Simulizi: Nini maana ya mapenzi

Simulizi: Nini maana ya mapenzi

SEHEMU YA 376

Leo ndio ilikuwa siku ambayo Dora na Sia walipanga kwenda kwa babu wa Bagamoyo, kwahiyo walikutana na kuanza safari ya kwenda kwa huyo Babu ambapo alianza kuingia Dora na kueleza azma yake kisha akaonyeshwa wabaya wa Erica walioshiriki kumletea ule ugonjwa alishangaa kuona Derick nae aliungana na wale wanawake, Yule mganga akamueleza,
“Yani ni hivi, huyu mwanamke wa kwanza alienda kwa huyu mwanaume kuchukua majina ya huyo binti na kisha alipotajiwa akamtumia huyu mwanamke wa pili kisha huyu mwanamke wa pili ndio alimuendea kwa huyu mzee na kumfanya walivyomfanya, lengo lao walitaka awe chizi na mwisho wa siku rafiki yako angegongwa na gari na kufa, sema haijawezekana kuwa chizi maana rafiki yako ana imani kubwa sana na Mungu. Ila mimi nitakusaidia kukupa dawa ya kumponya kabisa na tunaweza kuwarudishia wale makombora”
“Ila ndugu zake wamekazana na maombi”
“Hii dawa waambie waache hayo maombi yao maana miungu ndio itamsaidia huyo mgonjwa wao”
“Sasa sitaweza maana hata wakiniona wananitimua, hivi nitawezaje kuwaambia waache maombi na waamini hizi dawa?”
“Najua unanijua dawa zangu huwa haziongopi na hakuna kinachoshindikana kwangu, vyote vinawezekana kuna dawa ya kunywa nitakupa ambapo muda nitakayokupa utainywa, na leo ukirudi kwako unainywa halafu kesho jiandae nenda kwa huyo rafiki yako, ukiwa unakaribia kwao inywe baada ya hapo hakikisha unaingia kwao saa saba mchana, ukiingia tu kwanza watakuwa na mshangao wa ulivyopendeza, kitendo cha wewe kuwapa salamu kitafanya wasikilize kila utakacho waambia ndio utaanza kufanya dawa kama nilivyokuelekeza na keshokutwa mtamleta huyo mgonjwa hapa kwangu ili apone kabisa maana akija hapa ndio funga kazi, yani usijali hao wenyewe watambeba mgonjwa wao na kumleta hapa, yani kwangu hakuna kinachoshindikana yani wasiokusikiliza watakusikiliza, mimi ndio kila kitu, ukisikia wananisifia babu wa Bagamoyo ujue kuna kitu kwangu ambacho wengine hawana”
Kwakweli Dora alifurahi sana kwani alitamani siku zote kupata dawa ya kusikilizwa kila anachosema, alimshukuru Yule mganga ambapo alimpa kwanza dawa hiyo ya kusikilizwa na kuinywa kama alivyoelekezwa kisha nyingine aliambiwa anywe akifika na nyingine akifika kwakina Erica, kisha akampa dawa za kumfanyia Erica na maelekezo kuwa nyingine amnyweshe na nyingine amuogeshe. Dora alishukuru sana na kuulizia ile dawa ya kusikilizwa vizuri,
“Kwahiyo nitasikilizwa na kila mtu?”
“Yani hii dawa inaenda kulainisha matamshi yako, hakuna utakachosema kisisikilizwe, hii ndio hutumiwa na wanasiasa wengi sana. Sababu wewe umekuwa mteja wangu mzuri ndiomana nimekupa, unaweza shangaa mtu kaja kakwambia jambo la ajabu tu ila umemfuta kumbe sababu yah ii dawa, matapeli wengi huitumia ndiomana anamlainisha mtu kwa maneno na mtu anatoa kila kitu baada ya hapo anajuta maana maneno yale hayana ukweli hata kidogo”
“Kwahiyo hata hawa wanaojifanya wanapenda maombi”
“Achana na habari za maombi kwangu, wewe ukifika anza na salamu ili sauti yako yenye kivutio iwaingie masikioni na hapo unajikuta umewalainisha na gafla wanaanza kukusikiliza wewe”
“Oooh asante sana babu, nashukuru sana”
Kisha akatoa laki tatu kwenye chungu cha babu kama hela ya shukrani halafu akatoka na Sia kuingia, aliambiwa aweke kifungua kilinge akatakiwa kuweka elfu hamsini sababu ya swala lake, basi Sia aliweka ile pesa, Yule babau akamwambia,
“Usishangae pesa ndefu ni sababu kazi yangu ni ya uhakika yani ukitoka hapa, leo ukimfanyia huyo mtu hiyo dawa basi nakwambia hafurukuti kwako”
Kisha akampa dawa kama alizopewa Dora za kumvuta James, ila yeye alitaka na dawa nyingine ya kumuita Erick ili aweze kumpa hiyo dawa,
“Sawa sawa, hapa hakuna kinachoshindikana ila kukuongeza dawa nyingine inabidi uandae elfu hamsini nyingine ya shukrani”
“Sawa hakuna tatizo”
Basi Yule mganga akampa dawa nyingine Sia ya kuchoma ili kumvuta Erick na akifika ampe tunda atakalokuwa ameweka dawa kisha ampe Erick na baada ya hapo ndio ampe chakula chenye dawa ili awe wake kabisa,
“Kwahiyo hii ya kuchoma uwe unachoma huku unasema Erick njoo yani unasema hivyo mpaka utakapomaliza, utaona mwenyewe yani atakuja bila kumuita sasa ndio umpe hilo tunda ale yani jitahidi kumlaghai ale hilo tunda. Ila ni vizuri uchome mchana ili jioni afike maana anaweza akalala huko huko na inakuwa rahisi kumpa chakula chenye dawa”
“Sawa, nashukuru sana”
Basi akatoa na ile hela ya shukrani na kutoka nje kisha kuongozana na Dora huku wakiondoka, yani njia nzima alikuwa akimshukuru Dora kwa kumpeleka kwa Yule mtaalamu,
“Yani sina la kukwambia nashukuru sana”
“Wewe usijali, mambo yakishakamilika niite nije nimuone shemeji”
“Sawa, hata usijali”
Muda huo Dora hakuelewa kuwa anayefanyiwa hizo dawa ni Erick Yule Yule mchumba wa Erica.

Bite alitulia na mdogo wake akiendelea kumfanyisha mazoezi mazoezi ya baadhi ya vitu, akapiga simu Yule mwanamaombi na kuwaambia kuwa amesharudi kwahiyo ataenda kesho yake kwaajili ya kumuangalia Erica na kufanya maombi pamoja nao,
“Kwahiyo utafika muda gani?”
“Nitafika nadhani mchana sababu nahitaji tufanye maombi na tusome neno kiasi”
“Karibu sana”
Bite alishukuru na kuagana nae, mama yao alivyofika alimwambia jinsi alivyoongea na Yule mwanamaombi,
“Oooh afadhali aje, nahamu sana ya kumfahamu huyo mama maana kanitia moyo sana yani sana kwa kipindi hiki cha Erica, namshukuru sana kwakweli, amakweli Mungu kamtumia huyu mama”
“Basi kesho anakuja mama”
Basi mama Erica alikaa na mwanae Erica huku akifurahi tu maana alivyoambiwa Yule mama anafika alijikuta akipata amani ya moyo kabisa.
Jioni yake alifika Erick kama kawaida ila kumuuliza chochote hawakuweza na walimwambia tu kuwa Yule mwanamaombi anafika kesho, akauliza tu ni muda gani,
“Kwahiyo kesho saa ngapi?”
“Kasema mchana”
“Kesho kuna kazi nilikuwa nataka kuzimalizia ila nitakuja kwaajili ya hayo maombi kwani hata mimi najiona nikihitaji maombi pia”
“Karibu sana”
Basi Erick aliendelea kuongea ongea na Erica pale kwani yeye ilikuwa fahari tu kwake kila anapoongea na Erica.
Ila Rrick na siku hiyo aliporudi hotelini alijaribu kumpigia tena Rahim kwani alitaka kujua ukweli wa ile hela.
 
SEHEMU YA 377

Salma aliruhusiwa kurudi nyumbani, basi Rahim akamchukua kwenye gari yake na kurudi nae nyumbani, alifika nae huku akimpa pole kw akumpiga,
“Pole ya nini unanipa shetani mkubwa wewe”
“Kheee nimekuwa shetani!”
“Ndio ni shetani wewe, huna upendo hata kidogo mwanaume gani wewe. Ni malaya ila nakuvumilia, nimekuvumilia sana hadi kukuzalia mtoto ila mwanaume huna huruma unathubutu kunipiga kweli mwanamke nikiwa na mtoto mchanga kama huyu? Yani nyie wanaume mnapenda sana kutuonea wanawake”
“Wewe endelea kuongea ila dawa yako wewe ni kukuolea mke wa pili”
“Thubutuuu mlete huyo mke uone kama hajaondoka anatambaa”
“Hivi hujionei huruma Salma, kumbuka ndio kwanza umetoka hospitali. Huwezi kunyamaza”
“Sitanyamaza kamwe hadi uache uonevu wako, mmezidi kutuonea ila tunyamaze kama samaki baharini kameza maji, jamani mimi sinyamazi yani Rahim ukifikiri nitanyamaza sahau, siwezi kuvumilia uonevu kama huu”
“Aaah wewe, nadhani unanitafutia lingine, kwaheri”
Rahim aliamua kuondoka, ila Neema sababu alikuwa nje alisikia yale maongezi na kuingia ndani kwa mwenzake na kumpa pole ya ile kupigwa, ila Salma aliitikia kwa chuki maana hakuwa na furaha,
“Usiwe hivyo mwanamke mwenzangu, najua umeumia. Ni kweli wanaume wana roho mbaya ila sio wote. Unajua unaposema kwa mtu kuwa mwanaume kanipiga bila makosa na kukwambia umueleze chanzo hakika ukimueleza chanzo kama chako atakuona kuwa wewe ndiye mwenye makosa, siku ile nimeongea na wewe kuwa inatakiwa tujue wanaume zetu wanapenda nini ili tuenende na kile wanachopenda ila hukutaka kunisikiliza”
“Wewe Neema unaongea tu ila mwenzako akinyolewa zako tia maji”
“Sio hivyo Salma, ionekane kweli umeonewa labda mwanaume kaanza tu kukupiga bila sababu ila sio kama ulivyofanya wewe yani unampa sababu mwanaume ya kukupiga. Nakupenda rafiki yangu, nakupenda kama mwanamke mwenzangu ila napenda ujirekebishe na uwe mpya rafiki yangu. Nakwambia kila siku hakuna mwanaume anayependa mwanamke mwenye gubu, hakuna mwanaume anayependa mwanamke wa kubishana nae ndani ya nyumba, hakuna mwanaume anayependa mwanamke mkorofi na hakuna mwanume anayependa mwanamke mshirikina”
“Kwahiyo mimi unaniona mshirikina eeeh!”
“Kama unachoma dawa ambazo mumewe hazifahamu unafikiri ni nini? Unafikiri mumeo atakuitaje? Hivi mfano mumeo angeingia chumbani na kukukuta mkewe ukiswali angefikia hiyo hali ya kukupiga? Na kama angekupiga basi Mungu angemfundisha somo ila sio kwa ulichokuwa unafanya wewe, yani unampa mwanaume sababu za kukupiga, sio vizuri ndugu yangu. Tumeamua kuolewa basi tutulie kwenye ndoa zetu na tuwatii waume zetu”
“Kwahiyo wewe mambo uliyofundwa huko wakati unaolewa ndio unaniletea mimi eeeh! Mwanaume akuonee umuangalie tu, mwanaume akutukane umuangalie tu, siwezi kwakweli”
“Salma nadhani hunielewi, kuna mambo mtu ukifanyiwa kweli kila mtu anajua kama unaonewa lakini sio kwa stahili unayoenda nayo wewe, yani wewe ndiye unayempa sababu Rahim amfikirie Erica, ila ungejirekebisha kwa hakika angeamua kuishi nawe kwa upendo”
“Ngoja nilale mie nimekusikia”
Basi Neema alitoka ila kwa kiasi Fulani maneno aliyosema Neema yalimuingia kwani ukizingatia hata ile dawa kuifanya ilikuwa ngumu kwahiyo alijikuta akielewa tu taratibu kile kilichosemwa na Neema.

Ilikuwa ni jioni ambapo Dora na Sia walifika mjini na kuachana, basi Dora alienda kwao moja kwa moja akanywa ile dawa, alitaka kujaribu kuona inavyofanya kazi, akampigia simu mzee Jimmy akimuomba waonane ili waongee, yani mzee Jimmy alikubali kiurahisi sana, na kwenye mida ya saa tatu usiku wakakutana, Dora alianza kumueleza mzee Jimmy anachotaka ili kuangalia kama huyu mzee atamuelewa au la,
“Nimechoka kutembea kwa miguu, nahitaji gari la kutembelea”
“Umeniambia kwa haraka sana Dora, ila nitakupatia”
Kwakweli Dora hakuamini maana alikuwa akijaribisha tu kuona ile dawa inavyofanya kazi, kwahiyo swala la kukubaliwa na mzee Jimmy kwake ulikuwa ni ushindi mkubwa sana, kisha akamwambia tena,
“Sina hela ya kutumia ujue, halafu kesho nataka kwenda saluni nikatengeneze nywele na ninataka kununua nguo nyingine na viatu”
“Kwahiyo unataka kiasi gani?”
“Naomba milioni nne”
“Sikia basi, leo nitakupa milioni mbili halafu kesho njoo ofisini kwangu uchukue mbili nyingine”
“Wow, nitakuja kesho asubuhi mpenzi wangu”
“Kitu kingine ningependa unioe”
“Mmmmh kuna nini leo mbona kila kitu nakuitikia Dora?”
Ikabidi Dora abadilishe mada maana huyu mzee asije akamshtukia bure, akamuuliza kuwa gari la kutembelea atampa lini,
“Kesho njoo ofisini kuchukua hizo milioni mbili zingine halafu nitaangalia utaratibu wa wewe kupata gari maana kidogo sasa hivi mambo yangu hayajakaa sawa”
“Nashukuru sana”
“Halafu leo si utanipa tena”
“Mmmh leo nimechoka labda kesho”
“Sawa hakuna tatizo”
Yani Dora alifurahi sana vile ambavyo amesikilizwa vizuri na mzee Jimmy kisha akataka kuondoka kwahiyo Mzee Jimmy akaenda na Dora ATM na kutoa milioni mbili akamkabidhi Dora kisha kumpeleka kwao, yani Dora aliingia kwao akichekelea sana. Alienda chumbani kwake akiwa na furaha isiyo kifani na kujisemea,
“Hivi nilikuwa wapi kunua hizi dawa jamani! Sasa hivi ningekuwa tajiri mimi maana kila kitu ningekuwa nacho, huyu mzee leo kalainika kama sio yeye, kesho naenda kwa huyu mzee kwanza kuchukua hela yangu kisha naenda kwakina Erica kuharibu kabisa, hakuna cha maombi wala nini na wao wataanza kama mimi kuzunguka kwa waganga tuwe wengi mjini”
Akacheka na kujilaza kwa furaha maana kwake ilikuwa ni ushindi mkubwa sana.
 
SEHEMU YA 378

Dora asubuhi na mapema aliamka na kujiandaa kisha akanywa ile dawa na kwenye mida ya saa tatu akaenda ofisini kwa mzee Jimmy, alifika na kumkuta Yule mzee ofisini kwake na kumsalimia, Yule mzee alitabasamu tu kisha kumwambia,
“Dora umekuwa mrembo sana, yani nakuona unazidi kupendeza”
Dora alikuwa akicheka huku kimoyomoyo akisema ‘mambo ya babu wa Bagamoyo haya’
Basi kabla hata hajaeleza swala la kufata pesa, alikuta Yule mzee kashamuwekea pesa kwenye bahasha na kumpatia ila Dora akamwambia,
“Ningeomba uniongezee mbili nyingine”
“Dora, saivi sipo vizuri sana maana mambo yamejichanganya ila usichukie ngoja nikakutolee”
Dora alisubiria na mzee Jimmy alienda kumtolea milioni mbili zingine na kuja kumkabidhi kisha akaahidiana nae kuonana jioni, halafu Dora akaondoka.
Mzee Jimmy alijiuliza sana kuwa inakuwaje amekuwa hivyo kwa Dora, yani Dora anakomba hela zake kama kitu gani. Hakuelewa ila alijiona ni sawa kabisa kumpa zile pesa Dora wakati gata alikuwa akihisi mambo kuwa sio sawa kwenye kampuni yake.
Dora aliondoka na kuelekea benki nyingine kuweka zile pesa alizopata kwa mzee Jimmy kisha akapitia mahali ale kabisa akivuta vuta muda wa kwenda kwakina Erica.

