Simulizi ya kipelelezi: Jiji la kamari (gambling city)

Simulizi ya kipelelezi: Jiji la kamari (gambling city)

HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 79
"Mume wangu hata siku moja aliwahi kuwaza kurudi nyumbani?"
"Hiyo ndiyo ilikuwa ndoto yake kubwa kila siku akilala na kuamka ila alipanga kufanya hivyo mambo haya yakiisha yote kwa sababu maadui zetu wanapenda kuzitumia familia kama udhaifu mkubwa hivyo kama angekuwa anakutana na nyie kila mara mngekuja kuingia kwenye matatizo makubwa mno. Hiyo ndiyo sababu kubwa ambayo ilimfanya yeye kukaa mbali kabisa na nyie mpaka kazi ikiisha na kwa bahati mbaya sana hajafanikisha ndoto zake. Alitamani haya yakiisha awachukue mzunguke dunia nzima kwa pamoja mkifurahia kama familia, alikuwa ni mwanaume ambaye kabla ya kufanya jambo lolote lile basi familia ilikuwa inakuja kwanza kwenye mdomo wake na moyoni mwake"
"Naweza kuuona hata mwili wake?"
"Huo ni haki yako na mwanao ila kwa sasa umehifadhiwa na nakuahidi hii kazi ikiisha mtamzika kwa heshima na kumuaga wewe na mwanao"
"Nitakushukuru sana kwa hilo"
"Mimi sio wa kunishukuru bali unatakiwa kunilaumu sana kwa kuanzisha haya yote"
"Siwezi kukulaumu kwa sababu aliwahi kuniambia siku ile ananiaga kwamba wewe ndiye mtu mhimu sana kwenye kuifanikisha kazi hii hivyo naomba uimalize kazi hii kwa ajili ya heshima ya mume wangu. Kama ukilifanikisha hili nina imani hata yeye huko aliko atakuwa mwenye furaha kubwa sana na kujivunia uwepo wako hapa duniani."
"Shika hii kadi ya benki, ina bilioni mbili ndani. Ni matumaini yangu kwamba itakusaidia kwa namna moja ama nyingine kwenye malezi ya mtoto lakini mimi pia muda wote nitakuwa karibu yenu na kama kuna kitu chochote kinahitajika usisite kuniambia na kunitafuta kwa hii namba. Najiona kwamba familia hii ni jukumu langu kuhakikisha mnaishi salama kama kumbukumbu bora ya moja kati ya watu bora sana kuwahi kutokea kwenye maisha yangu ambaye ni James" mwanaume aliongea maneno mazito sana mbele ya mke wa James na wakati huo alimpatia kadi ya benki na karatasi ndogo ambayo ilikuwa na mawasiliano yake na namba ya siri ya kadi hiyo ya benki ambayo ilimtoa machozi mke wa James kwa sababu namba hiyo ya siri ilikuwa ni tarehe na mwaka wa kuzaliwa wa mwanae wa pekee.
Mwanaume hakuwa na jambo la kusubiri tena zaidi ya kuondoka hilo eneo maana muda ulikuwa unazidi kwenda sana na hayakuwa yamebakia masaa mengi sana ili kukuche. Alitoka nje mke wa James akiwa anampungia mkono huku machozi yanamtona na mwanaume huyo alimpungia mkono mwanamke huyo akiwa anamuonea huruma na kumsikitikia sana. Alijihisi ana hatia nzito mno kwenye moyo wake kwani kila ambaye alikuwa anajaribu kuwa naye karibu alikuwa anapoteza maisha hivyo mbele yake alitakiwa kuikamilisha kazi kama kumbukumbu kwa walio muachia kazi hiyo na wale ambao waliweza kufa kwa ajili yake yeye.

THE UNTOLD (ISIYOSEMWA)
Ilikuwa ni blogu ya kijana mmoja ambayo ilikuwa inaendesha kipindi na kutoa taarifa zile ambazo ulimwengu au watu wengi hawakuwa wanazijua au kuwa na taarifa juu ya uwepo wake. Jambo hilo lilimpa umaarufu kijana huyo kwa watu ambao walikuwa wanazifuatilia habari ambazo alikuwa anazitoa, upekee wake kwenye habari ndio ulimfanya kuanza kupendwa na watu kwa sababu alikuwa anachambua taarifa ambazo zilikuwa hazipatikani kirahisi, taarifa ambazo ulimwengu ulikuwa unazificha yeye ndizo ambazo alikuwa anazileta mezani kwa watu wake waweze kuzipata na kuzijua.
Alikuwa ni kijana ambaye alikuwa na maono makubwa sana kwenye ulimwengu wa habari ndiyo maana alikuwa anaifanya kwa moyo sana na kumfanya kuwa tofauti sana na watu wengine ambao nao walikuwa kwenye hiyo dunia ya habari. Alikuwa anafanya kazi kwa bidii sana usiku na mchana bila kupumzika na ofisi yake ndiyo ilikuwa kama nyumba kwake maana alikuwa analala hapo hapo na kumaliza kila kitu hapo hapo.
Usiku akiwa amekishika kitabu kimoja cha hadithi moja ya kusisimua sana ambayo iliandikwa na mwandishi FEBIANI BABUYA, kitabu ambacho kilikuwa kinaitwa GEREZA LA HAZWA alihisi kama kuna kitu hakipo sawa. Mtaalamu huyo wa habari ambaye alikuwa anajulikana kwa jina la Fabian the real, alikuwa anapenda sana kumsoma mwandishi huyo pale anapokuwa anapata muda kwa sababu alikuwa anajifunza mambo mengi sana lakini pia kupata burudani safi sana ya mapigano kutoka kwenye hizo simulizi za kijasusi.
Alikuwa amefuga mbwa ndiyo maana alihisi kuna kitu hakikuwa sawa, alisimama na kukifunika kitabu baada ya kusikia mbwa anabweka mara moja na kutulia. Alichukua panga na kufungua mlango ila alishtuka sana baada ya kukutana na mtu akiwa ndani ya mavazi meusi, alipiga makelele akiwa anakimbilia ndani na kujikunyata ukutani maana mtu ambaye alikuja hapo alikuwa anatisha sana.
Max alitoa kitambaa usoni na kumtaka bwana mdogo huyo kusogea kwenye komputa yake, alitoa frashi kwenye mfuko wake na kuiweka mezani kisha naye akakaa kwenye kiti ambacho kilikuwa pembeni mwa kijana huyo.
"Nataka kukufanya uwe mtoa makala maarufu zaidi duniani, nataka nikufanye uwe mwandishi unaye fuatiliwa zaidi duniani lakini pia nataka nikufanye uwe mwandishi mdogo tajiri zaidi Afrika " Max alitamka akiwa anamwangalia kijana huyo ambaye alikuwa anatetemeka sana.
"Sijaja hapa kukufanyia jambo lolote baya ila nataka ufuate maelekezo ya kile ambacho mimi nakitaka. Kwenye hiyo frash kuna siri zote za kiongozi mmoja mkubwa sana hapa nchini, kuanzia watu ambao wamewafukia chini, mali ambazo amelitapeli taifa, biashara zake zote chafu ambazo huwa anazifanya lakini pia kuna majina ya watu wote ambao huwa anashirikiana nao wa nje ya nchi na mabenki mbali mbali ambako ameficha pesa hizo bila kusahau na biashara ambazo amewekeza nje ya nchi kwa hizo pesa ambazo amezichukua kwa lazima kutoka kwa wananchi" mwanaume alikuwa anamuelekeza taratibu kijana huyo bila haraka yoyote ile.
"Kukikucha, majira ya jioni muda ambao watu wengi wanakuwa mtandaoni, unatakiwa kuwapa taarifa na kuchapisha kwenye mitandao kwa kuwaambia kwamba una habari kubwa zaidi kuwahi kutokea duniani, una habari ambayo dunia haijawahi kuijua na huenda kama dunia ikiiijua basi habari hiyo ndiyo itaitikisa dunia kwa mwezi mzima pengine hata mwaka mzima. Hakikisha unawapa taarifa ambayo itamfanya kila mtu aweze kutaka kukufuatilia usiku huo na wape taarifa kwamba habari hiyo inatoka saa nane na nusu usiku, yaani asitokee mtu hata mmoja wa kuweza kulala na kushindwa kuwa mtu wa kwanza kuipata habari hiyo kwa sababu hata ulimwengu hautamsamehe kwa hilo kosa lake"
"Tumie kava la kutisha sana lakini yenye ujumbe mkubwa ndani yake ili kuwavuta zaidi watu wengi watamani kuyajua yale ambayo yatakuwa yamejificha ndani ya hilo kava. Hiyo habari ukifanikiwa kuitoa ni habari ambayo inaenda kukufanya kuwa mtu utakaye fuatiliwa zaidi mitandaoni duniani kote, utapata wafuasi mapya mamilioni kwa mamilioni na wengine wataanza kuzifuatilia na kazi zako za nyuma na huenda utakuwa mwanzo wako wa kwenda kufanya kazi kwenye mataifa makubwa kwa kulipwa pesa nyingi sana kama ukitaka lakini pia huenda utakuwa mwanzo wako wa kupata madili mengi sana ya pesa nyingi. Ni habari ambayo itawafanya waandishi wakubwa zaidi duniani kila mtu kutaka awe mtu wa kwanza kukuhoji wewe hivyo wewe ndiye unaenda kuiteka dunia kuanzia usiku wa kesho na habari yako itakuwa zaidi hata ya kauli wa raisi wa nchi" mwanaume aliongea mambo ambayo yalimtisha sana kijana huyo.
Kwa maelezo hayo habari hiyo ilikuwa nzito kuliko hata anavyo ifikiria yeye na habari kama hizo mara nyingi huwa zina faida sana lakini pia huwa zina madhara makubwa mno hususani kwenye upande wa uhai.
"Na vipi kuhusu usalama wangu baada ya kuitoa hiyo habari?" Fabian the real aliuliza akiwa ana wasiwasi sana kwenye moyo wake.
"Una faida kubwa moja ambayo inayalinda maisha yako ndiyo maana hauna hata ulinzi lakini hakuna mtu ambaye amewahi kukufuata hapa kuyachukua maisha yako au kuyatisha, unajua ni ipi? Ni kwa sababu unachambua kwa weledi habari za kutisha lakini haugusi kabisa maslahi ya mtu yeyote yule hususani wanasiasa na matajiri. Kama ungekuwa unawazungumzia hawa watu niamini mimi bwana mdogo ungeshakufa muda mrefu sana, hivyo hata kesho ukisema una habari kubwa sana ya kuiteka dunia watu watatamani sana kuijua ila hakuna mtu ambaye atakuwa na wasiwasi kwamba unataka kumzungumzia ni yeye maana haukuwahi kufanya hivyo huko nyuma"

