa mtindo hatari wa judo na kuzungushwa kwa kasi ya ajabu na kufungashwa mgongoni kwangu kisha nikachezea kichapo cha ngumi mbili makini za mbavuni.

Maumivu makali yalisambaa mwilini kwangu, mbavu zikabana na kunifanya niachame mdomo wangu kutafuta hewa. Kabla sijajua nifanye nini kujiokoa na dhahama ile nikashtukia nikipigwa kabari matata shingoni.

“Safi sana, huyu naye apelekwe kule kule tulikomweka kiherehere mwenzake,” yule mwanamume niliyemkuta mle kwenye kile chumba cha tarakilishi zinazoongoza mfumo wa kamera za usalama alisema. “Kumbe watu wenyewe wepesi namna hii!”

Endelea...
 
utata.JPG

386

Sikuweza hata kufurukuta kwani kabari ile ilikuwa makini sana kama niliyefungwa na pingu na kadili nilivyojitahidi kujinasua ndivyo kabari ilivyozidi kukazwa na kunifanya nipumue kwa shida. Kisha nilianza kufanyiwa upekuzi wa haraka, na hapo nikagundua kuwa nyuma yangu kulikuwa na wanaume wawili makini.

Sasa nilianza kuona hatari ikininyemelea lakini nikaamua kujilegeza sana kiasi cha kushindwa hata kusimama na hivyo nikaanza kumwelemea yule mtu aliyenipiga ile kabari, akainama kidogo kunitazama usoni kwa wasiwasi. Tathmini yangu ikanitanabaisha kuwa alishaanza kupoteza umakini.

Sikutaka kusubiri zaidi hivyo muda ule ule nikakusanya nguvu zangu na kumtandika kiwiko cha mkono wangu tumboni, akaguna kwa maumivu na kulegeza mikono yake, kisha nikampiga kichwa matata cha kinyume nyume na kuuvunja vibaya mwamba wa pua yake huku akipiga yowe kali la maumivu. Akaniachia bila kupenda huku damu nyingi ikimtoka puani.

Na wakati huo huo niliruka juu nikampiga teke la shingoni yule mwenzake aliyekuwa akinifanyia upekuzi. Akayumba kidogo.

Yule mwenzao niliyemkuta mle ndani ya kile chumba cha tarakilishi zinazoongoza mfumo wa kamera za usalama, ambaye sasa alikuwa mbele yangu, alipoona vile akavuta kilimi cha bastola yake mkononi kunilenga lakini shabaha yake ilikuwa dhaifu kwani haraka nikawahi kuinama, ile risasi iliyofyatuliwa ikapita na kusafiri halafu ikapenya kwenye kifuani cha yule mtu aliyekuwa akinifanyia upekuzi. Risasi ile ikamsomba na kumtupa chini akiwa maiti.

Kuona vile, yule mtu niliyempasua mwamba wa pua kwa kichwa changu akawa ni kama aliyepigwa na butwaa na lile likawa kosa kubwa kwake, niliruka nikamchapa pigo moja la nguvu makini la kareti shingoni mwake kwa kutumia mikono yangu yote miwili. Lile pigo lilikuwa na athari kubwa dhidi ya mtu yule kwani muda ule ule nikamwona akianza kulegea na kuanguka sakafuni.

Sasa ile ikawa nafasi nzuri ya kumrukia yule jamaa niliyemkuta katika chumba kile, kwa kasi ya ajabu niliruka huku nikijizungusha pale mezani na kufanikiwa kumnasa kwa kabari makini ya miguu yangu na hapo ile bastola mkononi ikamtoka na kuanguka chini, hivyo akabaki akifurukuta kwa nguvu zake zote kujinasua kwenye ile kabari yangu bila mafanikio.

Macho yalianza kumtoka pima huku mishipa ya shingoni ikimtutumka kama mizizi. Muda huo nikamwona yule mtu niliyekuwa nimempiga pigo baya la kareti shingoni mwake kwa kutumia mikono yangu yote miwili na kisha akalegea na kuanguka chini akijizoa zoa toka pale chini sakafuni huku akijikung’uta kichwa chake kutoa wenge, mkono wake mmoja ulikuwa ameshika pua yake iliyokuwa inavuja damu na mkono wake mwingine ukiwa umeshika bastola na kuilekezea kwangu.

Kuona vile nikawahi kuifungua ile kabari yangu shingoni kwa yule jamaa niliyemkuta kwenye kile chumba na kisha nikamchapa pigo moja maridadi la kifuani, akajibamiza ukutani. Nilipogeuka kumtazama yule mtu mwingine niliyempasua mwamba wa pua nikamwona akininyooshea bastola kisha akavuta kilimi cha bastola yake kunilenga.

Haraka nilijirusha na kuteleza kwa tumbo sakafuni juu ya ile meza yenye tarakilishi na kuangukia upande wa pili wakati risasi za yule mtu zikinikosa. Yule mtu alikuwa anafyatua risasi ovyo kunilenga huku mimi nikijitahidi kuzikwepa zile risasi kwa kuhama hama kwa kujificha nyuma ya meza na viti ndani ya kile chumba.

Hatimaye nikawa nimeifikia ile bastola ya yule jamaa wa mwanzo niliyemkuta mle ndani kule ilipoangukia. Nikaiokota haraka huku nikijitupa chini upande mwingine, na wakati nikianguka pale chini nikafanikiwa kuiona miguu ya yule mtu niliyemvunja mwamba wa pua akiwa upande mwingine wa ile meza.

Bila kujishauri nilivuta kilimi cha bastola yangu mkononi na hapo risasi moja ikavunja mfupa wa mguu wake na kumfanya apige yowe kali la maumivu huku akirukaruka kama ndama. Risasi yangu ya pili ikamalizia ule mguu wake wa pili uliosalia, akaanguka chini sakafuni na kunifanya kukiona vizuri kichwa chake. Risasi yangu ya tatu ilimmaliza kabisa kwa kukifumua kichwa chake.

Yule jamaa wa kwanza niliyemkuta mle ndani ya chumba akawa kama amezinduka kutoka kwenye usingizi, akawahi kuruka hewani na kunizaba mateke mawili ya kifuani. Nguvu ya mapigo yale ya ufundi ilitosha kabisa kunirusha na kunibamiza ukutani. Maumivu makali yalisambaa haraka mwilini mwangu.