Erick siku hiyo alienda mapema kabisa kwakina Erica maana alitaka Yule mwanamaombi amkute tayari akiwa amefika, aliowakuta pale ni Bite, mamake Erica, Angel na Erica mwenyewe maana Mage siku hiyo alisema hatoweza kufika sababu alikuwa na mambo mengi ya kufanya. Baada ya muda waliwasiliana na Yule mwanamaombi na kumuelekeza hapo na alipofika kituoni ni Erick ndio alienda kumfata na gari yake huyo mwanamaombi, alifika kituoni na kukutana nae na kumsalimia kisha kupanda kwenye gari yake ila gafla akajisikia kama kwenda kwa Sia yani hakuwa na raha kabisa mule kwenye gari alitaka tu amfikishe Yule mwanamaombi kwakina Erica halafu yeye kuondoka, walifika kwakina Erica na kushuka, kisha kuongozana na Yule mama hadi ndani ila walipoingia tu ndani Erick alitaka kuaga ili aondoke ila Yule mama alimwambia asiondoke kwanza hadi wamshukuru Mungu, Erick alikubali ila alikuwa akitaka waombe haraka haraka na waondoke, Yule mama alianza maombi na yale maombi yake yalichukua kama robo saa hivi yani Erick hakupenda kwakweli ingawa alisema kuwa nay eye anahitaji hayo maombi ila kwa muda huo moyo wake haukuwa kwenye maombi hayo kabisa, basi walipomaliza, aliaga tena na kutaka kuondoka.
Yule mama alimshika mkono Erick kabla hajaondoka, Erick alihisi kama kuna moto unaingia kwenye mwili wake na kujikuta akianza kupiga kelele basi Yule mama alianza kumuombea Erick yani Yule mama hakushughulika kwanza na Erica aliyemgonjwa ila alishughulika na Erick maana aliona kuna kitu hakipo sawa kwa Erick, alimuombea sana Erick tena kwa muda mrefu, Erick alijikuta tu akikaa chini huku akilia na bila kujua anacholia ni kitu gani, huyu mama alipomaliza kuomba alimwambia Erick,
“Kuna nguvu za giza zilikuwa zinakuta mwanangu ila Mungu ni mwema. Roho wa Bwana alinionyesha nikuombee na sasa uko huru”
Kisha Yule mwanamke akawaomba waimbe pamoja nae nyimbo za kuabudu wakaanza kuimba, na wakati wa kuimba kuna mtu akafungua mlango na kuingia ndani, mtu huyo alikuwa ni Dora, halafu Dora kama alivyoshauriwa na Yule mganga wake alianza kwa salamu,
“Hali zenu jamani!”
Yule mama alihisi kuna kitu sio cha kawaida kipo kwa Yule msichana, wote walibaki wakimshangaa Dora, ila huyu mama alimvuta Dora mkono na alipomvuta tu Dora alianza kupiga kelele kama mtu mwenye mashetani ndipo Yule mama alianza kumuombea, Dora alianguka chini na kujikuta akisema kila kitu alichoambiwa kwa mganga yani hakuacha kitu aliropoka hadi dawa alizopewa na yule mganga, ndipo Yule mama alipokazana kumuombea Dora na alimuombea sana na kugundua kuwa Dora ana tatizo lingine la jinni mahaba, kwahiyo akafanya kazi ya kumuombea na hilo tatizo pia, ilichukua muda mrefu sana katika kumuombea Dora hadi akatoa dawa zote alizoenda nazo kwa wakati huo, kwakweli walishangaa sana kwani hakuna aliyeelewa kuwa Dora angekuja na dawa za namna ile maana lazima angeogopa sababu walishamwambia kuwa wamejikita kwenye maombi.
Alipomalizana nao ndipo alipoanza kumuombea Erica maana alishamuombeaga sana na maombi yake karibia yote ni juu ya ugonjwa uliompata Erica, alimuombea sana na baada ya muda Erica alisimama na kufanya ndugu zake wote wafurahi, Yule mama alianza kumshukuru Mungu kwa kumponya Erica.
Walipomaliza Erica alianza tena kuongea ila aliongea taratibu sema ilikuwa ni furaha sana kwani alikuwa akiongea, kwakweli waliomba kwa pamoja na hadi maombi yanamalizika Dora alijikuta hana hamu kabisa hata ya kurudi kwao alijikuta akitoa machozi tu kama anajutia kwa yale aliyokuwa akiyatenda.
Huyu mama aliwaeleza mambo yatakayowasaidia zaidi,
“Yani kuanzia sasa mnatakiwa kuwa watu wa maombi, sio kujutia tu yale uliyoyafanya nyuma ila kusimama imara na kuendelea mbele, inatakiwa tumuombe Mungu kila mara sio tu tunapopatwa na matatizo. Ukiacha kumuita Mungu basi shetani anaweza kukuangusha kwa urahisi mno. Kwahiyo ni muhimu sana kufanya ibada”
Wote waliitikia pale ila Erick hakujua kama ataweza kuanza kufanya ibada, halikadhalika na kwa upande wa Dora ila walisema kuwa watajitahidi.
Usiku ulipoingia ilibidi Erick aage kuwa anaenda kwao, ikabidi ampe lifti na Dora ya kurudi kwao muda huo Dora hakuwa hata mtu wa kuongea ongea tena mpaka alipofikishwa kwao na kushuka kisha Erick alirudi kwao moja kwa moja yani hakujisikia kabisa kwenda hotelini maana alikuwa na hamu ya kufika kwao.
 
SEHEMU YA 379

Sia alishangaa sana kuwa kufanya kote dawa mpaka jioni Erick hakufika kwao, aliumia mno na ukizingatia alishaandaa tunda la kumpa Erick, alipoona usiku umeingia alijiandaa na kusema ataenda yeye mwenyewe kwakina Erick kumpa lile tunda ale kwani ile hela aliyotoa kwa mganga ilimuuma sana alitaka apate majibu ya anachokitaka.
Basi akaondoka na kwenda kwakina Erick, alipofika aligonga na mlinzi alimfungulia, akamuuliza,
“Hivi leo Erick yupo?”
“Tena amefika muda sio mrefu”
Basi akasogea hadi kwenye nyumba ya kina Erick na kuingia ndani maana alishazoeleka pale sababu ya Tumaini, akakutana na Erick mlangoni ilionyesha kama Erick alikuwa akitoka, akamsalimia Erick kisha kumpa lile tunda,
“Nini tena?”
“Chukua hili apple ule Erick, ni ishara ya upendo wangu kwako”
Erick alichukua lile tunda na kumfanya Sia atabasamu kwani alijua Erick akila tu bnasi kwisha habari yake, ile cha kushangaza Erick alisogea mpaka kwenye ukuta wa nyumba yao na kulirushia lile tunda nje.


Erick alichukua lile tunda na kumfanya Sia atabasamu kwani alijua Erick akila tu basi kwisha habari yake, ila cha kushangaza Erick alisogea mpaka kwenye ukuta wa nyumba yao na kulirushia lile tunda nje.
Kitendo kile kilimuumiza sana Sia, alijikuta kama kapatwa na uchizi hivi hata akatamani kumpa matusi Erick, yani muda huo hakuwaza tunda ila aliwaza laki yake tu, aliamua akimbilie nje upande ambao Erick alirusha lile tunda maana hakutaka ile dawa ipotee, aliona vyema aliwahi ili afanye kila hila Erick ale lile tunda, kiukweli Erick pia alimshangaa jinsi alivyoonekana kushtushwa na kile kitendo cha kutupa tunda.
Sia alikimbia akatoka nje hata mlinzi wa ile nyumba akamshangaa kuwa huyu dada imekuwaje kachanganyikiwa au nini, alikimbia na kuzunguka ule upande ambao Erick alirusha tunda, hakuamini macho yake kuona kuna kijana yupo kulifakamia lile tunda, alimshtua
“Kheee wewe kwanini umeokota hilo tunda?”
“Dada jamani, nilikuwa napita na hili tunda likanipiga kichwani kwa bahati nimelidaka ila najua matajiri wana hela sana yani tunda kama hili la gharama linatupwa? Nikaamua kulila, ubaya wangu ni nini au kosa langu ni nini?”
Sia alichukia sana kwani huyu kaka ndio kwanza alikuwa akimalizia lile tunda, kiukweli Sia hakuwa na la kufanya na kuamua kuondoka hata kuingia tena kwakina Erick hakutaka.
Sia aliingia kwao kwenye mida ya saa tano usiku, wakati anafungua mlango kuingia ndani alishtukia kuna mtu nyuma yake, kumuangalia alikuwa ni Yule kijana aliyemkuta akila tunda,
“Kheee wewe umenifata hadi kwetu kwanini?”
“Nisamehe ila sijaweza kuacha kukuangalia kwa urembo wako, nakupenda sana, yani sijaweza kuacha uondoke machoni pangu, nimekufatilia toka pale hadi hapa”
Sia alipumua maana ya siku hiyo yalikuwa makubwa kwake, kufatiliwa na asiyehusika tena ni jambo lililomkera sana, akajiuliza afanyeje na Yule kijana hakujua, alimuacha nje na kufunga mlango kisha kuingia ndani na kulala kwani kichwa chake kilikuwa kimevurugika haswaa ukizingatia kuna chakula alishapika kwaajili ya Erick na alishamuwekea dawa atafanyaje sasa, hakuwa na la kufanya zaidi ya kukubali kile kilichotokea.
Palivyokucha aliamka na kutoa vyombo vichafu nje pamoja na kile chakula alichokuwa amemtayarishia Erick, kisha akaenda kuchota maji na kusahau kama kulikuwa na kijana usiku akimfatilia sababu alikula lile tunda, basi alivyorudi na maji yake alishangaa kumuona Yule kijana akila kile chakula, kwakweli Sia alishtuka sana,
“Mungu wangu na chakula umekula, uwiiii nitafanyaje mimi. Wewe nani kakuruhusu kula chakula changu?”
“Nilikuwa na njaa sana, nikahisi kuna chakula umekifunika kwenye hivi vyombo kuliko kukitupa nikaona bora nile.”
“Haya nenda kwenu”
“Siwezi kuondoka hadi uniambie kuwa unanipenda, nakupenda sana yani nakuona kama malaika”
“Kheee makubwa, sasa hapa kwangu utaumia, nenda zako tu”
“Siwezi, nakupenda sana”
Kwakweli huu ulikuwa ni mtihani mkubwa sana kwa Sia ingawa ingekuwa hivi kwa Erick ingekuwa ni ushindi mkubwa sana kwake, inamaana huyu kijana asingemuona Sia angepata shida sana kumtafuta ila uzuri Sia mwenyewe alitoka kuangalia tunda lake kuwa limeangukia wapi.

Salma alikuwa mpole gafla maana mumewe hakurudi kabisa tangu ameondoka sababu ya kelele zake, ana maumivu ya kupigwa na mumewe hataki kurudi, ila leo alipata ugeni yani mama yake na dada yake, walikuja kusalimia na kumkuta akiwa na mawazo sana, mdogo wake alikuwa na mtoto na ndiye aliyewapokea na kuwakaribisha, waliingia ndani na kuanza kumpa hongera Salma na pole maana hawakufika toka ajifungue, mamake alimuuliza kuwa imekuwaje hana furaha kuwaona,
“Mama nyie ni wabaya sana, yani kama sina ndugu vile, kweli nimejifungua hadi leo ndio mnakuja? Mimi hospitali nakuja kuangaliwa na wakwe na majirani sijui na ndugu wa mbali? Siku nimeruhusiwa sina wa kunifata kweli? Mlichonifanyia sio sawa, hata kama wewe sio mama yangu mzazi ila haikutakiwa unifanyie hivi, angekuwa ni mtoto wako wa kumzaa ungemfanyia hivi? Bora mama yangu mzazi angekuwepo kwakweli, nateseka sababu sina mama”
Yule mama alisema,
“Yani Salma hii ni sababu ya kufanya tushindwe kufika kwa muda, yani Salma huna zuri hata moja wewe, hivi mimi kama nina roho mbaya ningemuonyesha Yule mzee kuwa wewe ndiye unafaa kuwa mke wa mwanae? Kwanini nisingeonyesha hao wanangu ila nikakuonyesha wewe? Yani Salma unashindwa kuuliza tatizo ni nini ila unabaki na lawama tu”
“Wewe mama ndio zako tu huna lolote, sijui ningemuonyesha mzee Yule watoto wangu. Kama ipo ipo tu, hata ungeonyesha watoto wako labda wasingependwa, usijitetee wala nini mmenifanyia roho mbaya tu hakuna cha sababu wala nini, ulinionyeshea mimi sababu hukutaka nikae nyumbani, ulihisi nitakuja kuteseka kwenye ndoa kwa kuolewa na mtu nisiyemfahamu”
Kiukweli hawakumuelewa kuwa imekuwaje hadi maneno yote yale yanamtoka, ila mdogo wake ndio akasema,
“Dada ana hasira hivyo sababu alipigwa na shemeji”
“Halafu wewe hayakuhusu muone vile ndiomana hunenepi”
“Sasa wewe Salma ni mnene jamani! Hata unamsema mdogo wako bure tu”
“Kwanza sihitaji kuja kuniona, ondokeni siwataki nyumbani kwangu”
Hakuna walichoongea akawasikia zaidi zaidi akaamua kuwatimua tu ikabidi wabebe mizigo yao na waondoke.
Walipoondoka tu kama kawaida Neema alimfata Salma na kumuonya,
“Unajua Salma unafanya mambo kwa hasira sana, umeudhiana na mume ila unachukia hadi ndugu kwa mtindo huo utamuudhi hadi mama mkwe halafu utajikuta ukiiacha ndoa yako”
“Neema sikia, nikiachika mimi hapa si utabaki wewe mkwe mwema, sitaki mafundisho yako, kafundishe ndugu zako huko”
“Ila wewe dawa yako inachemka, najua wa kumleta kwako na utakaa sawa tu”
“Hebu nitolee upuuzi si umefurahi hivi mume wangu hajarudi nyumbani, niache mie”
Kwakweli Neema alisikitika sana vile mwenzake alikuwa haelekezeki.
 
SEHEMU YA 380

Dora leo aliamka na kutulia kwao huku akijitafakari sana, alikuwa akiwaza kuhusu mambo mbalimbali, mara nyingine aliona ni sawa kukombolewa ila mara nyingine aliwaza vitu vingine ila alijikosoa mwenyewe,
“Ila hela zisizokuwa na halali si nzuri kutumia, ila bora nilichukua kabisa hela za mzee Jimmy, asifikirire sijui nimebadilika ndio nitarudisha hela zake thubutuuu hii ni matunda ya kazi niliyofanya juu yao, ila mmmh kweli nilikuwa na jinni mimi mbona sijisikii hata hamu jamani, nipo kawaida kabisa. Ila kwa Yule mganga siendi tena yani tena, kwa Mungu ndio kuna nguvu kwakweli, kwa mganga hamna kitu. Ila mimi hii hali ya tamaa nadhani na mama yangu kasababusha maana anataka nilishe familia nzima bila kujali pesa nitatoa wapi”
Muda kidogo Mama yake alienda kumkurupua na kumwambia,
“Hivi Dora unajua kama mdogo wako hajarudi kabisa tangu jana”
“Aaaah mama jamani, hata salamu jamani! Hajarudi ndio ila mbona mimi sitafutwagi hivyo nisiporudi?”
“Wewe ushakuwa mkubwa, halafu nishakuchunga nimechoka ila mdogo wako hana tabia kama zako”
“Ila kumbuka Yule ni wa kiume na mimi ni wa kike yani ulitakiwa kunichunga mimi zaidi ya Yule ila unamchunga Yule na kuniacha mimi ni haki kweli hiyo?”
“Yule hajawahi kutokurudi nyumbani hata kama kakua ila sio kama wewe, mdogo wako hadi saa nne hii haonekani nakwambia hata hujali yani upo tu. Jiandae hapo tuanze kumuulizia mdogo wako maeneo mbalimbali”
Hiki ndio kitu ambacho hakupenda kwa mama yake huyu yani alionekana kumjali zaidi mdogo wake ambaye walipishana miaka miwili tu, yeye hakujaliwa kama mdogo wake alivyojaliwa, ni wa kiume ila hajaonekana nyumbani mama yake tumbo joto, hakujua ni wapi ataanza kumtafuta basi akaenda tu kuoga ili kujiweka sawa.
Alipotoka kuoga akakuta simu yake inaita, akaipokea na mpigaji alikuwa ni Sia,
“Eeeeh Sia, unatatizo gani?”
“Nina tatizo kubwa kwakweli”
“Tatizo gani?”
“Naomba njoo kwetu ili unisaidie hili tatizo nitalitatuaje, nakuomba sana nakuomba”
“Sawa hakuna shida nakuja”
Sababu aliona kuendelea kubaki kwao mama yake angemsumbua na hizo habari za kutokumuona mdogo wake, kwahiyo alijiandaa na kutoka na kuona ni veyema aende kwa kina Sia kuliko kubaki kwao.
Alivyofika kituoni, alimpigia simu Sia naye alienda kumpokea, basi akaanza kuongea nae tatizo alilokuwa nalo kulekule njiani,
“Ni hivi ndugu yangu maana ushakuwa ndugu yangu sasa, ile dawa niliyotakiwa kumuwekea Yule mwanaume kagoma kula tunda na kalitupa”
“Kalitupa? Eeeh ikawaje, nadhani jana kulikuwa na mikosi moja kwa moja maana hata mimi dawa zangu hazijafanikiwa kiasi kwamba sitaki tena kutegemea waganga, hebu nieleze imekuwaje?”
Basi Sia akamueleza jinsi alivyomkuta huyo kijana akila tunda na jinsi alivyofatwa na yule kijana na jinsi alivyukula kile chakula asubuhi.
“Uwiiii na chakula kala?”
“Ndio kala, yani hata sielewi nafanyaje na Yule kijana maana amekazana kuondoka hataki”
“Ila dawa za Yule babu kiboko, basi lile tunda huwa linakama sumaku yani asingekuona kijana wa watu angepata shida hadi angekoma ila vijana wengine waroho jamani unaona watu wanatupa halafu wewe unaokota na kula si uroho huo loh! Na tena hadi chakula kala sababu ile dawa inamvuta kula chakula ulichoweka dawa nyingine, uwiii ndio uwe nae sasa”
“Nitakuwaje nae? Kwanza simtaki halafu inaonyesha bado hana maisha, maswala ya kuishi na mtu mwenye shida ya nini? Nilikuwa namfanyia Yule sababu nilijua ningeishi kama malkia”
“Pole mwaya, sasa sijui nitakusaidiaje”
“Sijui ila naomba unisaidie yani maji yamenifika shingoni, siwezi kwakweli”
Basi wakaendelea kuongozana hadi nyumbani kwakina Sia kisha Sia akamuonyesha Dora kijana mwenyewe, Dora akashtuka sana na kuita,
“Kheee Steve!!!”
Sia akamuuliza,
“Unamfahamu kumbe!”
“Mdogo wangu huyu”
Dora alimfata Steve ambaye hakuwa hata na habari yoyote ile kwani aliona kama amefika pale kwa Sia.