79 inafika mwisho.
 
HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 80
"Hilo ni jambo la kwanza, lakini jambo la pili, ukisha itoa tu hiyo habari huenda utakuwa binadamu utakaye hitajika zaidi na vyombo vya usalama kwa ajili ya mahojiano ila kabla ya kuhitajika na vyombo hivyo mhusika ambaye utamzungumzia kwenye hiyo habari anaweza kutaka kukupata haraka sana ili akutumie uweze kumsafisha tena kisha akuue lakini wakati unaitoa tu habari hiyo kuna watu watakuja hapa wakiwa kwenye mavazi meusi, watakuchukua na kuondoka na wewe kukupeleka sehemu salama hivyo wakati ambao watataka kukuteka wakija hapa hakuna kitu watakikuta zaidi ya chumba hiki kuwa kitupu na huko utatakokuwa mimi nitakuja baada ya kazi kuisha na hapo utakuwa huru kuendelea na maisha yako kwa sababu hakuna binadamu atakuja kukugusa tena mpaka siku unakufa"
"Wewe ni nani na kwanini unataka kunihakikishia kwamba nitakuwa salama mpaka mwisho wa maisha yangu yote?"
"Bwana mdogo ni maamuzi mabaya sana kutaka kunifahamu mimi"
"Kama umefanikiwa kuniamini mimi na kunipa siri nzito kama hizi bila kuogopa kama nitatekeleza au nitakusaliti basi na mimi nahitaji unijibu ili nifanye kazi na mtu ambaye namjua kwamba ni nani na kwanini anataka niifanye kazi hii"
"Sijaja kukubembeleza usije ukajisahau kwenye hilo lakini hapo umeongelea mambo mawili, kunijua mimi na kujua kwanini nataka kufanya haya. Hayo ni mambo mawili tofauti kabisa kwenye dunia yangu na utafanikiwa kulijua moja tu pekee. Mimi ni mtu kutoka ndani ya shirika la kijasusi la nchi hii, kuna wakati huwa unapenda sana kuzungumzia habari za kijasusi na mashrika yake na namna yanavyofanya kazi kwenye taarifa zako, basi mimi ni mmoja wa watu ambao wanatoka huko na unatakiwa kulihifadhi hili jambo kwenye moyo wako mpaka siku ambayo unaingia kaburini. Jina langu naitwa Donald Daniel lakini wao wanapenda kuniita DONNY" alimweleza kijana huyo akiwa amemkazia macho sana, ni kama alimuongezea sana hofu na kumtolea ile hali ya kujiamini maana aliogopa sana.
Watu hao alikuwa amezoea tu kuwaangalia kwenye video za maigizo na kuwasoma kwenye vitabu na kupenda sana kuzichambua habari zao ila siku hiyo alikuwa naye uso kwa uso.
"Zipitie vizuri taarifa zote ambazo zipo humo ndani na uzielewe kisha ndipo uzifanyie kazi ya kuzitoa kwenye habari. Siku ya leo yote hautakiwi kukutana na mtu yeyote yule hata kwa bahati mbaya na hautakiwi kutoka nje ya geti la hii sehemu. Zima simu zako zote na funga kabisa mlango wako mtu yeyote asije akajua kama upo iwe ni kama sio siku ya kazi kwako na baada ya hapo usiku utaitoa habari hiyo kwa usahihi sana. Usije ukawaza kufanya jambo la kijinga kwa sababu utaiponza familia yako yote na wewe mwenyewe ambapo naweza kukupata ndani ya dakika miamoja tu pekee na nitakufanyia kitu kibaya sana bwana mdogo. Jambo hili lifanye kizalendo lakini pia lifanye kama kazi kwa sababu kuna malipo yake. hii kadi ambayo nimeiweka hapa mezani ni ya benki, ndani yake kuna milioni miatisa ambayo ni kama malipo ya hii kazi ambayo unaenda kuifanya. Namba ya siri ni mwaka ambao ulianza kuifanya kazi yako ambapo ni mwaka mmoja ulio pita. Tutakutana wakati mwingine tena" mwanaume alimaliza na kuondoka humo ndani kama vile bado alikuwepo.
Zilipita dakika thelathini ndipo Fabian the real aliposhtuka kutoka kwenye hamaki ambayo alikuwa nayo. Alikuwa anaona kama dunia inazunguka tu na haelewi inaenda wapi wala yeye yuko wapi kwenye dunia hiyo, alikutana na mtu wa ajabu, akampatia taarifa za kutisha sana lakini alimfanyia jambo kumbwa sana kumpatia milioni miatisa hapo hapo akiwa amekaa lakini aliahidiwa kwenda kuwa mtu maarufu sana duniani na ulinzi mkali kupewa lakini pia alipewa onyo kali sana kama angefanya jambo la kijinga basi angeishia sehemu mbaya sana.
Kijana huyo alihema kwa nguvu sana na kuishika frash hiyo baada ya kufunga sehemu zote kama alivyo elekezwa ili aweze kujua ndani kuna nini? hata kitabu alikiweka pembeni kwanza maana moyo wake ulikuwa unamuenda mbio sana. Frash ilikuwa na taarifa zote na madudu yote ambayo alikuwa ameyafanya Denis Kijazo kwenye maisha yake na ulimwengu mzima ulikuwa unaenda kushuhudia kile ambacho kilikuwa kinaendelea nyuma ya tabasamu feki la kiongozi huyo ambaye alipendwa sana na watu ambao walikuwa hawaujui ushenzi ake ambao alikuwa nao.