Pigo lingine la teke la yule jamaa liliponijia nikawahi kuliona na kuinama kidogo kulikwepa, yule jamaa alikuwa na nguvu nyingi miguuni hivyo pigo lake lilipopita na kukata upepo bila mafanikio lilisababisha mvumo wa upepo masikioni mwangu. Pigo lingine la teke liliponijia nalo nikawahi kulikwepa hivyo likaenda kukita ukutani na kuacha alama.

Yule mtu alionekana kuwa fundi sana wa kurusha mateke na alionekana kuumudu vyema mtindo ule wa urushaji wa mateke, na hapo nikawa nimetambua uwezo wake uko wapi, na hilo lilikuwa kosa lake kubwa kwani wakati pigo lake lingine la teke liliponijia nikawahi kulikwepa kwa kuchana msamba huku nikimchapa ngumi makini ya kwenye korodani.

Pigo langu likamfanya abweke kama mbwa koko huku akizishika malighafi zake. Sikutaka kumchelewesha, nikamchapa teke kali la shingoni. Hata hivyo aliwahi kuliona lakini hakufanikiwa kulipangua vizuri, likamtegua kiwiko cha mkono wake. Nikaachia mapigo mengine mawili ya haraka haraka yaliyotua kifuani na kichwani.

Yule mtu akapiga yowe kali huku mapigo yangu yakionekana kumlevya na kumfanya apepesuke, kisha nikaruka teke lingine la kijizungusha (flying round kick) ambalo lilitua kifuani kwake, akapiga mweleka sakafuni. Nikawahi kumfikia pale chini ili nimwongezee dozi kamili lakini bahati mbaya alikuwa hajiwezi kwa hali.

Damu nyingi ilikuwa ikimtoka puani na masikioni, na mdomo wake ulikuwa umepasuka na kuanza kuvimba. Jicho lake moja pia lilikuwa likitokwa na damu na alikuwa akihema ovyo kutafuta hewa safi. Alijaribu kujiinua lakini hakufanikiwa.

“Rais amefichwa wapi?” nimwuliza yule mtu huku nikimtazama kwa hasira.

Go to hell, you bastard!” yule mtu aliongea kwa shida huku maneno yake yakisikika kwa taabu. Muda huo sikutaka utani, nilimkwida shingoni na kumchapa makofi mawili ya nguvu usoni ili kumweka sawa.

“Niambie haraka, Rais yupo wapi?” nilimuuliza tena kwa hasira hata hivyo nilishangaa kumwona akiangua kicheko cha dharau na nilipomtazama usoni haraka nikagundua kuwa hakuwa tayari kunijibu.

“Unadhani n’takwambia?” yule mtu aliongea kwa shida huku damu nyingi zikimtoka mdomoni kisha akakohoa kidogo na kuendelea. “Mnapoteza muda wenu bure wala humuwezi kuizuia mipango yetu…”

“Mipango gani?” nilimuuliza yule mtu huku nikimtazama kwa udadisi, nikamwona akipumua kwa shida sana, halafu alikuwa kama aliyetaka kuongea jambo fulani, kinywa chake kilifunguka kwa shida na mara damu nyingi zilimtoka mdomoni. Muda mfupi uliofuata nikayaona macho yake yakipoteza nuru na kuanza kufumba taratibu, mwili wake ukalegea na hatimaye akakata roho.

Endelea...
 
utata.JPG

387

Sikutaka kupoteza muda zaidi mle ndani wala sikuwa na muda wa kuwafanyia upekuzi wale watu, niliiokota ile bunduki niliyoichukua kwa wale makomando waliokuwa wakilinda kule nje. Kabla sijatoka mara mlango wa kile chumba cha tarakilishi zilizokuwa zinaongoza mfumo wa kamera za usalama ukafunguliwa taratibu kisha mtutu wa bastola ukatangulia mbele.

Haraka niliwahi kujibanza nyuma ya ule mlango huku mkono wangu mmoja tayari ukiwa umeifikia bastola yangu kiunoni. Yule mtu aliyefungua ule mlango alisita kidogo kuingia mle ndani na badala yake akasimama pale mlangoni kama anayefanya tathmini ya mazingira ya mle ndani.

Kupitia uwazi mdogo uliokuwa nyuma ya ule mlango nilimwona yule mtu. Alikuwa akiyakaza macho yake kutazama mle ndani, nikahisi kuwa alikuwa ameshtuka baada ya kuiona maiti ya mwenzake ikiwa imelala pale karibu ya mlango sakafuni huku ikivuja damu.

Mara nikamwona akianza kurudi nyuma kidogo na kuchungulia kwenye uwazi mdogo nyuma ya ule mlango. Muda ule ule nikajitokeza na kuachia risasi moja makini ambayo ilipenya upande wake wa kushoto wa kifua chake hadi kwenye moyo wake. Yule mtu akaanguka chini pale mlangoni.

Taratibu nilinyata hadi pale mlangoni na kumshika miguu kisha nikaanza kumburuta nikimwingiza mle ndani ya kile chumba, kisha nikatoka huku nikiufunga ule mlango kwa nje. Halafu nikaufuata mlango mwingine wa upande wa kulia. Nikajaribu kuufungua, ukafunguka.

Hata hivyo nilishangazwa kuona chumba kilikuwa kitupu hakina mtu, kikiwa na meza moja ya kiofisi yenye tarakilishi kubwa aina ya IMac Retina 5K pamoja na viti vitatu, kiti kimoja kikiwa nyuma ya ile meza na viti viwili mbele ya ile meza lakini hakukuwa na mtu eneo lile.

Hata hivyo sikutaka kuendelea kushangaa pale, niliingia ndani ya kile chumba na kusimama, nikayazungusha macho yangu kukagua mazingira ya chumba kile. Na hapo nikajikuta nikilazimika kuisogelea kwa karibu zaidi ile tarakilishi iliyokuwa juu ya meza.

Niliitazama kwa ukaribu ile tarakilishi nikahisi kama sikuwa naona vizuri kutokana na mambo niliyoyaona kwenye kioo cha tarakilishi ile. Picha iliyokuwa ikionekana katika tarakilishi ile ni ya chumba kipana chenye mitambo.

