SEHEMU YA 349
Mama yake ndiye aliyemuita baada ya kuona muda mrefu umepita na mwanae hajatoka ndani, Erica alitoka na kumsalimia mama yake, mama yake alimuangalia na kumuuliza,
“Vipi mbona macho yamekuvimba hivyo?”
Erica hakuweza kujizuia kwa mama yake, alijikuta akimfata na kumkumbatia huku akianza tena kulia, mama yake akamwambia,
“Wewe vipi tena, kama babako kafa mara ya pili jamani? Kilio hiko vipi mwanangu eeeh!”
“Mama, leo nimeamini maneno yako kuwa mwanaume sio wa kumuamini”
“Eeeeh vipi tena? Ila kila siku nakuambia, mwanaume sio ndugu yako mwanangu”
“Kwakweli mama Erick kanifanyia kitu ambacho sielewi mpaka muda huu”
“Niambie mamako usinifiche, nilishakwambia mimi ni rafiki yako kwahiyo kuwa huru kusema chochote”
Erica alianza kumuelezea mama yake yaliyotokea kwa Erick na jinsi Sia alivyomtumia picha Erica,
“Ooooh katoto kangu jamani, kwanza tulia, tuliza akili zako, usipaniki, hayo mambo ni ya kawaida tu na huwatokea wengi sana. Tuliza akili, hakuna sehemu imeandikwa kuwa Erick ni mwanaume peke yake kwahiyo hakuna wengine, hapana wapo. Na sio kwamba nilivyosema wanaume hawajatulia basin i wote, hapana waliotulia wapo sema tu ni ngumu kuwatambua sababu tumezoea msemo kuwa samaki mmoja akioza basi wote wameoza”
“Lakini mama kwanini anifanyie hivi? Kwanini lakini? Kwanini nina mkosi hivi juu ya mapenzi? Sina raha mama, kwanini mimi?”
“Hapana, usijiumize kichwa sana. Ngoja nikuulize, hizo picha Erick alipigwa akiwa anachekelea kabisa kuwa na Sia au?”
“Hapana alikuwa amelala”
“Basi huna sababu ya kupata presha mwanangu, ingawa wanaume ni waongo ila bado anayetakiwa kukupa majibu ni Erick. Ndoa ni uvumilivu mwanangu, na uvumilivu unaanzia kwenye mahusiano. Sikia nikwambie, usipaniki wala nini, muulize Erick kwa upendo tu na atakwambia ukweli”
“Nitawezaje kumuuliza kwa upendo mama ikiwa nimeumia hivi?”
“Ndiomana nakwambia shusha presha, shusha hasira, ukiona upo sawa ndio umuulize. Kumbuka Sia ni rafiki mkubwa wa Tumaini, kwahiyo kuna uwezekano mkubwa hata Erick hajui kama alipigwa picha, kwahiyo wewe tulia na umuulize”
“Ikiwa kama ni kweli mama?”
“Ikiwa kweli maamuzi ni yako kusuka au kunyoa ila uvumilivu unaanzia kwenye mahusiano”
“Uvumilivu wa kumvumilia mwanaume muhuni mama?”
“Sasa kuna asiyekuwa muhuni?”
“Bahati mama ni mpole, hana hayo mambo”
“Kwahiyo unataka Bahati amuache mkewe na akuoe wewe, au unataka kuwa mke wa pili? Hebu nitolee ujinga mie, wewe mwenyewe ulikuwa unaimba wimbo hapa nampenda Erick, nampenda Erick, mvumilie ndio maradhi yako hayo”
Erica alizidi kunyong’onyea ila mamake alivyoona vile aliamua kumbembeleza, sasa maana alimuona kakosa raha kabisa,
“Aaah mwanangu jamani usijali, Erick ataongea nawe vizuri tu. Halafu mwanangu acha kupenda sana utaumia, nipende mimi mama yako niliyekubeba tumboni miezi tisa sio Erick aliyekufahamu ukubwani, usiwe kama Sia, kifo cha mama yake hajajaribu kujiua ila kuachwa na mwanaume amejaribu kujiua, na tena hata ajisikiliziii vizuri, kashapona na kwenda kwa mwanaume, Yule hana akili mwanangu, usiwe vile, sawa mama”
“Sawa mama, nimeelewa”
Basi mamake alimtaka Erica aoge na avae vizuri na awe na amani tu.
