Israeli yashambulia televisheni ya taifa ya Iran baada ya kutoa agizo la wananchi kuondoka Tehran
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema awali kuwa Israeli imedhibiti anga ya Tehran, jambo alilolieleza kama “mabadiliko katika kampeni nzima”.
Makombora ya Israeli yamepiga kituo cha televisheni ya taifa ya Iran kilichopo Tehran, baada ya Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) kutoa agizo kwa raia kuondoka katika eneo fulani la mji mkuu huo.
Shambulizi hilo lilisitisha kwa muda matangazo ya moja kwa moja, huku mtangazaji akiondoka ghafla wakati studio ilipojaa moshi.
Shambulizi hilo lilitokea muda mfupi baada ya IDF kuitaka jamii kuondoka katika maeneo ya Wilaya ya Tatu ya Tehran, ambako ndiko studio hiyo ya televisheni ilipo.
“Katika saa chache zijazo, jeshi la Israeli litafanya mashambulizi katika eneo hili dhidi ya miundombinu ya kijeshi ya utawala wa Iran... uwepo wenu katika eneo hili unaweka maisha yenu hatarini,” IDF ilichapisha kwenye X.
Netanyahu aliongeza kuwa Israeli iko “katika njia ya” kuangamiza mpango wa nyuklia wa Iran na uwezo wake wa makombora ya masafa marefu.
Wakati mzozo kati ya mataifa haya mawili ya kikanda ukizidi kupamba moto, waokoaji wa Israeli walisema watu wanane wameuawa kufuatia mashambulizi ya makombora ya Iran kwenye miji ya Israeli, na kufanya idadi ya waliouawa tangu Ijumaa kufikia 23.
Mamlaka za Iran zilisema jioni ya Jumapili kuwa raia 224 wameuawa kutokana na mashambulizi ya Israeli, pamoja na maafisa 17 wa juu wa kijeshi.
Mashambulizi haya ya hivi karibuni yametokea wakati viongozi wa kimataifa wakiwasili nchini Canada kwa ajili ya...