TANESCO wamekuwa na kawaida ya kukata umeme bila mpangilio, hali ambayo inasababisha wanaunguza vitu vyetu, hiyo imekuwa tabia yao hawasemi tatizo, wanaporudisha wanaweza kuendelea na "mchezo" wa kukata na kuwasha ndani ya muda huohuo, hii inakera sana.
Kuna wakati ratiba zao za kukata umeme wamekuwa wakitangaza kupitia mitandao ya WhatsApp kwenye magroup, sasa wangapi wanatumia mitandao hiyo?
Mbona wanapokuwa na madai yao wao mfano kutaka watu walipe na vitu kama hivyo wanazunguka sehemu mbalimbali wakiwa na magari ya PA lakini ukataji umeme ujumbe wanatuma kwenye WhatsApp!
Habari ndugu mteja, asante kwa kuwasiliana nasi kupitia ukurasa huu, tafadhali pokea ufafanuzi wa TANESCO Kuhusu Changamoto ya Kukatika kwa Umeme Mkoa wa Katavi.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linapenda kufafanua hoja iliyotolewa na mwananchi kutoka Mpanda, Mkoa wa Katavi, kuhusu changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Ikumbukwe kwamba Mkoa wa Katavi ulikuwa nje ya mfumo wa Gridi ya Taifa kwa muda mrefu. Hata hivyo, kutokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkoa wa Katavi uliunganishwa na Gridi ya Taifa mapema mwaka huu 2025.
Ili kuhakikisha huduma ya umeme inakuwa ya ubora na ya kudumu,TANESCO inafanya matengenezo mara kwa mara kwenye vituo vyake vya kupokea, kupoza, na kusambaza umeme.
Matengenezo haya yanahitajika ili kuimarisha upatikanaji wa umeme wenye viwango bora, ilikuwezesha wateja kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii. Hali hii mara nyingine inahitaji kuzimwa kwa umeme ili kufanikisha matengenezo hayo na ndicho kilichotokea kwa mtoa hoja kwamba umeme ulikatwa kutokana na matengenezo yaliyokua yamepangwa kufanyika.
Hata hivyo TANESCO imekua ikitumia njia mbalimbali za mawasiliano kuwafahamisha wateja kuhusu makatizo ya umeme ikiwemo makundi ya WhatsApp, jumbe fupi za maneno (SMS) na vyombo mbalimbali vya habari hususani katika maeneo yanayoathirika, ili kuwasaidia kupanga shughuli zao mapema na katika siku ya katizo husika pia Shirika lilitangaza kupitia tangazo lililoambatanishwa hapa chini.
Shirika linaahidi kuendelea kutoa taarifa na kuimarisha njia zake za mawasiliano ili kuwafikia wateja wengi zaidi.