Mchana wa siku hiyo, Erica akiwa chumbani alisikia mama yake akimtimua mtu akataka kujua kuwa anayetimuliwa ni nani, akatoka na kushangaa ni Derick alifika na mama yake, alimsikia mama ake akisema,
“Wewe mama sina shida na wewe ila huyu mwanao simtaki kabisa hapa kwangu, mtoto mchawi huyu”
“Lakini kaja kuomba msamaha”
“Msamaha kitu gani wa kichawi, mtoto hafai huyo alitaka kumbaka mwanangu”
Inaonekana hata mama Derick hakulijua hilo kwani alishtuka sana kusikia mwanae alitaka kumbaka Erica, ilibidi amtulize kwanza mama Erica ili wakae wakizungumza, mwishowe mama Erica alikubali kuwakaribisha ila kiukweli hakupenda kabisa uwepo Derick mahali pale.
Erica alipowaona ni wao, alirudi zake chumbani kwake tu kwani hata yeye hakutaka uwepo wa Derrick ukizingatia kamuaibisha sana.
Basi akawasha tena simu yake, na muda huo huo Rahim akampigia simu tena, kiukweli hakujisikia kuipokea kwahiyo aliiacha iite hadi ikatike.
Kisha akajaribu tena kuipiga namba ya Erick napo haikupatikana na kuzidi kumtia simanzi, akachukia sana, huku asitamani hata kuongea na mtu mwingine kwa wakati huo, ila mama yake alimuita maana Derick alienda kuomba msamaha, kwahiyo muda huu Erica alienda kuwasikiliza sera zao, akawasalimia pale na kukaa, mama yake akaongea,
“Haya, wewe Derick, omba msamaha kwa Erica kwa hayo madudu uliyomfanyia”
“Erica, naomba unisamehe sana, nimefanya kitu ambacho hakitakiwi kabisa, sisi ni ndugu Erica na tuishi kindugu, sisi ni dada na kaka kwahiyo tupendane na tuishi vizuri”
Sababu erica hakutaka kuweka maongezi marefu akaamua kumsamehe tu, muda huo mtoto wa Erica aliyekuwa amelala aliamka na kulia kiasi na kuanza kwenda sebleni, kwahiyo Erica alimchukua mwanae na kumpakata, ila mama Derick akasema,
“Jamani huyu mtoto sikumuona alivyokua, daha kafanana na mtoto mtoto wa ndugu yangu anaitwa Rahim”
Derick akadakia,
“Ndio baba yake huyo, kumbe mama hujui?’
“Babake!”
“Ndio mama”
Mama Derick alimuangalia Erica na kumwambia,
“Kheee pole Erica, ulianzaje kuzaa na Yule? Yani matendo yake Yule si mazuri hata kidogo ila mamake huwa haamini kama mwanae mchafu hata umwambie vipi, sina cha kuficha wala cha kukupa moyo, kwakweli Rahim hakufai”
Erica akasema kwa aibu maana hakutaka mama Derick ajue ila mambo yote yako wazi,
“Ila nilishaachana nae huyo Rahim”
“Kwakweli pole yani pole sana, Yule ndugu yangu mtoto amepata ni John tu, ni mpole na anapenda kweli ila sio Rahim, hata mke wa kuoa hakujua amuoe nani, ikabidi babake amuolee tu mke, yani Rahim sijui labda akikuua ataacha ila pole sana”
Mamake Erica nae hakutaka hayo mambo ya kujadiliana kuhusu Rahim ilihali ni Rahim aliyeharibu maisha ya mwanae kwahiyo aliikatisha ile mada,
“Jamani sitaki kusikia habari za huyo mtu, huyu ni mjukuu wangu na atabaki kwenye himaya yangu, badilisheni mada kama zimeesha ondokeni”
Mamake Erica alionekana kuwa na kirirani tu kila muda. Basi waliongee ongea na kuaga ambapo walishikana mikono na kuagana.
Jioni ilipofika mama Erica alimuuliza mwanae,
“Kwanza Erica ni nani alikutumia picha na ujumbe kwamba Erick yupo na Sia?”
