SEHEMU YA 442
Roma mara baada ya kubeba bunduki aliangalia kama ilikuwa na risasi na baada ya kuona zipo za kutosha alimgeukia Mika.
“Dogo unajua kutumia bunduki?”Aliuliza Roma na kumfanya Mika kutingisha kichwa kwamba alikuwa akijua kutumia na Roma alitegemea hilo kwani alikuwa akielewa kama Samweli Nguluma ambaye ni baba yake Benadetha alikuwa bosi wa kundi la kiharifu la ZoaZoa basi Mika asingekosa mafunzo muhimu ya namna hio.
“Shika lipiza kisasi kwa kumuua Shedrack”Aliongea Roma baada ya kumrushia ile siraha huku akiwa na uso uliojaa usiriasi.
“Lakini Bro kama nitamuua dawa nitapataje?”Aliuliza huku akionyesha wasiwasi.
“Wewe niamini mimi dogo”Aliongea Roma.
Baada ya Kengeu kusikiliza yale maongezi jasho lilianza kumtoka ,kwa upande wa Aishapova licha ya kwamba hakuwa akijua lugha ya kiswahili lakini kwa picha iliokuwa ikiendelea alijua ni kipi kinaenda kutokea , lakini aliamini Roma hakuwa mjinga mpaka kumuua kwani ni kweli kabisa Mika alikuwa amewekewa sumu ambayo inakwenda kushambulia vinasaba vya damu.
“Mika fikiria vizuri ukiniua mimi huwezi kupona tena , nimeyashikilia maisha yako”Aliongea Kengeu kwa namna ya kujitetea huku hata sauti yake iliolegea ikianza kutoa mikwaruzo.
“Mika usimsikilize huyo nina kuhakikishia afya yako itakuwa sawa , lipiza kisasi kwa kumpiga risasi tuondoke”Aliongea Roma na kauli yake iliogopesha baadhi ya watu.
Mika ijapokuwa baba yake amemfundisha kutumia siraha , lakini kwenye maisha yake hakuwahi kuua kabisa na siku hio kwake ni kama inakwenda kuwa mara ya kwanza , mikono yake ilimtetemeka mno.
“Dogo acha kupoteza muda , muue tuondoke”Aliongea Roma huku upande wa Aishapova akitamani kujinasua , lakini kutokana na uwezo wa kimaajabu aliokuwa nao Roma , aliona hata kama atakimbia basi angekamatika tu na huenda angekufa hata kabla hajatoweka hivyo aliishia kusubiri kuona hatima yake..
“Paaa!!.. Paa.!!.”
Risasi mbili zilitoka kwenye siraha alioshikilia Mika na kumpiga Shedrack Kengeu kifuani na kudondoka palepale, hakuweza hata kujitetea kabisa, lilikuwa ni tukio ambalo lilifanya watu wachache waliobakia hapo ndani kukimbia.
Mika alidondoka chini huku akianza kuhema kwa tabu , ilikuwa ni kama mtu ambaye amekimbia maili nyingi sana.
Kuua mtu kwa mara ya kwanza ni jambo kubwa sana kwenye maishaya binadamu , lakini ukifanikisha kuua huwezi kuwa mtu wa kawaida tena , hio ndio laana inayotokana na kumuua binadamu mwenzio.
“Vipi dogo mbona unatapika?”Roma alijikuta akitamani kucheka kwani mara baada ya Mika kumaliza kumpiga Shedrack Kengeu kwa risasi alianza kutapika, lakini hata hivyo alishindwa kujibu zaidi ya kuanza kutoa kilio palepale..
“Nadhani unaona kwamba kuua sio jambo rahisi kwenye maisha ya binadamu Dogo, umesema baba yako amempiga mama yako risasi si ndio?”Aliuliza Roma na Mika alitingisha kichwa kuitikia.
“Kama wewe umeona ugumu wa kumuua mtu ambaye huna ukaribu nae sana , je unahisi baba yako amejisikiaje kumuua mama yako ambaye ameishi nae kwa muda mrefu , mwanamke ambaye amempenda?”
“Viba.. vibaya..”Aliongea huku akitetemeka akiangalia maiti ya Shedrack Kengeu iliokuwa ikiloewa kwenye dimbwi la damu.
“Unachojisikia sasa hivi mara baada ya kumuua adui yako ambaye amehatarisha maisha yako ni zaidi ya mara kumi anachojisikia baba yako mara baada ya kumuua mke wake , naamini kuna sababu ambayo imemfanya kumuua , tofauti na kukimbilia huku kwenye hoteli iliojaa mambo ya ajabu ungetafuta sababu kwanini mama yako mzazi kapigwa risasi, kuja eneo hili ni kuharibu maisha yako ya baadae”Aliongea Roma kwa kufoka.
“Bro nimekuelewa sitorudia tena kujichanganya na maswala kama haya…”Aliongea kwa namna ya kujitetea na Roma alimgonga gonga kwenye mgongo kumtuliza.
Roma mara baada ya kuangalia alipokuwa amesimama Aishapova aligundua ameshatoweka hata hivyo hakutaka kujihangaisha nae.
“Bro nawezaje kupona sasa , yule mwanamke kakimbia?”
“Kuna mtu naamini anaweza kukusaidia kukutibu , kuhusu Aishapova nikimuua sitopata majibu ninayotaka , kama ameweza kutengeneza siraha za kibailojia na kuingia nazo Tanzania naamini kuna jambo kubwa linaendelea”Aliongea Roma na kumfanya Mika kushangaa kidogo lakini Roma hakutaka kuendelea kubaki nani ya hilo eneo , alimpa ishara ya kuingia kwenye gari na kuondoka eneo hilo..
Ukweli Roma alitaka kwenda kuthibitisha kama kwenye mwili wa Mika kuna hiko kinachoitwa ‘Genetic weapon’ na mtu pekee ambaye angeweza kuthibitisha hilo ni Profesa Clark.
Roma alipokuwa anaingia eneo la Mapinga alimpigia simu Profesa Clark ili kujua yupo wapi na alijibiwa kwamba yupo sehemu inayoitwa Makongo juu , sehemu ambayo ndio atakapo ishi kwa muda wote atakaokuwa hapa Tanzania.
Roma ilibidi amueleze Profesa Clark juu ya mtu aliekuwa nae ambaye alikuwa akihitaji msaada kutoka kwake ndani ya masaa 72 na baada ya Profesa Clark kumsikiliza kwa umakini alimwambia aje moja kwa moja mpaka nyumbani.