Kwakina Erica ilikuwa ni furaha kubwa kumuona Erica akiwa mzima tena na walipokaa kumuuliza kuhusu hao wenye visasi nae waliomfanyia hayo mambo alishangaa pia maana hao watu hata hakuwa na ukaribu nao na wala hakuwafahamu ila ambaye alitajwa kuhusika pia ni Derick na ndiye aliyemuumiza zaidi kwani ni ndugu yake halafu kumfanyia mambo ya ajabu, Mage alipofika walimueleza yaliyotukia jana yake akashangaa sana na kuamua kumpigia simu Derick akimtaka aende tu ila hakusema kama Erica amepona, alilalamika kutimuliwa siku za nyuma ila mage alimkazania kuwa aende hatotimuliwa tena, basi derrick aliahidi kwenda muda huo.
Derick alifika pale na kuwakuta ndugu zake wakiwa ndani, alishangaa kumuona Erica ni mzima kabisa, Mage alimkalisha chini Derick na kumuuliza kwanini afanye hivyo,
“Hapana mimi sihusiki”
“Derick, kila mtu amekuona wewe kama muhusika hata sijui unakataa vipi? Unajua wewe ni ndugu yetu hivi huoni aibu kumfanyia hivyo ndugu yako?”
Muda huo Babuu na Rahim nao walifika kwani walitaka sana kuomba msamaha kwa kile kilichotokea kabla kwani bado Rahim hakuwa na furaha ya kufukuzwa kwakina Erica, ila kwavile leo walimkuta Derick akiwa kabanwa kwahiyo hawakufukuzwa, waliingia tu ndani na kusalimia kisha Derick kuendelea kutoa maelezo na muda huu aliamua kueleza alivyoulizwa na mke wa Rahim na jinsi mke wa Rahim alivyompa dawa,
“Kwahiyo mke wa Rahim ndiye aliyemfanyia Erica vitu vya ajabu?”
“Ndio, alinituma nimtajie majina matatu ya Erica, yeye aliniambia anataka Erica aachane na Rahim ila sikujua kama angempa ugonjwa kama ule, na siku ile alinipa dawa nimpake Erica kwenye paji la uso ila ni Fetty ndio alinizuia na mpaka muda huu sikujua alikuwa na maana gani”
“Hivi wewe Derick una akili kweli? Yani mtu anamteketeza ndugu yako sababu ya chuki zako unakubali? Yani wewe ni zero kabisa”
“Ila Mage nilikwambia, huyu dogo hamna kitu ona sasa Erica angekufa sababu ya mambo yake”
Muda huo akili ya Rahim ilipoteza dira kabisa kusikia mkewe ndio muhusika wa ugonjwa wa Erica na vile alivyomkuta na madawa ndio kabisa, aliinuka na kutoka bila kuaga na bila kuondoka na aliyefika nae, hakuna aliyemuelewa anaenda wapi ila aliondoka.
Pale kwakina Erica walibaki wakimsema Derick ila bado mama Erica hakutaka undugu na Derick kabisa maana aliona huyu mtoto ni muuwaji,
“Nipo tayari kujirekebisha”
“Hapana kwakweli, wewe uliyesababisha mwanangu achungulie kaburi, hapana kwakweli”
Baada yay ale maelezo mama Erica hakutaka maelezo mengine zaidi ya kumtimua tena Derick maana hakutaka kumuona kabisa.
 
SEHEMU YA 381

Basi Dora aliamua kumbembeleza mdogo wake pale ili arudi nae nyumbani, akamwambia Sia amwambie mdogo wake kuwa anampenda ili aweze kurudi nae nyumbani, yani mdogo wake ilionyesha kashaelemewa na mapenzi ya Sia, kiukweli ilimuuma sana Dora kuona dawa alizompeleka Sia zimeenda kumdhuru mdogo wake kwani muda wote atakuwa akimuwaza Sia na Sia ataona ni usumbufu sababu hajamtaka huyu dogo, kwakweli aliwaza sana kuwa atawezaje kumfanya mdogo wake awe sawa tena yani afanye tu kitu bila kumuwaza Sia, basi aliagana na Sia pale na kuondoka na mdogo wake ila mdogo wake njia nzima anamwambia dada yake jinsi Sia alivyo mzuri na jinsi anavyompenda,
“Mdogo wangu sio akili zako hizo umerogwa”
“Sijarogwa dada, nampenda Yule msichana yani nampenda kutoka moyoni”
Hakuna alichoongea kikasikilizwa basi wakaendelea tu kurudi nyumbani, walipofika njiani kuna mtu alisimamisha gari karibu yao alikuwa ni Erick akielekea nyumbani kwakina Erica, alimuuliza Dora kuwa anajisikiaje toka ile jana kutolewa yale mashetani, basi Erick alishusha kioo na Dora alisogea kuongea nae,
“Nijisikiaje wapi, nimezua makubwa na mambo yangu ya waganga”
“Kivipi?”
“Kuna mtu nimesoma nae chuo anaitwa Tumaini sasa nilikutana nae na rafiki yake anaitwa Sia, nilivyokuwa nawaeleza habari za mganga ndio Yule Sia akapenda sababu kuna mwanaume wake alitaka kumteka ndio nikaenda nae kwa huyo mganga halafu kibao kimegeuka kwa mdogo wangu”
“Sikuelewi, hebu nieleze vizuri”
Kwakweli Erick kitendo cha kusikia jina la dada yake na jina la Sia vikamchanganya sana na kujikuta akitaka kujua kilichoendelea, basi Dora alimueleza ilivyokuwa kama alivyoelezwa na Sia. Kwakweli Erick alijikuta akimchukia Sia kupita alivyomchukia mwanzo na akaelewa kuwa kwanini Sia alitaka kumpa tunda lile jana yake, pia alimuhurumia Yule mdogo wake Dora ambaye hakufikiri kuwa amerogwa ila alijua ni upendo tu upo kwa Sia.
Erick alifikiria kidogo kisha akachukua simu yake na kumpigia mama yake na Erica ili amuulize namba za yulee mwanamaombi, na baada ya salamu alimuomba hizo namba kisha mama yake Erica alimtumia.
Erick alipozipata aliwaambia wakina Dora kuwa wapande nae kwenye gari awasiliane na Yule mwanamaombi kisha wampeleke Yule mdogo wake, Dora alifanya hivyo na walipowasiliana na Yule mwanamaombi waliamua kuanza safari ya kwenda huko.
Walifika nyumbani kwa Yule mama ambapo alianza maombi kwa Yule kijana na alipomaliza alianza kuwafundish wote watatu,
“Mnatakiwa kumtegemea Mungu katika maisha yenu yani msijali chochote muangalieni Mungu tu”
Dora akauliza,
“Kwahiyo tuwe tunaomba kila muda”
“Ndio kila muda ni wakati wa kumuomba Mungu”
“Mmmh nitaweza kweli?”
“Kwanini usiweze? Hakuna kisischowezekana chini ya jua”
“Tatizo nyumbani kwetu, mama yetu mwenyewe hana hayo mambo ya dini, sijui kama nitaweza halafu kuomba sijui”
“Uwe unakuja hapa nikupeleke kanisani, kunakiuwa na vipindi vya maombi yani utajifunza humo kuomba hata usiwe na shaka”
Dora alikubali pale kuwa atajiunga na hiko kipindi, kisha huyu mwanamaombi aliendelea kumwambia,
“Yani msipokuwa makini na maombi hayo madudu yatawajia tena na sio mazuri kwakweli, mnatakiwa kukumbuka maombi”
Wakaitikia na kumuaga kisha wakaondoka na Dora kurudi nyumbani na mdogo wake huku Erick akibadilisha safari na kwenda kwakina Sia kwani hakupenda kabisa kile alichokisikia.

Neema kama alivyoahidi kuwa ataenda kumtafutia mtu ili aweze kuongea na Salma, na kweli alienda kuongea na mmama mmoja mshika dini haswaaa aliitwa Zainabu, alimwambia tatizo la ndugu yake na huyo mama aliacha shughuli zake ili akaongee nae kwani alijua kama wakimpa maneno ya dini basi ataacha kuwaza ujinga anaouwazaga, basi walifika pale na kumkuta Salma akiandaa vitu vyake vya kupika, Neema alimkaribisha Zainabu ili aongee na Salma, Zainabu alimsalimia Salma, ile salamu tu Salma akahisi kuna jambo kisha akasema,
“Neema nadhani kuna kitu unakitafuta na utakipata tu, mimi nimekwambia nahitaji mshauri? Umeniona mimi nina matatizo ya akili? Neema naomba uachane na mambo yangu, na kama wewe ni mshauri haswaa basi subiri mume wangu umshauri sio kuniletea mimi habari zisizoeleweka”
“Dada, hata kunisikiliza ninachotakanachotaka kusema jamani”
“Halafu wewe Zainabu unafikiri sikufahamu au nini? Kuolewa kwenyewe hujaolewa sasa utanishauri nini mimi kama sio utumbo? Achana na habari zangu”
Huyu Zainabu hakujua kama Salma anamfahamu kuwa anaitwa Zainabu na hajaolewa ila hakupenda vile alivyosemwa na Salma,
“Dada angalia kauli zako, naweza kuwa sijaolewa ila nikawa na kauli thabiti kushinda wewe, na sio kwamba sijaolewa basi sina tabia zinazofaa ila muda wangu tu haujafika”
“Huna lolote, umeamua kuja kumtamani mume wangu. Tena sitaki ushauri wako, na wewe Neema kama ndoa yako imekushinda achana na ndoa yangu”
Basi Zainabu akawa anatoka, na getini akakutana na Rahim ndio anataka kuingia ndani, akamsalimia ila Rahim alimuangalia sana Zainabu alipenda mavazi yake na ongea yake kwani alionekana ni mwanamke aliyejiheshimu ila kwavile alikuwa na ugomvi na mke wake akabaki tu akimuangalia Zainabu kisha Neema nae akatoka kumsindikiza Zainabu.
Rahim alienda hadi kwa mke wake na kumwambia,
“Siku ile nilikupiga ila leo sitakupiga, subiri hapo hapo”
Salma akiwa anashangaa tu maana hakuelewa ni nini kinakuja mbele yake, akashangaa Rahim akitoka ndani na karatasi la taraka huku akisema kuwa amemuacha na hamtambui tena kama mke wake toka siku hiyo.
 
SEHEMU YA 382

Erick moja kwa moja alienda kwakina Sia ila hakumkuta Sia muda huo kwa hakika kama angemkuta basi siku hiyo angekuwa halali yake maana alipanga kumpiga kwa hiko alichotaka kumfanyia na kujikuta akimchukia sana ingawa hakujua kama mdogo wake Dora itakuwaje ila alipata amani kiasi maana Yule dogo alishafanyiwa maombi, basi akaenda kwakina Erica na usiku ulikuwa umeshaingia, Erica alikuwa na furaha sana kipindi hiki hata mtoto wake Angel alikuwa na furaha pia, ila Erick alifurahi zaidi kumuona Erica akiongea vizuri kama mwanzo kiasi kwamba anaweza kuongea nae wakiwa wawili tu, nyumbani kwao walishaelewa kuwa wale wanapendana kwahiyo waliwapa nafasi ya kuweza kuongea, kwa muda huu Bite alitoa mkeka nje kisha Erick alikaa na Erica kwenye mkeka kwenye kibaraza cha nyumba ile huku wakiongea,
“Erica sikujua kama kwenu kuna mikeka”
“Ipo ila haina wakaliaji ndiomana ipo ndani tu muda wote”
“Halafu Erica nimefurahi sana, sijui kama unaweza kuona furaha yangu ilivyokubwa, ila kesho nitatimiza ahadi yangu”
“Ahadi gani?”
“Kesho nakuletea ile gari yako”
“Wow, asante Erick”
“Jifunze kuniita mume wangu sasa”
Erica akacheka tu maana neno mume wangu hakuwahi kulijaribisha katika ulimi wake, Erick akamuangalia na kumwambia,
“Usicheke mke wangu, mimi ni mume wako”
Erica bado alikuwa akicheka sana, ni mama Erica ndio aliingilia yale maongezi kwa kuwaambia kuwa pale nje kuna mbu wengi, kwahiyo waliingia ndani ila siku hiyo Erick aliongea kwa muda mrefu zaidi kwani alikuwa na furaha sana ya kuona Erica ni mzima kabisa.

Muda huu Sia alikuwa nyumbani kwakina Erick, lengo lake ilikuwa ni kuonana na Tumaini maana alimuita ila hakuthubutu kumwambia kuhusu habari za kwa mganga wala nini, alifika kule kisha Tumaini akaanza kumueleza azma ya alichomuitia,
“Nimekuita hapa ili tupange namna ya kwenda kwakina Erica”
“Basi twende kesho”
“Sawa, ila tumejipangeje?”
“Kwani tujipange vipi jamani Tumaini”
Basi Tumaini akamwambia namna alivyopanga kuwa wafanye na mama yake Erica anaweza kumruhusu Erick kuwa na Sia,
“Sikiliza tunafika pale kwa lengo la kumuona Erica na kufuta yote wanayofikiria kuwa sisi tumemroga Erica, baada ya hapo wewe Sia utasema kuwa una mimba ya Erick, nina uhakika mamake Erica ataelewa tu kwani pia ni mwanamke na anajua jinsi inavyosumbua kulea mimba na mtoto bila ya baba, kwahiyo atataka Erick awe karibu na wewe”
“Jamani Tumaini kwanini siku zote hizi tustumie njia hiyo, nimeipenda sana”
“Ndiomana nikakuita tujipange, Erick kanifukuza dukani kwake sababu ya Erica nina uhakika nah ii nyumba ingekuwa yake pia angenifukuza yani Yule Erica dah basi tu”
Wakakubaliana juu ya hilo jambo na wakaona njia pekee Sia ajifanye kila muda anaenda kutema mate, basi baada ya kupanga cha kufanya Sia aliamua kuondoka sasa na Tumaini kumsindikiza, njiani Sia akamuanza tena Tumaini,
“Hebu fikiria Tumaini ungekuwa na gari si ungenipeleka tu rafiki yako, hivi kweli Erick hana pesa za kukununulia gari?”
“Mwenzangu nilishamwambia hadi basi akasema mpaka mambo yake yakae sawa”
“Yani shoga yangu saivi ungekuwa unafurahia maisha tu hata sio kuhangaika kwa miguu mara vibajaji sijui pikipiki, nina uhakika Erick hela anayo ila anamalizia kwa Yule mjinga Erica”
“Hivi kweli Erick anaweza kumjali Erica kushinda anavyonijali mimi? Inawezekana kweli?”
“Kama haiwezekani mbona kakufukuza dukani!”
“Najua kanifukuza sababu ya hasira tu ila kuhusu gari Erick ataninunulia”
“Mfano ukute kamnunulia Erica kabla yako?”
“Hilo haliwezekani na hakika ikitokea hivyo nitamueleza baba ukweli wa kila kitu maana huwa simwambii mambo mengine ila kama ikifikia hiyo hali kweli nitamueleza baba na vile mamake Erick ambavyo hampendi Erica nitamwambia na yeye”
Basi wakaongea ongea na kukubaliana na maneno yao na muda wa kukutana kesho kisha wakaagana na Sia kupanda daladala la kurudi kwao.

