383
Hata hivyo, kwa Monica aliyetumwa, ujumbe huu ulikuwa na maana ya kawaida ya kuwa mama yule alikuwa amenitamani kimapenzi ndiyo maana akatuma ujumbe ule, na mwanadamu yeyote yule wa kawaida angeweza kuutafsiri ujumbe huu moja kwa moja vile vile, lakini kwa mwanadamu asiyekuwa wa kawaida huu ulikuwa ujumbe mzito sana.
Naam! Nami sikuwa mwanadamu wa kawaida! Niliielewa maana ya mtu wa kariba yangu kusema ameyapenda macho yangu nilipomtazama, hii ilimaanisha kuwa mtu huyo aliutambua uwezo mkubwa niliokuwa nao ndani yangu wa kumsoma mtu na hivyo alitamani kuwa karibu nami kwa ajili ya kupata ulinzi, au kama ni adui basi alitamani tukabiliane!
Wakati huo sikuwa nimemchukulia mama huyo kama adui, nilimwona ni
first lady anayempenda na kumheshimu mumewe, na zaidi ya yote akiipenda sana nchi yake. Sasa leo tukiwa ana kwa ana, nilipata tena nafasi ya kuyaona macho yake yaliyokuwa kama ya simba jike anayewinda na ambaye alikuwa tayari kunirarua. Yalikuwa yanatoa cheche!
Sasa hapakuwa na muda wa maongezi bali shughuli kwa kwenda mbele, tulipaswa kuoneshana nani zaidi, kati yangu ambaye nilikuwa na jukumu la kumkomboa Rais wa Nchi au mwanamama yule aliyefanya kila liwezekanalo kuhakikisha anatimiza haja ya mabwana zake wa jamii ya siri ya
Triangle.
Wakati nikiamini kuwa nilikuwa mpelelezi mashuhuri niliyepitia mafunzo makali ya kijasusi nchini Misri na kuanza kazi zangu kivitendo kule ufukweni Mombasa, nchini Kenya, nikiwa na umakini wa hali ya juu huku nikizifuata kanuni zote nilizofundishwa kambini na zile nilizojifunza kulingana na matukio niliyoyapitia, sikujua mwanamke yule alipatia wapi mafunzo yake!
Hata hivyo, macho yake tu yalidhihirisha kuwa alikuwa ni mtu hatari sana zaidi ya vile nilivyomfikiria. Kama ni ujasusi basi alikuwa amefunzwa akafunzika!
Wakati mawazo hayo yakipita haraka kichwani kwangu, kwa kasi ya ajabu nilishtukia nikipigwa teke la kichwa na pigo hilo likanifanya nisiweze kuona vizuri mbele yangu. Hofu ikaniingia na kuhisi kuwa dakika zangu za kubaki duniani zilikuwa zikihesabika.
Nikiwa bado najihisi kuchanganyikiwa nilikusanya nguvu na pigo jingine la teke lilipokuja niliwahi kulidaka kabla halijanifikia tumboni kisha nikauzungusha mguu wa yule mama kwa nguvu na kwa kasi ya ajabu na bila upinzani nikafanikiwa kuutengua mfupa wake wa goti na hapo yule mama akapiga yowe kali la maumivu.
Alipoanguka chini mfupa wa goti lake ulikuwa tayari umevunjika, nikawahi kunyanyuka kwa kupiga samasoti ya chini na kumfuata lakini wakati nikifanya hivyo nilisita pale nilipojikuta nikitazamana na mtutu wa bastola yake mkononi. Alikuwa ameshika bastola yenye kiwambo cha kuzuia sauti.
“Ulidhani utashinda kirahisi! Unajidanganya bure, kijana…” mwanamama yule alizungumza huku akicheka.
Niliipima sauti yake nikagundua kuwa ilikuwa mbali na mzaha. Sasa jasho jepesi la hofu likaanza kunitoka maana nilikuwa nimeingia kwenye mtego ambao kwa akili za kibinadamu nisingeweza kujinasua kirahisi, hivyo akili yangu ilianza kufikiria haraka namna ya kujinasua.