Ndani ya dakika chache tu aliweza kufika eneo la Makongo Juu na haikumpa shida kuipata nyumba ya profesa kwani nyumba zote za jiji la Dar zilikuwa na mfumo wa anuani ambao umeunganishwa moja kwa moja kwenye GPS hivyo aliendesa mpaka nje ya jumba lenye geti na ukuta mrefu uliozungushiwa nyaya za umeme na kupiga honi na geti lilijifungua lenyewe.
Aliingiza gari mpaka ndani na kwenda kuliegesha mbele kabisa na mlango wa kuingia na kisha akamwamuru Mika kushuka..
Lilikuwa jumba kubwa mno la kifahari la ghofora mbili , lenye bustani nzuri zilizozunguka pande zote na kuifanya nyumba kuwa katikati.
Mika alijikuta akipagawa mara baada ya mwanamke mrembo wa kizungu kutoka ndani ya nyumba hio
“Roma hakika unajua kunifanya niwe bize , nipo hapa kwa siku mbili tu lakini tayari ushanitafutia mtu wa kumfanyia majaribio”Aliongea kwa Kingereza huku akimwangalia Mika ambaye alikuwa akimwangalia kwa namna ya kushangazwa na uzuri wake
“Nadhani siingilii pia ratiba zako zingine na kampuni isije nikakosana na mke wangu”
“Hakuna cha kuniweka bize , ni kazi nyepesi sana ambayo mwanafunzi wangu yoyote yule angeweza kuifanya , lakini kwasababu sikutaka Catherine na Rothchild kunifanya bidhaa kwa faida yao ndio maana nipo hapa Tanzania , muda huu huenda ningekuwa nimejichimbia ndani ya maabara nikifanya majaribio, lakini hata hivyo najisikia vizuri ninakuona mara kwa mara”
“Huko kuniona mara kwa mara ndio kunanisababishia matatizo na familia yangu”
“Ooh! tena nimekumbuka mkeo mchana alionekana alikuwa na hasira sana kiasi ambacho kiliniogopesha na sio mimi tu kila mmoja alimuogopa hata kumsogelea na kumuongelesha , sijawahi kukutana na mwanamke mrembo lakini kauzu kam mke wako”Aliongea huku akicheka.
“Haha..nitajitahidi kwenda kumuweka sawa , Unaweza kuchukua damu yake hapa hapa au ni mpaka maabara?”Aliuliza Roma.
“Hapa hapa panafaa zaidi, Kuna kitu nataka pia nikuonyeshe ndio maana nilikuambia umlete moja kwa moja , nifuateni”
Walitembea hadi kwenye mlango uliokuwa kushoto baada ya kupita sebuleni na kuingia kwenye chumba kikubwa ambacho kilionekana kama ofisi ya kujisomea kwani kilikuwa na mpangilio wa vitabu vingi pamoja na meza na tarakishi, kwa haraka haraka Roma aliamini huenda Clark alikuwa akisoma kwani kwenye meza kulikuwa na kitabu ambaco kimefunguliwa, lakini pia alijiambia huenda nyumba hio inakaliwa na zaidi ya mtu mmoja.
Profesa Clark alichukua kadi kama zile za benki kwenye meza , lakini hii ilikuwa na utofauti kidogo ni kadi ambayo ilikuwa na michoro myeupe kama ya radi rangi ya silver upande mmoja , baada ya kuichukua alisogea mpaka mwanzo wa kabati upande wa kulia mwa chumba na kusogeza vitabu na kilionekana kifaa kama simu iliobandikwa ukutani na alichukua ile kadi na kuibandika juu yake kwa sekunde tano tu , kulisikika mlio wa lock za mlango kuachiana na hapo upande mmoja wa kushoto wa kabati ulionyesha kufunguka na kuacha uwazi na kumfanya Roma kuguna.
“Hii nyumba imekaa kijasusi jasusi inaonekana sio ya kawaida ,inaonekana ina mambo mengi ya siri”Aliongea Roma.
“Sio wewe tu , hata mimi nilishangazwa pia na hii nyumba, lakini inaleta maana kwani ni nyumba iliokuwa chini ya umiliki wa siri wa Profesa Shelukindo”
“Unamaanisha nini?”
“Dear Roma naona upo kwenye mshangao mkubwa, katika maisha yangu ya kimasomo nadhani mimi ndio nilikuwa mwanafunzi wa pekee kutoka kwa Profesa Shelukindo na alinipenda haswa kutokana na kwamba tulikuwa tukifanana kwenye mambo mengi sana likija swala la taaluma ya uvumbuzina hilo linanifanya kumpa heshima yake”
“Kuna siku moja wakati nawasiliana nae alianimbia kama nitabahatika siku moja kutamani kuishi Tanzania na yeye hayupo hai basi kuna mtu napaswa nimtafute, sikuwahi kumzingatia sana kwani licha ya kuwa mwalimu wangu lakini pia alikua mtani wangu , hivyo hata baada ya kuniambia hivyo sikuweza kuchukulia sana jambo hilo kwa usiriasi mpaka leo ulivyo ondoka kule chuoni”Aliongea na kisha akaendelea
“Roma unajua kwanini mara baada ya kusikia kifo cha Profesa Shelukindo nilifanya safasi siku hio hio?”
“Kwasababu ni mwalimu wako na mlikuwa mkishirikiana kwenye mambo mengi”Alijibu Roma.
“Ukiachana na kushirikiana kwetu , Profesa Shelukindo aliniahidi nitakuja kumrithi kazi zake zote na kuendeleza kile ambacho hakukikamilisha , unaweza kusema kwamba alitaka kuniachia mikoba yote ya tafiti zake na kuendeleza , lakini nilihuzunika sana mara baada ya kugundua alikufa bila hata ya kutimiza ahadi yake , nilikuwa ni mwenye shauku ya kujua ni hatua gani aliokuwa amefikia katika maswala ya sayansi , lakini nilijikuta nikirudi Uingereza nikiwa mwenye huzuni”Aliongea Profesa wakiwa wamesimama kwenye chumba hicho pasipo ya kuingia, Roma alishangazwa na maneno hayo.
“Clark mbona unaongea ukiwa umebadilika ghafla na furaha kutoweka machoni mwako?”
“Kwasababu ninayofuraha na huzuni kwa wakati mmoja, lakini huzuni imenizidia kwa wakati huu”
“Kwanini?”
“Kwasababu niliishi kwa huzuni kwa kuamini Profesa Shelukindo hakutimiza ahadi yake , lakini ukweli ni kwamba ahadi yake aliitimiza , huzuni yangu ni juu ya muda wote ambao niliupoteza kwa kumlaumu kwa kutoikamilisha ahadi yake kwangu”Aliongea na pale pale hakumpa Roma nafasi ya kuuliza swali , alisukuma mlango na akatangulia kuingia kisha akafuatia Roma halafu Mika.