Ndani ya chumba hicho kulikuwa na kiti cha chuma na juu ya kiti kile nilimwona Daniella akiwa amefungwa kwa kamba madhubuti, hali yake haikuwa njema, ilionekana kuwa alikwisha pata mateso ya kutosha. Mdomo wake ulifungwa gundi maalumu nyeusi aina ya ‘sole tape’.

Mwili wangu ukasisimka baada ya kuona kando yake kulikuwa na watu wanne waliovaa suti ghali za kijivu, nyuso zao hazikuwa na utani, wakiwa wamesimama kukizunguka kitanda fulani cheupe cha chuma huku wakionekana kumlazimisha jambo mtu aliyelazwa juu ya kitanda kile akionekana kudhoofu kidogo.

Mwonekano wa wale watu ulionesha kuwa walikuwa na hali njema sana kiuchumi, na hata kimadaraka. Mmoja wa watu hao alikuwa mzungu na mkononi kwake alikuwa ameshika faili moja kubwa la rangi nyekundu, nikahisi kuwa ulikuwa mkataba ambao alitakiwa kusainishwa Rais Masinde, kwa hiyari au kwa nguvu.

Sasa nikayakaza macho yangu kumtazama vizuri yule mtu aliyelazwa pale kitandani, nikamtambua. Alikuwa ni yeye… Rais Albert Masinde, na alionekana yupo hoi, huenda hakuwa anakula chakula.

Jambo lile liliyabadili kabisa mapigo yangu ya moyo. Hasira zikanichemka ndani mwangu na damu ndani ya mishipa yangu ikaanza kwenda mbio. Niliitazama saa yangu ya mkononi, nikagundua kuwa zilikuwa zimeshapita dakika ishirini tangu nilipoianza safari ya kungia mle ndani baada ya kutoka kuwasiliana na mkuu wangu, Kanali Othman Mjaka.

Sikupoteza muda, nilitoa simu yangu na kumpigia Kanali Mjaka, nikamwelea hali halisi ya mahala pale na kuwaomba wafike mahala pale haraka iwezekanavyo na ikiwezekana waongeze nguvu ya kutosha.

Kisha nilianza kutafuta namna ya kufika kwenye kile chumba walichokuwemo wale watu. Katika kuangaza angaza macho yangu mara nikagundua kulikuwa na kipande cha marumaru sakafuni ambacho kilitofautiana kidogo sana ua lake na vipande vingine. Ni kama ilivyokuwa kule kwenye ile nyumba yenye mitambo ya mawasiliano, nyuma ya Naf Beach Hotel katika Mtaa wa Duara.

Ilikuwa kazi ngumu sana kugundua jambo lile kwa mtu wa kawaida, ila kwangu ilikuwa kazi rahisi sana. Nilikikanyaga kile kipande na mara ukuta ukasogea pembeni taratibu na kuacha mlango mmoja uliofungwa.

Sikusita, mtutu wa bunduki ukiwa umeshikwa vyema mkononi, nilikishika kitasa cha mlango ule na kukinyonga, ule mlango badala ya kufunguka ukafyatuka kwa juu na kuwa kama unaoanguka kwenda ndani taratibu, kisha mbele yake kulibaki na uwazi ambao ulikuwa sawa na chumba kidogo.

Kule chini kulikuwa na mwanga hafifu, bila hata kujiuliza mara mbili nikaanza kuteremka ngazi kwenye ule mlango nikielekea kule chini, mtutu wa bunduki ukitangulia mbele kuchunga usalama wangu. Niliposhuka chini nikajikuta nimetokea kwenye ukumbi mmoja mpana uliojengwa chini ya ardhi.

Hata hivyo nilijikuta nikitazamana na mlango mkubwa wa vioo ambao mara tu nilipoukaribia ukafunguka, nikaingia. Hii ni ile milango maalumu ambayo mtu huhitaji kuigusa, kwani unapoikaribia inajifungua yenyewe.

Nilitembea hatua nne nikakutana na mlango mwingine wa mbao ngumu za mpingo, ulikuwa mlango madhubuti. Nilipojaribu kuufungua nikagundua kuwa ulikuwa umefungwa kwa ndani.

Haraka haraka nilimwomba Mungu awe upande wangu katika kumalizia kazi hii, sikuwa na muda wa kupoteza, nikakilenga kitasa chake kwa ile bunduki ya kivita niliyoishika vyema mkononi, nikaachia risasi tatu mfululizo na kitasa kikasalimu amri na mlango kufunguka.

Kwa kasi ya aina yake nikajirusha huku nikijiviringisha hewani na kutua ndani ya chumba kile. Niliposimama nikawaelekezea mtutu wa bunduki wale watu ambao walikuwa wameshtushwa sana na kitendo kile.

You are under arrest… Hands on your heads!” niliwaambia kwa sauti kali huku nikiwatumbulia macho yaliyowiva kwa hasira. Wote walinitazama wakiwa wamepigwa na butwaa, hakuna aliyeonekana kuamini.

Kwa uficho nilimwona mmoja wao akipeleka haraka mkono wake kiunoni kuchukua bastola yake, bila huruma niliachia risasi toka katika ile bunduki na kumfumua kichwa chake kwa risasi. Alirushwa hewani kimo cha ndama na kuanguka chini akiwa marehemu.

Wale watu wengine watatu walibaki midomo wazi wakitetemeka, haikuwa rahisi kwao kuamini kama walikuwa chini ya ulinzi. Baada ya kuona jinsi nilivyokifumua kichwa cha yule mwenzao kwa risasi, wote wakaogopa na kuweka mikono yao nyuma ya vichwa vyao. Nilimtupia jicho Daniella nikamwona akinitazama kwa matumaini makubwa.

Endelea...
 
utata.JPG

388

Huenda hakuamini kama muujiza ulikuwa umemtokea katika dakika ile. Pengine alishakata tamaa ya kuniona. Pamoja na kwamba nilikuwa na kazi nzito lakini moyoni nilikuwa na furaha sana baada ya kuwaona wote, Daniella na Rais Masinde.

Hata hivyo nilipomtazama Rais Masinde niliona kama aliyekuwa yuko ndotoni. Hakuwa akielewa nini kilichokuwa kikitokea mbele yake. Nikamwamuru mmoja wa wale watu watatu kwenda kumfungua kamba Daniella, muda wote nilikuwa makini kuzichunguza nyendo zao wote.