Saa kumi na mbili asubuhi ndani ya jiji la Dar es salaam kulikuwa kumekucha sana, watu walikuwa mtaani kuendelea na shughuli zao za kila siku kama ilivyo kawaida japo hawakuwa wakielewa yale ambayo yalikuwa yanaendelea chini chini kwenye taifa lao maana kila siku yalikuwa yanatokea mambo ya kutisha sana.
Asubuhi hiyo wakati watu wanaendelea na mambo yao, zilikuwa zinaonekana gari nyeusi za bei ghali sana kumi na tano zikiwa zimeongozana barabaranai. Watu wote walisimamishwa na kila usafiri uliwekwa kando na vyombo vya ulinzi ambavyo vilikuwa barabarani na gari hizo zote kumi na tano zilikuwa zinaelekea Ikulu. Gari zote hakuna hata moja ambayo ilikuwa na plate number bali sehemu ambamo zilitakiwa kuwekwa namba hizo, iliwekwa bendera ya taifa la Tanzania ikiwa inapepea na kuvutia sana.
Huo ulikuwa ni msafara wa mkurugenzi mkuu wa shirika la kijasusi la nchi ya Tanzania Chuki Steward akiwa na majasusi wake ambao wengi alikuwa amewarudisha kutoka nje ya nchi mahali ambako walikuwa wanafanya shughuli za kitaifa. Msafara huo ulifika kwenye geti kubwa la Ikulu lakini haukuruhusiwa kabisa kuingia na walinzi wakuu wa sehemu hiyo huku wakitaka taarifa za kutosha na kama hakukuwa na taarifa basi walitakiwa kuwasiliana na ofisi kuu ya ulinzi wa Ikulu ndiyo itoe amri ya mwisho. Lakini wakati walinzi hao wakiwa wanaendelea kubishana na mwanaume ambaye alionekana kuwa kiongozi wa msafara huo, Chuki mwenyewe alishuka kwenye gari.
Walinzi wote walionekana kushtuka na kuogopa sana baada ya kumuona mkurugenzi wa shirika la kijasusi ambalo lilikuwa linaitwa THE WINGS OF TANZANIA INTELLIGENCE SERVICE (WTIS). Mwanamke huyo ni kama aliwekwa kwa bahati mbaya sana kwenye hiyo sehemu kwa maana alibadilika sana na kuanza kuonyesha makucha yake kitu ambacho kilifanya aanze kuogopwa sana kwa sababu hakuwa anataka mazoea na mtu yeyote yule.
"Bwana mdogo unaitwa nani wewe ambaye una ujasiri wa kuusimamisha msafara wangu na kusema kwamba unataka kupata ruhusa ya mlinzi mkuu wa Ikulu ambaye nimemuweka mimi mwenyewe pale"
"Naomba unisamehe sana bosi, sikujua kama wewe upo humu ndani"
"Nimekukuuliza jina lako"
"Naitwa Lameck"
"Una miaka mingapi Lameck?"
"Thelathini na tatu bosi"
"Mimi unanifahamu?"
"Ndiyo bosi"
"Wewe ni moja kati ya vijana ambao mlitakiwa kuondolewa idarani ila nikaamua kukubakisha kwa sababu niliona ni mzalendo hivyo usije ukataka kunikera dakika za mwisho nikakuua na asubuhi yote hii"
"Naomba nisamehe sana bosi"
"Fungua geti halafu toa taarifa haraka sana kwa maajenti wa ndani kwamba nataka kukutana na raisi muda huu" alitoa amri kwa kijana huyo ambaye alikuwa anatetemeka sna na kutii akiwa ameinamia chini. Mara ya kwanza alitoa amri bila kujua kwamba ni nani ambaye alikuwa ndani ya msafara huo, alihisi ni vijana wapo wenyewe tu lakini aliogopa sana baada ya kugundua pia kwamba mkurugenzi ambaye alikuwa ni bosi wake yeye mwenyewe alikuwepo humo. Alijuta sana kutokuuliza mapema juu ya jambo hilo maana huenda lisingeishia hapo angemtafuta tena na ambacho kingemkuta ingekuwa ni hatari kubwa sana kwake.

Raisi wa Tanzania Justin Mtadei alipewa taarifa juu ya ujio wa mtu huyo wa ghafla sana, ni taarifa ambayo hata yeye ilimshtua sana lakini alikubali kukutana naye. Licha ya mlinzi wake mkuu kugoma kuhusu hilo jambo maana lilikuwa la ghafla sana na halikuwepo kabisa kwenye ratiba yao kwenye mfumo wa ulinzi lakini yeye alidai kwamba lazima amsikilize kiongozi huyo wa shirika kubwa zaidi nchini mwake ukitoa Ikulu kwani alikuwa ni mhimu sana kwa ulinzi wa nchi pamoja na raisi mwenyewe kwa ujumla na mpaka aliwahi sana asubuhi hiyo basi kuna jambo kubwa sana ambalo lilikuwa limempeleka hapo Ikulu.
Msafara uliingia ndani na baada ya kushuka wanaume hao wavaa suti walianza kutawanyika maeneo mbali mbali ndani ya Ikulu na kuanza kupeana ishara, yule ambaye angeshindwa kupokea ishara yao walikuwa wanamuua na kumhifadhi sehemu na hiyo pati ilikuwa inaendelea kimya kimya humo ndani bila mtu yeyote yule kushtuka maana mifumo ya ulinzi yote ilikuwa ipo mkononi mwa mkurugenzi huyo na hata vijana wengi ambao walikuwa hapo Ikulu walikuwa vijana wake ni wachache sana ambao hawakuwa kwenye mkono wake na hao ndio ambao vijana wake walikuwa wanadili nao kimya kimya kwa sababu walijua kabisa kwamba hapo kulikuwa na vijana wa Denis Kijazo pia.
Chuki alikuwa ameongozana na wanaume kumi ambapo wawili walikuwa wamebeba mfuko ambao ulikaguliwa kila mlango na baada ya kuhakikisha kwamba hana madhara yoyote kila sehemu milango ilikuwa inafunguliwa mpaka alipofika ulipokuwa mlango wa raisi. Hapo alisimama baada ya kukutana na mlinzi mkuu wa raisi ambaye alisimama mlangoni kuonyesha ishara ya kuwazuia kuingia ndani.
"Unaitwa Aswile sio? jina lako nitalikumbuka baada ya hili kuisha na nitakutafuta mimi na wewe tuweze kuongea kwa mapana na marefu maana vijana siku hizi mnakosa sana heshima" Chuki aliongea kwa hasira sana na wakati huo walisikia sauti ya mheshimiwa raisi ikiwa inamtaka mwanamke huyo aachiwe aweze kuingia ndani lakini watu walinzi wake walizuiwa mlangoni basi akaingia mwenyewe na mlango ukafungwa, yaani wa ndani wa ndani na wa nje wa nje.
"Heshima yako mheshimiwa"
"Imekuwaje unaingia na ulinzi wote huu sehemu ambayo ni salama zaidi ndani ya taifa hili?"
"Hao wote ni walinzi wa humu mheshimiwa, waliona nina mzigo wakaamua kunisindikiza nao mpaka ndani kuhakikisha kama upo salama"
"Mhhh vijana wako mwenyewe leo waanze kuwa na wasiwasi na wewe? Ni mzigo gani huo?"
"Ni wewe tu kama unataka kuuona"
"Waambie waulete"
"Wanaume wawili waliingia humo ndani na mwili ambao baada ya kuufungua raisi alishtuka sana na kutoka kukimbia maana mwili ulikuwa umekatwa katwa vibaya mno. Ulikuwa ni mwili wa Dax, Karistus Dickson waweza kumuita KD au 002 akiwa ni namba mbili huku namba moja (001) wake akiwa ni Max.