Roma aligundua mlango huo ulikuwa ukiwaruhusu kwenda chini kwenye vyumba vya ardhini.
Baada ya kufika chini Clark alitumia kadi ileile kufungua mlango mwingine na ulipofunguka ndipo Roma alipo onyesha mshangao wake.
********
MASAA MACHACHE NYUMA
Ni mara baada ya wageni rasmi kumaliza kupata chakula cha mchana , ikiwa ni muda wa saa tisa za adhuhuri, Profesa Clark alionekana kupiga picha na wanafunzi mbalimbali ambao ni wahitimu ndani ya chuo hicho.
Wanafunzi waliokuwa wakihitaji kupiga picha nae walikuwa wengi hivyo ilichukua zaidi ya lisaa limoja mpaka pale makamu mkuu wa chuo alipomfuata na kuondoka nae kitendo ambacho pia kilimpa ahueni Profesa Clark kwani alikuwa ashaanza kuchoka.
Muda huo Edna alikuwa ashaondoka mara baada ya kufuatwa na Innocent dereva wake wa kampuni hivyo Profesa na yeye alitakiwa pia kurejea hotelini kwake kusubiria taratibu zingine za kuonyeshwa mahali ambapo angetakiwa kuishi kwa muda wote atakaokaa hapo Tanzania.
“Profesa samahani najua umechoka sana , lakini kuna daktari mmoja ambaye anahitaji kuonana na wewe japo kwa dakika chache”Aliongea Bi Asha Abdulah ambaye ndio makamu mkuu wa chuo cha UDSM akiwa na yeye pia profesa wa chuo hicho.
“Profesa kwasababu wewe ndio umeomba nadhani atakuwa ni mtu muhimu ninaepaswa kuonana nae”Aliongea Profesa Clark huku akitabasamu.
“Usije ukanifikirai vibaya Profesa lakini ukweli ni kijana wangu , hivyo katumia ukaribu kupata nafasi ya kuonana na wewe , alionyesha hali ya kuwa na jambo muhimu hivyo niliona nikuelezee ufanye maamuzi , anafahamika kwa jina la Dr Issai Singano”Aliongea.
“Dr Issai Singano!!!!”Alimaka
“Hili jina sio geni kwangu nililisikia wapi?”Alijikuta akijiwazia kwenye kichwa chake
“Ndio Profesa kwa muonekano wako naamini ushawahi kusikia jina lake , hata yeye alianiambia kama nitakutajia jina lake utamfahamu”Aliongea na kumfanya Profesa Clark kusimama na kufikiria kidogo , jina la Issai singano halikuwa geni kwake na baada ya kufikiria kwa dakika kadhaa aliweza sasa kupata mwanga na aijikuta akimwangalia Makamu Mkuu wa chuo kwa namna ya kumshangaza.
“Oh! My God , nilishasahau kabisa kuhusu hili jina , nimekuwa mjinga sana nimewezaje kusahau”Aliwaza tena huku akionekana anajilaumu.
“Makamu asante sana , nadhani nitaonana nae kwenye gari yangu haina haja ya kwenda mpaka kwenye ofisi yako”Aliongea Profesa Clark huku mwonekano wake ukibadilika na kuwa na uchangamfu lakini na shauku kwa wakati mmoja.
Bi Asha Abdullah mwenyewe alishangazwa na mabadiliko ya Profesa Clark ,wakati alipoombwa msaada na Dr Singano alisita sita , lakini kwa kubembelezwa sana alikubali na hio yote ni kutokana na ukaribu wa familia ya Dr Singano upande wa wakwe zake na familia yake.
Zilipita kama nusu saa zingine ilibidi Profesa kuagana na baadhi ya viongozi na watu mashuhuri ndani ya chuo hicho ndipo alipoweza kuelekea kwenye gari yake iliomleta na kabla hata hajaingia ndipo aliposogelewa na mwanaume mwenye mwonekano wa kijana mweusi mrefu wa saizi ya kati alievaa suti ya rangi nyeusi.
“Dr Issai Singano Right?”Aliongea Profesa mara tu baada ya kusogelewa na huyo mwanaume.
“Yes Professor , Nice to meet you”Aliongea na wakapeana mkono huku Clark akionyesha hali ya furaha mara baada ya kuonana na Dr Singano.
“Dr Singano nadhani tunayo mengi ya kuzungumza , je umefika hapa na gari?”Aliuliza Profesa na Dr alimuonyeshea upande wa pili gari yake aina ya Range rover V8 .
Kwasababu gari iliomleta Profesa Clark mpaka hapo ilikuwa ni ya hoteli aliofikia basi ilibidi ampe dereva maelekezo ya kutangulia na yeye ataongozana na Dr Singano na kuingia kwenye garri yake.
“Nikiri niliposikia jina lako nilipata mshituko , Mtu alienitajia jina lako miezi michache iliopita ni Profesa Shelukindo , Mwalimu wa heshima kwangu, kwa maelezo yake aliniambia nikutafute kama nitafika Tanzania lakini nikasau kabisa kutokana na siku tuliokuwa tukiongea tulikuwa katikati ya kutaniana”Aliongea Profesa Clark.
“Ndio hata Profesa pia alishawahi kunipatia maelekezo maalumu , ambayo aliniitaji niyafikishe kwako”
“Kweli!! ,Profesa Shelukindo alikuwa nani kwako?”
“Sijui niwekeje ila naweza kusema ni ndugu yangu wa mbali kwa upande wa bibi yangu mzaa baba, niliweza kukutana nae kwa mara ya kwanza kwenye msiba wa baba yangu mzazi na kuanzia hapo ndio ukaribu kati ya mimi na Profesa ulianza”Aliongea na kisha alivuta mkoba uliokuwa siti ya nyuma na kuufungua na kuibuka na Notebook kubwa ya rangi nyeusi na kisha akamkabishi Profesa Clark.
‘Hio ni Diarybook yake ambaye aliniambia nikupatie, lakini pia alinipa maelekezo kama ukifika nchini nikupeleke kwenye nyumba yake ambayo alikuwa akipendelea kupumzika”Aliongea na kumfanya Clark kushangaa lakini alifungua ile Diary taratibu taratibu na ilionekana ilikuwa na maandishi mengi ambayo yalionekana yapo kisayansi zaidi , alisoma baadhi na alionekana kuyaelewa lakini hakuona kitu cha maana zaidi , lakini alipofika katikati ndipo alipoona kadi katikati ya Notebook hio na aliinua juu na kutoa macho , alionekana alikuwa akiijua.
