Doctor Mama Amon
Platinum Member
- Mar 30, 2018
- 2,311
- 3,513
SWALI KWA KIKWETE: KAMA AMANI YA KUDUMU SIO TUNDA LA HAKI WATANZANIA TUNATOKAJE OKTOBA 2025 NA KUFIKA KWENYE UFALME WA HAKI NA AMANI TUNAKOPASWA KWENDA?
Mpendwa Jakaya Kikwete,
Rais wa Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Tangu 21 Desemba 2005 hadi 5 Novemba 2015.
Nakuandikia tena kupitia jukwaa hili, kama ambavyo huwa nafanya kila inapobidi, lakini leo barua yangu ikiwa na maneno 1,300 pekee.
Tarehe 05 Januari 2026, ulishiriki katika Uzinduzi wa Jengo la Ofisi ya Uhamiaji na Makazi ya Askari lililopo Micheweni, mkoa wa Kaskazini Pemba, huko Zanzibar.
Uzinduzi huu ulikuwa ni sehemu ya Sherehe za Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zinazohitimishwa leo, tarehe 12 Januari 2026.
Katikati ya mshangao wa watu wengi, hata bila kutoa pole Kwa watanzabia waliopoteza ndugu zao kupitia mauaji ya wiki ya uchaguzi mkuu wa oktoba 2025, ulimpongeza Rais Samia eti kwa sababu ya "kusimamia ipasavyo" masuala ya "utulivu na amani".
Kwa mtazamo wako Tanzania "Tumemaliza 2025 kwa utulivu na amani."
Hivyo ulitoa wito kuwa sasa Watanzania wote "Tuendelee kuomba Mungu changamoto za 2025 zisijirudie tena."
Hata hivyo, kwa kuangalia orodha ya "changamoto" za mwaka 2025, ambazo ni madudu yaliyofanywa na Serikali ya Samia wito wako unakubalika lakini pongezi zako kwa Samia hazina uhalali wowote.
Madudu ya Samia katika mwaka 2025 ni pamoja na haya:
(1) Kutekwa Kwa uhuru wa mahakama,
(2) kusambaratishwa Kwa umakini wa Bunge,
(3) kukamatwa na kufungwa kwa watu kiholela, mfano ni Tundu Lissu,
(4) kutekwa na kuuwawa Kwa watu, mfano ni Mohamed Ally Kibao,
(5) kutekwa na kupotezwa Kwa watu, mfano ni Deusdedit Soka, Mdude, na Balozi Polepole,
(6) Kufuta Usajili wa makanisa yanayohubiri haki, mfano ni Kanisa ya Ufufuo na Uzima,
(7) Kuzuia vyama vya Siasa vya upinzani kufanya KAZI zake, mfano ni Chadema,
(8) Kuvuruga usalama wa nchi kwa kuagiza silaha za kivita kiholela na kuzisambaza nchini,
(9) Kuiba madaraka ya umma na kuyakabidhi wa Rais, wabunge na madiwanu kijeshi kupitia ratiba ya uchaguzi Mkuu wa 2025,
(10) Kupanga na kutekeleza mauaji ya waandamaji zaidi ya 1,500 Kwa kutumia kisingizio kuwa ni vibaka wenye silaha,
(11) Kufanya uteuzi batili wa Viongozi wa serikali nchini Tanzania baada ya uchaguzi Mkuu wa 2025,
(12) Kuanguka kwa katiba ya nchi na kufutwa Kwa utawala wa sheria,
(13) Kuteka vyombo vya habari na kuvitumua kufanya propaganda za kuwajingisha raia, mfano ukiwa ni propaganda ya kuulaghai Umma uamini kuwa amani ni bora kuliko haki.
(14) Kuviingiza vyombo vya ulinzi na USALAMA katika siasa za kusimika Rais haramu na hivyo kumpa kiburi Cha kuendesha nchi Kwa kutumia "Kanuni ya amani ya bunduki" badala ya kutumia "kanuni amani ya moyoni"
(15) kuleta majeshi ya kigeni kuwatesa na kuwaua raia wakati wa uchaguzi mkuu Ili kufanikisha KAZI ya kusimika Serikali ya kijeshi nchini
(16) kuporwa rasilimali za nchi na kuzipeleka ughaibuni Kwa kutumia Mikataba ya uwekezaji wa kilaghai
(17) Kutumia mikataba ya kununua vifaa vya keep jeshi kutoka Uturuki na uae kutakatisha matrilioni ya fedha za mikopo ya Serikali, na hivyo kupora hazina ya Taifa na kuihamishia Uturuki na uarabuni, kwa msaada wa Angela Kiziga.