Dora alirudi kwao na mdogo wake kiukweli mama yao alifurahi ila mdogo wake Dora alikuwa bado kama hayupo sawa maana alionekana yupo yupo tu, kisha hakuongea neno na kwenda kulala, Dora nae hata hakujisumbua kumueleza mama yake maana huwa hana maongezi sana na mama yake, alienda tu chumbani kwake, kuingia tu akapigiwa simu na James, akapokea,
“Dora, naomba nije nikuchukue yani hatujaonana jana, na leo naona kama mwaka. Niambie ulipo nije Dora”
Dora akasema kuwa atampigia ila akaona ni tatizo tayari maana alishatengeneza tatizo kwa James, ile anataka ampigie Erick amuombe namba ya mwanamaombi ili ampigie mwenyewe ajieleze na alichomfanyia James, gafla akapigiwa simu na mzee Jimmy, Dora alipokea ila kwa mashaka kiasi, leo mzee Jimmy hakuwa hata na salamu aliazna tu kusema maneno,
“Msichana tapeli wewe, yani umenitapeli hela zangu hivi hivi kwahiyo na gari langu lingetoka yani sina hamu na wewe na nitakufundisha dunia ilivyo”
“Sasa mimi nimekutapeli wapi na umenipa mwenyewe?”
“Ni kweli nimekupa mwenyewe ila haiwezekani roho iniume hivi kwasasa, ukitaka njoo nikufaidi nilipizie hela zangu”
Dora akakata simu ya huyu mzee huku akiwaza kuwa hao wanaume afanye nao nini ila hakuwa na la kufanya mwishowe akawaza au arudi tena kwa babu wa bagamoyo maana alimjibu mzee Jimmy ila aliogopa vitisho vyake ukizingatia hela zake kwa kipindi hiko kashazila sana, mwishowe aliamua kulala tu kwani hakutaka kuwaweka mawazoni zaidi.

Kesho yake kama Erick alivyoahidi alienda na gari nyumbani kwakina Erica, kwakweli wote walishangaa maana lile gari lilikuwa zuri sana tena lilionekana la gharama, Erick akaongea kwa furaha,
“Gari hii nimeiagiza muda sana toka nipo South kwaajili ya zawadi ya mpenzi wangu Erica, nampenda sana huyu mwanamke na nitafanya kila kitu kwaajili yake”
Nyumbani kwao walishangilia sana, ila gafla geti lilifunguliwa na aliyeingia alikuwa ni Tumaini na Sia.
 
SEHEMU YA 383


Nyumbani kwao walishangilia sana, ila gafla geti lilifunguliwa na aliyeingia alikuwa ni Tumaini na Sia.
Basi wakajikuta wote wakiwaangalia maana waliingia bila ya kugonga hodi ingawa ni kawaida kwa geti lao watu kuingia bila hodi ila hawa waliwashangaa, Tumaini akasogea karibu na mdogo wake,
“Yani Erick umeshindwa kunipa mimi gari unampa Erica kweli?”
Erick alimuangalia na hakumjibu kitu, badala yake alikabidhi funguo na kadi ya gari kwa Erica kitu ambacho kilimuumiza moyo sana Tumaini na kujikuta akishindwa hata kusema zaidi, kisha alimuangalia Sian a kumtaka waondoke, Sia akamwambia,
“Mbona hatujatimiza lengo letu?”
“Twende Sia, hatuwezi kufanya kitu tutakuja kwa wakati mwingine”
Wakaamua kuondoka maana hata Erick mwenyewe alionekana kutokuwajali kabisa kwani aliendelea na mambo yake ya kutoa zawadi ya gari tu kwa Erica.
Ilikuwa ni furaha sana nyumbani kwakina Erica, ingawa bite mwanzoni alikuwa na mashaka na Erick ila kwasasa alianza kumuonea wivu mdogo wake kuwa anapendwa, ingawa hata yeye kashawahi kupewa zawadi ya gari mara nyingi tu ila hakupewa kwa namna ile ya upendo ambayo mdogo wake alipewa, baada ya hapo Erick aliomba ruhusa aende na Erica wakatembee tembee kidogo na hiyo gari kisha watarudi ila mama Erica aligoma,
“Hapana mwanangu hatoenda popote kwakweli, naogopa yasije yakampata mengine makubwa”
Mage akatetea,
“Ila mama, huyu kijana kaonyesha upendo mkubwa sana, sio sababu ana pesa hapana ila sababu ana upendo, wangapi wana pesa ila hawana upendo? Tena wenye pesa ndio wanajulikana sana kwa kukosa upendo ila huyu kijana ameonyesha upendo wa ajabu, mimi ningeona ungemruhusu tu akatembee kidogo na Erica”
Aliamua kuuliza kwanza,
“Kwani mnataka kwenda wapi kutembea tembea?”
Pale pale akili ya Erick ikamcheza na kumwambia,
“Nataka niende na Erica kwa Yule mwanamaombi tukapate baraka yah ii zawadi”
Basi mama Erica kusikia vile akakubali na kumfanya Erick afurahi sana kutoka na Erica, kisha Erica alienda kujiandaa na kutoka na Erick.

Tumaini alikuwa na hasira sana moyoni, yani alikuwa njiani na Sia akiongea maneno mengi mengi kwa hasira na chuki,
“Hivi kweli mtu akuache ndugu yake usote na miguu safari zote wakati uwezo wa kukununulia gari anao halafu anaenda kumnunulia gari mwanamke kweli? Yani Erick wa kunifanyia mimi hivi? Kumbuka mimi ndiye ndugu yake wa pekee ila kamthamini Yule mwanamke ambaye kaonana nae ukubwani tena ni mimi ndiye niliyemkutanisha nae ila bado ananidharau?”
Tumaini aliamini ni yeye aliyewakutanisha Erick na Erica bado hakujua kuwa Erica ndiye msichana ambaye Erick alimpenda toka wanasoma sababu ukweli wa hilo hajawahi kumwambia zaidi ya kumwambia kuwa anampenda sana, kwahiyo aliamini tu ni yeye aliyewakutanisha, Sia alimbembeleza pale huku nay eye akijilaumu,
“Unajua duniani kuna dawa Tumaini, ukisikia mtu karogwa ndio hiki kinachotokea kwa Erick, hebu kumbuka mapenzi yangu na Erick kabla ya ujio wa huyo kidudu mtu Erica, tulikuwa tunapendana, hata nikimfumania Erick ananiomba msamaha na maisha yanaendelea, wazazi wangu wote wamekufa wakiamini kuwa Erick ndiye mume wangu, yani ilikuwa mimi na Erick tu mpaka jinni kisirani alivyovamia penzi letu”
“Yani Sia najuta mimi, najuta kufahamiana na Erica. Nilimuona ni msichana mstaarabu na kutaka awe mdogo wangu, najuta mimi. Natamani kurudisha siku nyuma ili hata ile siku niliyokutana na Erica isiwepo katika maisha yangu, haiwezekani huyu msichana akachanganya akili yangu kiasi hiki”
Kisha Sia akamuuliza kuwa kwa muda huo sasa wataenda wapi,
“Sia, muda huu twende ofisini kwa mamake Erick, mimi nitamueleza uchungu wangu na wewe umueleze kuwa una mimba”
“Mmmh akisema tukapime?”
“Hawezi sema hivyo yani usijali, mimi nitatengeneza matukio yote utakuja nyumbani mara kwa mara ukijiliza kwa baba kuwa una mimba ya Erick, yani najua Erick atachukia sana, hata akikusukuma tu tunapata sababu yani nitakuwaisha hospitali na kusema mimba imetoka halafu umepata matatizo makubwa sana sababu alikusukuma vibaya, si anajifanya yeye ndio mtoto pekee kwa mama yake yani lazima mama yake ahisi homa gafla, haiwezekani Erick afanye hivi unajua yani najiuliza huyu Erica kampa nini ila sipati majibu kabisa.”
Basi safari kwa muda huo ilikuwa ni kuelekea kwa mama Erick huku wakiwa na mawazo sana maana lile tendo la kumuona Erick akimkabidhi gari Erica liliwaumiza sana.

Nyumbani kwakina Dora bado alimuona mdogo wake kutokuwa sawa kama alivyotakiwa kuwa, akakumbuka maneno ya Yule mwanamaombi kuwa hawatakiwi kuacha kuomba kwani kile kitu ni vitu ambavyo kimepandikizwa na kimenuiziwa kwahiyo kinaweza kutoka vizuri kwa maombi tu ila wakiacha itakuwa ni tatizo, Dora alimfata mama yao na kumwambia habari za kwenda tena na mdogo wake kwenye maombi, ila mama alikuwa mkali sana,
“Weee Dora, wewe na maombi wapi na wapi? Halafu huyu mdogo wako aende kwenye maombi kwani ana mapepo huyu? Labda hayo maombi uende wewe maana akili zako zimechanganyikiwa ila sio mwanangu”
“Sasa mama unamuona yupo sawa huyo anajifungia tu!”
“Yupo sawa ndio, atatoka na ataenda kujumuika na wenzio ila swala la kuanza kumuangaisha mwanangu kwa hao wachungaji hata sitaki, kwanza ni waongo wanajifanya wanaombea kumbe wanataka sadaka”
“Haya mama, hiyo sadaka utatoa wewe au mimi ninayempeleka?”
“Kama una hela hiyo ya sadaka si ulete tujichane humu ndani”
“Kiukweli mama wewe ndio uliyenipoteza mimi, ni kweli wasemao mtoto umleavyo ndivyo akuavyo yani hivi nilivyo ni matunda yako ya malezi mabaya”
“Hebu nitolee ushetani wako mie”
Dora akaona isiwe tabu akajiandaa na kwenda yeye kwa mwanamaombi kwani bado alihitaji kuongea nae vitu vingi sana, haswa kuhusu mzee Jimmy na kuhusu James.
 
SEHEMU YA 384

Tumaini na Sia walifika ofisini kwa mama yake Erick na waliomba kuonana nae ambapo aliwaambia wamsubiri kidogo ili muda wa kula chakula cha mchana aende nao na wamueleze kilichowasibu, nao walifanya hivyo na muda ulipofika mama Erick alitoka na kwenda nao sehemu ya kula huku akiwasikiliza hoja zao walizokuja nazo, alianza Tumaini kuelezea,
“Mama, yani Erick ni ndugu yangu kila leo namuomba aninunulie gari anasema mpaka ajipange”
Huyu mama alimjibu Tumaini kabla hata hajamaliza,
“Sasa hilo ndio tatizo mwanangu? Baba yeni ana pesa si ni kitendo cha kumwambia tu baba nahitaji gari ya kutembelea akupe jamani! Eeeh Tumaini!”
“Hapana mama hilo sio tatizo, ila tatizo ni kukuta kampa gari Erica, tena gari lenye thamani ya milioni ishirini na tano, kweli Erick anatoa gari la namna hiyo kwa mwanamke jamani!”
“Sijakuelewa Tumaini, umesema!”
Ikabidi Tumaini arudie maelezo yake kwakweli mama Erick alishangaa sana kuona mwanae kafikia hatua hiyo na kuona kuwa sio kawaida labda kuna kitu alichofanyiwa na huyo Erica,
“Usinione nimenyamaza mwanangu Tumaini yani najitafakari, kweli Erick kafikia hatua hiyo jamani! Si bora angekupa wewe hilo gari, mbona kaanza mambo ya ajabu huyo Erick? Halafu huwezi amini tofauti na kipindi kingine ila kipindi hiki Erick hana muda na mimi kabisa, akinisalimia mara moja imetoka yani huyu mtoto hata sijui nifanyeje”
Tumaini akaendelea kuongea na kumwambia,
“Sasa mama, hili la kumpa gari Erica na kuninyima mimi sio kosa sana ila kosa kubwa la mwanao ni kuwa Sia ana mimba yake na ameikataa eti yupo kulea mtoto wa Erica”
Yani hapa ndio wakamchanganya vizuri mama Erick na kusema,
“Yani isingekuwa kesho nasafiri basi ningeenda mwenyewe huko kwakina Erica, nahitaji kuonana na mama yake kama anamfundisha mwanae hiyo tabia ya kuibia wanaume, yani mtoto uzae na mwanume mwingine ila umbambikie mwanaume mwingine alee, hiyo inawezekana kweli? Kasichana kanaonekana kapole kale kumbe kamezalia nyumbani? Jamani, ni aibu sana halafu mwanangu hata kuona haoni anamkazania huyo msichana kweli kuna mambo duniani, nilikuwa nasikia kwa watu tu kuwa kuna watu wanaroga ili wapate mapenzi na kweli nimeamini ila Yule Erica hajaroga kwaajili ya mapenzi bali ameroga kwaajili ya pesa za mwanangu”
Tumaini alimsapoti mama Erick kuwa ni kweli Erica atakuwa kamroga Erick sababu ya pesa zake,
“Ni kweli kamroga mama, yani Yule binti hata chuoni alikuwa akisifika kwa tabia za kichawi yani kamfanya vibaya mdogo wangu najuata kumfahamu”
“Ila nitamtafuta mamake mdogo na Erick ili tumtafute Yule msichana aliyechanganya akili za Erick wakati yupo shule ndio apambane na huyo Erica”
Sia alitulia tu huku akisikilizia kuwa mimba yake inapewa shauri gani ila alipoona zinaongelewa hoja zingine tu bila hoja ya mimba yake kugusiwa akaamua kugusia hoja ya mimba yake,
“Mama, na vipi kuhusu hii mimba niliyonayo ya Erick?”
“Mwanangu tulia, Erick atakuoa atake asitake, kwani mtoto bora ni Yule anayelelewa na wazazi wawili yani baba na mama asiniletee mambo ya baba yake mie”
Sia alifurahi kusikia vile maana hata kama hakuwa na mimba ila ile kauli ilimpa moyo sana na kumfanya ajihisi rah asana, kisha mama Erick aliwaaga na kurudi ofisini maana kuna mambo alitaka kumalizia na kesho yake asafiri.
Tumaini na Sia waliondoka pale wakiwa na matumaini makubwa sana kwani walijua kama mama yake Erick atalichukulia lile swala basi lazima watafanikiwa kusambaratisha penzi la Erica na Erick.

Dora alifika kwa Yule mwanamaombi na kuanza kuongea nae juu ya mambo yanayomsibu ila mwanamaombi akamshauri kuwa na huyo James amlete kwenye maombi pia,
“Mmmh sijui atakubali nitajaribu”
“Halafu mbona mdogo wako hujaja nae?”
“Mama kagoma, yani mama ni mbishi sana”
“Sasa mdogo wako anatakiwa kukombolewa maana ile dawa ilimkoroga haswaa ukizingatia hakulazimishwa kula ila alikula kwa hiyari yake mwenyewe, ulitakiwa kuja nae”
“Nitajitahidi basi nikija tena nije nae, ila kuna mzee mmoja nilikula hela zake ananisumbua sana”
“Kama utaweza huyo mzee pia ungemleta kwenye maombi maana silaha ya hao watu ni maombi tu”
“Mmmh Yule mzee sijui kama atakubali, nitajaribu”
“Unatakiwa kuingia kwenye maombi, unatakiwa na wewe ujifunze maombi”
“Ila ngoja nikuulize, hivi mfano wakati natumia zile dawa kuna pesa nilichukua kwa watu je nifanyaje nazo?”
“Unazo hizo hela?”
“Ndio ninazo?”
“Zilete tufanye maombi na kisha zipelekwe kwenye kusaidia watoto yatima”
Hapo palimshtua Dora, yani atoe pesa zake alitamani hata kubadilisha mada, kwa bahati walifika Erica na Erick kwa Yule mwanamaombi na kumkuta Dora pale akiongea nae, wakamsalimia kisha wakaanza na wao kuongea na Yule mwanamaombi ambaye aliwafanyia maombi na kuwataka kusimamia maombi tu, sababu Dora aliacha kwanza waombewe wale kwahiyo mwanamaombi alijua akimalizana na wale ataanza tena na Dora ila wakati wakina Erica walipotaka kuondoka tu Dora nae alisema wasubiri waondoke wote na kumuaga Yule mwanamaombi,
“Ila bado hatujamalizana binti, bado sijakufanyia maombi!”
“Nitakuja badae”
Akatoka nje na Wakina Erica na kupanda ile gari ambayo Erick alisema kuwa kamnunulia Erica, muda wote kwenye gari alikuwa akisifia tu,
“Gari nzuri sana jamani, kwakweli Erica umepata bahati kumpata huyu Erick”
Erica akawa anacheka tu kisha Dora aliendelea kuongea,
“Ila Erick unajua kama Erica alikuwa na mahusiano na ndugu yake Derick?”
Erica alichukia sababu alimuona Dora anaanza kuongea mada zisizomuhusu na kumuuliza,
“Unaelekea wapi Dora maana sisi tunarudi nyumbani”
“Basi nishusheni tu hapo kituoni”
Basi walivyofika kituoni wakamshusha, Erick alijifanya kama hajasikia lile swali la Dora maana hakutaka kupata tena kitu cha kumuumiza moyo kwa muda huo wa furaha.
 