“Nipeleke kwenye nyumba yake ya mapumziko”Aliongea Profesa na Dr Singano hakuuliza mara mbili na aliwasha gari na wakaondoka eneo hilo kwa haraka na ndani ya madakika kadhaa ndipo walipokua kufika Makongo Juu.
********
Ilikuwa ni maabara ndogo ya kisasa , ijapokuwa haikuwa na vitu vingi lakini ilikuwa kwenye mpangilio mzuri sana na ilikuwa na vifaa muhimu vyote.
Kwa maelezo ya Profesa Clark ni kwamba maabara hio ilikuwa ikitumiwa na Profesa Shelukindo mara chache sana, lakini kubwa zaidi ni kwamba ilikuwa imebeba asilimia miamoja ya taarifa zote zilizokuwa zikihusiana na tafiti zote ambazo Profesa Shelukindo amefanya kwenye maisha yake mpaka alipofikia.
Kwa maana rahisi ni kwamba kila kilichokuwa humo ndani alielengwa kukimiliki ni Profesa Clark.
Roma alishangazwa na uwezo mkubwa wa Profesa mpaka kutunza siri zake za tafiti na kuweka mpango ambao ulikuwa madhubuti kiasi kwamba kumfikia mlengwa , lakini swali lingine liliibuka.
“Kama umesema alikusudia wewe kupata taarifa zake kupitia maabara hii , je ni kipi ambacho Yan Buwen alipata kutoka kwake?”
“Hilo siwezi kujua , lakini nilichokipata humu naweza kusema kwamba Profesa alikiandaa kwa ajili yangu na ni kazi zake zote ambazo amefanya miaka kwa miaka pale aliposhia lakini pia matarajio yake ya mbelemi”Ilishangaza sana , lakini hata hivyo Roma hakutaka kuuliza sana.
Mika ilibidi achukuliwe damu yake hapo hapo kwenye hio maabara ili Profesa kuifanyia majaribio na baada ya kazi hio kumalizika wote walitoka nje huku Profesa akiahidi kufanyia kazi ndani ya muda mfupi.
“Lakini Roma vipi kama nikishindwa kupata Genetic Codes na kuweza kudhalisha Antidote yake ndani ya masaa sabini na mbili maana maswala yanayohusiana na DNA yanahitaji muda”Aliongea Profesa.
“Clark nakuamini utapata majibu ndani ya muda mfupi, hivyo usiwe na wasiwasi na wewe fanya kazi yako”Aliongea Roma na Profesa Clark alivuta pumzi na kuzishusha.
“Okey nitajirahidi kadri ya uwezo wangu ili kabla masaa yote hayajaisha niwe nimepata majibu”
Roma ilibidi awasiliane na Benadetha na kumuambia yupo na kaka yake aje kumchukua.
Nyumbani kwa Benadetha ni Tabata hivyo Roma ilibidi wakubaliane na Benadetha wakutane Mwenge.
“Vipi yule rafiki yako?”Alivunja Roma ukimya akimuulizia Rufi.
“Bro unamaanisha yule mrembo Rufi?”
“Ndio”
“Yule nilimsaidia mpaka kununua Apartment kule kwa Warioba , lakini hakutaka hata kunikaribisha mara baada ya kuhamia , hivyo nilimuacha jana ileile ndipo nilipoanza safari ya kwenda Bagamoyo”Aliongea Mika na kumfanya Roma kuitikia kwa kichwa.
Baada ya dakika chache tu Benadetha alievalia suruali na blazier aliweza kufika eneo la Mwenge akiendesha gari aina ya Harrier.
“Roma naomba unisamehe kwa kusumbua , sikuwa na jinsi baada ya baba kunilazimisha..”Aliongea Benadetha kwa upole.
“Usijali Benadetha wewe ni mfanyakazi wa kampuni ya mke wangu , hivyo kukusaidia ni wajibu wangu pia , ukiwa na mawazo huwezi kumsaidia Edna kwenye kazi zake vizuri”Aliongea Roma na Benadetha aliitikia kwa kichwa.
Roma baada ya kumkabidhi Mika kwa dada yake huku akimpa maelekezo mengine kuhusu kilichomkuta , basi aliagana nao na kuanza kuitafuta safari ya kurudi nyumbani kutatua mgogoro wake na mke wake, lakini ndio muda ambao simu yake ilianza kuita mfululizo na alipoangalia jina aligundua ni Mage.
“Roma una tabia mbaya sana wewe mwanaume?”
“Babe kwanini unaongea hivyo?”
“Acha kujifanyisha hujui, yaani wewe mwanaume umeshindikana”
Roma aliijikuta akitabasamu kwa uchungu na kugundua kosa alilolifanya , tokea alivyomuacha Mage kule hotelini hakuwa amemtafuta kabisa kujitolea maelezo kwanini Video yake ya ngono ilikuwa kwenye kile chumba cha mdukuzi.
Ilikuwa ni saa moja na nusu kwenda saa mbili za usiku na Roma ilibidi tu amuambie Mage waweze kuonana usiku huo ili aweze kumwelezea kilichotokea, alijua alitakiwa kuwahi nyumbani kumpoza Edna , lakini pia alikuwa na deni kwa Mage.
SEHEMU YA 443.
Mage ni kama alipata nafasi ya kumshikilia Roma usiku mzima na hata pale kulipokucha Mage alimwambia Roma amsindikize Mlimani City kununua baadhi ya nguo za kufanyia mazoezi na Roma kwasababu hakuwa ametumia mua mwingi na mrembo huyo ilibidi tu akubaliane nae.
Walitoka pamoja hotelini na kwenda mpaka Mlimani City ambapo Mage alinunua mahitaji yote alioyahitaji akisaidiwa kuchagua na Roma na mpaka wanakuja kutoka eneo hilo ilikuwa ni saa nne za asubuhi.
Roma hakusahau pia kununua zawadi kwa ajili ya mke wake , aliamini ingekuwa rahisi kwake kuomba msamaha akiwa na zawadi.
Baada ya kumpeleka Mage hadi nje ya nyumba yao hakutaka kuingia ndani zaidi ya kuondoka huku mpango wake ni kunyoosha moja kwa moja mpaka kwenye kampuni ya mke wake , kwani aliamini hata kama angeenda muda huo nyumbani asingemkuta.
Roma mara baada ya kufika aliweza kukutana na Recho ambaye alikuwa amekumbatia mafaili na alionekana alikuwa akitoka kwenye ofisi ya bosi wake.
“Roma upo hapa kwa ajili ya Bosi?”Aliuliza Recho mara baada ya kumuona Roma.