“Kama ni vita umeshinda, lakini niambie kwa nini umeamua kuisaliti nchi yako?” nikamuuliza yule mama huku nikitabasamu.
“
That’s non of your business!” yule mama alifoka kwa hasira huku akinitazama kwa umakini usoni. Macho yalikuwa bado yanatoa cheche.
“
So, what kind of a business are you doing?” nilimuuliza kwa utulivu.
Yule mama akaangua kicheko kilichonishangaza, lakini ghafla kicheko chake kilikoma huku sura yake ikiwa mbali na mzaha. Tabia yake hii ikaanza kunichanganya.
“Mbona hutaki kunijibu swali langu, mama?” nilimuuliza, akanitazama kwa utulivu na uso wake haukuonesha tashwishwi yoyote.
“Tayari umechelewa kwani hata nikikujibu hutofanikiwa kufika na majibu hayo kokote,” yule mama aliniambia huku akibinua midomo yake kwa dharau.
“Una maanisha nini?” nilimuuliza kwa utulivu.
“Umefanya makosa sana kukubali kazi hii, na mbaya zaidi kuja hadi humu ndani,” yule mama alisema. Nikazidisha tabasamu usoni kwangu. Na hapo akaongeza, “Na kama unadhani nakuongopea umekosea sana kwani huu ndiyo mwisho wako na habari zako zitaishia humu ndani.”
Nilimtazama yule mama kwa umakini huku nikijaribu kumpigia hesabu kali namna ya kumpokonya ile bastola. Hata hivyo alikuwa makini sana kuchunguza kila hatua niliyotaka kuchukua.
“Nilikutumia ujumbe siku unapewa tuzo pale Ikulu nikadhani labda una akili ya kuupambanua… kama ungekuwa umeniomba ushauri huenda ningekushauri usijiingize kwenye harakati hizi ila kwa sasa nafasi hiyo huna. Huu ni mtandao mkubwa sana usioweza kuvunjwa kwa urahisi na hivyo vijiharakati vyenu,” yule mama alisema kwa nyodo.
“Najua wewe ndiye Chameleon, sasa niambie Tiger ni nani?” nilimuuliza yule mama huku nikianza kupiga hatua kumfuata.
“
Shut up your mouth, you bastard!” yule mama alifoka huku akipeleka kidole chake cha shahaada kwenye kifyatulio tayari kufyatua risasi.
Hisia zangu ziliniambia kuwa sasa hakutaka tena masihara, alidhamiria kuniua, nikajirusha haraka pembeni na wakati huo huo risasi mbili alizozifyatua moja ilipita karibu kabisa na sikio langu ikapasua kioo cha dirisha na risasi nyingine ikachimba ukuta na hapo nikajua kuwa kweli yule mama alikuwa amedhamiria kuniua.
Nilijirusha tena nikadondokea nyuma ya kitanda wakati yule mama akiendelea kufyatua risasi ovyo mle ndani akinilenga, lakini nilikuwa mwepesi wa kujirusha upande huu na ule na hapo risasi moja ikanipunyua begani.
Sasa nilikuwa nakabiliwa na hatari kuliko wakati mwingine wowote. Sikuwa na namna, nikainua kitanda ili kujikinga na mashambulizi yale huku nikiupeleka mkono wangu haraka kuichomoa ile bastola ya Yusuf Taifa niliyoiokota kule sebuleni. Nikaikamata sawa sawa na kuanza kutafuta upenyo mzuri wa kucheza naye.
Mara mlango wa kile chumba ukafunguliwa kwa kasi ya ajabu, na sote tukashtushwa na tukio lile. Ni wakati huo nilimwona mwanamume mrefu mwenye mwili wa kimazoezi akiwa amevaa mavazi ya kimchezo,
tracksuit ya bluu ya timu ya taifa pamoja na viatu vyepesi vya mazoezi akiruka kwa namna ya kininja na kutua kando kabisa ya chumba huku akielekeza bastola yake kwa yule mwanamama.