80 inafika mwisho.
 
HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 81
"We mjinga umepitaje na mwili huu mpaka huku? ebu utoe haraka sana kwa sababu nitakufanyia jambo baya ambalo haujawahi kulifikiria kabisa kwenye maisha yako yote. Unakuja kumtisha raisi wa nchi Ikulu kwa sababu tu ni mkurugenzi wa shirika la kijasusi, nafasi ambayo naweza kukutoa muda wowote ule nikitaka?" aliongea kwa ukali sana raisi Justin Mtadei.
"Mazungumzo ambayo nahitaji tuyafanye mimi na wewe yanahusisha huu mwili kuwepo hapa na uwe unauona vizuri kwa sababu kile ambacho wewe unaogopa kukiona na kuona kinyaa muda huu kuna watu huwa wanakiona kila siku kwenye maisha yao kwa sababu tu ya kauli zako za kishamba na kipumbavu kuhamasisha mauaji na matendo mabaya sana ambayo yanawafanya wananchi wasiokuwa na hatia wakiteseka huku wewe ukiendelea kukuza kitambi chako tu na wanao wakiwa wanaringa na magari ya gharama sana mitandaoni wasijue kwamba hizo ni kodi za wananchi ambao wewe unatumia muda mwingi kuwadhihaki na kuwatukana" likuwa ni kauli ya kijasiri sana kuweza kuitamka mbele ya raisi wa nchi.
Raisi alishtuka baada ya kumuona mwanamke huyo amebadilika sana maana hakuwahi kumuona kwenye hali kama hiyo, siku zote alikuwa mtiifu sana kwake na msikilizaji mzuri sana lakini siku hiyo mambo yalikuwa tofauti mno, mwanamke huyo alikuwa siriasi sana na yeye ndiye alikuwa mwongeaji mkuu na raisi alitakiwa kuwa msikilizaji mkubwa. Mheshimiwa alimuita mlinzi wake kwa nguvu lakini lango hilo lililokiwa kwa ndani akiwa na mkurugenzi huyo na wanaume wa kazi wawili na mlinzi wake mkuu nje ya huo mlango alibebwa na wanaume wanne baada ya kupokea kipigi kizito sana kisha wakaondoka naye kwenda kumuua huku wengine wanne wakiwa wamebakia hapo kuhakikisha ulinzi unakuwepo na kama mtu mgeni angekatiza hapo hakuna ambaye angejua kwamba kuna tatizo maana walijipanga kama ilivyokuwa siku zote za kazi walinzi wa kawaida wakiwa hapo.
"Unamaanisha unataka kuipindua nchi?" raisi aliuliza kwa hasira kali sana
"Hapana mheshimiwa, ila wewe ndiye unatakiwa kuondoka kwenye hiyo nafasi na sio kwa hiari bali kwa lazima"
"We malaya una kichaa sio? unatishia kumtoa raisi kwenye nafasi yake, unayajua madhara yake? unahisi nchi na jeshi watakubali juu ya hili? Chuki usije ukafanya hili kosa ambalo hautaweza kulibeba kwenye maisha yako yote" aliongea akiwa anamsogelea mwanamke huyo, alikuwa ana hasira sana kudhalilishwa na mwanamke ambaye yeye ndiye alimuweka kwenye hiyo nafasi lakini alisimama baada ya wanaume ambao walikuwa karibu na Chuki kumsogelea bosi wao kuhakikisha hakuna mtu yeyote alikuwa anapitisha hata kidole chake kwenda kwa huyo mwanamke.
"Upo sahihi kuniita mimi malaya kwa sababu ya hilo jeshi ambalo unajisifia nalo hapa saivi. Lakini hali ambayo itatokea endepo ikiwa hivyo ni kama hiki ambacho unakiona hapa mbele yako kwenye huo mwili wa Dax. Watu watakufa sana, mauaji mengi sana yatatokea na huo hautakuwa mwafaka kwa sababu utaongeza zaidi matatizo, huenda hata mkuu wa majeshi ananitegemea zaidi mimi kuliko hata mimi ninavyo mtegemea au wewe unavyo mhitaji kwa ajili ya usalama wa taifa hili na usalama wako pia. Mimi ndiye mtu ambaye nina taarifa nyingi sana za siri za taifa hili, mimi ndiye mwenye taarifa za ndani sana kujua kwamba ni nani na nani wanahitaji kulivamia na kulipoteza taifa hili, je unahisi mimi na hilo jeshi yupi wa mhimu zaidi? jibu baki nalo kwenye moyo wako"
"Kitu pekee ambacho mimi nakijutia kwenye maisha yangu ni kushindwa kutambua yale ambayo yalikuwa yanaendelea mapema. Sikujua kwamba nilikuwa nimewekwa hapa kama toi la kuchezewa mpaka hili sakata lilipokuja kwenye njia yangu ndipo nilielewa kwamba hii nchi haikuwa sawa kama nilivyokuwa nadanganywa bali msaada wangu kama kiongozi wa usalama ulikuwa unahitajika sana"
"Chuki umesahau mahali ambako tumekutoa na kukuweka kwenye hiyo nafasi mpake leo unakuja kuingia kwenye njia zetu?"
"Najua sana mliko nitoa, najua kwamba mmenitoa nikiwa mtu wa kawaida tu ndani ya jeshi nikaingizwa huku na kwa sababu ya manufaa yenu mkanipa nafasi hii mtu ambaye mlijua kabisa kwamba sisitahili kwenye nafasi hii. Najua mlinipa hii nafasi kwa sababu mimi ni mwanamke na mlikuwa na uhakika kwamba mtaweza kuniendesha kirahisi sana kuliko kama mngemuweka mwanaume kwenye hii nafasi, ila unatakiwa kuelewa kwamba kuniweka mimi hapa hili ni kosa kubwa zaidi wewe kuwahi kulifanya kwenye maisha yako na huyo bosi wako ambaye amekuweka wewe kama kivuli hapo ulipo ukiwa hauna maamuzi yoyote yale" dharau zilizidi raisi huyo alimkimbilia Chuki kwa hasira sana lakini alirudi akiwa anayumba yumba baada ya kupokea kibao kikali sana kutoka kwa moja ya wanaume ambao walikuwa pembeni yake, mtu huyo alikuwa anacheza na bosi wao ambaye ndiye alikuwa ameshika hatima ya maisha yao.
"Chuki unathubutu kuruhusu huyo kijana anipige mimi, huo mkono ndani ya dakika kumi na tato zijazo naenda kuuchoma niule. Ngoja niite walinzi wote wa nje wafike hapa kisha hii taarifa imfikie mkuu wa majeshi"
"Pole sana mheshimiwa, Ikulu yote kuanzia hivi ninavyo ongea ipo chini yangu na wewe upo chini ya ulinzi kwa sababu za kiusalama wa nchi na nina hiyo haki ya kukukamata kama naona kwamba nchi haipo salama kutokana na wewe kuwa huru"
"Whaaaaat?"
"Najua kwamba wewe ndiye kiongozi mkuu wa hili shirika langu lakini kwa maslahi mapana ya taifa langu siwezi kukuacha ukiwa huru kwa sababu utaleta matatizo makubwa sana" mwanamke huyoa alimalizia maelezo yake huku akiwa anawaachia nafasi wanaume ambao walikuwa karibu yake hapo waweze kumfunga vyema kabisa mheshimiwa.
"Chuki una uhakika na hiki unacho kifanya? utajutia sana kwa kuichezea nafasi ambayo nimekupa uache mara moja hiki"
"Naelewa kwamba unategemea Denis Kijazo atakuja kukuokoa akipata taarifa ila nataka nikuhakikishie yeye mwenyewe kuanzia muda huu ana masaa ambayo hayazidi ishirini kuweza kuyanusuru maisha yake na kama anaweza anatakiwa kuikimbia nchi kwa sababu kuna uwezekano akafa au akaishia sehemu ambayo hatakuja kuliona jua mpaka siku ya mwisho ya kufa kwake. Sehemu ambayo atawekwa, atatamani ni bora angejiua yeye mwenyewe ila hataipata hiyo nafasi. Usiku nitakuja kukuonyesha nini maana ya hofu kwa huyo ambaye unategemea kwamba atakuja kukusaidia katika hili" aliongea akiwapa ishara wanaume hao waweze kuondoka na mtu huyo hilo eneo haraka sana.
Rasmi Ikulu ilikuwa imechukuliwa na mkurugenzi mkuu wa shirika la kijasusi la nchi ya Tanzania, raisi alikuwa amekamatwa kwa sababu ambazo zilisemekana kuwa za kiusalama zaidi sasa kazi ilikuwa imebakia kwa Denis Kijazo, mwanamke huyo hakutaka kufanya makosa kama ambayo waliyafanya wenzake. Jambo hilo lilifanyika kwa siri kubwa sana na hakuna mwananchi au mtu yeyote wa raisi huyo ambaye alikuwa ana hizo taarifa kwamba Ikulu haikuwa kwenye mikono ya raisi tena bali kwa watu wa usalama.