“Ni Sia mama”
“Aaah! Kumbe, mwenzio anataka kukurusha roho tu sasa wewe usionyeshe kama umeumia wala nini, onyesha kuwa upo kawaida kabisa, nay eye ndio atajisikia vibaya”
“Ila mama dah mapenzi haya, hapana kwakweli”
“Mapenzi ndivyo yalivyo mwanangu, kuna wakati utacheka na kuna wakati utalia, ndio mapenzi hayo”
Erica aliachana na mama yake na kwenda kufanya shughuli zake zingine.
Hadi usiku unaingia Erica hakutafutwa na Erick, swala hilo lilimuumiza moyo sana na kumfanya akose raha kabisa, hakuwa na usingizi ingawa ilikuwa ni usiku hivyo akachukua simu na kuingia kwenye mtandao ili kuone kama kuna jipya lolote labda Erick amemtumia ujumbe hakuona , ila leo aliamua kukagua akaunti ya Erick akaona hakuweka picha yoyote kwenye akaunti yake zaidi ya picha za maua na ujumbe ujumbe, akajiuliza kwanini hakuweka picha? Hakujua sababu, akaangalia na marafiki zake, akaona wote wale wa kwenye ofisi ya Erick ni marafiki zake, akiwemo na Sia, yani alijikuta akitamani sana kujua namba ya siri ya Erick ili ajiridhishe kuwa anaongeaga na nani mule kwenye mtandao. Akaona kuna jumbe Fulani kwenye ukurasa wa wazi wa Erick, akaona wa kwanza ukitoka kwa msichana,
“Erick nilikutafuta kweli, natumai wewe ndio Erick wangu wa kipindi kile”
Huo ujumbe ulitumwa jana, aliona moyo wake ukipasuka tu kwa wivu, akazidi kuangalia na kuona zingine za kawaida ila moyo ulikuwa unamuuma sana, mara akatumiwa ujumbe na Sia,
“Hulali shoga yangu, saa sita hii upo facebook! Pole sana, mapenzi yatakuua. Pole eeeh! Ila ndio ujifunze, sio kubambikia wanaume watoto, kwa taarifa yako shughuli niliyoifanya jana kwahakika nimepata mimba ya Erick na nitazaa nae uone kama atakufikiria wewe”
Erica aliumia sana ila alijiuliza kuwa huyu anayenishangaa silali, yeye amelala? Akamjibu
“Na wewe mbona hujalala? Na safari hii utakunywa sumu ya panya ufe kabisa, Erick ananipenda ingawa sijazaa nae ila ananipenda, unaweza ukazaa nae na asikupende, aliyekwambia kuzaa na mwanaume ndio kupendwa nani? Pole sana”
Aliamua nae kuwa na ujasiri kuliko kuendelea kujiumiza moyo, sia akamjibu tena
“Kama anakupenda mbona yupo na mimi?”
Erica akamjibu tena ili Sia aone kuwa hajaumia,
“Kuwa nae sio kwamba anakupenda sana, kuna watu hadi wanaolewa na hawapendwi kwahiyo kuwa nae wala sio sababu hiyo. Wewe hupendwi na ndiomana ukajaribu hata kujiua, ila mwenzio nina uhakika napendwa yani hata iweje Erick ananipenda sana, na kwa taarifa yako unafikiri kwa vipicha vyako ndio nitamuacha Erick! Hiyo haipo dada, tafuta njia nyingine”
“Yani Erica unanijibu hivyo?”
“Ndio, ulitaka nikujibu vipi? Na saivi hadi ndoa yani usage kabisa vichupa uchanganye na sumu ya panya unywe ili usiamke tena sababu kila ukishtuka tu utanikuta nae”
Sia hakumtumia tena ujumbe Erica, na kumfanya Erica ahisi kuwa Sian aye kaumizwa nay ale maneno, akaamua kuzima data sasa na kuweka simu pembeni ila kiukweli alikuwa akijikaza tu ingawa moyo ulimuuma sana kuhusu Erick.
Alijaribu kulala ila usingizi ulimpa kwa shida sana maana alilala saa kumi usiku.