“Weka silaha yako chini!” yule mwanamume alimwamuru yule mama. Mara moja nikaitambua sauti yake. Alikuwa ni Askofu Masinde. Hata yule mama pia alimtambua Askofu Masinde.
“Bishop!” yule mama alimaka kwa mshangao. Alitoa macho ya woga na mashaka.
“Weka silaha yako chini sasa hivi!” Askofu Masinde alisisitiza huku uso wake ukionesha kuwa hakuwa na mzaha hata chembe.
“Bishop, kwani na wewe u…?” yule mama alitaka kuuliza swali lakini akasita. Hata hivyo hakutaka kutii amri, na wala hakutaka kushindwa.
Kwa kuyatazama macho yake tu nilitambua kuwa sasa alipanga kuhamishia mkono wake wenye silaha kwa Askofu Masinde lakini asiwe mwepesi vya kutosha. Askofu Masinde alimuwahi na kumshindilia risasi moja ya bega!
Asiridhike, akataka kufurukuta tena, sasa ikamlazimu Askofu Masinde atumie risasi nyingine kumnyamazisha kabisa. Risasi hiyo ilitoboa shingo ya mama yule na kumlaza akiwa hoi bin taaban chini. Alikuwa anavuja damu kupita kiasi. Mkono wake wa kushoto uliokuwa umeshika bastola sasa ulishikilia jeraha lake.
Japokuwa alikuwa ni mtu mdhalimu aliyekaribia kuligharimu taifa lakini alitia huruma. Kinywa chake kilikuwa kinatema damu nyingi kwa mtindo wa kwikwi! Mara akakata pumzi.
“Jason, umesalimika?” Askofu Masinde aliniuliza kwa wasiwasi huku akigeuka kunitazama.
“Nipo salama kabisa, mjomba… umejuaje kuwa nipo hapa?” nilimuuliza Askofu Masinde swali la kijinga huku nikimkazia macho. Akacheka kidogo.
“Umesahau kuwa mimi pia ni mwanausalama mwenye mbinu zote za kijasusi?
Anyway, hatuna muda… Daniella anakuhitaji haraka, ameshagundua mahali alipofichwa Rais,” Askofu Masinde alinisihi.
“
I see! Lakini hapa pia panatakiwa kufanyiwa ukaguzi na kuwekewa ulinzi kabla hatujaondoka…” nilisema lakini Askofu masinde alinikatisha.
“Twende nikupeleke ukamsaidie Daniella, wanausalama watafika hapa wakati wowote.
So, the whole thing here is under control from now on,” Askofu Masinde alisema na kuanza kuondoka. Kisha alinihimiza, “Upesi! Upesi, Jason! Tunachelewa…”
Niliitazama saa yangu ya mkononi, nikagundua kuwa ilishatimia saa kumi na mbili kasoro dakika moja za asubuhi. Nikautazama mwili wa Mama Juliana Masinde kwa uchungu mkubwa, kisha nikaziokota bastola na kutoka nikimfuata Askofu Masinde kule nje.
Wakati natoka kupitia mlango wa jikoni nikajikwaa, nilipotazama chini nikakaiona chombo fulani hivi ambacho ukikitega sehemu hutoa mwanga mithili ya mlipuko wa umeme. Mara nyingi hutumiwa kumchanganya adui. Nikakiokota na kutoka haraka.
Nilimkuta Askofu Masinde nje kabisa, mtaani, akiwa ana-
trot, nikamkimbilia mpaka tukafikia mahali alipoegesha gari lake aina ya
Toyota Landcruiser GX V8 la rangi nyeusi. Tukajipakia garini, halafu Askofu Masinde akaliondoa gari lake kwa mwendo wa kasi. Magurudumu yalizunguka kwa kasi sana na kuchimba ardhi wakati akiliondoa lile gari.
* * *
Endelea...