Yule mtu niliyemwamuru kumfungua Daniella akaleta jeuri na kwa wepesi wa aina yake mkono wake ukaibuka na bastola, nikawahi kumchapa risasi ya bega lake la mkono ulioshika bastola, yule mtu akarushwa juu na kuanguka akijipigiza ukutani huku bastola ikimtoka na kudondoka mbali naye. Akawa anaugulia maumivu huku akiwa amelishika bega lake.

Nilikuwa nimeuvaa uso wa mbuzi na sikutaka utani wowote. Niliwatazama wote kwa hasira, nikawaonya kuwa nisingesita kumuua yeyote ambaye angejaribu kuleta hila. Wote wakanywea. Sasa nilimpa amri yule mzungu, ambaye alionekana ndiye kiongozi wao, ya kumfungua Daniella zile kamba walizomfunga.

Bila ajizi yoyote yule mzungu alianza kumfungua Daniella zile kamba katika kiti alichofungwa. Baada ya kumaliza kuzifungua zile kamba, nikamtaka arudi kwenda kusimama pale aliposimama mwenzake, wakati huo Daniella alikuwa huru. Akajifungua ile gundi aliyofungwa mdomoni, nami nikamkabidhi ile bunduki halafu nikatoa bastola yangu.

Sasa tuliwazingira wale watu, tukawaweka mtu kati, mimi nikiwa upande huu na Daniella upande mwingine, huku macho yetu yakiwa makini kuhakikisha hawaleti utata wowote wala kutokea mashambulizi toka nje ya chumba kile.

Kisha nilimwambia Daniella awafunge kamba wote watatu na kuwafanyia upekuzi. Tukawakuta na bastola pamoja na nyaraka zingine. Tukavikusanya vitu vyote pamoja na lile faili kubwa jekundu. Na muda ule ule nikasikia mtetemo kwenye simu yangu ulioashiria kuwa ujumbe mfupi wa maandishi uliingia.

Nikaitoa ile simu na kuutazama ujumbe ule, na hapo nikagundua kuwa Kanali Mjaka na timu ya makomando walikuwa tayari wamelizingira lile ghala kwa nje na kufanikiwa kuwadhibiti walinzi na watu wengine waliokuwepo kule nje. Nikaipiga simu yake na kumwelekeza njia ya kupita.

Dakika mbili zilizofuata kundi la watu wakiwemo makomando wa Kikosi maalumu cha kushughulika na operesheni hatari, SOG, likaingia. Kikosi hiki kilikuwa kimesheheni maofisa wenye mbinu na ujuzi wa hali ya juu, mimi na Daniella tukiwa sehemu ya kikosi hicho.

Ndani ya wale watu niliweza kuwatambua RSO wa Mtwara Mama Komba, mkuu wa SOG Kanali Othman Mjaka, na Luteni Lister. Moja kwa moja Kanali Mjaka akanifuata pale niliposimama na kunishika mkono.

Well done…! Well done!” Kanali Mjaka alisema huku akiniachia na kisha alimshika mkono Daniella.

Albert! Oh my God!” niliisikia sauti ya Askofu Masinde iking’aka kwa mshtuko mkubwa. Nikageuza shingo yangu kutazama upande ilipotokea sauti ile na kumwona Askofu Masinde akiwa katikati ya kundi lile la wanausalama na macho yake akiwa ameyaelekeza kitandani alipolala Rais Masinde.

Na hapo wote tukakumbuka uwepo wa Rais Albert Masinde mle ndani. sasa alikuwa katika usingizi mzito. Kanali Mjaka akamsogelea huku akitazama huku na kule halafu akamgusa hapa na pale.

“Haraka mwite Dk. Chitemo na watu wake, mheshimiwa Rais awahishwe kwenye huduma ya kwanza,” Kanali Mjaka alisema, na hapo komando mmoja akatoka mbio na baada ya muda mfupi wakaingia watu wanne wakiongozwa na Daktari Chitemo, wakiwa na machela, wakashirikiana haraka haraka kumtoa Rais mahala pale na kumbeba mpaka juu.

Dakika tano baadaye maofisa wa usalama walikuwa wametawanyika eneo lote ndani ya lile ghala na kufanya ukaguzi kila mahali. Humo ndani ziligundulika silaha nyingi za kivita kama bunduki aina ya US Barrett M82 na silaha nyingine kali yakiwemo maguruneti, vyote vikiwa vimefichwa.

Kisha Kanali Mjaka akaamuru ghala lile lilindwe huku akimwagiza Mama Komba kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, SACP Deus Kashani, na kumtaka aje kuongeza nguvu akiwa na askari wake waaminifu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wenye silaha za kutosha wafike na kutawanyika kuzunguka eneo lote hadi bandarini.

Wakati hayo yakiendelea, madaktari wa Idara ya Usalama wa Taifa wakiongozwa na Daktari Chitemo walikuwa wameondoka na Rais Masinde, na taarifa nilizozipata baadaye ni kwamba baada ya kumpatia huduma ya kwanza, alichukuliwa na helikopta maalumu na kupelekwa jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Mzena iliyopo eneo la Makubusho, kwa huduma zaidi.

* * *

Endelea...
 
utata.JPG

389

Uso kwa uso na Tiger…




Saa 8:30 mchana…

NI Jumatatu… Kwa wengi hii ilikuwa Jumatatu ya kawaida kama zilivyokuwa Jumatatu zingine zilizotangulia, siku ya kwanza ya juma. Lakini kwangu hii ilikuwa Jumatatu ya tofauti kabisa. Jumatatu ya kukumbukwa daima, ambayo mimi na Daniella tulikuwa tumehitimisha kazi ngumu ya kumkomboa Rais Albert Masinde katika kile kilichoitwa ‘Operesheni Utata’.

Ilikuwa ni operesheni ngumu sana kuwahi kufanyika nchini lakini iliyotuchukua muda mfupi mno kuikamilisha. Jambo hili lilimshangaza kila mmoja ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa, hata mkurugenzi mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, David Mshana aliyetupendekeza kuifanya kazi ile!