(18) Kuirejesha tanzania katika mfumo wa siasa za chama kimoja
(19) Kuendesha nchi Kwa kutumia TAMKO la OIC badala ya TAMKO la UN kuhusu Haki za Watu.
(20) Kuwageuza watanzania wa huko ngorongoro kuwa wakimbizi na watumwa ndani ya nchi Yao.
(21) Kuendesha nchi kiukoo na kifalme Kwa kuteua wanafamilia na marafiki wa familia katika nafasi kadhaa za kiserikali.
(22) Kuasisi na kueneza utamaduni wa Kiarabu wa kutoa adhabu ya ulawiti kwa wakosoaji wa serikali hapa Tanzania Bara, utamaduni ambao ni jinai na kinyume Cha kanuni za maadili asilia.
(23) Kuasisi na kueneza utamaduni wa kutukuza kifo (culture of death) nchini Tanzania kwa kubuni na kutekeleza sera ya utekaji, utekaji, upotezaji wa watu, mauaji ya watu hadharani kwa risasi, kuua watu Kwa simu, na kufadhili vikosi vinavyotekeleza matukio haya, na hivyo kukiuka kanuni kwamba uhai wa mtu asiye na hatia (purity of innocent human life) ndio kizio turufu cha utakatifu wa kimaadili (moral innocence) katika jamii yoyote iliyostaarabika.
(24) Ameanzisha kumbukumbu mbaya katika taifa letu kwa kuwa RAIS wa kwanza wa Nchi aliyetunukiwa taji la Mwanasiasa Katili wa Mwaka Duniani.
(25) Amevunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuufuta kabisa kutoka mioyoni mwa Watanganyika waliopoteza ndugu zake oktoba 29 na kunyimwa fursa ya kuwazika kutokana na maagizo ya Rais mwenye asili ya Zanzibar.
Yote haya ni mambo yanayopingana na ndoto ya Kila mtanzania ambayo ni kuishi katika UFALME wa haki na amani ya moyoni badala ya kuishi katika UFALME wa dhuluma na amani ya bunduki.
Hivyo, ukimya wako tangu majanga haya yaanze kutokea, umezua maswali mengi kuhusu nafasi yako kama Rais mstaafu kiasi kwamba hadi sasa unatuhumiwa kuwa wewe ni mhandisi mkuu wa majanga haya ukiwa unafanya kazi ya kuelekeza matukio kutokea nyuma ya pazia.
Na ukweli kwamba katika hotuba yako niliyoiweka hapo juu umempongeza Samia badala ya kumkosoa Kwa kufanya madudu haya umeongeza sababu ya watanzanua kuendelea kuamini kuwa hizi tuhuma dhidi yako ni za kweli, na hivyo kuimarisha chuki halali dhidi yako.
Kwa kuwa hotuba yako inaonekana kuunga mikono propaganda potofu kwamba amani ya bunduki ni bora kuliko amani ya moyoni, Sasa nitajielekeza katika uchambuzi Kwa kuanzia katika kona hii.
Kuna mjadala unaoonekana kuanzishwa na serikali ya Samia ili kuyumbusha kimkakati maarifa ya umma kwa kutumia utata uliomo katika maana ya neno "amani".
Mjadala huu unatengeneza mgogoro wa kimaarifa (epistemological crisis) ndani ya Taifa, na hivyo kuliua Taifa kimya kimya Kwa kushambulia ubongo ambao ni kikonyo cha maarifa ya kijamii.
Ni mjadala unaowagawa Watanzania katika pande mbili kutokana na uwezo wao wa kujibu swali lifuatalo: "Haki ni bora kuliko amani au amani ni bora kuliko haki?"
Mkakati huu unapaswa kupigwa marufuku haraka na kwa hoja thabiti, kama nitakavyoanza kufanya kupitia uchambuzi huu.