Nchi ilikuwa imechafuka kwa habari mbaya ambazo zilikuwa zinaendelea nchini. Wananchi walikuwa wakipiga sana kelele kuhitaji kusikia chochote kutoka kwa raisi wao kitu ambacho kilikuwa nyuma kabisa na matarajio yao kwani waliamini kwamba angetoa kauli zozote zile za kuridhisha. Mauaji mengine ya kikatili ambayo yalianza kusambaa asubuhi hiyo hususani kutoka kwa watu ambao aalikuwa wapinzani wa serikali ambayo ilikuwa madarakani yalianza kuleta tafrani kubwa sana nchini huku baadhi ya watu wakiwa wanatishia kuondoka nchini maana haikuonekana kuwa sehemu ya amani tena kama walivyokuwa wameizoea miaka na miaka.
Watu hao walisambaza taarifa za upotevu wa makomando saba ambao walidaiwa kuuawa wote na kibaya hawakufa kwa ajili ya kulipambania taifa bali kuyapambania maslahi ya watu fulani. Watu hao pia kwa kutumia mitandao ya kijamii walianza kusambaza habari kama utani kwamba serikali ilikuwa imepinduliwa na ili kuthibitisha hilo walimtaka raisi ajitokeze au mkuu wa majeshi ajitokeze hadharani ili kupinga tuhuma hizo zikiwemo ya makomando wake kupoteza maisha.
Hizo habari zilimkuta Denis Kijazo akiwa kwenye mawazo sana, alikuwa anayatafakari sana yale ambayo alifanikiwa kuyaongea na Profesa Mande. Akiwa kwenye hayo mawazo mazito ya kuamua hatima yake ingekuwaje ndipo alipata hizo habari ambazo zilimshtua mno na kumfanya aanze kutokwa na jasho huku akitetemeka kwa hasira sana. Aliitoa simu yake na kuhitaji kuipiga kwa mkuu wa majeshi lakini kabla ya kufanya hayo yote, mlinzi wake alifika humo ndani na kumsihi kwamba mkuu wa majeshi alikuwa amefika. Alikuwa na hamu sana na mtu huyo na alifika kwa muda mwafaka kabisa hivyo alimtaka aingie ndani haraka sana.
"Ni kipi kinaendelea nchini ambacho hata mimi sina taarifa nacho?"
"Makomando wote saba wamepotea"
"Umechanganyikiwa?"
"Hapana mheshimiwa, jana wakati nakupa taarifa kuhusu Dax ni kweli walifika alipokuwa anaishi na kukuta ameuawa hivyo waliamua kwenda alikokuwa anaishi mkewe kwa kuhisi kwamba mtu huyo angekuwa huko hivyo ingewezekana wakampata huko"
"Enhe"
"Walienda na kumkuta lakini aliwaua kikatili sana"
"Whaaaaat? Makomando wote saba?"
"Hapana waligawana, kule walienda wanne na watatu walikuwa wanakuja kuniletea mwili wa yule bwana mdogo ili niufanyie uchunguzi"
"Sasa unasemaje kwamba wamepotea wote?" mkuu wa majeshi hakuongea lolote, aliitoa simu yake na kuifungua video ambayo waliipata kutoka nyumbani kwa mke wa Dax. Ni video ambayo ilikuwa inaonyesha jinsi makomando watatu walivyouawa kikatili sana lakini mmoja aliachwa.
"Huyu kwanini aliachwa?"
"Hakuna na nia ya kumdhuru Max ndiyo maana hapo alikuwa na nafsi ya kumpiga risasi lakini alimuacha na mtu huyo alionekana kumpa maagizo ambapo hatukusikia kinacho ongelewa lakini baadae komando huyu alionekana akiondoka na mtoto, ni wazi kwamba alimpa nafasi ya kuishi ili akamlee huyo mtoto"
"Sasa kwanini aliua baba na mama na akamuacha mtoto?"
"Kwa sababu mtoto hana hatia yeye alikuwa anadili na wahusika wake tu"
"Na hao watatu wako wapi?"
"Hao waliokuwa wanakuja kuuleta mwili kwangu mpaka sasa hawapatikani, nimewaagiza vijana wawatafute lakini wamezunguka kila sehemu ya jiji na hakuna kitu wamekiona hivyo ni ishara kwamba kama hawajauawa wametekwa"
"Hapana, hili jambo haiwezekani alifanikishe mwenyewe, lilikuwa ni jambo la haraka sana sasa kivipi ayafanya mambo yote haya kwa wakati mmoja? maana yake lazima nyuma yake ana mtu mwenye nguvu sana ndiye anamsaidia. Familia yake imesafirishwa kwenda Arusha, namhitaji akiwa hai, nina imani leo Ted anaenda kumpata haraka sana ila kabla ya hili nahitaji kukutana na mkurugenzi wa shirika la kijasusi huyu atakuwa na taarifa nyingi sana juu ya hili na siku hizi simuelewi sana"

81 inafika mwisho.
 
HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 82
"Hapatikani mkuu"
"Mara ya mwisho umemuona lini?"
"Tangu tufanye mkutano na wewe alionekana kupinga sana maneno yako na baada ya hapo sijamuona tena. Nilihitaji msaada wake kama atakuwa na hizi taarifa lakini imeshindikana kabisa kwa sababu siwezi kumpata"
"Huyu mwanamke kuna shida mahali, naanza kuwaza kwamba huenda ananizunguka kimya kimya, nimepata taarifa muda sio mrefu kwamba kuna msafara umeenda Ikulu natakiwa kuwasiliana na raisi haraka sana nijue ni jambo gani ambalo nafichwa hapa" aliongea haraka haraka sana huku akiichukua simu na kupiga namba hiyo lakini kitu cha kushangaza aliambiwa kwamba aangalie vizuri kwenye kuandika namba haijawahi kuwepo namba kama hiyo. Aliisoma namba moja moja na ilikuwa ni ile ile ambayo alikuwa anaitumia kuwasiliana na raisi huyo kila siku ajabu wakati huo alikuwa anaambiwa kwamba aangalie vizuri maana hakukuwahi kuwepo kwa namba kama hiyo.
"No, natakiwa kwenda Ikulu. Kuna jambo halipo sawa, haya mambo wanaweza kuyafanya tu watu wa usalama, inawezekanaje namba ya raisi wa nchi nambiwe kwamba haijawahi kuwepo? kuna jambo baya sana linakuja kwangu na sijui. Naenda saivi Ikulu"
"Mkuu usifanye hivyo"
"Kwanini?"
"Kwa sababu wakati huu watu wengi wameandamana mtaani wakitaka majibu ya maswali yao na lazima watakuwa wamelenga Ikulu. Kuna uvumi ambao unasambaa sana mtaani na mitandaoni kwamba wewe ndiye unaliendesha taifa kitu ambacho ni kibaya sana kwenye tafsiri itapelekea watu waone raisi hana umuhimu sasa na wakithibitisha hilo watapoteza kabisa imani na taifa lao na huenda wataanza kukuchukia sana wewe. Hakuja jambo baya kama ikifikia hatua wananchi wakapoteza kabisa imani na wewe, hilo ndilo jambo baya zaidi kwenye uongozi wowote ule maana wanaweza kufanya jambo la kuishangaza dunia kwa wakati mmoja tu na pesa zako au nguvu zako zisifanye lolote"
"Hivyo kwa sasa kama wakikuona unaenda kule watathibitisha maneno ambayo yanasambaa mtandaoni na watu ambao wanataka wewe ufe au kukuona umeshindwa kwenye hiyo nafasi watakuwa wamepata ushindi mrahisi sana wa mezani. Subiri ufike usiku ndio utakuwa muda sahihi zaidi wa kwenda na kama ukikuta jambo lolote haliko sawa basi nipe taarifa mapema jeshi liweze kuichukua nchi kabla mambo hayajawa mabaya zaidi" Kijazo aliitikia kwa kichwa kukubaliana na mtu huyo maana alikuwa ameongea ukweli. Alimtaka mwanaume huyo aondoke na kwenda kuzisaka taarifa kwa namna yoyote ile kisha angemrudia na baadae wajue nini cha kufanya, Ikulu hakukuonekana kuwa sawa huku kiongozi mkuu wa usalama nchini akiwa hajulikani alipo wala kupatikana kwa njia ya simu.
NGARENARO, ARUSHA
Usiku ndani ya jiji la Arusha kulikuwa kumetulia sana huku wakionekana watu kadha wa kadha wakiwa mtaani hususani vijana wengi wahuni na wavuta bangi ambao walikuwa wakitegea watu ambao wanajichanganya na kuchelewa kurudi makwao usiku kuwa sehemu ya kipato chao, lakini ilikuwa ni tofauti sana majira ya usiku wa siku hiyo.
Hummer moja ya gharama sana yenye rangi nyeusi ilikuwa inakatiza mitaa hiyo ya Ngarenaro ya chini usiku huo ikionyesha kabisa kwamba mtu ambaye alikuwa ndani ya gari hiyo hakuwa na pupa wala haraka ya alikokuwa anaenda hivyo vijana baadhi ambao walifanikiwa kuiona gari hiyo walifurahia sana na kumuona mwenye hiyo gari kuwa boya sana kujiamini mpaka kukatiza majira kama hayo eneo hilo hali ambayo iliwafanya waanze kuifuatilia gari hiyo kwa ukaribu sana lakini walishtuka baada ya kuona gari hiyo inaelekea eneo la JENGO LA SABA ambako hakuna mtu hata mmoja alikuwa anaruhusiwa kukatiza mida kama hiyo lakini vijana watatu walijizira na kuamua kuifuatilia gari hiyo ambayo ilisimama umbali mrefu kidogo kutoka lilipokuwepo eneo hilo.
Walikuwa wanasogea taratibu baada ya kuona kuna mtu anashuka humo akiwa na mavazi ya kutisha sana meusi, kijana mmoja alichomoa bisi bisi yake na kumkimbilia mwanaume huyo ili amuweke chini ya ulinzi ila wakati anakaribia kuifikisha bisibisi hiyo shingoni, mwanaume huyo aligeuka kwa kasi ya ajabu sana na kumtwisha kijana huyo shoka la shingo kisha akazamisha kisu kikali sana kwenye shingo yake. Hakumaliza hata sekunde tano akibaki kimya kabsia, mwanaume huyo alimsukuma akadondokea pembeni akiwa maiti na mwili wake ulikuwa unatisha sana.
Wenzake walikuwa wametoka mbio na wakati wanakaribia pale walikutana na hiyo hali ambayo iliwafanya wote kushtuka sana na kudondoka chini huku wakianza kulia kwa sauti kali sana za kuomba msaada. Wote walitupa chini visu ambavyo vilikuwa kwenye mikono yao kisha wakakimbia kwa kasi sana huku kila mtu akienda njia yake wakitoa vilio vya kuhitaji msaada wa haraka sana lakini mitaa ilikuwa imewachoka hivyo kulikuwa kimya sana hakuna mtu hata mmoja ambaye aliweza kuamka na kusogelea eneo hilo.
Mwanaume ambaye alikuwa amefika hapo alikuwa ni Max, rasmi alikuwa amefika eneo hilo kama alivyokuwa ameelekezwa na Ted ili akafanikishe zoezi zima la kuweza kuiokoa familia yake na kama asingefanya hivyo basi alikuwa anamkosa mkewe na mwanae ambaye alikuwa anampenda sana. Mwanaume hakuwa na uhakika wa kuimaliza kazi hiyo lakini aliona kwamba ndiyo ilikuwa njia pekee ya kuweza kuimaliza vita ambayo ilidumu kwa miaka mingi sana na kumfanya kuonja kifo ambacho wanadamu wengi sana walikuwa wanakiogopa.
Kwenye mwili wake alikuwa ndani ya vazi lake jeusi, na koti kubwa sana jeusi huku usoni akiwa amejifunika na juu kofia lake la pama likiwa limemkaa vyema sana. Kwenye mikono yake alikuwa na kisu na shoka lake lakini kwenye kiuno chake alikuwa na bastola nne ambazo zilifunikwa na koti kubwa ambalo lilikuwa linamfika chini ya magoti. Max alikuwa na taarifa zote kuhusu huko ambako alikuwa anaelekea hivyo alianza kuufuata uchochoro ambao aliamini ungemfanya atokezee huko ambako alikuwa anaelekea wakati huo.
Hatua mia moja za kutembea zilimfanya awe anatazamana na jengo hilo kubwa sana, alitembea taratibu na wakati anakaribia kulifikia lango kuu la jengo hilo lilifunguliwa akakutana na kikosi cha wanaume ambao walikuwa wamevaa nguo mithili ya mabanditi waishio milimani, hakuwa na shaka nao maana aliwahi kupata taarifa kwamba watu hao waliwahi kusalitiwa na serikali wakaenda kujichimbia milimani huko mpaka pale walipokuja kukutana na Denis Kijazo.
Wanaume hao wote walipisha pembeni na mwisho kabisa alionekana Ted akiwa amesimama, alikuwa anampigia makofi Max
"Kweli wewe ni mwanaume wa shoka haswa mpaka umeamua kujitoa sadaka kwa ajili ya familia yako! nimekuheshimu sana kwa hilo ila kwa bahati mbaya sana umekuja kufa na familia yako. Leo nataka nikuzike mimi ukiwa hai hapa hapa halafu nione ni kwa namna gani uliweza kupona huko ambako nasikia uliwahi kuzikwa kwa mara ya kwanza" Mwanaume huyo ambaye alikuwa anatisha sana aliongea kwa sauti yake nzito akiangaia pembeni ambako kuna vijana walikuwa wanaendelea kuchimba kaburi.
"Mimi na wewe tuna mengi sana ya kuzungumza lakini kwanza ongea na hawa vijana na kama utafanikiwa kuwadondosha wote basi mimi nipo ndani nakusubiri na mlango upo wazi ndipo utapata nafasi ya kuweza kuiona familia yako kwa mara nyingine. Nimezisikia sifa zako za namna ulivyo mtaalamu sana kwenye hii tasnia ya mapigano ila kwa leo ngoja nijionee kwa macho yangu mwenyewe, mtaa mzima huu nimeweka kamera hivyo tangu unafika nakuona, nimeshangaa sana unamuua kijana wa watu ambaye ni kibaka tu kwa hasira ambazo ulitakiwa kuzimalizia kwangu. Nakusubiri na kama ukichelewa basi namuua mwanao" aliendelea kujigamba Ted akiwa kwenye vazi la jeshi lakini juu alikuwa ndani ya vest nyeupe, alimhakikishia mwanaume huyo kwamba alimuona tangu anafika ndiyo maana wakati anafika tu hapo lango lilikuwa linafunguliwa.
"Msimuue, nileteeni akiwa mzima hata kama mtamvunja miguu" aliwapa amri vijana ambao walikuwa hapo kwa ajili ya Max. Vijana hao waliitikia kwa ishara ya kuinamisha vichwa kisha yeye akawa anaondoka akiwa ameongozana na wanaume wawili, Herman ambaye alikuwa kijana wa kuaminiwa sana na meja jenerali Francis Mboye lakini siku ya mwisho alikuja kumsaliti wakati anaenda kwa Denis Kijazo ambako alijiua mwenyewe na alimuahidi kijana huyo kwamba angekuwa na mwisho mbaya sana lakini kijana wa pili alikuwa ni Kenedy. Huyu alikuwa kama mkono wa kulia wa Ted. Mwanaume huyo kwenye kiuno chake alikuwa na upanga mkali sana na kwenye bega lake alikuwa ameliweka shoka lake ambalo alikuwa anapenda sana kulitua ambalo lilikuwa na cheni inayong'aa isivyo kawaida.
Walikuwa wamesimama wanaume kumi na watano mbele ya Max, hao wote walikuwa ni wauaji wa kutisha sana ambao waliufanya mtaa huo kuanza kuogopeka sana na ndio ambao walikuwa ni walinzi wa sehemu hiyo ambayo ilikuwa inatengeneza sumu mbaya sana ambayo ilikuwa inaua na ilikuwa inauzwa kwenye masoko makubwa sana ya siri duniani lakini pia eneo hilo lilikuwa likitumiwa sana kuweza kutengenezea madawa ya kulevya. Huo mlima Max alitakiwa kuupanda ndipo aweze kupata nafasi ya kukutana na mtabe mwenyewe Ted mwanaume ambaye alidai kwamba alikuwa ana miaka kumi na mitano bila kukutana na mtu ambaye angeweza kumfaa kwenye dunia ya mapigano akajiona amepigana na mwanaume mwenzake maana wengine alikuwa anawaona kama wachumba tu.
Kijana wa kwanza ambaye alikuwa karibu kabisa na alipokuwa Max alikuwa na cheni ya chuma kwenye mkono wake ambayo alikuwa anaizungusha kwa mbwembwe sana kiasi kwamba akiirusha kuelekea kwenye shingo ya Max lakini kuanza kwake kwa mbwembwe kulimponza. Max aliikwepa hiyo cheni kisha akaidaka kwa mkono na kuivutia kwake kwa nguvu ambapo ilimfanya mwanaume huyo kukosa balansi na kumfanya aende vibaya, shoka lilitua kwenye kifua chake kama vile mtu alikuwa anapasua kuni. Kifua kiligawanyishwa kati kati kisha ukafuatia mkono ambao ulikuwa na kisu, mkono huo ulizamisha kisu hicho kwenye sikio ambacho kilizama na kuchomolewa kisha mzoga wa mwanaume huyo ukaachiwa chini kama alikufa miaka miwili ambayo ilikuwa imepita.