“Ndio”
“Mhmh nikajua umekuja kwa ajili yangu”
“Hehe.. hio ni kazi ya boyfriend wako sio ya kwangu”Aliongea Roma.
“Mhmh… ila nakushauri ni bora ukaja muda mwingine maana bosi anaonekana kuwa ni mwenye hasira mno mpaka nimeshindwa kua na amani, nilijikuta nikiwa natetemeka kama nipo chumba cha barafu”Aliongea na kumfanya Roma kufikiria kidogo
“Kama tunaishi pamoja sina jinsi zaidi ya kutafuta namna ya kumpoza, jana ni kweli nilikosea lakini ilinipasa kutoa msaada pale ulipokuwa ukihitajika, lakini kutokurudi nyumbani daa..! nitajua bwana”Aliwaza Roma kwenye kichwa chake.
Roma mwenyewe alijishangaa mno kwenye maisha yake hakuwahi kumuhofia mwanamke , kwa mfano usiku wa jana aliweza kuyamaliza kirahisi na Mage , lakini likija swala la Edna alionekana kuwa na hofu mno na kuona hakika maisha yake yamepiga hatua kubwa.
Roma alisogelea mlango wa ofisi ya CEO huku akisikilizia sauti hafifu ya AC iliokuwa ikipuliza na kisha akavuta pumzi na kugonga mlango.
“Come in”Sauti hafifu iliitikia kutoka ndani na Roma alisukuma mlango na kuingia ndani huku akifikiria namna ya kumlegeza Edna.
“Ooh jamaniii.. haijalishi ni mara ngapi namuona CEO akiwa ameketi kwenye kiti chake cha ubosi , lakini niseme kwamba uzuri wake ni wenye kuyawasha macho yangu muda wote, ni hasara kweli kweli uzuri kama huo kuuficha ndani ya hii ofisi , dunia inahitaji uzuri wako na hata kuwa balozi wa bidhaa nyingi za urembo huenda zingeuza sana”
Wanawake siku zote wanapenda kusifiwa kuhusu mwonekano wao hata kama mazingira hayaruhusu kufanya hivyo na ndio mbinu pekee ambayo Roma aliona inaweza kumlegeza mke wake kidogo, Roma alijiambia pasipo ya kuwa Chawa asingetoboa , lakini licha ya hivyo aliona kabisa mbinu yake imegoma kwani mwonekano wa Edna ulikuwa wa aina yake.
Edna hakuinua kabisa macho yake kumwangalia zaidi ya kuendelea kupekua makaratasi yaliokuwa kwenye meza yake , ni kama alikuwa peke yake ndani ya ofisi.
“Tafadhari zungumza shida yako iliokuleta”Aliongea Edna kwa sauti kavu na kumfanya Roma kukuna kichwa.
“Aah, Edna najua unafanya mazoezi kila siku asubuhi hivyo leo nimepitia dukani kukunulia zawadi”
“Director Roma if you don’t have pressing matters in hand please leave my office”Aliongea Edna kwa Kingereza na mpaka hapo Roma aliona kazi anayo , mpaka Edna akikubadiishia lugha inamaanisha kwamba kuupata msamaha isingekuwa jambo jepesi.
“Okey ngoja tusizungumzie hili sasa hivi , Edna najua umekasirishwa na kitendo changu cha jana kukuacha peke yako lakini kulikuwa na dharula kweli , nilihitajika kuyaokoa maisha ya mtu”
“Ni vizuri kusikia hivyo Mr Superhero, najua kabisa ujasiri wako kati ya wanaume wote ambao nimekutana nao na imenishangaza sana kuweza kuwa na mwanaume wa aina yako, lakini hilo sio tatizo kwangu kwani sihitaji sana ujielezee , ni bora ukajizuia ili kuyatoa kwa mtu ambaye ameathirika”
“Halafu naamini wewe ni mwanaume ambaye huna haja ya kujielezea kwa mwanamke licha ya kwamba uliniacha mwenyewe bila ya kujali watu walichukuliaje lakini pia ukalala nje kwa raha zako , usijielezee maana nahisi utakuwa ni mwenye kutia huruma”
“Edna sio kama unavyofikiria , yaani usiku wa jana ulikuwa ni wa kashikashhi sana , Benadetha mdogo wake alipatwa na matatizo makubwa mno na ilinipasa kumsaidia, ni jambo ambalo lilinifanya nichukue muda mwingi kushughulikia, hivyo nikakosa muda wa kurudi nyumbani, lakini nashukuru nimeweza kufanikisha na kumrudisha akiwa salama salimini”
“Okey endelea nakusikiliza..”Aliongea Edna huku akimwangalia Roma kwa macho yasio na furaha.
“Ndio nishamaliza , ilikuwa ni kama hivyo”
“Okey vizuri sana , ni jambo zuri kwa binadamu kusaidian , hivyo Mr Roma Ramoni naomba utoke kwenye ofisi yangu”Aliongea na Roma kwa muonekano wa Edna aliona akijitetea zaidi ni kuharibu.
“Edna vipi hii zawadi ambavyo nimekuchukulia”
“Sihitaji”Aliongea na Roma aliishia kuachama na kutoka nje kinyonge.
Edna alikuwa na hasira kweli kwanza kabisa yeye ndio aliependekeza kwenda na Roma kwenye sherehe ili kwenda kujigamba kwa kuonyesha ameolewa , lakini kabla hata sherehe haijaisha akaachwa mwenyewe tena bila hata ya usafiri kadhia iliomfanya kupiga simu kufuatwa , lakini sio kuachwa kwa sababu nyingine bali ni kwasababu ya mwanamke kapiga simu , lakini haya mwanamke huyo kamshikilia mume wake mpaka asubuhi na mume wake pasipo kujali hata kutoa taarifa..
Wivu na hasira vilimfanya kutamani kupasua tarakishi yake aliokuwa akiitumia muda huo , uwepo wa michepuko ulikuwa ukimtesa , lakini licha ya hivyo mume wake haonyeshi kabisa hatia, kwanini asiwe na hasira.
Roma baada ya kutoka ofisi ya mke wake na mfuko wa zawadi alionunua ,hamu ya kwenda kazini kwake ilimwishia hivyo moja kwa moja alitoa maagizo kwa wanajeshi wa The Eagles kuhakikisha usalama wa Profesa Clark.
Roma mara baada ya kurudi aliweza kumkuta mama yake akitengeza bustani kwa kupanda mbegu za maua na kumwangalia , Blandina mara baada ya kumuona Roma ndio kwanza anaingia alijikuta akishindwa kuelewa moyo wake na kujiambia ni kheri kumpa Roma vidonge vyake.
