JICHO LA ASKOFU KATIKA JAMII NA UCHAFU!
Wanaonekana katika picha hizi ni wanafunzi wa Shule ya Duke of York, Kenya wakiota jua na wengine wakiwa wanapumzika katika mabweni mwaka 1957. Fuatilia kwa umakini kisa hiki!
Kwa mujibu wa Odhiambo Levin Opiyo, Shule hiyo ilipoanzishwa mwaka 1949, Gavana wa Kenya wakati huo, Sir Philip Mitchell aliondoka Ikulu kwenda kuishi katika nyumba iliyokuwa Ngong kwa ajili ya kuwaruhusu wanafunzi wa kwanza kutumia makazi rasmi ya Ikulu kama mabweni hadi majengo ya shule yaliyokuwa yanajengwa yatakapokamilika.
Odhiambo anaeleza pia katika ukurasa wake ya kuwa shule hiyo ilikuwa kwa ajili ya wanafunzi wazungu (weupe) tu hadi mwaka 1960. Ilikuwa imeajiri watu kwa ajili ya kufanya kazi kama za kutunza majengo, kufanya usafi wa mazingira na kufua nguo za wanafunzi.
Chakula cha wanafunzi kilikuwa ni pamoja na nyama choma ya kondoo (roast lamb), piza na keki vilivyotayarishwa na mpishi aliyetakiwa kufuata kanuni ngumu za lishe katika kuandaa vyakula hivyo.
Baada ya Uhuru, Duke of York ilibadilishwa na kuwa Lenana School. Nilifika Lenana School mwaka 1999 kuhudhuria Mkutano wa Walimu na Watumishi wa Scripture Union of Kenya (Umoja wa Kujisomea Biblia nchini Kenya. Niliongoza ujumbe wa watu 4 kutoka Tanzania ambao ni Wilson Adam, Gloria, Asifiwe Aloyce na mimi mwenyewe. Aliyekuwa Mgeni Rasmi katika Mkutano ule alikuwa ni Waziri wa Elimu wa Kenya wakati ule, Mhe. Kalonzo Musyoka.
Lenana School ni shule maarufu sana nchini Kenya kwa miaka mingi. Ukitaka kujua ilikuwa ni shule ya aina gani, kwa hapa nchini Tanzania ingeweza kulinganishwa na shule kama Tabora Boys na Azania kwa shule za serikali au Minaki, Tosamaganga, Pugu, Mazengo, Rungwe hata Umbwe kwa shule zilizokuwa za misheni.
Ukiachia mbali mambo mengine yatakayoiacha wazi midomo yako, suala la kuajiri watu kwa ajili ya kutunza majengo ya shule ni jambo lililo muhimu sana katika uimara na ubora mzima wa majengo. Hao huitwa estate managers na ni wahitimu wa kozi maalum katika vyuo vikuu kama Chuo Kikuu cha Ardhi.
Lakini sidhani kama wahitimu wa Chuo Kikuu cha Ardhi wameajiriwa kwa ajili ya kuyatunza mazingira ya majengo yote ya umma zikiwemo shule zetu. Ukienda Azania, Tambaza, Pugu na hata Zanaki unaweza kufikiri ni magofu ya kale.
Ukifika shule hizo na shule nyingine, usifanye kosa la kuingia chooni.
Kwa shule za wavulana kama Azania, zilikuwa na sehemu maalum ya haja ndogo ambapo kila wakati maji yalitiririka kutoka katika mabomba yenye matundu maalum ukutani ili kutiririshia mikojo katika mabomba maalum. Nilipokuwa Kidato cha Kwanza, niliukuta mfumo huo pale Azania ukiwa taabani ingawa ulikuwa unafanya kazi, lakini nilipoondoka Kidato cha Sita hali ilikuwa mbaya sana.
Hata 'Bwawa la Kisusulinge' 'the Amoeba Pond' pale Azania nililikuta likiwa na maji na samaki kadhaa. Lakini sasa, ninapowauliza wanafunzi wa pale wanasema limefukiwa na mchanga.
Lakini kilichonishangaza ni kuwa, nilipokuwa nchini Uingereza, mfumo huo unaendelea tena kwa ubora zaidi. Shule kama Azania au Zanaki wanaajiriwa wataalamu wafuatao: Watunza bustani (gardeners), wahandisi wa mifumo (engeneers), watu wa kufanya matengenezo, nk.
Chuo Kikuu cha Ardhi kinatoa wahandisi wa mazingira kila mwaka lakini wengi hawana ajira wakati majengo yetu ambayo yalijengwa kwa mabilioni ya mikopo ya fedha yanazidi kuoza kwa kukosa uangalizi. Mitaro ya Maji machafu katika Jiji la Dar es Salaam iliziba na njia zake zote hazifanyi kazi. Ukitaka kujionea kwa jinsi gani sisi ni wachafu, tembelea Barabara zote za katikati ya Jiji wakati mvua inanyesha kama Barabara ya Umoja wa Mataifa, nk.
Wakati wa mvua mifuniko ya maji machafu hufunguliwa ili kuruhusu maji machafu yenye kinyesi yatitirishwe na maji barabarani. Hali inakuwa mbaya zaidi kama mvua iliyonyesha ni kidogo na hivyo maji machafu yanaonekana.
Je, wewe ni mkazi wa Dar es Salaam? Je wewe ni miongoni mwa waliosoma shule zilizotajwa? Je, wewe ni mtumishi katika serikali na unaona hali ya majengo ya serikali? Je, maelezo hayo ya askofu katika maeneo hayo yana ukweli kwa kiasi gani? Je, unafikiri majengo yote ya serikali yameajiri wahandisi kama estate managers na kama environment engeneers? Je, unafikiri hili Jiji la Dar es Salaam limeajiri kweli wahandisi wa mazingira?
Je, nini kimekushangaza? Je, nini maoni yako?
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula
Itunge, Dar es Salaam; 6 Februari 2026; Saa 2:50 asubuhi