SEHEMU YA 407
Mama Erica alishangaa kwanza na kuuliza kwa makini,
“Erica ana mimba?”
“Ndio Erica ana mimba”
Mama huyu alihisi kama kizunguzungu.
Ni Bite alitokea nyuma yake na kumshika mama yake, kisha kumwambia Yule mzee aondoke zake, yani huyu mama aliingia ndani kwa kushikiliwa na Bite ni wazi alipata mawazo sana, hakutegemea kama mwanae kapata maamuzi ya kuzalia watoto wawili nyumbani yani alijihisi vibaya sana, alikaa chini na kuwa kimya kwa muda kidogo kisha alipopuma akaanza kuongea,
“Hivi huyu mtoto ananitakia nini mimi jamani? Anataka kunifanya nini Erica? Kila siku naimba wimbo hapa asibebe mimba kumbe ananicheka kuwa utaona jamani! Kuzaa imekuwa shida eeeh! Bite, sikuwazaa nje ya ndoa nyie, iweje mwanangu awe mtu asiyejielewa, ni mapenzi gani anayoyaendekeza yeye jamani!”
“Mama, punguza jazba”
“Siwezi Bite, yani siwezi kwakweli. Nimemkubali Angel kama mjukuu wangu ila Erica hathamini kujua ni aibu gani mama yake naipata mtaani, kuishi na mtoto kisiri siri hata unatoka nae unajua kabisa utasemwa ila upo tu, na mtaani walishaanza kusema kuwa tumeleta mtoto wa kiarabu na wanacheka balaa, halafu leo aonekane na mimba nyingine jamani! Hivi jamii itaniangaliaje mimi, watu watanitazamaje, itaonekana sijui kulea kabisa jamani, mbona dada zake hampo hivyo, huyu Erica ni mapenzi gani yanayomsumbua yeye hadi anakuwa hivyo?”
“Mama, angalia afya yako, usiongee sana ukapata presha. Tumsubiri huyo Erica arudi na tumuulize pengine ni uongo”
“Sidhani kama ni uongo”
Kisha mama yao akainuka na kwenda chumbani kwa Erica kupekua na kwa bahati nzuri au mbaya, akakiona kile cheti cha hospitali ambacho kinaonyesha kuwa Erica ni mjamzito, yani hapo ndio alihisi presha kupanda zaidi, Bite alipata kazi ya kumtuliza tu mama yao na alipoona kuwa inakuwa ni ngumu aliamua kumpigia simu Mage ili kumueleza na Mage aende nyumbani.
“Unasema Erica mjamzito? Kasema mwenyewe au nani kawapa hizo habari?”
“Ndio mjamzito na mama kachanganyikiwa kabisa maana habari hizo kuzipokea kwake imekuwa ngumu si unajua ni swala la aibu! Yule mzee wake alifika hapa na kusema huo ujinga wa Erica”
“Huyu mtoto anatia aibu kwakweli, mara nyingine bora angekuwa mbuzi tu tungekunywa supu yake kuliko kwa mambo anayoyafanya. Kachanganya ndugu weee kaona haitoshi, katembea na kaka yake, haitoshi, kaenda kutembea na baba na mwana haitoshi, kazaa nyumbani bado haitoshi na sasa kuleta mimba nyingine nyumbani kweli! Si bora hela ya kumsomesha mjomba angetugaia tu tujilie zetu raha kuliko kusomesha kichaa kama Erica jamani! Jitu linakatazwa kufanya mapenzi bado tu yumo, ni hamu gani alizonazo yeye anayeshindwa kuzizuia! Nimechukia sana, nakuja huko hata kama muda umeenda nakuja. Kwanza yuko wapi?”
“Unafikiri yupo nyumbani basi! Asubuhi asubuhi kamvalisha Angel kamdanganya mama kuwa anaenda kliniki, alipoondoka badae kapiga simu kuwa atachelewa kurudi na mpaka mida hii yani saa mbili usiku saivi hajarudi, kashindikana Yule”
“Nakuja huko”
Akakata simu na kuendelea kumbembeleza mama yao pale,
“Mama, Mage kasema anakuja pia kwahiyo mama shusha presha. Huyu Erica safari hii hata ndoa ya mkeka tutamfungisha kwakweli maana si kwa aibu hii anayotutia”
“Nakwambia Bite, sijawahi kumpiga Erica toka akue maana neno nisamehe ndio humtoka upesi kuliko maneno yote ila leo hata aseme nisamehe mara mia nitampiga tu, yani leo nitampiga sana mpaka akili imkae sawa”
“Sasa mama, ukimpiga hivyo na mjamzito si mimba itatoka?”