Hakuna aliyeamini kuwa tulifanikiwa kumpata Rais ndani ya saa ishirini na nne tu! Sisi wenyewe hatukuamini. Na hakuna ambaye angeamini baada ya kusikia…

Yaani kuanzia saa moja za asubuhi siku ya Jumapili tulipopewa jukumu la kumsaka Rais Masinde, na mkuu wetu wa Kikosi, Kanali Othman Mjaka, hatimaye tulifanikiwa kumkomboa Rais Albert Masinde mnamo saa kumi na mbili na ushee asubuhi siku iliyofuata, yaani Jumatatu. Hii haikupata kutokea! Tulikuwa tumefanya kazi usiku kucha.

Kwa takribani siku tatu sasa si mwili wala akili yangu iliyokuwa imepata fursa ya mapumziko. Tangu Jumamosi nilipokuwa jijini Dodoma na baadaye tukio la kwanza la kigaidi kutokea usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili pale Capital Social Hall jijini Dodoma, muda wote nilijikuta nikiwa mashakani.

Mimi na Daniella tuliopewa jukumu la kuhakikisha tunamkomboa Rais Masinde tulikuwa na kazi kubwa sana ya kukimbiza watu huku sisi pia tukikimbizwa, tulijua kuwa watu tuliokuwa tukiwakimbiza walikuwa watu hatari sana; na tulijua vile vile kuwa tulikimbizwa na watu hao hatari.

Kila dakika ilitukuta macho kimwili na kiakili, kuzisaka roho za watu waliomteka Rais huku tukizilinda roho zetu wenyewe.

Sasa siku hii ya Jumatatu… baada ya kutoka kule katika eneo la Bandari ya Mtwara, kwenye ghala lililokuwa katika kitalu namba 164, mimi na Daniella tulipelekwa kule hotelini tulikofikia, tukachukua vitu vyetu na kisha tukaelekea nyumbani kwa Daktari Chitemo, tukachukua vitu vyetu na hatimaye tukaungana na Luteni Lister pamoja na Kanali Mjaka katika Kiwanja cha Ndege cha Mtwara, tulikoikuta ndege maalumu ya kuturejesha haraka jijini Dar es Salaam, ikitusubiri.

Tulifika katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam mnamo saa moja na dakika hamsini na tano za asubuhi, hapo tulimkuta mkurugenzi mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, David Mshana, tukaambiwa tulitakiwa kwenda kumalizia kazi yetu kabla hatujaenda kupumzika.

Halafu tukaingia ndani ya gari maalumu la Idara ya Usalama wa Taifa lililokuwa likitusubiri pale kiwanjani, gari hilo likatuchukua sisi watatu: yaani mimi, Daniella na Luteni Lister na kutupeleka hadi kwenye jumba fulani la kifahari eneo la Masaki.

Tulifika katika jumba hilo, tukateremka na kulijongea geti kuu la kuingia ndani ya uzio wa jumba lile la kiongozi fulani mstaafu wa ngazi za juu katika serikali wa awamu iliyokuwa imetangulia. Mlinzi wa getini alifungua geti na kutukaribisha huku akitutazama kwa wasiwasi kidogo. Ni wazi alijua sisi ni akina nani!

“Tuna shida na mzee,” Luteni Lister alimwambia yule mlinzi.

“Shida sasa hivi?” yule mlinzi alituuliza huku akitutazama usoni kwa umakini.

“Ndiyo sasa hivi,” Daniella alijibu haraka.

Yule mlinzi alitutazama kwa wasiwasi kisha bila kuhoji akainua simu ya mezani iliyokuwapo katika kibanda chake na kupiga ndani ya jumba hilo kubwa la ghorofa mbili, akampa ujumbe mtumishi wa ndani ambaye naye alikwenda kumwamsha mheshimiwa huyo mstaafu.

Yule mzee alipotoka ndani alikuwa amevaa kaptura nyeusi ya kadeti na singleti tu, na hapo alikutana na sura zetu, hakuuliza chochote kwani moja kwa moja aliwatambua Luteni Lister na Daniella.

“Enhe, niwasaidie nini, vijana, maana naona mmenijia asubuhi asubuhi?” yule mzee alituuliza huku akitutazama kwa zamu.

“Mheshimiwa, sisi ni maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, tumekuja kukuchukua kwani unatakiwa Ikulu kabla ya saa tatu asubuhi hii,” Luteni Lister alimwambia yule mzee.

“Ikulu? Kuna nini Ikulu maana sisi wengine tulishaachana na mambo ya Ikulu zamani,” yule mzee alijaribu kujitetea.

“Sisi wajibu wetu ni kukufikishia ujumbe kama ulivyo, hayo mengine utayajua huko huko,” Luteni Lister alisema na kumfanya yule mheshimiwa mstaafu abaki kaduwaa.

Kisha alitutaka radhi halafu akarudi ndani na kubadilisha nguo, na muda kidogo baadaye tukaondoka naye kwa kutumia gari tulilofika nalo hapo kwake na kwenda kumkabidhi kwa mkurugenzi mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, David Mshana, kwenye viunga vya Ikulu ya Dar es Salaam.

Baada ya hapo niliachana na akina Luteni Lister na Daniella, nikapewa gari lililonipelekea nyumbani kwangu Upanga ambako nilijimwagia maji kisha nikabadilisha nguo zangu. Halafu tukaondoka na dereva wangu hadi ofisini kwa mke wangu Rehema, kwenye jengo la Benjamin William Mkapa eneo la Posta.

Rehema aliponiona alifurahi sana, tukaongea kwa dakika tano tu, nikamweleza kuwa japokuwa nilikuwa nimerudi salama toka Mtwara lakini nilitakiwa kuelekea Dodoma kukamilisha majukumu yangu.

Rehema alisikitika kwa sababu hatukuwa na muda wa kuwa pamoja siku hiyo lakini akanitakia safari njema naa kuniombea ulinzi wa Mungu uwe juu yangu. Tukakumbatiana kisha nikaondoka na kuingia kwenye gari hadi katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam kwa safari ya Dodoma.

Sasa nilikuwa nimerejea ndani ya Jiji la Dodoma… eneo lilipoanzia sekeseke kabla sekeseke hilo halijahamia Mtwara. Niliitazama saa yangu ya mkononi nikagundua kuwa ilishatimia saa nane na nusu za mchana.