Kimsingi, amani ni "hali ya utulivu", kwa maana ya kutokuwepo Kwa vurugu mahali fulani na katika muda fulani.
Na kuna utulivu wa aina nyingi, Kwa kutegemea vigezo gani vinatumika kubainisha aina hizi.
Kwa kuangalia anwani ya makazi ya utulivu husika, utulivu unaweza kuwa moyoni mwa mtu au nje ya moyo wake.
Kwa kuangalia jinsi utulivu unavyopatikana, tunaweza kupata utulivu wa aina mbili.
Mosi, kuna utulivu unaopatikana kihalali; na pili, kuna utulivu unaopatikana kiharamu.
Na Kwa kuangalia mazingira ya utekelezaji wa mikakati ya kutafuta na kudumisha utulivu Kuna mazingira ya aina mbili pia.
Yaani, mazingira halali Kwa maana ya mazingira yaliyo rafiki Kwa haki za watu, na mazingira haramu Kwa maana ya mazingira yanayivuruga haki za watu.
Na kwa mujibu wa kanuni ya utakatifu wa kimaadili usio na madoa ya uovu wenye kupingana na kanuni ya utakatifu wa kimaadili inayoruhusu madoa ya uovu (principle of integral morality as opposed to the principle of proportional morality) tunafahamu kuwa, utakatifu timilifu wa kimaadili ni mseto wa mambo matatu.
Kuna lengo lililotakata, tendo lililotakata na mazingira ya utendaji yaliyotakata, pasipo na pingili YENYE doa la uovu popote.
Ndio kusema kuwa, halali na halali huzaa halali, halali na haramu huzaa haramu, na haramu na haramu huzaa haramu.
Kwa hiyo, ni wazi kuwa kuna aina kuu mbili za utulivu, yaani utulivu halali na utulivu haramu.
Yaani, Kuna aina kuu mbili za amani. Yaani amani halali na amani haramu.
Amani halali haiambatani na doa lolote la ubabe wenye kusigina utu wakati amani haramu inabeba chembe za ubabe ndani yake.
Wewe kama Kamisaa wa Siasa Jeshini unajua fika hizi aina mbili za amani, maana huko jeshini huwa tunaongelea sana "usimamizi wa amani kwa kutumia njia za kidiplomasia au mbinu za kijeshi".
Yaani, unajua kwamba: Kuna amani itokanayo na ridhio la moyoni baada ya kila mtu kuona kwamba haki inatendeka kwa usawa na kwa wote, kwa mujibu wa kanuni ya kiutu isemayo kuwa "mwenye haki ndiye mwenye nguvu", yaani "consensual peace".
Hii ni "amani ya moyoni inayotokana na haki" na ni amani ya kudumu kama italindwa kwa kutumia mbinu halali.
Na unajua kwamba kuna amani itokanayo na mabavu baada ya mwenye nguvu kumnyamazisha mnyonge wake, kwa mujibu wa kanuni ya kibabe isemayo "mwenye nguvu ndiye mwenye haki," yaani "coercive peace."
Hii ni "amani isiyo na makazi moyoni inayotokana na vitisho vya kijeshi" na ni amani ya mpito kama haitalindwa kwa mbinu halali zinazojumuisha usukuhishi, uamuzi na fidia Kwa upande ulioobewa.
Mabavu ya kipolisi na kijeshi huwa ni kwa ajili ya kufanikisha amani ya aina ya mpito Kwa msaada wa mtutu wa bunduki tu.
Lakini yaweza na inapaswa kuwa ni mbinu ya kuelelea kwenye "amani inayotokana na haki" na sio vinginevyo.
Hivyo, mara nyingi, Polisi humkamata mhalifu anayetumia silaha kwa njia ya mabavu na hivyo kutengeneza "amani inayotokana na vitisho" kama njia ya kupalilia "amani inayotokana na haki" kupitia mfumo wa utoaji haki, baada ya mkamatwaji kufikishwa mahakamani, akasilizwa kwa ukamilifu na haki ikatendeka.