SEHEMU YA 385

Dora alirudi kwao ila alikuwa na mawazo sana, kwanza aliwaza kupeleka zile pesa kwa mwanamaombi yani aliona haiwezekani kwakweli maana aliona pesa kazihangaikia sana zile, ila akiwaza vitisho vya mzee Jimmy hofu ilimshika pia, ila muda huo aliamua tu kurudi nyumbani, akamkuta mama yake amekaa tu na mawazo, akamsalimia na kumuuliza
“Ni mdogo wako dora, kasema anaenda tena kwa mwanamke wake alipokuwa juzi, nasikitika sana maana kaniambia anataka amuoe kabisa”
“Kheee ila mama nilikwambia kuwa niende nae tena kwenye maombi”
“Hukuniambia mdogo wako anasumbuliwa na nini zaidi ya kukazania maombi, kumbe mdogo wako anasumbuliwa na mapenzi jamani! Sasa nayo ni kitu cha kuombewa? Nimemwambia amlete huyo mwanamke nimfahamu, ananisikitisha sana kwani bado hajajipanga kimaisha ila anataka kuoa, kuoa ni jambo jema ila kwa muda gani ndio tatizo hapo”
“Sasa mama, unavyoona mwanao yupo kwenye hali ya kawaida?”
“Ndio, ila ni mapenzi tu yanamsumbua”
Muda kidogo Dora alipigiwa simu na mpigaji alikuwa ni James, basi leo hakuona tatizo zaidi ya kuonana nae tu kwani alitaka kujaribu kumshawishi waende wote kwenye maombi.
Kwahiyo aliachana na habari za kushauriana pale na mama yake na kwenda kuonana na James, ni kweli James alikuwa na shauku sana ya kumuona Dora ila alivyomuona tu akili yake kama ilicheza na kurudi gafla, akashikana nae mkono kama salamu kisha huyu James alijikuta akimuuliza Dora,
“Kwani akili yangu ilifanyeje?”
“Sijui, hata mimi nakushangaa”
“Hivi nimeitafuta hata familia yangu kweli?”
“Sijui, ila kuna mahali nataka twende”
“Wapi na kufanya nini?”
“Ni kwenye maombi, kuna lengo moja la kujikomboa kutoka kwenye mambo ya kishirikina”
“Inawezekana nilifanyiwa mambo ya kishirikina eeeh ndiomana sikukumbuka familia yangu”
“Ndio inawezekana”
James alikubali maana akili yake kwa muda huo hakuielewa kabisa, ilikuwa kama imerudi gafla, kwahiyo kitendo cha kumuona Dora ambaye alimfanyia dawa na kumfanya ampende aliweza kurudisha fahamu na kumbukumbu zake, basi Dora aliondoka nae na kuelekea tena kwa Yule mwanamaombi.
Dora alifika na kuongea na Yule mama kuwa aongee taratibu na James ili asigundue kuwa ni yeye ndiye aliyemfanyia madawa maana kitendo cha James kumuona tu akili yake imerudi, Yule mwanamaombi akamwambia Dora,
“Sababu wewe ndiye uliyemfanyia na wewe umekomboka ndiomana kitendo cha yeye kukuona wewe kimerudisha akili yake”
“Kwahiyo kuhusu mdogo wangu itabidi Yule mwanamke naye aje huku?”
“Ndio, inatakiwa tumkomboe pia sababu kuamini ushirikina ni kitu kisichofaa, mdogo wako ungekuwa unamleta mara kwa mara kwenye maombi angekomboka pia”
Basi Yule mwanamaombi alianza kumuombea James na hadi James alijihisi yupo vizuri ila Dora aliaga na kuondoka na James kwani hakutaka kuulizwa kuhusu swala la hela zile alizozipata kipindi cha madawa.
Alifika njiani na kuagana na James kisha yeye kwenda kwao, kwa muda huo James alijiona yupo huru sana kupita muda wowote ule ila alishangaa kwa Dora kumfahamu mtu wa maombi wakati ana matendo yasiyofaa.

Ilikuwa ni saa kumi na mbili jioni inaenda saa moja wakati James amefika nyumbani kwake ila kiukweli hakuwa na furaha kabisa kwani alijihisi ni muda mrefu hajaiona familia yake na wala hakujisumbua kuitafuta,
“Hivi mimi nimeanzaje jamani? Mbona sikumbuki nimeanzaje?”
Alimkuta msichana wa kazi pale nyumbani akisema kuwa dada yake aliondoka hapo siku nyingi tu na yeye binafsi kuna siku anarudi ila siku zingine harudi au anarudi usiku sana,
“Jamani hata kama nina tabia chafu ndio kufanya hivyo kweli!”
“Ndio na mara nyingine ulikuwa unampiga dada”
Hapo ndio alichoka kabisa maana swala la yeye kumpiga mke wake hakuwa nalo hata mkewe amfanye nini kwahiyo kufikia hiyo hali ya kumpiga mke wake aliishangaa sana yani hakuelewa kabisa kuwa alianzaje anzaje.
Hakutaka kukaa hata hapo nyumbani kwake kwani moja kwa moja aliamua kuondoka na kwenda nyumbani kwa mkwe wake ili akamuone mke wake na mtoto.
Alifika kwenye mida ya saa mbili usiku, akagonga na kufunguliwa mlango, aliyefungua alikuwa ni Mage maana ndio alikuwa anatoka kuelekea kwake, na alijua ni Erica na Erick wamerudi, kwakweli alivyoingia James walishangaa sana, Bite hakutaka hata kuongea na mume wake badala yake alienda zake kulala kwani alikuwa na hasira sana na huyu mtu, mama yao nae alimtimua tu kwani hakutaka kumsikiliza wala hakutaka kumuona kwahiyo ilibidi James aondoke zake.
Mage alisogea kumuaga mama yao, ambaye alilalamika kwanza,
“Mnaona sasa huyo Erick na Erica hadi muda huu hawajarudi jamani hebu nisaidieni kuwatafuta maana kila nikiwapigia simu wanadai wanakuja yani Napata hasira sana”
“Ila mama sidhani kama kuna ubaya wa wao kuwa pamoja na watarudi tu”
“Muda gani sasa? Na ole wake huyo Erick aniombe safari ijayo kuwa anataka kutoka na Erica”
Muda kidogo Erick alikuwa amemrudisha Erica nyumbani ila mama yao hakupenda hivyo hakutaka hata Erick kukaa kwa muda mrefu na kumtaka aondoke tu, kisha alimuangalia mwanae Erica ila leo hakumsema sana kwani aliamini bado hajapona vizuri kwahiyo alimuacha akalale tu.

Sia alitulia ndani kwake ila nje kulikuwa na mdogo wake Dora amejibanza tu ikabidi kwa siku hiyo amkaribishe ndani maana usiku ulishaingia na kujikuta wapo ndani na kuzoeana huku wakipiga story mbalimbali ila katika stori zote walizokuwa wanapiga Yule Steve alijikuta akiwa na mada moja tu kwa Sia, alimwambia kuwa anampenda sana yani hakuwa na mada nyingine zaidi ya kumwambia anampenda sana, kwakweli Sia alishangaa sana nguvu ya ile dawa hadi ingekuwa kwa Erick angefurahi sana maana dawa ina nguvu hatari hadi wakati mwingine alihisi Yule kijana akiongea kutoka moyoni kwani alionekana kuongea kwa hisia sana hata hakuweza kumtimua nje.
Kwasababu hakutaka ndugu zake wengine wajue kama Yule kijana kafika tena kwahiyo aliamua kumwambia alale kwenye kochi la pale chumbani kwake.
Ila usiku wa manane alishtuka kukuta Yule kijana akianza kumpapasa, sababu alijikuta na yeye kuwa na hamu sana akashindwa kumzuia na kujikuta akifanya nae mapenzi na kulala kama wapenzi.
Kulipokucha Sia alimuangalia Steve na kujuta sana kwani anayemtaka yeye si Steve ni Erick ila ndio imetokea vile ila na vile vile alijishangaa kuwa kumfukuza huyu mtu hawezi na alipenda kumuangalia tu jinsi anavyomuimbia wimbo wa nakupenda maana alitamani kweli siku moja atokee mtu wa kumwambia anampenda kiasi kile.
Sia aliamka na kuoga kila kitu kisha kumuamsha Steve ili aende kwao, Steve aliamka pia ila akamwambia Sia,
“Sawa, mimi nitaenda kwetu ila ningeomba nikakutambulishe kwetu maana nataka nikuoe”
“Kheee unioe?”
“Ndio, nakupenda Sia, nahitaji kukuoa yani wewe ndio mwanamke wa maisha yangu nakupenda sana”
Yani alijisikia kucheka na kulia yote yale yalifanywa na nguvu ya dawa inamaana vijana kama wale hawakumuona kabla? Na pia hakupenda kuchombezwa na kijana ambaye anaonekana yupo kawaida tu wala hana hela wakati yeye alikuwa akimtaka Erick ilia pate na hela za Erick ndiomana alitaka hata kumfanyia dawa maana anaamini kuwa hata lile gari alilopewa Erica lilikuwa ni mali yake.
Kwa muda huo ilibidi amchombeze chombeze Steve ili aondoke ila Steve aliahidi kwenda tena badae maana alijiona hawezi lolote bila ya Sia, alimuona Sia kuwa mwanamke wa maisha yake.
.
.
.
.
.
ITAENDELEA ALHAMISI
 
SEHEMU YA 387

Steve alirudi nyumbani kwao ila alitumia muda mfupi sana kukaa pale nyumbani maana alioga na kubadilisha nguo kisha kubeba nguo zake baadhi kwenye begi lake la mgongoni na kutoka ila nje mama yake alimsimamisha na kuanza kumuuliza maswali,
“Unajua Steve toka siku tuliyokutafuta sikuelewi kabisa, haya umerudi muda mfupi ushajiandaa unaondoka tena, unaenda wapi mwanangu?”
“Mama, nilishakwambia kuwa nataka nioe”
“Uoe? Kwa maisha yapi uliyonayo mwanangu Steve? Dada yako mwenyewe hajaolewa, labda dada yako angekuwa ameolewa ingekuwa rahisi maana mahali yake tungepeleka huko unapotaka kuoa, ila mwanangu kuoa gani kwa haraka hivyo na maisha gani uliyonayo wewe?”
“Mama, nampenda huyu mwanamke sitaweza kufanya chochote bila kumuweka katika akili yangu, nampenda sana nahitaji awe mke wangu nisije kumkosa bure”
“Kheee makubwa, ndiomana dadako anasema umerogwa”
“Achana na maneno ya Dora mama, mimi sijarogwa wala nini. Siku namuona Yule mwanamke yani moyo wangu haukutaka kuondoka kwenye sura yake, mama humjui huyo mwanamke ila ukimuona utasema nina haki ya kumpenda, naomba nikawe nae karibu tafadhali mama yangu”
“Kheee makubwa, kwakweli mimi kama mama siwezi kukuruhusu kufanya hivyo, Steve huna maisha yoyote wewe”
Steve hakumsikiliza mama yake zaidi ya kuondoka tu kwani kwa wakati huo akili yake ilikuwa kwa Sia tu. Mama yake alibaki akisikitika ila bado swala la kurogwa kwa mwanae halikumuingia akilini kwani alikuwa anajua mtu akirogwa basi lazima awe zezeta ila mtu anasema mwenyewe hakuhisi kuwa amerogwa.
Steve aliondoka na kwenda hadi kwakina Sia, sema pale Sia alikuwa na chumba chake kwahiyo toka siku ya kwanza alifikia hapo na hata muda huo alifikia hapo hapo, Sia hakuwepo ila alitulia nje akimsubiri.

Siku ya leo Erica alitulia akiongea na dada yake bite ambapo alimueleza na ujio wa James kuwa ilionyesha James alienda kwa lengo la kumuomba msamaha,
“Dada, shemeji James alianza mahusiano na rafiki yangu Dora na Yule rafiki yangu kanihakikishia kuwa ameathirika tafadhali dada yangu usimrudie shemeji kabla ya kwenda kupima”
“Mmmh naogopa, mfano nikimkuta kaathirika, nitafanyeje hapo?”
“Dada, wewe ni mtu mzima nakushauri ufanye mambo kiutu uzima yani mtu anapoona umefanya jambo aone kweli akili yako imepevuka, sitaki kukushauri uachane na shemeji au kukushauri uendelee nae ila mkishapima na kujua basi utumie busara zako kwa kuendelea nae au kuachana nae”
“Mmmh mdogo wangu mbona unaniacha njiapanda, ni vyema unishauri mapema ili nijue cha kufanya”
“Hapana dada, ushauri wangu kwasasa ni huo yani James akija tu mwambie mkapime”
“Haya sawa, wewe na huyo Erick wako mliwahi kupima? Sio mnashikana shikana tu, mshawahi kupima?”
“Ndio, mimi na Erick tulipima kabla sijapatwa na matatizo, nampenda sana ila nilimwambia tukapime kwanza, nishapita sehemu nyingi bila kupima Mungu kanisaidia ila kwasasa natakiwa niwe makini sana ndiomana nachukua shauri la kupima”
“Mdogo wangu ni kweli ulikuwa muhuni sana?”
“Hapana dada, yani mimi nilikuwa nakuwa na mahusiano kwa muda sidhani kama mtu ambaye hajachanganya wanaume kwa muda mmoja basi anawekwa kwenye kundi la umalaya. Sikuchanganya wanaume ila nilikuwa labda nikiachana na huyu ndio nakuwa na mwingine, na yote nilikuwa kwenye safari ya kutafuta penzi la dhati, sikuwa na nia nionekane malaya dada ila watu wamenihisi vibaya”
“Pole mdogo wangu ila mara nyingine na mimi bora hata ningekuwa kama wewe niweze kupata penzi la dhati kuliko hapa nilipoangukia”
“Dada, kuwa kama mimi sio suluhisho maana penzi la dhati halitafutwi kwa mtindo huu ila penzi la dhati ni kutulia kwa uliyenaye, na kama haeleweki basi usiwe chanzo cha kuyavunja hayo mahusiano bali chanzo awe yeye mwenyewe”
“Mmmmh mdogo wangu unaongea tu sababu umempata Erick anayekupenda sana, kwakweli hadi Napata wivu kwa mapenzi yenu, natamani na mimi ningepata anipendaye kama ulivyopata wewe mdogo wangu, yani safari yangu ya mapenzi naiona ni ndefu sana, na hivi mume wangu haeleweki ndio kabisa yani. Nilijua nikiwa na mtoto itakuwa nu furaha sana kwa James ila imekuwa ndivyo sivyo”
“Dada, basi zamani nilikuwa natamani kweli mume wangu nimzalie mtoto wa kwanza wa kiume kwani nilijua ukizaa mtoto wa kiume basi utapendwa sana na mwanaume, basi siku nimejifungua mtoto wa kike nikawa mpole sana ila ndio mtoto niliyepewa na Mungu nikashukuru sasa kilichonishangaza ni kwako dada umezaa mtoto wa kiume ila bado shemeji anakufanyia vituko, na vile vile Rahim mtoto wangu hakumtaka basi mkewe alinitambia kweli kliniki sijui mtoto wangu wa kike hatakiwi eti yeye kabeba mimba ya mtoto wa kiume, nilimjibu ila roho ilikuwa inaniuma sana sasa nimeshangaa eti amepewa talaka na mtoto wake wa kiume loh!”
“Mdogo wangu wanaume hawatabiliki yani umpate tu mwenye mapenzi nawe na watoto, maana mtoto ni mtoto haijalishi ni wa kike au wa kiume si unaona wewe, Rahim hamjali mtoto wake ila umempata mtu mwenye mapenzi ya dhati na mtoto wako, Erick anampenda mwanao kama mwanake kwamaana hiyo hata ukizaa naye atawapenda watoto wote kwa uzuri kabisa ila ni swala la kumuomba Mungu pia ili asibadilike maana sisi binadamu tunaweza kubadilika kama vinyonga”
“Mmmh Mungu amsaidie Erick wangu, ila kwanini dada mwanaume ukimuuliza makosa yake anakubadilishia mada?”
“Wanaume hawawezi kujitetea kama sisi tunavyojua kujitetea yani sisi tukipata upenyo wa kujitetea weee lazima tushinde sasa mwanaume huwa anaona ni vyema abadili mada maana kwenye swala la kujitetea kwao ni gumu sana, utaona kuna wanaume wengine wamefungwa kwa kuonewa kabisa ila sababu kujitetea hawawezi mpaka kwenye kesi apate mwanasheria mzuri ila mwanamke akisimama kujitetea uwiii unaweza kuhisi hajawahi kutenda kosa”
“Ila wapo wanaume wanaojitetea”
“Mwanaume sio anajitetea ila anakupa maneno laini kukulainisha tu ila kujitetea huwa hawawezi kama sisi wanawake. Mwanamke kaumbiwa vingi sana vya kufanya umuonee huruma tofauti na mwanaume”
Basi walijaribu pale kushauriana mambo mbalimbali na mdogo wake kwani kiukweli alikuwa akitamani sana maisha ambayo mdogo wake aliyaishi kwa kipindi hiko, maisha ya kupendwa na Erick.
 