Nilipoingia tu chumbani kwangu, kwenye chumba maalumu nilichoandaliwa, kitanda kikubwa kikanilaki kwa namna ya mapenzi ambayo sikupata kuyaonja kabla. Mara tu ubavu wangu ulipoligusa godoro hilo laini, huku nikiwa na mavazi yangu yote ikiwa ni pamoja na viatu miguuni; nilijikuta nikimezwa na lindi zito la usingizi.

Ukweli ni kwamba kichwa changu kilikuwa kimechoka sana na bado nilikuwa na maswali mengi yaliyohitaji kujibiwa haraka ili kulifumbua fumbo ambalo lilimtia Rais wa Tanzania hatarini; lakini bado jambo hili halikunipokonya usingizi.

Yote yangeweza kusubiri. Usalama wa Rais na wa Nchi haukunitia hofu tena. Nilikuwa na hakika kuwa kama Mungu alikuwa ameruhusu niwe hai hadi muda huo basi pia kila kitu nchini kingekwenda sawa sawa na mkutano wa Nchi za Jumuia ya Madola ungefanyika bila tatizo lolote.

Endelea...
 
utata.JPG

390

Kwa sasa hakukuwa na nilichokihitaji zaidi ya mapumziko ili niipate tena afya yangu ya mwili na akili kwa kiwango changu halisi ili kuniwezesha kuendelea na majukumu yangu ya usalama wa nchi hii. Usingizi ukiwa dawa pekee ya mapumziko, ndipo nikalala.

Na nililala hasa… Usingizi ulikuwa mzito, usingizi ambao haukuwa na ndoto zozote isipokuwa ile niliyoifikiria kama ndoto, ambayo ilinifanya nidhani kuwa kila mara nilikuwa nikisikia mlio wa simu yangu ya mkononi ikiita kwa fujo. Nilipokuja kufumbua macho yangu nilishangaa kuona kulikuwa na mwanga mkali wa jua la mchana.

Nilizungusha macho yangu kutazama huku na huko nikijiuliza nini kilikuwa kinaendelea, na nilipoitazama saa yangu, nilishangaa sana.

Nilikuwa na uhakika kuwa nililala siku ya Jumatatu, mnamo saa nane na nusu za mchana! Lakini saa yangu iliniambia kuwa muda huo ulikuwa ni saa sita na nusu za mchana siku ya Jumanne! Iliwezekanaje kuwa nililala zaidi ya saa ishirini na moja?

Niliichukua simu yangu ambayo pia ilikuwa pale pale kitandani, nikakuta kulikuwa na miito ya simu zilizopigwa lakini sikuwa nimezipokea (missed calls) zaidi ya sitini na jumbe fupi za simu takriban hamsini, kutoka kwenye namba mbalimbali. Baadhi ya namba zile nilizitambua lakini nyingine zilikuwa ngeni.

Nilisonya halafu nikajizoa zoa pale kitandani huku nikipepesuka. Ndiyo kwanza nikagundua kuwa nilikuwa nimedhoofika kiasi gani kwa uchovu, maumivu na pengine njaa ya muda mrefu. Kwa kifupi nilikuwa kama mgonjwa.

Niligeuka kukitazama tena kitanda kwa tamaa, na kilionesha kuendelea kunialika. Hata hivyo, niliishinda hamu ya kulala tena kwa kujilazimisha kuyavua mavazi yangu na kisha nikaelekea bafuni. Niliingia kwenye beseni kubwa la maji na kufungulia maji ya baridi ambayo niliyaacha yauchezee mwili wangu kwa muda wa kutosha, yakafanikiwa kunirudishia nusu ya afya yangu.

Nusu ya pili ya uhai ilinirudia baada ya kufanya mazoezi ya viungo kwa dakika ishirini halafu nikajimwagia tena maji. Ndipo sasa ule uJason Sizya wangu ukanirudia tena. Sura yangu ilichangamka kama kawaida, ikivutia katika suti yangu safi nyeusi ambayo niliivaa. Kisha nilielekea kwenye mgahawa, nikaagiza chakula.

Mhudumu aliponiletea chakula nilichoagiza pamoja na matunda ya aina mbalimbali alileta pia na chupa kubwa ya mvinyo mwekundu aina ya Dompo. Niliushambulia haraka haraka ule msosi kuitibu njaa yangu, na dakika kumi na tano baadaye nilikuwa nimeumaliza ugali wa dona na kumteketeza kuku mzima na kisha kuyanyanyasa matunda.

Halafu nilikaa kama dakika tano hivi kisha nikaanza kukisindikiza chakula hicho kwa mvinyo mwekundu huku nikitafakari kuhusu mustakabali wa maisha yangu ya kishushushu.

Wakati nikiendelea kunywa mvinyo taratibu mara simu yangu ya mkononi ikaanza kuita, nilipoitazama vizuri nikaliona jina la mkuu wangu wa Kikosi, Kanali Othman Mjaka. Haraka nikaipokea ile simu na kuiweka kwenye sikio langu la kushoto kusikiliza. Baada ya dakika moja tu ya kupokea maagizo muhimu simu ilikatwa.

Sikuwa na hamu ya kuendelea kukaa pale, niliinuka na kulipia chakula changu na ule mvinyo, halafu nikaelekea haraka chumbani kwangu.

* * *



Saa 8:35 mchana…

Kanali Mjaka aliitoa miwani yake usoni na kuiweka juu ya meza ofisini kwake huku akitutazama kwa umakini mimi na Daniella. Mchana huu wa Jumanne ulitukuta ndani ya ofisi za SOG zilizopo jijini Dodoma, tulikokuwa tumeitwa na mkuu huyo wa Kikosi.

Ilikuwa ni ndani ya ofisi kubwa na nzuri sana iliyokuwa na mazingira nadhifu mno na yaliyovutia zaidi kwa mpangilio wa samani za kisasa, ikiwa na zulia jekundu sakafuni na meza ndefu ya ofisini yenye viti ishirini. Viti kumi upande wa kushoto na viti vingine kumi upande wa kulia.

