Mkataba wa ajira, kama ilivyo desturi kwa mikataba mingine kwa mujibu wa sheria, huzaliwa, huishi na kufa; kama ilivyo kwa binadamu na viumbe hai vingine.
Unazaliwa mara baada ya mwajiriwa na mwajiri kutia saini zao. Hapo ndipo wanapouanzisha, utekelezaji wake unapoanza kuchukua hatua na kifo ni pale tu yanapoanza kujitokeza baadhi ya mambo au masuala yanayoainishwa na sheria.
Aidha, zipo taratibu maalum za kumaliza au kuua mkataba wa ajira na hii ni katika mazingira yote, iwe kwa hiari na yale ya kumaliza kwa kulazimika kulingana na sababu mbalimbali.
Kumalizika au kukoma mkataba wa ajira kwa hiari au kufikia ukomo wa kazi kulingana na wepesi wa kutekeleza majukumu ya kazi yenyewe.
Kanuni ya 4 (1)-(7) na ya 5 (1)-(5), zote ni Kanuni za Ajira na Mahusiano Kazini, Kanuni za Utendaji Bora za Mwaka 2007, zinaeleza hakuna shida kama ilivyo kumaliza, kukoma mkataba wa ajira kwa kulazimika kutokana na sababu mbalimbali za kinidhamu.
Katika uhusiano kazini, jambo mojawapo linalomfukuza mtu kazi au kusababisha kukoma mkataba wa ajira, ni utovu wa nidhamu. Hiyo ni mojawapo, kati ya sababu za msingi zinazoweza kumfanya mwajiriwa au mfanyakazi kupoteza ajira yake.
Kimsingi, kanuni hizo zinaelekeza kuwa ni sahihi kumfukuza mfanyakazi kwa sababu za kinidhamu, lakini haimaanishi kuwa mwajiri amtafutie mwajiriwa kisa cha kuzusha au kupika, ili kumwondoa kazini.
Kinachosisitizwa hapa, ni lazima sababu hizo ziwe zimejitokeza na kuthibitika kweli na ziweze kuthibitishwa pale itakapotakiwa kufanyika hivyo.
Ujenzi wa hoja kwa kushikilia mkazo kuwa nilisikia au nahisi, zitasababisha tuhuma hizo kukosa mashiko mbele ya msuluhishi, hakimu au jaji kutegemeana na shauri lilikofika.
Kanuni ya 8 (1)(d) na 12 (1)-(5), zote za Ajira na Uhusiano Kazini na Kanuni za Utendaji Bora za mwaka 2007, sanjari na Kifungu cha 37 (2), Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, 2004 Sura ya 366, zote zinasisitiza ukweli na uthibitisho wa madai yanayotolewa.
Angalizo ni kwamba, sheria inaelekeza kuwa mwajiriwa au mfanyakazi, atafukuzwa kazi mara moja, bila ya hata kupatiwa barua ya onyo kwa kosa la mara ya kwanza au “summary dismissal”.
Kwa utaratibu huo, imafanya mwajiriwa, au mfanyakazi kupoteza haki zake zote za msingi kama kiinua mgongo. Kifungu cha 42 (1)-(4) cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya mwaka 2004 Sura ya 366 inalifafanua hilo.
Hivyo basi, ni kosa kwa mwajiri kumfukuza mfanyakazi kwa utaratibu wa mara moja, yaani ‘summary dismissal, isipokuwa kama hilo litafanyika katika mazingira ambayo sheria inaruhusu wazi kufanya hivyo na siyo kinyume chake.
Kifungu cha 41 (1)-(7) cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya 2004 sura ya 366 ina ufafanuzi.
Haki ya Kusikilizwa
Kila mtu ana haki ya kusikilizwa, kabla hatua ya kisheria kuchukuliwa. Ni haki ya asili, ambayo haiwezi kuondolewa na mtu au mamlaka yoyote ile. Kwa maana hiyo, pasipo kujali ukubwa wa kosa, hata kama kosa la mwajiriwa, mhusika anapaswa kupewa nafasi ya kutoa utetezi wake.
Atajitetea na kutakiwa kuwasilisha utetezi wake, dhidi ya: “Kwanini asichukuliwe hatua za kinidhamu?” Kanuni ya 13 (1)-(13) Kanuni za Ajira na Uhusiano Kazini, 2007 inaeleza.
Ni kosa kwa mwajiri au mkuu wa kazi kumfukuza mfanyakazi, bila ya kumpatia nafasi ya kumsikiliza au kujitetea. Hii siyo hiari ya mwajiri kuamua kumpatia mwajiriwa haki husika, bali ni haki ya msingi. Hiyo ni kwa sababu, haki yenyewe ipo kwa mujibu wa sheria, hivyo utekelezaji wake ni lazima.
Haki ya Malipo Stahiki
Kifungu cha 44 (1)(a) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, Sura ya 366, kinaelekeza haki za msingi alizo nazo mwajiriwa atakayefukuzwa kazi, kutokana na sababu za kinidhamu. Hiyo ni pamoja na kulipwa mshahara au ujira wake.
Mshahara utalipwa kwa kuzingatia tarehe ya mshahara wa mwisho mpaka siku ambayo mwajiriwa amefukuzwa, mathalan kama tarehe ya mwisho ya kupokea mshahara itakuwa Juni 30, 2019, kisha mhusika atafukuzwa Julai 17, 2019; pesa itakayotolewa ni kwa kuzingatia siku ambazo mhusika amefanyakazi. Yaani jumla ya siku 17 kuanzia tarehe 1 hadi 17 Julai. Inatajwa kuwa haki ya msingi, wala isipuuzwe kulinda maslahi ya pande zote mbili.
Ingia hapa ujisomee sheria ya ajira na mahusiano kazini
Sheria ya ajira na mahusiano kazini
==============
Michango ya wadau
----
----
----