Kwa jadi na historia ya ubinadamu, kanuni ya kiutu isemayo kuwa "mwenye haki ndiye mwenye nguvu", na iliyo msingi wa "amani inayotokana na haki," ndio njia sahihi ya kuhakikisha kuwa "changamoto za 2025 zisijirudie tena."
Sababu ya uwezekano huu ni kwamba ridhaa inayotokana na maamuzi huru na ya haki inadumu.
Lakini, kanuni ya kibabe isemayo kuwa "mwenye nguvu ndiye mwenye haki", na iliyo msingi wa "amani inayotokana na vitisho," ni njia sahihi ya kuhakikisha kuwa "changamoto za 2025 zinajirudia tena," katika siku za usoni, japo siwezi kusema kwa uhakika ni lini.
Sababu ni kwamba ridhaa inayotokana na kulazimishwa pamoja na dhuluma haidumu.
Kutokana na yaliyosemwa hapo juu naamini kuwa unaweza kuelewa na kukubaliana nami katika hitimisho kuwa:
Amani ya moyoni, kwa maana ya amani inayotuliza moyo Kwa sababu ya kutokana na haki badala ya amani ya kivita inayotokana na vitisho vya kijeshi, ni utulivu wa kisiasa, kiuchumi na kijamii, ambao ni tunda la ridhaa huru ya wadau.
Huchochewa na dhamira thabiti ya serikali katika kutekeleza majukumu yake ya kuheshimu, kukuza, kuhami na kupalilia haki za binadamu, kwa mujibu wa kigezo huru cha mastahili kinachofahamika kabla ya kutumika.
Msingi wake ni ukweli kwamba watu wote katika jamii ni walengwa wanaonufaika na mgawanyo wa haki na majukumu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, wakiwa tayari kupokea haki na majkumu hayo kwa hiari na bila kulalamika.
Hivyo, napendekeza kwamba unapaswa kukumbushwa kuwa, wewe kama Rais Mstaafu, unalo jukumu la kuwaelimisha Watanzania wote akiwemo Samia Suluhu Hassan na watu baki wote wenye mawazo kama yake kwamba:
Changamoto za 2025 zitajirudia tena endapo viongozi wetu hawatakubali kutofautisha kati ya "amani ya moyoni" dhidi ya "amani ya kivita" katika namna yao ya kufikiri, kuhukumu na kutenda.
Naamini kuwa kama ungefanya kazi hii mapema mara tu baada ya kukamatwa Kwa Tundu Lissu na kabla ya mauaji ya Oktoba 2025, mauaji hayo, yaliyoteketeza uhai wa watu zaidi ya 1,500, yasingetokea na uchaguzi Mkuu usingevurugika kwa kiwango cha wapiga kura waliojiandikisha wapatao asilimia 80 kukataa kujitokeza kupiga kura, na hivyo Tanzania kulazimika kusimika serikali ya kijeshi isiyo na uhalali wa KISIASA ambao huanzia katika sanduku la kura halali.
Na hata kauli za Sasa za Samia zingekuwa zinaeleweka zaidi, maana angekuwa anaongelea "amani ya moyoni" badala ya "amani ya kivita".
Lakini, kwa sasa, kila anapotumia neno "amani" raia tunamsikia akitamka "amani ya kivita" na hivyo kumweka kundi Moja na wakoloni wa kizungu hapa Tanganyika na wakoloni wa kiarabu huko Zanzibar.
Kwa mfano, juzi wakati Samia anawapongeza Taifa Stars alisema kuwa, "Waliotaka Kuharibu Amani tuliyonayo Washindwe na Walegee".
Tulichosikia akisema pale ni kwamba, "Waliotaka Kuharibu amani ya kivita tuliyonayo Washindwe na Walegee."
Katika mazingira haya, hata kauli yako kwamba "Amani tuliyonayo ni nguzo muhimu" masikioni mwetu inasikika kumaanisha "Amani ya kivita tuliyonayo ni nguzo muhimu."
Yaani, kuna bonde la ufa kubwa lebte kuvunja mawasiliano kati ya viongozi ambao ni waongeaji na wananchi ambao ni wasikilizaji wanaolengwa na serikali.
Imefika mahali sasa umma umeanza kuamini kuwa kila mtu anayetumia neno "amani" kumaanisha "amani ya kivita" ndiye mzalendo wa kweli, wakiwemo wale rafiki zetu wanaoimba wimbo wa "amani ni bora kuliko haki".