Yeye Kanali Mjaka alikuwa ameketi kwa utulivu kwenye kiti chake kikubwa cha kiofisi cha ngozi halisi kinachozunguka na chenye magurudumu madogo yaliyokiwezesha kusogea, nyuma ya meza yake kubwa ya ofisini, mwisho wa ofisi ile. Juu yake ukutani kulikuwa na picha kubwa ya Rais wa Nchi, Dk. Albert Masinde

Mbele yake kulikuwa na meza kubwa ya ofisini ambayo juu yake kulikuwa na tarakilishi mpya kabisa aina ya iMac Pro, mashine ndogo ya kuchapa barua aina ya HP LaserJet, mashine ndogo ya kurudufu nyaraka na ‘trei’ mbili za chuma zilizokuwa na maandishi ya ‘IN’ ikimaanisha kazi zilizokuwa zikiingia na ‘OUT’ ikionesha kazi zinazotoka.

Pia juu ya ile meza mbele ya Kanali Mjaka kulikuwa na simu ya mezani, majalada kadhaa ya kiintelijensia, vitabu vya sheria na vya kiintelijensia, kidau cha wino, mhuri na kichupa kidogo chenye wino mweupe wa kufutia maandishi.

Upande wa kulia wa ofisi ile kulikuwa na kabati moja la mbao na makabati mawili mengine ya chuma na upande wa kushoto wa ile ofisi, ukutani kulikuwa na rafu ya mbao iliyopangwa vitabu na majarida mbalimbali ya kijasusi, na juu ya rafu ile kulikuwa na picha kubwa ya mwasisi wa Taifa.

Na pembeni ya rafu ile ukutani kulikuwa na runinga pana iliyounganishwa na chaneli nyingi za habari za kimataifa.

Nilikuwa ndani ya suti yangu nadhifu ya rangi nyeusi, viatu vyeusi vya ngozi halisi vilivyong’arishwa kwa Kiwi, nywele fupi zilizokatwa kwa mtindo wa kupendeza na miwani myeusi iliyoongeza utanashati wangu, na kando yangu aliketi mwanamke mrembo kabisa, aliyependeza kwa suti yake nadhifu ya kike ya rangi ya maruni na viatu vya maruni vya mchuchumio vyenye visigizo virefu, unaweza kusema ni Muhindi lakini pia unaweza sema ni Mwarabu, yote yangewezekana.

Pamoja nasi, mle ndani ya ile ofisi ya Kanali Mjaka, pia kulikuwa na maofisa wengine kumi na wawili wa usalama, makomando kutoka Kikosi maalumu cha SOG, ambao pia walishiriki kwa namna moja au nyingine kumalizia harakati hizo kule bandarini Mtwara na kwenye ile nyumba yenye mitambo ya mawasiliano iliyokuwa katika Mtaa wa Duara, nyuma ya Naf Beach Hotel. Miongoni mwa wanausalama hao kutoka SOG walikuwamo wanaume wanane na wanawake wanne.

Hiki kilikuwa kikao maalumu na kilitambulika kuwa kikao rasmi na halali cha kupashana taarifa za kiintelijensia (Situation Report - SITREP) kuhusu ya hali ya ulinzi na usalama nchini, na kupanga mikakati ya kukamilisha malengo ya kazi zilizokuwa zikitukabili.

Mzungumzaji mkuu alikuwa kiongozi wetu, Kanali Othman Mjaka ambaye kutokana na wadhifa wake, na kwa mujibu wa chain of command ndiye aliyekuwa akipokea maagizo kutoka makao makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa kupitia channel husika, kutupa maelekezo na kusimamia utekelezaji.

Endelea...
 
utata.JPG

391

Na kama kawaida, Kanali Mjaka ndiye aliyefungua kikao kwa kutoa pongezi kwa kazi iliyofanyika.

“Hongereni sana kwa kazi ngumu, kazi ambayo Idara ya Usalama wa Taifa ilituumiza sana vichwa vyetu. Haikuwa kazi rahisi lakini kwa nguvu za Mola kila mmoja wetu ameifanya kwa upande wake na kwa pamoja tumeikamilisha,” Kanali Mjaka alisema. “Nadhani mmejionea wenyewe, kikulacho ki nguoni mwako…”

Watu wote mle ndani ya ofisi ya mkuu wa SOG tulibetua vichwa vyetu kuafikiana na maneno ya mkuu wetu, Kanali Mjaka.

“Watu wote ambao mheshimiwa Rais alikuwa amewaamini sana ndio ambao walishiriki kuhujumu jitihada zake za kuhakikisha anaikwamua nchi hii,” Kanali Mjaka alisema.

“Kwa hiyo, ni kweli kwamba mheshimiwa mstaafu wetu wa awamu iliyopita ndiye kiongozi wa syndicate hii kwa nickname ya Tiger?” nilimuuliza Kanali Mjaka ili kupata uhakika wa kilichotajwa kwenye nyaraka tulizozipata toka kwa yule mzungu, mwakilishi wa mkuu wa jumuia ya siri ya Triangle, kule kwenye ghala lililo katika kitalu namba 164.

“Ni kweli! Kiongozi mstaafu aliheshimiwa sana kama mmoja wa washauri wakubwa wa Rais Masinde lakini inasikitisha sana kuona yeye ndiye amekuwa kiongozi mkuu wa kutufanyia hujuma mbaya kama hii!” Kanali Mjaka aliongea kwa uchungu sana, ofisi yote ilikuwa kimya kabisa ni kiyoyozi tu kilichokuwa na uhuru wa kutoa mlio humo ndani, kisha akaendelea.

“Amekuwa kiongozi wa nchi hii kwa miaka kumi na amefanya kazi nzuri sana katika kipindi chake lakini inasikitisha kuona kwamba yeye ndiye kiongozi wa watu walioshiriki hujuma hii chafu japokuwa alijitahidi sana kupotosha ukweli ionekane kuwa Tiger ni mtu mwingine kabisa, labda mkuu wa majeshi au mnadhimu wa jeshi. Mheshimiwa Rais amesikitishwa sana na jambo hili, haelewi kwa nini mtu huyu ameamua kuwahujumu Watanzania!”

Ofisi yote ilizizima kwa ukimya, kila mmoja akijaribu kutafakari ki vyake. Baada ya kitambo fulani cha ukimya nilivunja ukimya kwa kumuuliza Kanali Mjaka swali. “Na vipi hali ya mheshimiwa Rais kwa sasa?”

“Kwa maelezo ya madaktari, sasa hali ya mheshimiwa Rais imeimarika, mwili wake ulikuwa na upungufu wa maji kwa kuwa alikuwa ameanzisha mgomo wa kula tangu alipotekwa,” Kanali Mjaka alisema na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.