Kitendo cha kutokurudi kwake jana usiku kilimfanya yeye na Bi Wema kuwa katika hali zisizoelezeka .
“Roma nini kilitokea jana na ukashindwa kurudi , kiasi cha kumfanya Edna kuwa na sura ambayo tulikuwa tukianza kuisahau, Usiniambie umetafuta mwanamke mwingine wewe mtoto mtukutu? Ndio sababu hukurudi”Aliongea Blandina.
“Mama sio hivyo , kwanini kila mtu anaona kila mwanamke ninaekutana nae ni mwanamke wangu”
“Sasa uniambie kwanini Edna anaokana kukasirika mno?” Aliongea na ilibidi Roma aeleze kilichotokea.
“Sasa kwanini ukaamua kulala huko huko na usirudi numbani hata kama ulichelewa, Roma unavyofanya sio vizuri mkeo anajaribu kujitahidi kuweka ukaribu lakini wewe kutwa kumchokoza , utaniua kwa presha mimi kwa makosa yako”
“Nilikosea najua lakini niliweka kipaumbele kuomba msamaha kwa kwenda ofisini kwake , lakini hakutaka hata kuniangalia usoni licha ya kumletea zawadi”
“Zawadi gani umempelekea?”
“Nilimnunulia Headphone ambazo zingemsaidia kusikiliza mziki akiwa anachukua mazoezi”
“Mh bora angalau ukampelekea kile anachopenda kuliko kwenda kumpoza na zawadi ya namna hio , hata ni mimi ningekataa,Yaani Roma jamanii”Aliongea Blandina huku akirudia kazi yake.
Roma siku yote alikaa nyumbani huku akiisikiliza mziki kwa kutumia Headphone zake alizomnunulia Edna na zikakatiliwa, muda wa chakula cha mchana aligundua Lanlan hakuwepo pamoja na Qiang Xi.
“Mama Lanlan na Qiang Xi siwaoni hapa?”
“Babu yako kaja kumchukua na kuondoka nae na kasema atamrudisha kesho ilinibidi nimpigie Edna simu kumpa taarifa maana alikuwa ashaondoka tayari kwenda kazini”
“Hakuna kitu kingine alichosema zaidi ya kumchukua Lanlan?”
“Hakuna alichosema , alimpigia simu Edna tu na kumpa Lanlan aombe ruhusa kwa mama yake na wakaondoka”
“Kwanini hajanipigia mimi”
“Kama unajijua ni baba kwanini hurudi hata nyumbani kwa kuwahi na kujua mtoto kalala vipi , unaitwa baba lakini bado huchukulii cheo hicho kwa ukubwa wake, Lanlan anaweza asiwe mtoto wako wa damu lakini tayari anakuita baba hivyo una jukumu kubwa kwake, huoni babu yake anajitahidi kumkubali kama mjukuu”Aliongea na kumfanya Roma kujisikia hatia.
“Lakini mama unanisema sana leo , ila Lanlan namchukulia kama mtoto wangu wa kumzaa na nitahakikisha nampa malezi yote kama baba mengine yalikuwa dharula tu”
“Sawa nimekusikia baba na nakuamini katika , ila mimi ile sura ya Edna ikiwa kwenye ukauzu ndio inanikosesha amani , hivyo jitahidi kumuweka sawa”
“Hahaha..Mama bwana nikajua naigopa mwenyewe kumbe tupo wengi”Aliongea Roma
Nyumba ilikuwa imepooza kweli maana Sophia hakuwa mtu wa nyumbani tokea awe maarufu na hata muda huo alikuwa Afrika ya kusini ambako alienda kwa ajili ya kutengeneza Vidio ya wimbo wake mpya anaopanga kuachia mapema kabla ya mwezi wa nne.
Muda wa usiku Edna hakurudi na Roma aliamini Lanlan angekuwepo huenda angerudi, lakini hata hivo alijua huenda ni kwasababu bado alikuwa na hasira, lakini alikaa kama nusu saa tu Edna aliweza kurudi na Roma alimwangalia kutoka juu na kutabasamu huku akifikira namna ya kuyamaliza.
Siku iliofuata baada ya kuamka na kushuka chini kusalimiana na wanafamilia wengine pamoja na kumuulizia Edna , aliambiwa katoka kwenda kuchukua mazoezi.
Roma baada ya kupata taarifa hio alienda mpaka gereji ya magari na kuchukua baiskeli ambayo alifanya kuiagiza mtandaoni na kuletwa jana yake mchana ikiwa ni mwendelezo wa kufikiria namna ya kumpoza mke wake.
Alitoka na baiskeli hio na kuendesha uelekeo ambao aliamini Edna angekuwa akichukulia mazoezi na ni kweli ndani ya dakika chache tu za kuendesha alimuona akiwa anakimbia akiwa amevalia suruali ya track Suit na jezi ya Wananchi(Yanga) , Roma alijikuta akitabasamu kwa namna Edna alivyokuwa ameimarika kwenye swala la mazoezi , kwani mwili wake ulionekana kuanza kukomaa na hata ule unyonge kuanza kupotea na alikuwa mwepesi kwenye kukimbia.
Wanaume aliokuwa akipishana nao Edna waliishia kugeuka nyuma na kuangalia kazi ya uumbaji.
Ilikuwa ni siku ya tano tokea Edna kuanza kukimbia ndani ya mtaa wa Ununio kila asubuhi na katika siku zote hizo aliweza kusogelewa na wanaume takribani wanne waliokuwa wakichukua mazoezi na kujaribu kumuongelesha lakini matokeo yake hakuna ambaye hata alipewa nafasi kwani waliishia kughairi baada ya kuona ukauzu wa Edna.
Kati yao kuna wazungu wawili ambapo pia walikuwa wageni ndani ya hilo eneo ambao walijaribu bahati zao lakini waliishia kutolewa nje na ilipelekea mpaka kuanza kujaribu kutaka kumjua zaidi mrembo huyo asie taka shobo na majibu walioyapata yaliwafanya wasimsogelee tena.
Hivyo Edna hakusogelewa tena baada ya kugundulika ni mke wa bwana Roma Ramoni mtoto wa Raisi wa Jamhuri , lakini pia waligundua wao ni vikapuku tu kwani Edna alikuwa tajiri mkubwa nchini kiasi kwamba mwanzoni waliamini wangeweza kumpata kwa kumhonga pesa , lakini walipokuja kugundua alikuwa na hela zaidi ya uchafu wa jiji la Dar walichoka kabisa na kukata tamaa.
Edna hakupenda macho yaliokuwa yakimwangalia lakini hata hivyo alikuwa akitaka na yeye kujifunza mbinu za kijini , ndio maana hakujali sana waliokuwa wakimkodolea macho na kuendelea na mazoezi yake.