“Na itoke tu, asiniletee ujinga nyumbani kwangu”
Bite alielewa kuwa mama yake ana hasira sana na anaongea yote yale sababu ya hasira maana alichukizwa vilivyo kwa kilichotokea nyumbani kwake, walikaa wakimngoja kwa hamu huyo Erica arudi.
Nyumbani kwakina Rahim, yani mrs.Peter alichukizwa sana na kitendo cha Salma kumparamia Zainabu ili apigane nae mpaka ilibidi waamulie tu huku Neema akimshika Salma ila Salma aliendelea kuongea maneno ya ajabu,
“Na wewe Neema hebu niache, mwanamke una roho mbaya wewe kama mchawi muone vile. Ndiomana kutwa kucha kujifanya unanifundisha jinsi ya kuishi na mume kumbe unanionea wivu na unataka kumleta mtu wa kunirithi, mwanamke una roho mbaya wewe niachie”
Alipoona Neema hamwachii alimng’ata mkono ili amuachie ilibidi Neema amuachie na kuelekea tena kwa Zainabu ila Zainabu alitulia tu kumuangalia Yule binti akimparamia mwilini, Mrs.Peter alishindwa kuamulia na kuamua kwenda kumuita Rahim.
Zainabu alipoona Salma anazidi kumsumbua alimshika mikono na kumnasa vibao, yani kitendo kile ndio kama kilimtia ukichaa Salma maana alijikuta akianza kutupa vitu vya kwenye nyumba ya mama mkwe wake bila kujali ni vitu vya kwa mama mke.
Basi Rahim na John walifika na siku hiyo alikuwepo Babuu ambaye alikuwa akiongea na Rahim, walipoingia ndani kile kitendo cha Salma kiliwachukiza sana yani walichukia mno, Rahim alienda kumshika Salma na kutaka kumpiga sana ila ndugu zake wakamzuia kuwa asifanye hivyo, basi alimkalisha chini kwa hasira, kwakweli mrs.Peter aliangalia mule ndani kwake na kusikitika sana kisha akasema,
“Salma, sikutegemea kama upo hivi kwakweli sikutegemea kabisa kumbe mwanangu alikuwa hakosei kukupiga, mwanangu hakukosea kukupa talaka yani sikutegemea kama tumemuolea Rahim mwanamke chizi kama wewe. (Kisha akamuangalia Zainabu na kumwambia) Zainabu mama hata tusizunguke mbuyu nahitaji sana uwe mke wa mwanangu na kesho tutakuja kwenu kujitambulisha ili kufanya mambo haraka haraka”
Muda ule ule Salma alianza kulia kama amefiwa vile, kwakweli iliwashangaza sana na mara alinza kusema anacholilia,
“Mmenipotezea muda wangu kusubiria toto lenu malaya, nimemvumilia kwa kipindi chote kwanza linaumiza balaa ila nimevumilia halafu mananifanyia hivi! Sikujua kama familia hii ina roho mbaya kiasi hiki, na wewe Zainabu yatakukuta tu maana hii sio familia ya kuishi nayo ni makatili hawa”
Akainuka na kumchukua mwanae halafu akaondoka, hakuna aliyemfata kwani kile kichaa chake hakuna aliyekitaka kwa muda huo kwani alikuwa ashaharibu vya kutosha pale sebleni.
Mage nae alipokuwa anaenda kwao alijikuta kuwa na hasira sana na mdogo wake na kuamua kumpigia simu kwanza ili kuyabwaga ya moyoni.
Muda huo, Erick na Erica walikuwa njiani kurudi nyumbani ambapo Angel alikuwa amelala, kwahiyo Erica alipoona kuwa dada yake anapiga simu sana aliamua kupokea ili kujua tatizo ni nini, alipokea na kumsalimia dada yake ila dada yake hakupokea ile salamu na kuanza tu kumshushia maneno,
“Wewe mtoto usiye na akili hata moja yani kwako moja haikai mbili haisogei, hivi unafikiriaga kwa kutumia nini? Huwa unatumia ubongo wewe au makalio yako ndio yanakutuma kufanya ujinga”
“Ujinga gani tena dada?”