Halafu sasa ulifika ule wakati wa kujikita kwenye mjadala rasmi wa kupeana taarifa za kiintelijensia kuhusu ya hali ya ulinzi na usalama nchini, na kupanga mikakati ya kukamilisha malengo ya kazi zilizokuwa zikitukabili, ambapo Kanali Mjaka alitoa maelezo mafupi kuhusu hali ya usalama nchini.

Kwa dakika kumi hivi Kanali Mjaka alitusomea taarifa maalumu iliyotolewa na makao makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa kuhusu mashambulio yote yaliyotokea katika miji yetu ya Dodoma na Mtwara, athari zilizojitokeza kwenye mashambulio hayo ikiwemo taarifa ya watu waliokuwa wamepoteza maisha yao na waliojeruhiwa.

Pia alitueleza kuhusu mkakati wa siri wa baadhi ya Nchi za Jumuia ya Madola hususan zilizokuwa zimepitisha sheria iliyokuwa ikilalamikiwa ya haki za binadamu, kutangaza kuwa zingesusia mkutano wa Nchi za Jumuia ya Madola uliokuwa ufanyike Jijini Dodoma kwa sababu ya hali ya kutokuwepo usalama nchini Tanzania, na kwamba zilitaka mkutano huo uahirishwe au kuhamishiwa katika nchi nyingine licha ya maandalizi yote yaliyofanyika.

Taarifa hizi zilimkera sana Rais Masinde na alipanga kutoa hotuba na kutangaza kuwa wote walioshiriki kwa namna moja ama nyingine kwenye hujuma ile hawaitakii mema nchi ya Tanzania, na kusisitiza kuwa “Kikundi ama Nchi yoyote iliyoshiriki kwa namna moja ama nyingine ihesabike kuwa adui wa Tanzania” na kuahidi kuwa serikali ya Tanzania ingehakikisha inalinda mipaka na rasilimali zake kwa gharama yoyote pasipo kuyumba.

Taarifa hiyo pia iligusia uwepo wa chembechembe ya usaliti nchini. Uchunguzi wa awali ulionesha kuwa wote waliohusika katika sakata hilo ni watu wakubwa au waliopitia nyadhifa kubwa serikalini na ndiyo maana hawakuwa wababaishaji; bali watu wenye uzoefu wa hali ya juu katika kupanga, na kutekeleza mipango mikubwa ya kisaliti.

Hii iliashiria uwepo kwa chembechembe hizo za usaliti nchini zilizokuwa zikifanya kazi kwa ushirikiano au maelekezo ya kundi kubwa zaidi. Baadhi ya makundi yaliyowekwa katika orodha ni Jumuia ya siri ya Triangle, Jumuia kadhaa za wanaharakati wa haki za binadamu na Nchi kadhaa za Afrika zilizopitisha sheria, iliyokuwa ikilalalmikiwa, ya haki za binadamu ambayo Tanzania tuliikataa.

Na hivyo, Idara ya Usalama wa Taifa ilipanga kuanza kuelekeza nguvu zake zote katika ukusanyaji wa taarifa za kiintelejensia ili kuzitambua nchi zote, vikundi, washirika wake, wafadhili wake, na jinsi wanavyofanya kazi.

“Sasa…” Kanali Mjaka alianza kutuoa maelezo baada ya kumaliza kutusomea taarifa maalumu iliyotolewa na makao makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa.

“Kutokana na uvundo tulioufichua, makao makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa wanataka kuhakikisha hujuma hii inahitimishwa kabisa kwa kuisafisha nyumba yote, hivyo kazi bado imebakia kwetu SOG. Makao makuu wanataka uchunguzi uanze mara moja, wachunguzwe viongozi wote wa kada ya uwaziri, wakuu wa ngazi za mikoa na wilaya na taasisi zote nyeti… mmoja baada ya mwingine, na ndani ya miezi miwili kila ofisa aniletee tafutishi zake nini kimegundulika, maana lazima kuna makandokando,” Kanali Mjaka alisema.

Halafu Kanali Mjaka alitueleza kwa kirefu kazi tuliyokuwa tunapaswa kuifanya, na namna tulivyotakiwa kuifanya. Mengi ya maelezo yake yalirejea Amri ya Kazi (Operation Order) ambayo kila ofisa wa usalama alikuwa amepewa na aliijua.

Hata hivyo tuliambiwa kuwa kazi ya uchunguzi huo pia iliwahusisha maofisa wa Taasisi ya SPACE, kama kitengo cha ufundi (Technical) kwa kuwa maofisa hawa walikuwa na mafunzo maalumu ya kutumia vyombo vya kisasa vinavyotamba katika sanaa ya ujasusi.

Kazi kubwa ya maofisa hawa ilikuwa kutoa msaada (support) kwetu ambao tulitakiwa kuwa katika medani (field) katika kuunganisha nukta zinazopungua kwenye taarifa ambazo tungekuwa tukizifuatilia.

Kwa kifupi maofisa wa Taasisi ya SPACE (ufundi) ndio waliotakiwa kufanya kazi ya kunasa radio za mawasiliano ya adui, kusikiliza mazungumzo ya simu (telephone bugging) na kuchungulia barua pepe (email interception) za wote ambao tungewatilia shaka na kutaka kupata taarifa zao, ndugu na washirika wao.

Maofisa wa Taasisi ya SPACE pia wangetumika kufanya ufuatiliaji (surveillance) wa watuhumiwa, na washirika wao, kufungua milango ya nyumba zinazolindwa kwa mitambo maalumu ya kuzuia wahalifu bila kuacha ushahidi wowote, na kufanya upekuzi wa siri (secret searches) katika nyumba zinazoshukiwa kuhifadhi watu au vitu vinavyotafutwa.

Na mwisho wa kikao Kanali Mjaka aliendelea kutukumbusha kwamba kila ofisa wa usalama aliyepo kwenye Kikosi maalumu cha SOG alikuwa amewekwa kwenye mizani, na kuonekana anafaa kwa kila hali. Kwa sababu hiyo makao makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa wana uhakika wa kuona kazi ikitendeka kwa weledi na kwa kufuata misingi na kanuni za Idara.

* * *

Endelea...
 
Back
Top Bottom