Edna asubuhi hio alikuwa akikimbia kwa spidi kuliko siku zote na hio yote ni kutokana na kwamba kichwa chake hakikuwa sawa kwa yale yaliokuwa yakiendelea kati yake na Roma.
“Babe kunywa maji kidogo , jua lishaanza kuwa kali?”Aliongea Roma mara baada ya kumfikia Edna, lakini hakupokea zaidi ya kusimama huku akihema akiangalia chupa ya maji na kisha kugeukia baiskeli ambayo Roma alikuwa akiendesha Roma na kujiuliza kaitoa wapi , Edna hakuwahi kuiona hio baiskeli na hata hivyo hakujua kuendesha.
“Vipi unaionaje hii baiskeli , nilinunua kwa kuiagiza jana Kupatana na kumwelekeza muuzaji ailete nyumbani kwangu , niliona inafaa kabisa ukiwa umechoka kukimbia nikupandisha na kukurudisha nyumbani, Edna mke wangu umechoka sasa unaonaje ukapanda nikakurudisha nyumbani?”Aliongea Roma na kumfanya amwangalie, aliona ni jambo la aibu kwake kupanda baiskel , hiyo bila kumjibu chochote Roma aliendelea kukimbia.
Roma alijua hawezi kumlainisha Edna kirahisi kutokana na alivyo , hivyo ilibidi aendeshe akiwa upande upande na yeye.
“Edna naomba unisamehe , najua sio mara ya kwanza lakini siwezi kurudia tena , sitokuacha tena mwenyewe”Aliongea Roma lakini Edna ni kama hajamsikia kwani alizidi kukimbia akijifanyisha kiziwi
“Edna mpenzi wangu , usipo nisamehe na kuendelea kuninunia nitaongea kwa sauti ya juu kila mtu asikie nakuomba msamaha”Aliongea Roma na kuufanya moyo wa Edna kupiga kite , watu wengi walikuwa wakiwaangalia na wale ambao wasiomjua Roma waliamini mshikaji alikuwa akibembeleza kukubaliwa.
Edna alimwangalia Roma kwa ishara ya kumwambia asije akafanya anachotaka kufanya kwanni hatomsamehe.
“Edna usinifanyie hivyo , kama usipo nisamehe nitapiga magoti chini hadi unisamehe, niongeleshe hata kidogo basi angalau nisikie sauti yako”Alibembeleza Roma lakini Edna aliendelea kukimbia , lakini hata hivyo alikuwa akifurahi namna Roma alivyokuwa akiteseka kuomba msamaha.
Edna hakuwa na hasira tena ila hakutaka kumsamehe Roma kirahisi , hata hivyo alijua hawezi kuachana nae , hivyo ni wajibu wake kumsamehe lakini hakukubaliana na Roma alivyokuwa akiomba msamaha aliamini kadri atakavyoteseka kuupata msamaha wake ndio itamfanya siku nyingine kutorudia.
“Babe usiponiongelesha chochote nitakuomba msamaha kwa kupiga makelele , unanijua sina aibu hivyo swala dogo kama hilo halinishindi”Aliongea Roma lakini Edna alikuwa na wasiwasi , ni kama aliamini Roma angefanya kweli
“Mpenzi wangu Ednaaa… , naomba unisamehe nimekukosea mimi mume wako” Roma aliongea kwa sauti kubwa ambayo ilisambaa kweli na kufanya hata wale ambao hawakuwa na habari nao kugeuka na kuwaangalia.
Edna alijikuta akisimama huku akimwangalia Roma kwa mshangao , hakuamini kama angeweza kuongea kwa sauati namna hio
“Darling mimi ni mbwa..”Roma alitaka kuendelea lakini alishitukia akizibwa mdomo na mkono , Edna alitaka kukasirishwa na kitendo chake lakini kwa wakati mmoja alitamani kucheka.
“Roma umechizika , kwanini unaropokasauti mbele za watu?”
“Kwanini nijali watu , Kama yangu mbinu inafanya kazi inafanya kazi” Edna alijikuta akivuta pumzina kutamanni kumpiga Roma ngumi kwa jinsi alivyosababisha watu kuwaaangalia.
“Umeshinda baba , umeshinda daah!, sijaona mtu asie na aibu kama wewe”
“Edna naomba unisamehe sijali watu wananichukuliaje lakini nataka unisamehe siwezi kuendelea kukuangalia ukinichunia, nakuapia sitokukasirisha tena”
“Niachie mikono sasa watu wanatuangalia Roma.. hasira zangu zimeisha hata hivyo”
“Babe unamaanisha umenisamehe?”
“Siwezi kuendelea kukasirikia , lakini Roma ukinifanyia kitendo kama cha jana na kunifanya nione aibu mbele ya watu nakuapia nitahakikisha unajutia kwa maisha yako yote”
“Mpenzi usnitishie hivyo bwana mwenzio , sitorudia tena naapia”Aliongea Roma na Edna alitabasamu na kutingisha kichwa kwamba amemsamehe , Roma aliachia tabasamu hakuamini mambo yanekuwa marahisi hivyo , alijiambia inabidi awe makini siku za usoni hata kwenda kulala na wanawake zake.
Edna alipokea maji alioletewa na kunywa kidogo , hata hivyo alishachoka na watu walikuwa wakiwakodolea macho hivyo aliona ni muda wa kurudi nyumbani.
“Edna vaa hizi headphone masikioni , ni nzuri sana na zitakusaidia kuwa mwepesi wakati wa kukimbia zimetengenezwa mahususi kwa ajili ya watu wanaofanywa jogging asubuhi”Aliongea na Edna alizishika na kuziangalia kwa muda na kisha ilibidi tu avae, hata hivyo hakuwa mpenzi sana wa mziki.
Roma baada ya kumvalisha alimpa ishara ya kupandisha kwenye baiskeli aliokuja nayo ili amrudishe nyumbani, Edna alimwwangalia Roma aliekuwa akibembeleza kwa macho ya kulegea na alijikuta akitamani kucheka , alijiambia muda mwingine inafurahisha mwanaume mgumu kuamua kujishusha kwa ajili ya mwanamke.
Edna mara baada ya kupanda kwenye baiskeli Roma aliendesha kwa kuchanga pedeli kuelekea nyumbani huku Edna akiwa amemkumbatia Roma kwenye kiuno ili asije akadondoka.
Upepo wa baharini ulikuwa ukipuliza vizuri mno na kufanya Edna kufumba macho huku akifurahishwa na mziki, ilikuwa mara yake ya kwanza kupanda baiskeli kama hivyo na Roma alilitambua hivyo kuna buda alikuwa akishika breki makusudi ili kumfanya Edna azidi kumkumbatia.