SEHEMU YA 388

Kwa upande wa Rahim, mama yake alimuita maana bado hakuelewa kwanini Rahim ampe mke wake talaka na kumrudisha kwao,
“Unajua mwanangu Rahim ulichofanya hakipendezi kabisa, mwanamke katoka kujifungua ana mtoto mdogo ila bila aibu unampa talaka, kweli ni haki hiyo mwanangu?”
“Najua mama sijawahi kukueleza maovu ya Yule mwanamke ndiomana unamtetea, Yule mwanamke ni mshirikina sijapata kuona, siku ile nimempiga sababu nilimkuta anachoma dawa huku akinuiza maneno, ilionyesha alitaka kuniweka mimi ndodndocha wake, na ubaya zaidi kamroga Erica asiye na hatia kabisa”
“Kamroga Erica!”
“Ndio alimroga Erica kumbe hufahamu? Erica ameumwa sana ten asana kumbe muhusika ni huyo mkwe wako hata sijui kwanini alikuwa akimchukia Erica kiasi kile wakati mimi nilishaachana na Erica”
“Kwa maana hiyo mwanangu umemfukuza Salma sababu ya Erica si ndio!”
“Ndio mama, Yule mwanamke ni mshirikina”
“Kwamaana hiyo unataka kumuoa Erica badala ya Salma si ndio?”
“Mama, kungekuwa na uwezekano wa mimi kumuoa Erica basi ningemuoa. Kipindi niko mbali sikuwaza ni jinsi gani nampenda Erica ila sasa nampenda sana na nimejua thamani yake, Erica kanilelea mwanangu mama, mtoto wangu hujamuona tu ila anapendeza sana kupita watoto wangu wote, yani kupita hata huyo anayelelewa na Salma ambaye bado mdogo lakini yupo kama amebemendwa, hujamuona mtoto niliyezaa na Erica mama, Yule ndio mtoto kwakweli natamani kumuoa Erica”
“Hebu niondolee ujinga wako mimi, eti ndio mtoto kwa lipi alilokuwa nalo? Huyo Erica katembea na John, katembea na wewe, katembea na Babuu sijui Derick katembea nae halafu unataka umuoe umlete hapa nyumbani kwangu ili atembee na mume wangu pia? Yani mnataka na baba yenu apate mboga ya Erica? Hivi huna kinyaa Rahim, yani mwanamke umeshea na ndugu zako kweli humuonei kinyaa jamani! Huyo Erica simtaki kwenye nyumba yangu, yani simtaki kabisa kabisa”
“Mmmh mama nawe kwani humuamini mume wako?”
“Namua,ini vizuri sana ila siwezi jua huyo Erica anawavuta na nini kiasi kwamba hamuoni kinyaa kuwa nae”
Rahim aliamua kuinuka na kumuaga mama yake kisha kuondoka kwani alihisi kuwa anaweza kumuuliza mama yake maswali yasiyostahili bure kisha akaonekana hafai.
Basi alitoka na kumkuta Neema amekaa kwenye nyumba yao ila akasema,
“Nimepooza shemeji maana mwenzangu hayupo”
“Aaaah Neema ukitaka kuongea si ukaongee na mama kule maana hata yeye anahitaji apate mtu wa kupiga nae story”
Basi Neema akawa kama anainuka ili kumfata mama mkwe wake ila REahim alimsimamisha kwanza akimuuliza,
“Hivi Yule mdada ambaye ulikuja nae nikapishana nae getini ni nani na anaishi wapi?”
“Yule anaitwa Zainabu, anaishi mtaa wa nyuma huko, kashika sana dini Yule”
“Aaah je ameolewa?”
“Hapana hajaolewa”
“Basi napenda kupata mawasiliano yake maana kwasasa nahitaji kumpata mtu anayeijua dini vizuri ili aweze kunishauri na kunipatia mwangaza”
“Basi nitakupatia shemeji”
“Ungenipatia tu sasa hivi”
Basi Neema alimpatia Rahim mawasiliano ya Zainabu kisha Rahim alimshukuru sana na kuamua kuendelea na safari.
Alifurahi sana kupata mawasiliano ya Zainabu maana aliona kama atamkosa Erica basin i vyema awe na Yule Zainabu maana alimuona ni binti aliyetulia.

Sia alikuwa kwakina Tumaini siku hiyo na akaongea nae mengi na kujikuta wakipanga vitu vingi sana, Tumaini aliamua kumwambia Sia kuwa amewahi kuambiwa na Erica kuwa au anamtaka mdogo wake,
“Yani mimi Sia nakupigania tu ila nishawahi kuambiwa na Erica au unamtaka mdogo wako, jamani hiyo kauli inaniuma sana hadi leo”
“Pole sana wifi yangu”
“Yani anafikia hatua ya kuniambia na wewe tafuta mwanaume uolewe, kwakweli kauli ya Erica hii iliniuma sana”
Wakati wanongea ongea na kupanga panga, leo Erick alirudi nyumbani mapema sana, na walimshangaa kweli haswa Tumaini, ingawa alikuwa na chuki nae ila alimuuliza kilichomrudisha mapema vile,
“Erick, tatizo nini mbona leo mapema?”
“Kumbe huwa unachunguzahadi muda wangu wa kurudi nyumbani! Alichokwambia Erica sio kibaya, unatakiwa utafute mwanaume kweli uolewe dada yangu”
Kisha Erick akaondoka zake kuelekea chumbani, hakumsalimia Sia wala nini yani kamavile hakumuona kuwa yupo pale kwao.
Kile kitendo na yale maneno yaliwaumiza sana, Tumaini akamwambia Sia,
“Unaona alivyo na dharau sababu ya Erica! Yani anasahau hata kama mimi ni dada yake wa pekee”
Sia alitamani kumwambia Tumaini kuhusu babu wa Bagamoyo ila aliogopa kuonekana mshirikina kwani hakufikiria kama Tumaini angemsapoti kuhusu hilo swala la kwenda kwa mganga ingawa ni kweli kwa yale yaliyoendelea lazima na yeye angependa kwenda kwa mganga.
Muda kidogo Erick alitoka na kuchukua chakula kisha akakaa mezani kula, yani Tumaini na Sia walikuwepo tu wanamuangalia alikula kula kisha akawaangalia na kuwaambia,
“Tena kuna kitu nimesahau”
Tumaini alimuuliza kwa shauku kwani alijua atasema kuwa amesahau kuwakaribisha labda, ingawa chakula kilikuwepo ila walitaka Erick aonekane kuona uwepo wao kwa kuwakaribisha,
“Nini umesahau tena mdogo wangu?”
“Jumamosi, nakuomba wewe na huyo mwenzako mje pale kwenye duka lile nililokuondoa”
“Kivipi? Unataka kunirudisha?”
“Utajua siku hiyo hiyo, yani mje tu msikose”
Kisha Erick alimaliza kula na kuinuka akaenda chumbani kwake, kitendo cha kutokukaribishwa kwa muda huo hawakukichukulia maanani ila kitendo cha kuitwa Jumamosi kwenye duka ambalo alikuwepo yeye ndio kikachukuliwa maanani,
“Inamaana Erick anataka kunirudisha dukani?”
“Inawezekana, kwani ulimwambia baba yenu?”
“Nampata wapi huyu mzee unadhani? Ni yupo busy muda wote, yani akitoka asubuhi anaweza akarudi au asirudi hata tushazoea kuishi bila kumuona baba hata wiki na tunaishi nae nyumba moja”
“Sasa si umfate kazini kwake?”
“Aaaah Yule mzee wangu wa kumfata kazini? Yani yeye aliniambia nikiwa na shida na hela nimtumie tu ujumbe kwenye simu yake kisha ataniingizia kwenye akaunti yangu na huwa nafanya hivyo, yani unajua mimi nilikuwa naishi kwa mama na huku kwa baba nilikuwa nakuja mara moja moja sababu ya hivi kupooza ndani na baba hashindi nyumbani, tulianza kuja kukaa kwa baba baada ya kukubaliana na Erick kuwa tufanye hivyo ila sasa humu ndani tunaishi kama watu tusio fahamiana yani unaweza usirudi mwezi mzima na hakuna atakayekuulizia kuwa umekwenda wapi, baba yupo busy hatari yani hana muda wa kukaa na watoto wake kabisa, maisha yetu sisi ni tofauti na familia zingine ila siku nataka nikipata muda nimwambie baba yote ya moyoni ndiomana sijaenda kwa mama wiki nzima hii kwani nataka siku baba akiwepo nyumbani tu basi nimwambie kila kitu.”
“Nimekuelewa Tumaini, basi tusubiri tu hiyo Jumamosi tujue ni kitu gani ambacho Erick anasema twende kwenye duka lake”
Wakawa wanaongea ongea pale kisha kukubaliana kuwa siku ya Ijumaa basi Sia aende kulala pale ili Jumamosi waongozane na huyo Erick huko aliposema waende.
 
SEHEMU YA 389

Steve alikaa pale nje ya chumba cha Sia akimsubiria na siku hiyo Sia alirudi kwenye mida ya saa nne usiku na kumkuta Steve nje kwake, aliamua kumkaribisha tena ndani maana kuna muda alimuonea huruma ukizingatia sio kosa lake ila ni kosa ya dawa alizokuwa anamfanyia Erick, ila Steve kuingia mule ndani wala hakujiona kuwa anamatatizo kumsubiri muda wote huo Sian a aliendelea kumwambia jambo moja tu kuwa anampenda sana, leo Sia alijaribu kuongea kiasi na Steve kuangalia akili za ile dawa,
“Steve, unanipenda kwa kiasi gani?”
“Sijui hata nieleze vipi ila nakupenda Sia na ninakuona mpya kila muda”
Muda wote Sia alitamani haya maneno yangekuwa yanatoka kwenye kinywa cha Erick ila yalitoka kwa Steve na kumkosesha amani kabisa, basi muda ule Sia alianza kupika hukua kisaidiwa na Yule Steve kisha kwenye saa tano usiku wakala chakula na kuamua kulala, yani siku ya leo pia Sia alilala na Steve kama jana yake yani alilala nae kama mpenzi wake na kulivyokucha alijilaumu kulala nae kwani alijua kama Erick akigundua basi hatoweza kuwa nae tena maana ingawa na matukio yote ila bado alikuwa na imani ya kupiganiwa penzi lake kwa Erick maana aliona Tumaini yuko upande wake na mama Erick alikuwa upande wake. Basi kama kawaida alimuomba Steve aondoke na kumwambia kama kuja awe anakuja usiku sana,
“Ila kesho usije maana naenda kulala kwa rafiki yangu”
“Jamani, nimekuzoea sana Sia”
Ikabidi ampemaneno ya kulamlainisha na kuweza kuagana nae.

James leo alienda tena kwa lengo la kuangalia familia yake, alimkuta mama yao yupo ila leo hakumtimua bali alimwambia jambo moja tu,
“Si wewe unataka kurudiana tena na mwanangu?”
“Ndio, nahitaji kuwa karibu na familia yangu, nahitaji kuishi nao hata sijui niliingiliwa na kitu gani kilichofanya niisahau familia yangu”
“Sawa, basi kesho mguu wako na mwanangu na mimi mwenyewe tunaenda hospitali kupima yani lazima tupime afya yako na mwanangu tujue ndipo niruhusu uendelee kuishi na moto wangu”
“Sawa mama nimekubali”
Kwahiyo wakakubaliana nae kuwa kesho yake aende kuwachukua waende hospitali kupima ili kujua afya yake na mke wake, baada ya hapo akaaga na kuondoka.
Erica alimuuliza mama yake swali ambalo aliulizwa na dada yake,
“Hivi mama mfano mkimkuta shemeji kaathirika mtafanyaje?”
“Kuna cha kufanyaje hapo? Ni kumwambia tu ampe mwanangu talaka basi kila mtu aendelee na maisha yake”
“Mmmh mama hivi unadhani atakubali kiurahisi hivyo?”
“Atajijua mwenyewe hakuna aliyemtuma awe muhuni, mwanangu katulia yeye anataka kumtia uchizi tu masikini ya Mungu, acha mwanangu aendelee na maisha yake tu”
“Mfano mama shemeji akikuletea hela je!”
“Hivi unanionaje Erica, unasahau kuwa mimi ndiye niliyekwambia turudishe hela za Yule mzee Jimmy! Mimi nachagua hela, kuna hela na hela za kutumia sio kila hela inayoitwa hela ni ya kuipenda tu maana kuna hela zingine zinaweza kukutokea puani ndiomana nikasema turudishe hela za Yule mzee”
Erica akacheka tu ila simu yake ilianza kuita na namba ilikuwa mpya, akaipokea na mpigaji alikuwa ni mzee Jimmy,
“Jamani wewe mzee una nini lakini? Sitaki mawasiliano na wewe”
“Nipe mama yako niongee nae”
Erica akampa mama yake ile simu,
“Sikia, hata usianze kuniletea maneno yasiyoeleweka. Niliweka hela zangu kwenye mlango wako ukazipokea inamaana kuwa umekubali niwe mkweo, hiyo ni posa tu na siku ipo nitaleta mahari nimchukue mke wangu”
“Una akili wewe mzee? Umechanganyikiwa au?”
Simu ikakatika, Mama Erica aliangaliana na mwanae na kuanza kujadili mwenendo wa huyu mzee,
“Unajua huyu mzee simuelewi, anazungumzia hela gani jamani mbona anatuletea makubwa huyu kwenye familia yetu? Sijawahi kukubali hela ya huyu mzee maana akili zake nazielewa toka sijamfahamu machale yalinicheza ndiomana sijawahi kukubali hela zake, kweli jamani tukute hela za huyu mzee mlangoni tutumie tu inawezekana kweli?”
“Sasa hizo hela anazozisema zitakuwa wapi jamani?”
Bite alisikia maongezi yao na kusogea karibu kuendelea kusema kuhusu hisia zake za hizo hela,
“Jamani mimi nahisi kwamba hizo hela zimechukuliwa na Erick, mnaweza mkanielewa vibaya ila hizo hela ni Erick tu amezichukua hata sio mwingine”
Basi Erica akaongea kumtetea kidogo Erick,
“Angekuwa Erick angeuliza tu jamani, ila basi isiwe kesi Jumamosi Erick alisema kuwa atakuja Yule Moses kunichukua ili anipeleke mahalia ambako nitakutana nae basi nitamuuliza na hilo swala, inawezekana ni kweli Yule mzee aliacha pesa kwetu ila inawezekana hizo pesa labda zilipeperuka”
“Zipeperuke vipi na alisema zilikuwa kwenye bahasha. Kweli milioni tatu kwenye bahasha ipeperuke? Labda kama ni upepo wa kimbunga ila sio huu wa kawaida, halafu aliacha mlangoni jamani ipeperuke vipi, mtanielewa vibaya tu ila atakuwa Erick, mnaona ana pesa ila nataka mjue uwa pesa hainaga kusema inatosha”
“Hata kama ni hivyo bado Erick hawezi kuchukua pesa nyumbani kwetu”
Walibishana tu na kumalizia kazi za siku hiyo kisha kwenda kulala ambapo usiku Erick alimpigia simu Erica kama ambavyo alikuwa akimpigia simu zamani na kuendelea kumpa ratiba ya Jumamosi,
“Sijaja kwenu leo na kesho sitakuja sababu naandaa kuhusu Jumamosi na atakuja kukuchukua Moses, sitaki ujue ni wapi anakuleta ila utajua hiyo sehemu ukifika hata usijali umesikia mpenzi wangu eeeh!”
“Sawa nimekuelewa Erick”
Wakaongea mengi mengi na kisha kuamua kuagana na kulala.
 
SEHEMU YA 390

Kesho yake kama walivyopanga James alifika mapema kisha akawasubiri Bite na mama yake wajiandae halafu akatoka nao kuelekea hospitali, walipofika hospitali mama yao alikaa pembeni akisubiri waende kupima kiukweli James hakuelewa kwanini mama mkwe kaamua kufanya vile wakati yale ni mambo ya wana ndoa yani angeenda tu yeye na mke wake ila mama mkwe nae alionekana yupo bega kwa bega kutaka kujua kisa na mkasa.
Alitulia tu kwa muda kiasi wakingoja majibu na badae waliitwa kwa daktari kwaajili ya majibu na kupata majibu kuwa Bite ni mzima ila James ameathirika, kwakweli James alijaribu kuvuta picha ya wanawake wote aliopita nao ila hakujua ni yupi kamsababishia maambukizi ya virusi vya ukimwi, daktari aliwashauri pale ila waliondoka bila maelewano wala nini, na walipotoka nje kila mmoja aliondoka kivyake vyake yani James aliwaacha pale hospitali kana kwamba hakwenda nao hospitali kisha yeye kuondoka zake na kufanya Bite arudi kwa mama yake tu na kumwambia ilivyokuwa halafu na wao kuondoka.
Walipofika nyumbani mama yao alisema alijua tu,
“Yani nilitaka nishangae James awe na mahusiano na Yule Dora halafu atoke mzima hapana Yule James kayataka mwenyewe”
Erica akasema,
“Ila shemeji ni yeye mwenyewe ana tabia mbaya, tunaweza sema ni Dora tu ila usikute hata shemeji kapeleka ugonjwa kwa Dora kwani hiyo kansa ya shingo ya kizazi kaitoa kwa Dora!”
“Nimenyamaza kimya tu ila roho inaniuma sana yani siamini haya mambo naona kama maigizo vile ngoja tu nikae kimya”
Ilionyesha kuwa Bite hakuwa na furaha kabisa ila alijaribu tu kuweka furaha katika sura yake.