82 inafika mwisho.
 
HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 83
Hiyo ilikuwa ni kama ishara kwa wale wengine kumi na nne ambao walibaki wasiweze kumzoea mwanaume huyo vibaya, walitakiwa kwenda kwa tahadhari kubwa na sio kuanza kwenda kwa mbwembwe eneo hilo kwani wangeisha vibaya sana baadae waanze kumtafuta mchawi nani. Watatu walikuwa wameshika visu vyao na mapanga, walimsogelea kwa kasi sana mwanaume huyo huku wakiwa wanayachanganya mapigo yao ambapo aliofanikiwa kuyakwepa mateke makali ya wanaume wawili lakini wakati anaukwepa upanga wa mwanaume wa tatu alikutana na teke la shingo karibu na koromeo lililo mfanya arudi nyuma akiwa anahema kwa nguvu sana.
Mwanaume alitumia mguu wake wa kushoto kusimama kwa nguvu na wakati huo kuna upanga ulikuwa umarushwa kwa nguvu sana kuelekea kwenye paja lake maana watu hao hawakutakiwa kabisa kuweza kumuua hapo. Alishtuka ukiwa upo karibu sana hali ambayo ilimfanya kurukia pembeni sehemu ambayo ilikuwa na ukuta. Aliruka sarakasi kali sana ambapo alimpita mwanaume yule ambaye alikuwa amemfikia akiwa anauwahi na upanga wake na kusimama nyuma yake.
Mwanaume yule hakugeuka tena bali alisimama kwa sekunde kadhaa kisha akapiga goti lake chini na kujishika shingoni. Wakati Max anaruka kutoka kwenye ule ukuta alipishana na mwanaume huyo akiwa anakuja ule upande kwa kasi sana na lilikuwa kosa kubwa kwani mwanaume huyo alikutanishwa na kisu cha shingo ambacho kilimchana chana vibaya sana kiasi kwamba hakufanikiwa hata kuufikia upanga wake ambao ulikuwa umejichomeka kwenye ukuta.
wawili hawakumchukulia muda mrefu sana walikuwa wanarusha mapanga yao kwa kasi ya ajabu sana huku wakiwa wanalenga zaidi kwenye miguu. Mmoja alifanikiwa kumuonja kwenye mguu wake ambapo alishuka chini kidogo lakini wakati huyo alikiachia kisu kimoja ambacho kilienda kukita kwenye moyo wa mwanaume huyo na wakati anafanya hayo mwenzake alikuwa anashusha buti lake kuelekea kichwani kwa Max ila kwa bahati mbaya sana mwanaume huyo alishtuka sana baada ya kugundua kwamba mguu wake ulikuwa mwepesi mno kutokana na kukatwa na shoka katikati ya mfupa mguu ukadondokea pembeni.
Wakati anashuka chini akiwa analia kwa maumivu makali, alipigwa shoka la kichwa ambalo lilimfanya ashindwe hata kuongea kitu, aliachama mdogo mdogo na kudondoka chini akiwa ameyatoa macho yake, alikufa vibaya sana bila hata kuweza kuyafumba macho yake. Wanne walikuwa chini, sasa walijisogeza watano wakiwa wanaenda kwa mahesabu, yaliyo wakuta wenzao ilikuwa ni taarifa tosha sana kwamba hawakutakiwa kucheza vibaya na huyo mwanadamu vinginevyo wangeweza kuisha wote hapo.
Kasi ilikuwa ni kubwa sana kiasi kwamba alishindwa kuendana nao wote hivyo mwanaume alizamishiwa upanga kwenye mbavu yake mpaka alipiga goti chini. Ushindi ulikuwa karibu yao, alimuona mwanaume mmoja aliwa ameruka kwa nguvu sana na buti lake lilikuwa linaenda kuuvunja mguu wake lakini alimsubiri mpaka mwaume huyo alipo karibia kumfikia kisha akajivuta nyuma kwa kasi sana na sehemu hiyo ambayo mwanaume huyo aliutua mguu alilisimamisha shoka hilo na mwanaume huyo akajikuta mguu wake unatua kwenye shoka, yaani alikuwa amejikata mguu wake mwenyewe.
Alitaka kupiga makelele, alisogelewa kwa sarakasi moja kali sana kisha kisu kilizama kwenye mdomo wake likafuatia buti kali sana la shingo, shavu lake lilichanika vibaya mno. Mwanaume alikuwa amebakia na shoka tu kwenye mkono wake akiwa amepiga goti lake chini. Alichana sehemu ndogo ya koti lake na kujifunga sehemu ya mbavu ambayo alikuwa amekatwa huku akitoa pama lake na kitambaa usoni kisha alinyanyuka kama mzimu na wakati ananyanyuka aliliachia shoka lake ambalo lilitua kwenye goti la mmoja wa waliokuwa wamemzunguka, mwanaume huyoa alijikuta anadondokea mbele na kukosa balansi yake vizuri kitu ambacho kilifanya adakwe shingo yake na kuzungushwa kama nati ya kufungia tairi ya gari.
Upanga ulikuwa unakuja kwenye njia yake, aliutumia mwili wa mwanaume huyo ambaye alikuwa amemnyonga kuzuia upanga huo ambao ulizama na kumpa nafasi ya kurusha ngumi nyingi sana kuelekea kwenye kifua cha mwaume huyo kifuani. Kifua kilivunjwa vibaya sana kisha mwanaume huyo aliudaka upanga huo ambao aliutumia kuigeuza hiyo sehemu kuwa bucha, wanaume hao ambao walikuwa wamemzunguka hapo aliwakata vibaya sana ndani ya muda mfupi alibaki ameshika upanga ambao ulikuwa unamwaga damu nyingi sana akiwa anawaangalia wale ambao walikuwa mbele yake waliokuwa wamebakia kutoka kwa wale kumi na watano ambao alitakiwa kuwadondosha chini ndipo apate nafasi ya kuweza kuonana na Ted ambaye alikuwa ametulia ndani akiwa anaangalia mwanaume huyo alichokuwa anakifanya kupitia kamera za marejeo ambao alikuwa amezitega kila eneo ndani ya jengo hilo.
Max aliutupa upanga ambao ulikuwa kwenye mkono wake na kuwataka wanaume hao wamfuate yeye alipokuwa wao wakiwa na silaha kwenye mikono yao. Mwanaume mmoja ambaye alikuwa na upinde na mshale alirusha mshale kwa nguvu sana ila alikosea mahesabu yake kwani wakati anarusha alikuwa anaenda kwa kasi mno alipokuwepo Max lakini wakati anataka kuchomoa mshale wa pili alichelewa na ni muda ambao walipishana katikati hivyo akageuka kati akiwa ameushika upinde wake mkononi ila alibaki ameushika vile vile akiwa kama anataka kupiga lakini hakuweza mpaka wenzake wakawa wanamshangaa maana ilikuwa ni ghafla sana.
