Niliitwa kwenye usaili wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), nilipofika katika kituo nilichopangiwa nilikumbana na changamoto ambayo nimeona si sahihi.
Waombaji walikaguliwa vyeti pamoja na mavazi. Wale waliokuwa wamevaa jeans, T-shirt, raba au mavazi ambayo wasimamizi waliona hayakufaa, walipewa karatasi ya kuandika majina na namba zao za simu na wakaelekezwa kutofanya usaili.
Kilichonishangaza ni kwamba nilipouliza kwa nini hatukuona taarifa rasmi kuhusu aina ya mavazi yanayotakiwa, niliambiwa kuwa maelekezo hayo yalikuwa yamewekwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii wiki mbili zilizopita, na baadhi ya waombaji waliambiwa waangalie YouTube.
Kauli nyingine iliyotolewa ni kwamba kizazi cha vijana kimekuwa bize na TikTok. Swali langu ni: kwa nini taarifa muhimu kama hii isiambatishwe moja kwa moja kwenye ujumbe au taarifa ya mwaliko wa usaili?
Kwa kuwa waombaji waliitwa rasmi na kila mmoja akapangiwa kituo chake cha usaili, nadhani ingekuwa rahisi pia kutuma maelekezo yote muhimu, ikiwemo mavazi yanayotakiwa, kupitia njia hiyo hiyo.
Inadaiwa nafasi hiyo ya ufundi umeme ilikuwa na waombaji wengi, hivyo baadhi yetu tunajiuliza kama masharti kama haya yanaweza kuwa yanatumika kupunguza idadi ya wanaofanya usaili. Kama ndivyo, hilo si jambo sahihi na linahitaji ufafanuzi wa TRC ili mchakato wa ajira uwe wa haki, wazi na wenye usawa kwa waombaji wote.icha