Jioni ya siku hiyo kama ambavyo Tumaini na Sia walivyopanga kuwa walale nyumba moja yani pale nyumbani kwakina Tumaini na ilikuwa hivyo maana Sia alienda pale na walifanya vitu pamoja siku hiyo.
Erick alirudi kwao kwenye mida ya saa tano na ilionyesha alichoka sana kwani alijikuta tu akikaa sebleni na kushikwa usingizi hapo hapo, Sia alipoona vile alimuita Tumaini na kumwambia jinsi Erick alivyolala pale sebleni na kuanza kumpa wazo lake,
“Unaonaje nisogee pale kwa Erick unipige nae picha halafu tumtumie Erica au unasemaje?”
“Umekumbuka swala muhimu sana”
Basi Sia alienda kujifunga kanga kisha kuanza kupiga picha mbalimbali na Erick huku wakitamani hata kumvua nguo ila Sia alipoanza kumfungua shati Erick alishtuka na kuchukia sana kisha kuanza kumfokea dada yake,
“Ujinga ujinga wako kama huu ndio unafanya niondoe upendo wangu kwako. Wenzio huwa upande wa kaka zao yani hupenda wachumba wale ambao kaka zao wamewachugua ila wewe unataka kunichagulia mimi mwanamke! Sikupendi Tumaini”
Kisha akainuka na kwenda chumbani kwake ila bado haikuwaingia akilini kwani zile zile picha walimtumia Erica na kumpigia simu kuwa aingie kwenye mtandao walijua tu atapaniki sana.
Kisha wakalala.
Palipokucha walijiandaa kama kawaida na kuondoka na huyo huyo Erick kuelekea kwenye lile duka lake, walishangaa walipofika jinsi palivyopambwa na jinsi wageni walivyokuwa wakiwasili pale dukani, walijiuliza kuwa kuna nini wakapata kusikia tetesi kuwa siku hiyo ni siku ambayo Erick anataka kukabidhi duka lile kwa Erica, kwakweli Tumaini alichukia sana alihisi kama kuna donge moyoni mwake, akasikia kuwa Moses ndio anaenda kumchukua Erica, kwakweli walichukia sana,
“Natamani nisingeiona hii siku aaargh”
“Ila usijali Tumaini, unajua Erica kama aliziona zile picha kwa hakika hatofika hapa”
“Kweli eeh!”
“Ndio ni kweli hatofika”
Basi muda nao ulienda na Erica hakutokezea wakahisi kuwa kweli njama zao zimefanikiwa na kujiona kuwa ni wajanja jana yake kufanya vile ingawa hawakujua kuwa Erick anataka kufanya nini, laiti wangejua basi wangefanya makubwa kushinda yale waliyoyafanya jana.
Wageni walianza kuondoka baada ya kuona muhusika hafiki, kwakweli hata Erick alichanganyikiwa kwani kila alipompigia Erica simu hakupokea simu yake.
Muda kidogo aliona gari la Moses likifika eneo lile kwahiyo Erick alijua ni Moses kamleta Erica lakini alishangaa kumuona Moses akishuka mwenyewe bila ya Erica.



Muda kidogo aliona gari la Moses likifika eneo lile kwahiyo Erick alijua ni Moses kamleta Erica lakini alishangaa kumuona Moses akishuka mwenyewe bila ya Erica.
Kwakweli Erick alichanganyikiwa kabisa na kumsogelea Moses akamkunja kuwa ameshindwa vipi kumshawishi Erica kufika pale,
“Umeshindwa vipi Moses? Unajua nakuamini sana”
“Usinilaumu bosi, nimefanya jitihada zangu zote. Angalia Yule”
Kuangalia pembeni akaona gari ya Erica ikiingia yani hapo alijikuta akijawa na tabasamu tu na kusogea karibu ili kumfungulia mlango, kisha Erica alishuka kwelye lile gari, alikuwa amechelewa ila kile kitendo cha kufika tu ilikuwa ni faraja kubwa sana kwa Erick, akamkumbatia kwa furaha ya kumuona muda huo.
Hakutaka kusikiliza maelezo ya kwanini amechelewa bali alienda kumkabidhi lile duka, kwakweli Tumaini na Sia waliondoka kwani hawakuweza kuendelea kuangalia hadi mwishoni kitu kinachotokea. Erick alimwambia Erica,
“Najua ulikuwa unatamani sana kuanza biashara, kuanzia sasa huna haja tena ya kutafuta kazi Erica maana kazi yako itakuwa kusimamia hapa na kuangalia maendeleo ya duka lako”
Erica alimsogelea Erick na kumkumbatia huku akimbusu kwa furaha.
Sababu muda ulikuwa umeenda, basi Erick alitoka na Erica eneo lile na kwenda hotelini ambako alisema wawaandalie chakula kisha walikuwa pamoja na wageni waalikwa wengine waliobaki, na baada ya kula wengi waliondoka na kuwaacha wawili tu yani Erick na Erica, kwakweli Erick alikuwa akifurahia tu uwepo wa Erica hata kumuuliza kwanini kachelewa hakuwa na wazo hilo, mpaka Erica mwenyewe akamuanza,
“Erick, jamani mbona hujaniuliza kuwa kwanini nimechelewa”
“Aaaah nimejikuta nikiwa na furaha sana mpenzi wangu hadi nimesahau kama ulichelewa yani sijaumia kuondoka kwa wageni ila ningeumia kutokukuona wewe, eeh kwanini umechelewa kipenzi changu?”
“Ni hivi, basi niliamka asubuhi vizuri tu na kuandaa nguo zangu kwaajili ya kuja sasa nikashika simu nikakuta kuna ujumbe unasema niingie facebook, si ndio nikaingia nikakuta picha zako tena na Sia, kiukweli nilishikwa na wivu wa hali ya juu unajua Erick nakupenda sana yani sana. Kiukweli niliumia kuona tumepanga vizuri na wewe kweli unaenda kutembea na Yule mwanamke ambaye huwa nagombana nae kila siku? Niliumia sana mpenzi”
Erick akataka kuonyeshwa hizo picha, basi Erica akafungua simu yake na kumuonyesha Erick,
“Kumbe jana nilipokuwa nimechoka ndio wakafanya huu ujinga, tena mpiga picha atakuwa tumaini huyo. Ngoja nirudi nyumbani atanieleza, yani ni dada yangu lakini hajielewi. Sasa mpenzi wangu ungenihukumu bila sababu tu, sijui nani kanisaidia kuongea na wewe ukaelewa na kuja dah namshukuru sana”
“Yani nilikuwa nimechukia hata kujiandaa sikutaka tena basi nikawa nimekaa tu kwa hasira, basi hadi muda Moses anafika nilikuwa sijajiandaa na akaniambia twende nikamwambia siendi tena akaanza kunibembeleza kuwa huwezi kumuelewa ila bado nilimgomea nikaenda chumbani basi mama akanifata na kuanza kuongea na mimi, nikaona nisimfiche nimwambia kuwa kuna picha nimetumiwa zako na Sia, mama akasema hao wamenipangia njama sababu kwanini wasitume siku zote hadi siku niliyopanga kuonana nawe, basi mama aliongea nami pale nikaanza anza kumuelewa ndipo nilipotoka tena na Moses kusema kuwa jana mlikuwa wote kwenye maandalizi na mmerudi mmechoka kweli, niliingia ndani nikajifikiria nikasema kwavile nakupenda acha tu nije ndio nikaenda kujiandaa basi nilipomaliza nilimwambia Moses awe mbele na gari yake na mimi nitakuwa nyuma yake na gari yangu maana nilitaka kukufanyia surprise pia ujue kama najua kuendesha gari”
“kwanza Erica nisamehe mpenzi wangu maana kuchoka kwangu ndio kumefanya wale wajinga wanipige picha ila hakuna chochote kinachoendelea baina yangu na Sia, haya ndio mambo yaliyofanya kipindi unaumwa niishi hotelini tu sababu ya ujinga kama huu. Nisamehe mpenzi wangu”
“Usijali nimekusamehe sababu nakupenda sana”
Erick alitabasamu kwani alifurahi sana kusikia Erica akimwambia tu hivyo, akamsogelea karibu na kumbusu. Alikuwa na tabasamu usoni ila alipata chuki kubwa sana juu ya dada yake Tumaini kwani aliona hamtakii mema na mapenzi yake, kisha aliendelea kufurahia uwepo wa mpenzi wake Erica na baada ya maongezi yao aliamua sasa kumrudisha nyumbani kwao,
“Mmmh Erick, narudi mwenyewe nyumbani. Kumbuka nina gari, kwahiyo naenda mwenyewe tu”
“Usiku huu Erica, acha nikurudishe halafu mimi nitampigia dereva anifate ila naomba nikurudishe sitaweza kuwa na furaha nikisikia habari mbaya juu yako, bora itupate wote”
Erica alimuangalia sana Erica na kujiuliza upendo huu wa Erick siku zote alizokuwa akitangatanga na kuumizwa na mapenzi ulikuwa wapi upendo wa hivi? Hakupata jibu kwakweli.
Kwahiyo muda huo Erica na Erick walipanda kwenye gari wakielekea nyumbani kwao na wakina Erica.
 
SEHEMU YA 391

Walifika kwakina Erica ilikuwa ni usiku sana tayari maana ilikuwa inakaribia saa tano usiku, ila walipokuwa njiani tayari Erick alimuita dereva wake kwahiyo walivyofika kwakina Erica tu na dereva wake alikuwa ameshawasili basi akaingiza lile gari kwenye uwanja wa kina Erica na kumsaidia kufunga geti kisha kumuaga kwa kumbusu Erica na kuondoka amapo Erick alienda kupanda ile gari iliyokuja na dereva na kuondoka.
Erica alienda ndani kwao na kumkuta mama yake akiwa sebleni, kisha mama yake akasema
“Sijalala Erica nakusubiria wewe mwanangu. Najua na Erick itakuwa mmeitiana mambo mazuri tu ila mpaka muda huu unanipa mashaka mwanangu? Umeenda kufanya mapenzi na Erick?”
“Hapana mama, nimekubaliana nae mpaka ndoa”
“Usitake kunichekesha mie, hilo swala la kukubaliana mpaka ndoa liko wapi? Yani toka lini Simba na swala wakae pamoja halafu umwambie samba subiri nimchemshe huyo swala ndiyo umle. Erica mwanangu nakwambia kila siku wanaume sio wa kuwaamini kiasi hiko, sijakwambia hata picha za kijinga vile uziamini ila sababu mwanaume kaonyesha hitaji lake la kukuoa basi acha akuoe mwanangu kwanza”
“Sawa mama nimekuelewa hakuna tatizo mama yangu”
Kisha akamuuliza sasa kuwa ni kitu gani Erick alimuitia siku hiyo,
“Huwezi kuamini mama, Erick amenikabidhi duka yani ndio nitakuwa naenda kufanya biashara, sina sababu tena ya kutafuta kazi”
“Wow mwanangu hongera sana”
Bite alisikia na kwenda kusikiliza vizuri kwakweli alijisikia rah asana na kumuona mdogo wake kuwa na bahati ya hali ya juu. Ila akamuuliza kuhusu swali ya zile hela za mzee Jimmy,
“Eeeeh Erica umemuuliza na kuhusu hela za Yule mzee?”
“Aaah nimesahau ila nitamuuliza tu”
Basi mama yao akaendelea kuongea,
“Tena Bite kakumbusha, mwanangu Yule mzee yupo serious alikuja hapa anasema tumekula posa yake, na anasema kashaiambia familia yake kuwa atakuoa”
“Kheee huyo mzee ana wazimu mama”
“Tena ana wazimu kabisa mwanangu, yani Yule mzee hafai kabisa. Hebu umuulize Erick na kama akikataa basi huyo mzee niachieni mimi nitajua jinsi ya kula nae sahani moja, si anajifanya akili zake zimefyatuka basi zangu ndio hazipo kabisa.”
Basi Erica akaongea ongea na mama yake kisha akaenda chumbani kwake kulala.

Erick alienda nyumbani kwao na kufika tu alimuita dada yake kwani alikuwa na lengo la kumsema kwanza, Tumaini alitoka chumbani ila alikuwa amevimba kwa hasira jumlisha wivu maana kwake halikuwa swala la kawaida kuona mdogo wake anaacha kumpa yeye vitu vya thamani anampa mwanamke, anamuondoa yeye kwenye duka na kumpa mwanamke? Kwakweli aliumia sana, kwahiyo alikuwa amevimba kwa hasira hata kumsalimia Erick hakumsalimia tena na kumwambia,
“Niambie ulichoniitia”
“Unajua wewe Tumaini ni dada yangu ila hujielewi, hivi unadhani ungejielewa mimi ningefanya yote haya?”
“Usiniambie hivyo Erick, yani unamthamini mwanamke na kusahau kuwa mimi ndiye ndugu yako pekee niliyekuwepo! Hivi ukipata matatizo wewe ni nani atakayeumia hapa, unafikiri Erica ataumia kuzidi mimi?”
“Tumaini, Yule Erica si mke mwenzio ujue, yule ni wifi yako hutakiwi kuweka vita na ushindani na yeye. Nilikuthamini, nilikuheshimu dada yangu ila mambo yako unayoyafanya ndio yanafanya niwe hivi leo, haiwezekani wewe uwe upande wa Sia, huwezi kunichagulia mwanamke wa kuwa nae mimi, mara ulianza na Yule Asha sijui yani wewe dada yangu sijui una akili gani, hujui kama unatakiwa uwe upande wa kaka yako? Hivi mfano nipo na Erica haijalishi Sia alikuwa rafiki yako vipi ila unatakiwa uwe upande wa Erica ili uweze kuenenda na mimi kaka yako halafu ungeona kama ukitaka kitu ningegoma kukupatia. Hivi unadhani mimi ningeshindwa kumfungulia biashara nyingine Erica? Naweza na hata sasa naweza kumbadilishia biashara na kukurudisha pale ila kwanza akili yako hiyo isomeshe ijue inafanya kazi gani. Hivi kweli wewe wa kushirikiana na Sia kunipiga piga za ajabu unamtumia Erica ili iweje? Mara nyingine unaweza sema mawifi wakorofi sijui mke wa kaka mbaya ila kumbe mbaya ni wewe, hivi ukiwa karibu na wifi yako kungekuwa na tatizo? Mbona Erica hana tatizo na wewe ila kila siku wewe kuleta matatizo na Erica? Jirekebishe bhana”
Tumaini alichukia na kwenda zake chumbani maana hata hakutaka kusikiliza maneno ya kaka yake ingawa alichoambiwa na kaka yake kilikuwa cha ukweli.
Akawaza tu asubuhi aende kwao kwa mama yake labda akaongee nae kuhusu swala hilo maana yeye alihisi kuonewa tu.

James hakuwa na hali badala yake alikunywa sana pombe kisha akaenda kwa Yule mwanamke aliyezaa nae ambaye alikuwa ni msichana wao wa ndani, Yule mwanamke alivyomuona tena aliona kuwa neema imemuangukia kwa kumpata James tena baada ya mke wake kufanya varangati la kumrudisha James nyumbani, alimkaribisha vizuri sana na akampa malezi yote kama mume maana hakutaka tena kuachwa na James.
Yani siku hiyo aliona ndio siku ya kumuonyesha James ufundi wote aliokuwa nao ili James asinyakuliwe tena na mke wake,
“Jamani james, nilisikitika sana ambavyo uliondoka moja kwa moja sababu ya mkeo, kweli James ukagoma kabisa kuonana nami sababu ya mkeo! Ila nafurahi sana leo umekuja mume wangu”
Basi huyu dada alimpa James huduma zote na kumfanya James asahau swala la ugonjwa kabisa, alilala huku amechoka kwa furaha ya kupokelewa na Yule mwanamke jumlisha pombe alizokuwa amekunywa.
Kulipokucha, Yule dada aliamka na kumsalimia James maana aliona ndio mume wake nay eye alitamani sana ifike tena wakati ambao James angeenda kulala kwake, basi akaanza kuongea nae kimapenzi ili kumfanya ampende zaidi,
“Unajua James mimi ndio nakupenda, mtoto huyu kachukua jina lako nay eye anaitwa James sababu tu ya upendo wangu juu yako sio mkeo kumpa mtoto jina Junior sasa Junior ndio mavitu gani? Yani Yule mkeo hana hata upendo na wewe, ni mimi nikupendaye”
“Nashukuru sana mama James, nashukuru pia kumpata mrithi wa jina langu kwenye ulimwengu ila asirithi na tabia zangu”
“Hamna bhana James, wewe huna tabia mbaya ila mkeo hakujua jinsi ya kuishi na wewe. Nilikuwa naumia sana vile anakuacha uteseke eti sababu ni mjamzito, mbona mimi nilikuwa nakupa wakati nimebeba mimba ya James! Ni upendo tu, nakupenda sana tena natamani unioe kabisa kabisa”
James akatabasamu tu ila alijua wazi huyo msichana anamfurahia sababu hajajua ukweli kuwa ameenda pale baada ya kujigundua kuwa ameathirika kwahiyo alikuwa anaenda kujiliwaza tu na akili yake.
Sababu siku hiyo haikuwa siku ya kwenda kazini kwahiyo aliamka na kujiandaa tu kisha kuondoka kuelekea nyumbani kwake ili akavae nguo zingine kwani kwa muda huo shida yake ilikuwa kukutana na Dora amuulize pia kama nay eye ameathirika maana siku zilizopita alikuwa naye kwenye mahusiano.
 