Edna mwenyewe aligundua Roma alikuwa akimfanyia makusudi, lakini aliishia kuangalia kisogo cha Roma na kisha alimkumbatia vizuri.
Upande wa Roma hakuamini maisha yake yangefikia katika hatua hio ya kumuendesha mwanamke anaempenda kando kando ya bahari , ilikuwa ni ndoto ambayo aliamini isingeweza kutimia kutokana na namna watu walivyokuwa wakimwandama , maumivu ya kumpoteza Seventeen miaka iliompita yalimfanya kuamini haitotokea siku akarejewa na furaha na kuishi kama binadamu wa kawaida.
Alijikuta akivuta pumzi ndefu na kuzisuha huku akiserereka na baiskeli kueleleka nyumbani.
“Asante sana Edna mke wangu”Aliongea Roma na kumfanya Edna ambaye alikuwa akisikiliza mziki kuhisi Roma alikuwa akimuongelesha na kumfanya kupeleka mkono mmoja na kuvua zile headphone bila Roma kujua.
“Edna hivi unajua kwenye maisha yangu nimekutana na kila aina ya mwanamke kutokea nilipokua mdogo mpaka umri huu niliokuwa nao kwa kuzunguka karibia kila nchi? , mara baada ya kukuona kwa mara ya kwanza nilikuchukulia kama mwanamke tu mwenye sura ya kirembo ambaye unapaswa kutumiwa kwa starehe ya muda mfupi , safari yangu ya kuja Tanzania haikuwa kwa ajili ya kuoa lakini nilikubali kuona na wewe kwasababu tu ulikuwa ukifanana na Seventeen kwa kila kitu, Edna wewe ni mzuri lakini niseme tu huna Vibe kabisa , nilikukuta hujui kupika , muda wote umekaa kikauzu mno , haupo Romantic mpaka muda mwingine najiuliza ni kipi unachofikira kichwani kwako”
“Ukiachana na uzuri wako sikuwa na sababu yoyote ya kuendelea kubakia kama mumeo , wewe ni mgumu mno , ukauzu wako unafanya maisha kuwa magumu na kuna muda niliona huenda wanawake wengine ni ‘Wife material’ kuliko hata wewe…”
Edna alijikuta aking’ata meno yake kwa hasira huku machozi yakimtoka mfululizo kwa kauli ya Roma , alijihisi amekosewa kweli , alijiuliza ni kweli yote hayo yanayosemwa , inamaana tofauti na uzuri wake wote hakuna kitu kingine cha kuvutia kuhusu yeye,alimuona Roma anamuonea.
“Lakini Edna licha ya yote hayo siwezi kukataa kwamba wewe ndio uliehusika katika kunifanya nifikirie upya kuhusu maisha yangu na kuachana na mambo yaliopita , umenifanya nimeanza kuyaangalia maisha kwa namna ya utofauti kabisa , na sasa hivi nashindwa hata kuelewa ilikuwaje mpaka nikakubaliana na wewe kwa kila kitu tokea tulivyokutana , najiuliza kwanini sasa hivi nahisi maisha yangu bila wewe hayawezi kuendelea, najihisi kama nimerogwa kiasi kwamba muda wote sura yako inapita mara kwa mara kwenye akili yangu , Edna natamani maisha yangu kuendelea hivi mpaka mwisho wa maisha yangu hapa duniani , najua mara kwa mara nakukasirisha , lakini nataka utambue kwamba hata kama siku ikatokea hatuongeleshani kwa kukoseana , nitaendelea kubaki nyuma yako ili ukigeuka uweze kuniona , Edna asante kwa kuja kwenye maisha yangu na kunifanya nipate nafasi tena ya kuyaangalia maisha kwa namna ya tofauti , Edna nakupenda mno kuliko mwanamke yoyote yule”
“Kama mini ni wa muhumu kwenye maisha yako na unanipenda kwanini unanikasirisha mara kwa mara”Aliongea Edna na kumfanya Roma kutaka kudondosha baiskeli.
“Roma kua makini utanidondosha”
“Edna nilijua hunisikiii?”
“Niliacha kusikiliza , mziki wenyewe ulioniwekea mbaya”
“Dah .. kwahio umeweza kusikia nini nilichozunguma?”
“Nimesikia ukini nanga , umesema ninaboa , sina Vibe kabisa , sipo romantic muda wote nipo na ukauzu , naona umetokea kunanijua vizuri sana”
“Babe kwanini unachagua maneno mabaya tu , sikiliza voko yangu mwishoni nilihitimisha vizuri bwana”
“Endesha acha kuongea sana”Aliongea na kumfanya Roma kuongeza spidi kuelekea nyumbani.
Edna alijikuta akitoa tabasamu bila kupenda , aliangalia mgongo wa Roma kwa macho ya huba na kujikuta akivuta hewa huku akizidi kumkumbatia Roma, alijihisi mapenzi yake kwa Roma yalikuwa yakimkolea siku hadi siku.
Roma na Edna mara baada ya kufika nyumbani walikuta sehemu walipoegesha magari yao yameongezeka mawili , moja ikiwa ni Aud A8 na Benz SL 550.
Mpaka hapo walijua kuna ugeni ambao umefika , lakini Roma alijiuliza ni mtu gani ambaye anafika kuwatembea asubuhi asubuhi tena nyumbani
“Roma hio Lexus ni ya kwako . niliona wakati naenda mazoezini?”
“Ndio , lakini hayo magari mengine sio ya kwetu , unatammbua ni ya nani?” aliuliza Roma na kumfanya Edna atingishe kichwa kujibu kwamba hayatambui.
“BMW yako ipo wapi?”
“Jana ililipuka , nimesahau kukuambia, hio Lexus nimeichukua kwa mtu”Aliongea Roma kirahisi tu lakini alimfanya Edna kumwangalia kwa wasiwasi.
“Kulipuka kwa gari sio jambo la kawaida , Roma unafanya mambo mengi ya hatari ndio maana mama haishiwi na wasiwasi kila ukitoka nyumbani”
“Usijali kuna tukio lilitokea katika harakati zangu nitakuelezea”
“Okey! Lakini unaweza kuchukua gari lingine ukaachana na hili la kijapani , linaonekana vizuri lakini huwa sipendi brand yak…”
“Edna njooni kuna wageni kutoka serikalini wanawasubiria…”Sauti ya Bi Wema kutoka ndani iliwaita na walijikuta wakiangaliana na kisha walipiga hatua kuingia ndani.
ITAENDELEA-WATSAP 068715134