Walishtuka baada ya kuona kuna mshale umezama kwenye moyo wake, wakati wanapishana mwanaume alichomoa mshale mmoja kwa kasi sana kiasi kwamba hata mhusika hakushtukia hilo hivyo wakati anageuka mwenzake alikuwa amesha utupa mshale huo kwa mkono na kuuzamisha kwenye moyo wa mwanaume huyo ambaye alikuwa na mishale yake na upinde mkononi na mgongoni. Max alisogea taratibu mpaka pale chini na kuokota shoka lake na kuchomoa kisu ambacho alikizamisha kwenye mdomo wa mwanaume mmoja.
Lile jambo ambalo lilikuwa limetokea pale lilikuwa la kikatili sana kwa mwanadamu mwenye nafsi ya kawaida tu hali ambayo iliwafanya hata wale ambao walikuwa wanachimba shimo kwa ajili ya kumzikia mtu huyo kuanza kutetemeka sana, aliwaangalia na kuwapa ishara ya kuweza kukimbia eneo hilo kwani halikuwafaa, walitakiwa kwenye kuuza hata mitumba huko mtaani na kazi hiyo haikuwa inawafaa kabisa. Wanaume hao walikimbia sana kuelekea lilikokuwa geti kuu yeye akiwa anawaangalia walio bakia mbele yake.
Walianza kuja kwa pamoja wakati huo yeye aliliweka shoka lake begani na kisu akakichomeka kiunoni na kuchomoa bastola ambapo aliwamiminia risasi watu hao kwa kutumia bastola mbili ambapo walianza kukimbia hovyo maana wasingeweza kabisa kushindana na risasi ila hakuna aliyefanikiwa kukimbia, aliwaua wote na baada ya kuhakikisha wamekufa wote alitupa bastola hizo na kuanza kuelekea ndani sasa kukutana na Ted mwenyewe akiwa anavuja damu kwenye mbavu yake.
Aliingia kweney lango la kwanza ambapo alikutana na umati wa watu wengi sana wakiendelea kujaza madawa ya kulevya kwenye mifuko huku wengine wakitengeneza na wengi walikuwa ni wanawake ambao walikuwa uchi kabisa bila nguo kwenye miili yao. Alichomoa bastola moja kwenye kiuno chake na kupiga risasi nyingi sana juu, hakuna mtu hata mmoja ambaye alisimama tena, huenda ni nafasi ambayo wengi walitamani kuipata kuweza kukimbia humo ndani lakini haikuwahi kabisa kupatikana hivyo kutokea kwa nafasi hiyo hakuna mtu alisubiri ukizingatia milio ya risasi hizo ilitoka kwa mtu ambaye vazi lake lilikuwa na damu ya kutosha huku akiwa na shoka kwenye bega lake nalo likiwa linavuja damu ilikuwa ni ishara mbaya sana kwao hivyo watu hao walikimbia sana kutoka nje ya jengo hilo.
Baada ya kupita hapo ndipo aliingia sehemu ambayo baada ya kuugusisha mguu wake wake tu alisikia sauti kutoka kwa binadamu ambaye alikuwa anampenda sana kwenye maisha yake. mwanae wa pekee Naima ndiye alikuwa anaita
"Dady" mwanaume alihitaji kumkimbilia mwanae pale ambapo alikuwa amefungwa lakini kwenye njia yake walitokea wanaume wawili, Herman na Kenedy, hata hivyo alizuiwa kwa nguvu na Ted ambaye alikuwa amekaa kwenye kiti kikubwa sana pembeni yake akiwa amefungwa mke wa Max. Mwanaume alijikuta hata nguvu zinamuishia japo alishukuru sana Mungu kuweza kuwaona wote wakiwa wazima wa afya kabisa ila walikuwa kwenye sonona ambayo ilimuuma sana, ndiyo sababu kubwa ambayo ilimfanya asitake familia yake kuweza kuja Tanzania kwa sababu aliamini kwamba matatizo kama hayo yasingeweza kukwepeka kabisa.
"Mhhhh unakimbilia wapi ndugu yangu! leo tuna muda mrefu sana wa kuweza kuongea mengi sana mimi na wewe lakini unapaswa kuwa mpole. Umeniulia vijana wangu wengi sana sidhani kama itakuwa sawa na mimi nisipo mpoteza mmoja wa wale ambao unawapenda sana" Ted alikuwa anaongea akiwa anakizungusha kisu chake kwa mbwembwe sana huku akiwa anamsogelea mke wa Max
"No, no usije ukafikiria kufanya hivyo tafadhali" Max aliongea kwa huruma sana wakati mwanaume huyo amesimama nyuma ya sehemu ambayo mkewe alifungwa. Ted alimwangalia kwa umakini sana kisha akakipitisha kisu chake mbele na kukizamisha kwenye shingo ya mke wa Max Ariana huku akiwa anashuhudia kwa macho yake mwenyewe. Ted baada ya hapo alizamisha visu vingi sana kwenye moyo wa mke wa Max ambaye alikufa kwa maumivu makali sana mumewe akiwa anashuhudia na mwanae mdogo ambaye alikuwa kwenye kilio kikubwa sana kumlilia mama yake na hakukuwa na namna ya kuweza kumrejesha tena.
Mwanamke ambaye alikubali kumpatia zawadi ya mtoto, mwanamke ambaye aliachiwa na kaka yake Siza kwamba amlinde kwa gharama yoyote ile alikuwa amekufa mbele ya macho yake akiwa ameshindwa hata kumsadia. Mwanaume alijikuta chozi linashuka lenyewe kwenye macho yake akiwa bado haamini kile ambacho alikiona mbele yake.

83 inafika mwisho.
 
Shukran sana, ila ongeza urefu wa vipande chief.
 
Huyo mwanamke kiherehere kimemponza acha afe tu 🤔
 
Huyo mwanamke kiherehere kimemponza acha afe tu [emoji848]
Kweli kabisa wanawake ni wajinga sometines, unaweza ukawa upo kwenye hatari mwenyewe akaja eti kukusaidia matokeo kila kitu kinaenda
 
Max na Ted who is the best nani aje apa tubeti mshindi kwenye hilo pambano 🔥🔥
 
Mpaka hapo Max amefeli kuwalinda watu wake muhimu 🤔
 
Back
Top Bottom