SEHEMU YA 392

Tumaini alienda kwa mama yake na kweli alimkuta mama yake siku hiyo alikuwa mwenyewe nyumbani kwani ndugu zake wote walitoka, akamsalimia na kumuuliza
“Kheee mama mbona nyumba ipo kimya hivi?”
“Si unajua leo siku ya mapumziko basi wameenda kwenye matembezi huko na kuniacha mwenyewe. Eeeh na wewe mbona siku hizi huji nyumbani?”
“Mama, yani acha tu. Yule mdogo wangu, ndugu yangu ambaye mimi ndiye dada yake wa kipekee kanifanyia mambo ya ajabu sana”
“Mambo gani tena mwanangu?”
Basi Tumaini akamueleza kwa kifupi kaka yake alichokifanya na jinsi anvyomjibu,
“Ila mwanangu kwani huyo wifi yako una ugomvi nae? Na ndugu yako anafikia vipi kumthamini mwanamke kushinda wewe ndugu yake? Au karogwa?”
“Ndio nahisi hivyo mama, nahisi ndugu yangu karogwa. Huyo mwanamke sina ugomvi nae ila sitaki awe na kaka yangu kwani kazaa na mwanaume mwingine. Yupo msichana mama nayempenda kwa dhati kaka yangu ndiye nataka huyo awe wifi yangu”
“Tumaini mwanangu, kwani mtu akizaa ndio hafai kupendwa tena?”
“Hapana mama ila kazaa na mwanaume mwingine”
“Pengine alibakwa!”
“Hakubakwa mama, huyo msichana ni malaya”
“Hata kama ni malaya ndio kampenda, mwanangu mwanamke yeyote akipendwa na kaka yako mwache awe nae kama ana kasoro utamwambia tu kaka yako ili azichunguze mwenyewe ila sio wewe kumuwekea chuki au kumchagulia kaka yako mwanamke wa kuishi nae. Kumbuka huyo mwanamke hatoishi na wewe, ataishi na kaka yako, maswala ya kuchaguliana wachumba yalishapitwa na wakati mwanangu. Una uhakika gani huyo unayemtaka wewe katulia?”
“Nina uhakika mama, Sia namfahamu. Ni binti mpole, mwenye hofu ya Mungu na ana upendo ila sio huyo Erica jamani huyo msichana hafai mama yangu”
“Ndio hafai mwanangu ila si wewe ambaye utaishi na huyo Erica, sikia nikwambie cha kufanya ili kula sahani moja na kaka yako kuwa nae pamoja na umsapoti kwa anachofanya kama kizuri mpe hongera na kama kibaya usimponde ila mwambie ukweli nadhani unanielewa. Kaa na kaka yako ongea nae kirafiki ujue ni kwanini anampenda huyo anayempenda na kwanini anamchukia huyo unayempenda wewe. Ongea nae kirafiki na tena mwambie kaka yako upo tayari kuwa karibu na huyo wifi yako mwingine uone kama atakufanyia tena vitu vya ajabu.”
“Mama, unasema tu ila hujui kinachoendelea namchukia huyo Erica yani simpendi kabisa, ni mbaya Yule msichana na ana roho mbaya, kafanya undugu wangu na Erick uvurugike kabisa, simpendi namchukia”
Yani Tumaini hakutaka kusikia ushauri wa mama yake kabisa kwani yeye alihisi tu kuonewa na vitu mbalimbali kwani alihisi pia kaka yake karogwa kwani hakufikiria kama ni kitu kinachowezekana yani mwanamke wan je athaminiwe zaidi kuliko damu moja.

Rahim leo hakuwa na furaha kabisa kwani toka alipopewa namba ya Zainabu alikuwa akijaribu kumpigia ili ampe hoja zake alishangaa Zainabu akiongea nae maneno ya Mungu tu, ingawa alikuwa akitaka na ushauri kweli ila lengo lake kubwa kwa Zainabu ni kumtaka kimapenzi kwahiyo swala la Zainabu kumwambia maneno ya Mungu hakulipenda kabisa na akaona ni vigumu kumvaa huyo mwanamke, alikuwa na mawazo sana ila alifika Babuu na kuongea na ndugu yake ambapo alimuuliza kuwa ana mawazo ya kitu gani,
“Sikia Babuu, nishamtimua mke wangu simtaki tena najua unatambua hilo. Najua pia kumpata Erica kwasasa ni ngumu sana, ila kuna mwanamke nimemuona na nadhani ananifaa sana katika maisha yangu”
“Umemchunguza kaka”
“Aaah hapana ila anaonekana ni mwanamke mwadilifu. Tatizo linalonifanya niwe na mawazo sana ni jinsi ya kumuingia Yule mwanamke”
“Kwani tatizo ni nini mpaka ishindikane kumuingia?”
“Yani ni mwanamke mshika dini balaa, nimejaribu kumpigia simu mara kadhaa anaanza kunieleza sijui habari za Quran na mimi sitaki hizo habari kwakweli, sijui nitawezaje kumpata”
“Sasa ndugu yangu kuzunguka kote huko hujajua jinsi ya kumuingia mwanamke? Ukimtaka mwanamke ambaye unaona ni vigumu kuingilika jifanye na wewe upo upande wake, yani kama huyo alivyo jifanye na wewe ni Muislamu safi yani anza kwenda Msikitini ndugu yangu halafu unapita na pale kwao unajifanya kuongea mambo ya dini tu. Kama mwanamke mlokole na anashindwa kuingilika unajifanya nawe mlokole, ndugu eeeh wanawake ni viumbe dhaifu na wepesi kudanganyika yani ukijifanya umefata dini utampata ila ngoja nikuulize una lengo nae kweli au?”
“Akikubali naoa kabisa, yani mimi siwezi kumrudia Salma yani huyo Zainabu akikubali ndio atakuwa mke wangu na hivi kashika dini na mimi nina watoto wengi wengi basi ataweza kulea watoto wangu”
“Kama ni hivyo basi nitakusaidia yani tutakuwa tunaenda wote kwake, nitahakikisha hadi tunampata anakuwa kwetu kaka”
“Asante sana Babuu”
Kiukweli Babuu alijitolea kumsaidia Rahim kuhusu kumpata Zainabu sio sababu anahitaji ampate ila sababu hataki amfatilie Erica kwani anahisi Rahim akiwa na Erica basi yeye ataumia sana moyo wake.
 
SEHEMU YA 393

Nasma aliamua kurudi tena nyumbani kwake na safari hii aliamua kurudi na mama yake kwani aligoma kwenda na ndugu yake mwingine sababu hakuamini tena swala la kuishi na ndugu kwa mume kama Bahati, mama yake alikubali ili akaishi nae kidogo mpaka pale mtoto akichangamka zaidi, basi aliondoka na mama yake na kwenda nae nyumbani kwake.
Walivyofika mama yake alimuuliza vizuri kuhusu dawa alizopewa na baba yake na jinsi zilivyomgeuka, kumbe muda huo alifika dada yake Bahati aliposikia wanaongea ndani akajibanza pale nje akiwasikiliza,
“Yani mama tulifanya dawa ili Bahati anipende mimi tu awe haoni wala hasikii juu yangu sema zile dawa hajiweza kumfikia”
Kisha akaanza kumueleza alivyofanya dawa na kufanya Bahati abadilike kabisa maana kawa tena hashikiki na nyumbani halali maana jogoo jogoo haswaa yani kila jike lake, kumbe dada wa Bahati alisikiliza kwa makini sana akaona ile taarifa ni vyema akaipeleka kwa ndugu wengine wa Bahati maana walishangaa kwa kipindi hiko Bahati kubadilika kuwa na riho ya tofauti, ni kweli mwwanzo walishiriki katika kumpa dawa ila hawakutaka ndugu yao apewe dawa zaidi maana madhara ya dawa waliyaelewa kwahiyo ile habari ilimshtua kidogo na kuamua kwenda kuwaambia ndugu zao wengine.
Mule ndani Nasma alikuwa akiongea tu na mama yake bila kujua kinachoendelea nje kumbe wifi yake alishasikiliza kila kitu.

James alikutaka na Dora kama alivyopanga nae ili kuongea nae kuhusu lile swala ambalo lilikuwa likisumbua akili yake, alimuuliza
“Dora ushawahi kupima wewe?”
“Kupima? Aaah sijawahi”
“Basi ningependa ukapime”
“Kwani vipi James? Mbona sikuelewi?”
“Aaaah ukapime tu au twende nikusindikize”
Kwakweli akili yake haikuwa sawa kabisa na kuamua muda huo huo kwenda na James kupima, walifika hospitali na walipima wote wawili kwani hata James bado hakuwa na imani na majibu yake ya mwanzo, majibu yakaja kuwa wote wameathirika.
Kwakweli ile habari ilionekana kumchanganya sana Dora, ikabidi James ambembeleze tu na kwend akukaa nae kwenye gari yake maana yeye alishalia jana yake yakaisha kwahiyo alikuwa akimbembeleza tu Dora, yani Dora alilia huku akisema,
“Yani niliwahi kumwambia Erica kuwa nimeathirika ila nilikuwa namtania tu yani nilifanya kuwa na ukimwi kama kitu cha utani eti leo nina ukimwi kweli mimi Dora jamani, haiwezekani nilikuwa natania tu jamani”
“Yani Dora ulikuwa unatania kusema kuwa una ukimwi! Walioupata pia hawakutaka waupate ila imetokea tu yani wewe ukatania unao kweli! Au ndiomana wakakazania nikapime sababu wewe ulitania kuwa unao? Haya sasa unao kweli, kuwa mpole tu tuanze dozi”
Kiukweli Dora hakuwa na furaha kabisa hivyo kwa siku hiyo aliamua kwenda tena baa na James na kunywa sana pombe yani alirudi kwao ni usiku kabisa na alirudishwa na James na kwenda kulala tu kisha James naye alienda kwa Yule mwanamke ambaye alikuwa ndio mdada wao wa kazi.
Kulipokucha Dora aliamka akiwa na uchovu sana ukijumlisha bia za jana na mawazo basi aliamka na uchovu balaa, akainuka na kwenda kuoga ila bado alikuwa hajiamini amini kama ameathirika maana hakutegemea kabisa kama kuna muda atapatwa na virusi vya ukimwi.
Mama yake alimuona jinsi alivyo na mawazo ila Dora hakumwambia mama yake kuwa ni kitu gani kinamsumbua badala yake, aliishia tu kuongea nae mambo mengine, kisha mama yake akaanza kumueleza,
“Dora mdogo wako Steve, toka juzi hayupo hapa nyumbani yani simuelewi kabisa mdogo wako jamani ana matatizo gani?”
“Kheee hajarudi nyumbani?”
“Ndio hajarudi, jana na wewe umerudishwa hapa usiku wa manane jamani kuna watu wanazaa ila wengine sisi sijui tumezaa mavitu gani jamani yani watoto wangu wawili tu nyie ila ni kichefuchefu. Haya ukamlete basi mdogo wako ulipoenda kumtoa siku ile”
“Sawa mimi nitaenda mama ila nilikwambia tusimame kwenye maombi”
“Hayo maombi utakuwa nayo wewe bhana, jana umerudi hapa umelewa bwiii hayo maombi ya wapi ya walevi? Hata huyo anayekuombeeni naye atakuwa akili zake sio nzuri yani haoni kama anaombea vichaa, sasa ukamlete mdogo wako, mi ujinga huu siutaki kwakweli”
“Sawa mama nitaenda ila ngoja nipumzike kidogo halafu nitaenda”
“Hakikisha mdogo wako anarudi hapa nyumbani, sawa”
“Sawa mama”
Kisha Dora aliingia ndani kwake tena alikuwa na mawazo mengi sana ila alitulia kwanza ili atulize akili zake ndio ajiandae kwenda kwa Sia kumfatikia mdogo wake Steve.
“Safari hii huyo Sia itabidi nimpeleke tu kwa mwanamaombi ili mdogo wangu akomboke, yani ukisikia mchimba shimo kadumbukia mwenyewe ndio huku sasa, yani nimetumbukia hatari kwenye shimo nililochimba mwenyewe, nimeenda kwa mganga kumkorogea James dawa ila nimepata ukimwi, nilikuwa namdanganya Erica kuwa nina ukimwi ili anihurumie na nimeupata kweli. Nimempleka Sia ili amkoroge mwanaume wake mwishowe dawa zimempata mdogo wangu sasa nahangaika dah! Navuna nilichokipanda”
Kwa kiasi alikuwa anajuta kwa yale aliyoyatenda.

Siku ya leo Erick alienda kwa kina Erica na aliomba kumchukua tena ilia toke nae sema sababu ilikuwa ni mapema basi mama Erica aliruhusu waweze kutoka, na Erica akajiandaa na kuondoka na Erick,
“Tunaenda wapi Erick?”
“Utapaona tu, subiri tu”
Basi gari ikaenda na kuingia kwenye nyumba ya kifahari, akili ya Erica ikacheza na kuhisi pengine ile nyumba ni ya Erick, kwa hakika ilikuwa ni nzuri sana kiasi cha kutamani kuolewa na Erica muda huo, basi Erica aliingiza gari ndani na kushuka kisha kumfungulia mlango Erica ili ashuke na kumkaribisha,
“Najua toka tumeanza mahusiano sijawahi kukuleta kwetu, karibu kwetu leo”
“Jamani Erick kumbe unanileta kwenu! Mbona hukuniambia jamani”
“Ningekwambia ufanye nini sasa”
“Ili nijiandae, mfano kama baba yako yupo”
“Baba hayupo, na hata akiwepo ni vizuri tu ili akufahamu”
Basi akamkaribisha ndani na pale sebleni walimkuta Tumaini ambaye alichukia sana kuwaona, Erica alimsalimia Tumaini ila Tumaini hakuitikia ile salamu wala nini.
Erick alikaa na Erica pale pale sebleni na kumuuliza dada yake,
“Tumaini unaweza kuniambia ni kwanini unamchukia Erica?”
“Sina sababu ila simpendi tu, mimi nampenda Sia”
“Hivi unajua ambacho Sia alitaka kunifanyia kaka yako?”
“Sijui”
Basi Erick alimueleza kwa kifupi tu jinsi walivyompeleka mdogo wake Dora kwenye maombi sababu ya Sia,
“Haiwezekani yani hiyo kitu haipo kabisa, mimi Sia namfahamu vizuri sana na Sia hawezi kwenda kwa mganga”
“Huamini dada yangu, ila ni vyema ukamuuliza mwenyewe”
“Ngoja nimpigie simu”
Akataka kupiga simu ila kaka yake akamzuia na kumwambia,
“Hapana usipige simu ila jibebe uende nyumbani kwao ukaongee nae ana kwa ana ili akuambie machoni pako kama hii habari ni uongo au vipi?”
“Bado siamini, Sia hawezi kwenda kwa mganga, haiwezekani”
Basi aliinuka kweli na kwenda kujitayarisha kisha kuondoka zake tena bila hata ya kuwaaga wala nini maana alikuwa na chuki nao.

Tumainia alienda hadi kwakina Sia, akafika maeneo yale na kukuta Sia na Dora wamesimama nje wakiongea, huku Dora akisema
“Sia unajua ulichomfanyia mdogo wangu sio sawa kabisa, inabidi uende kwenye maombi ukatubu”
“Sio kosa langu ni kosa la mdogo wako na uroho wake”
Mara mdogo wake Dora alitoka kwenye chumba cha Sia na kusogea karibu kisha kumkumbatia Sia na kumwambia dada yake,
“Wewe ondoka zako tu maana mimi kwa Sia ndio nimefika”
Kisha akambusu Sia, haya mambo yote Tumaini aliyaona na kuyasikia kwakweli yalimstaajabisha sana.
 
Back
Top Bottom