Na kwa upande mwingine, inaonekana kuwa mtu yule anayetumia neno "amani" kumaanisha "amani ya moyoni" anaonekana adui wa Taifa na huenda akatimuliwa kutoka serikalini, kama ni mtumishi wa umma.
Kama hivyo ndivyo, sasa swali linaibuka: Itawezekanaje changamoto za 2025 zisijirudie tena wakati Serikali haitofautishi kati ya "amani ya kijeshi" dhidi ya "amani ya moyo," na wakati hili ni hitaji la lazima?
Jawabu langu ninalopendekeza kwako linazo sehemu mbili. Katika upande mmoja, napendekeza kuwa, sisi kama Taifa, lazima tukubaliane kwamba mbingu yetu ni ufalme wa furaha itokanayo na tunu chanya, unaoanzia hapa hapa duniani, ukijumuisha tunu kama vile usawa wa kiutu, uhai, uhuru, afya, maarifa ya kweli, urafiki, utajiri, usawa, ukweli, ustahili, uanademokrasia, urais, furaha, upendo, matumaini, ustawi, pamoja na haki za binadamu zikiwa ni kanuni za kuongoza tabia zetu katika kufukuzia hizi tunu chanya za kibinadamu.
Na katika upande wa pili napendekeza kuwa, ufalme wa furaha itokanayo na tunu chanya, nilioujadili hapo juu, ni kinyume cha ufalme wa mateso yatokanayo na tunu hasi, unaoanzia hapa hapa duniani, ukijumuisha tunu hasi kama vile ubaguzi wa kitabaka, kifo, utumwa, magonjwa, maarifa ya uwongo, uadui, umaskini, utapeli, ukatili, utapiademokrasia, uchifu, chuki, hofu, udumavu, pamoja na majukumu ya binadamu yakiwa ni kanuni za kuongoza tabia zetu katika kuziepuka hizi tunu hasi za kibinadamu.
Kwa ufupi, ndoto ya watanzania wengi ni kuishi katika UFALME wa HAKI na amani ya moyoni.
Mkakati wa kwenda huko ni kumpata dereca anayejua kuendesha gari la maendeleo kupitia kwenye barbara ya haki sawa Kwa wahusika wote, Kila wakati na Kila mahali.
Samia na timu yake hawana ujuzi Wala utatari wa kuendesha gari hili.
Hivyo, Samia na timu yake hawana sifa ya kukalia viti vya ofisi walizomo Kwa Sasa.
Kwa maoni yangu, Yafaa maamuzi haya yafanyike kuanzia sasa hivi:
1. Jakaya Kikwete ajiuzulu nafasi zote za uteuzi alizo Nazo, ukiwemo Uchansela wa UDSM, kwa SABABU sura yake na sauti yake kwa sasa ni alama na nembo ya madudu yanayofanywa na serikali ya Samia.
2. Samia avunje serikali na bunge mara Moja kwa SABABU ya uharamu wake
3. Samia aunde serikali ya mpito
4. Serikali ya mpito iunde tume ya maridhiano,
5. Serikali ya mpito isimamie katiba mpya, na
6. Serikali ya mpito iendeshe uchaguzi mpya.
7. Serikali Mpya ifutwe mikataba yote ya kikoloni na kurejesha matrilioni yaliyotakatishwa Kwa kutumia mikataba ya ununuzi wa vifaa vya kijeshi na kutoroshwa na Timu ya Samia kwenda huko Uturuki na Uarabuni (UAE), kwa msaada wa Angela Kiziga.
Nakutakia tafakari njema kuhusu tofauti kati ya "amani inayotokana na haki" na "amani inayotokana na vitisho vya kivita" na nafasi ya tofauti hiyo katika mustakabali wa Taifa letu.
Kwa ajili hii tuombe Mungu kama ulivyosema, lakini tusisahau kuwa akili za kuambiwa tunapokuwa huko misikitini na makanisani hazitoshelezi kila kitu, na hivyo ulazima wa kuchanganya na za kwetu, kama ulivyowahi kusema.
Wako katika ujenzi wa Taifa lenye Furaha Tele.