“Hivi wewe ni wa kumuaibisha mama kiasi hiki, uzalie Angel nyumbani na bado unabeba mimba nyingine nyumbani”
“Dada, mbona mimi sina mimba”
“Huna mimba wapi mjaa laana wewe, wakati zee lako limekuja kusema kuwa una mimba, na mpaka muda huu hujarudi nyumbani ushaanza kumuhangaisha Angel kwa wanaume zako huko, na mimi naenda nyumbani nikukute wewe, urudi muda huu huu nyumbani mjinga wewe”
Kisha dadake akakta simu na hapo Erica akajua kuwa siri ya mimba yake imefichuka kwao, kwa jinsi alivyokuwa akionge kwa mshangao ilifanya Erick aweke gari pembeni ili amsikilize kuwa tatizo ni nini, alimuona Erica akiinama chini huku akiwa na mawazo tele, alimuuliza
“Mpenzi, nini tatizo?”
“Nyumbani wamejua kama nina mimba yani sijui itakuwaje”
“Kwani kuwa na mimba ni tatizo?”
“Si tatizo kwa mtu aliyeolewa ila kwa mimi ambaye sijaolewa ni tatizo kubwa sana, unajua mimba ni kielelezo tosha cha uzinzi. Yani ukiwa na mimba huwezi kukataa kuwa hujazini, na mama kila siku ananikataza habari za kuzini, aliniambia mpaka niolewe maana nishamtia aibu kwa Angel. Nilijiapia kufanya hivyo na ndiomana sikutaka hata kutumia uzazi wa mpango sababu nilijua nitaweza kujizuia hadi ndoa”
“Sasa swala la uzazi wa mpango limekuja vipi hapo? Inamaana Erica hukupenda kuzaa na mimi?”
“Sio hivyo Erick, yani sijui kama unanielewa mpenzi. Swala ni hivi, nyumbani huko kimewaka moto maana wamejua nina mimba yani leo nahisi mama atanipiga kipigo kisichoelezeka, yani nimechanganyikiwa”
“Mmmh akikupiga si mimba yangu itatoka? Erica, sitaki itokee ya kipindi kile kutoa mimba yangu”
“Kwani kipindi kile nilipenda Erick, ila dada zangu ndio walinishikilia bango nitoe ile mimba ili mama asijue yani hospitali na kila kitu walifanya wao. Sasa leo nyumbani, uwiiii sijui nifanyeje”
Erick akafikiria kidogo na kusema,
“Erica, hata mimi nahitaji kuwa na damu yangu, nahitaji kupata mtoto kutoka kwako na hata hivyo sihitaji upate matatizo sababu ya starehe zangu. Kuna jambo nawaza hapa, naomba unikubalie”
“Jambo gani hilo?”
“Naomba leo usirudi kwenu, tukatafute hoteli ukakae huko kwanza halafu mimi nifanye harakati za kuwasiliana na kwenu kisha tufunge ndoa. Si mama anahitaji uzalie ndani ya ndoa? Basi itawezekana tukifanya hivyo mpenzi au unaonaje? Ila usikatae tafadhali”
“Erick umeongea jambo jema ila sasa nisiporudi nyumbani si ndio balaa zaidi?”
“Erica, waswahili husema heri nusu shari kuliko shari kamili, ushasema kwenu wana jazba leo hivi wakikuona si ndio balaa zaidi, kwanza ni Mungu tu kafanya huyu dada yako akupigie simu huku akiwa na hasira hivyo zilizokuchanganya na wewe maana wangeweza wasubiri urudi tu na upate kipigo, ni heri kusubiri hasira zao zipoe kuliko kuchukua maamuzi kwasasa, kubali Erica tafadhali, nami sitaondoka tutakuwa wote hapo hotelini na kesho nitaenda kuwatafutia nguo wewe na Angel, huku tukiendelea kujadili cha kufanya, kwasasa kubali swala hili”
Erica alifikiria kwa kina na kuwaza akirudi kwao sokomoko atakalokutana nalo, akaona ni bora akubaliane na wazo la Erick tu maana hakuwa na jinsi kwa wakati huo.
Basi Erick aligeuza gari yake na kuanza kwenda kwenye hoteli ambayo alihisi itawafaa kwa siku kadhaa.