Naam Bwana huyu alikuwa anajiita Victor Lustig. Wengine walimfahamu kama “Count Victor Lustig”, wengine kama Robert Miller jina mojawapo tu kati ya zaidi ya majina 45 aliyokuwa akitumia. Lakini nyuma ya majina hayo yote, kulikuwa na mtu mmoja mwenye akili ya kipekee katika sanaa ya udanganyifu; mtu ambaye aliwahi kuuza Eiffel Tower… si mara moja, bali mara mbili.
Alizaliwa mwaka 1890 katika mji wa Hostinné, eneo ambalo leo ni sehemu ya Czech Republic, lakini wakati huo lilikuwa ndani ya Dola ya Austria-Hungary. Asili yake haikuwa ya kifahari sana kama alivyopenda kujionesha; baadhi ya vyanzo vinasema familia yake ilikuwa ya kawaida, wengine wanasema ilikuwa maskini. Lakini jambo lisilopingika ni kwamba alipata elimu nzuri na mapema sana aligundua nguvu ya lugha. Hivyo alijifunza Kifaransa, Kiingereza, Kijerumani, Kicheki na lugha nyingine kadhaa. na lugha ndo ilikuwa silaha yake kubwa.
Alikuwa na kovu kwenye shavu la kushoto .. hadithi zinasema alichanwa na mke mwenye wivu. Haijulikani kama ni kweli au ni hadithi nyingine tu iliyoongeza mvuto wake. Kwa sababu Lustig aliishi kwa hadithi. Alijijengea taswira ya mtu wa tabaka la juu, mwenye heshima, mwenye sauti tulivu na mavazi ya kifahari. Hakuwa jambazi wa kutumia bunduki. Bali alikuwa jambazi wa akili.
Kwa mara ya kwanza kabisa katika matukio yake, alianza kwa ulaghai mdogo kwenye meli zilizokuwa zikisafiri kati ya Ulaya na Marekani. Aliwadanganya abiria matajiri kwa michezo ya kamari, mikataba hewa, au uwekezaji wa uongo. Lakini akili yake haikutosheka na pesa ndogo. Alihitaji kitu kikubwa. Kitu cha kihistoria....
Mwaka 1925, akiwa Paris, alisoma makala ndogo kwenye gazeti iliyolalamikia gharama kubwa za kulihudumia Mnara wa Eiffel. Mnara huo, uliojengwa mwaka 1889 kwa maonyesho ya kimataifa, haukupendwa na wote mwanzoni, na kulikuwa na mijadala ya kuubomoa. Watu wengi waliona kama ni mzigo wa kifedha.
Ndipo wazo la ajabu lilipozaliwa.
Je, kama serikali ingetaka kuuza mnara huo kwa chuma chakavu… kwa siri?
Baada ya wazo hilo...
Lustig alitengeneza hadithi kamili. Aliajiri mtengenezaji wa hati bandia kuandaa karatasi rasmi zenye stempu za serikali ya Ufaransa. Akajipa cheo cha Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Posta na Telegraph. Akakodisha chumba cha kifahari katika Hôtel de Crillon, moja ya hoteli za hadhi ya juu zaidi Paris. Kisha akaalika wafanyabiashara wakubwa wa chuma chakavu kwa mkutano wa siri.
Aliwaambia kuwa serikali imeamua kuubomoa mnara huo kimyakimya ili kuepuka hasira za umma, na wanahitaji mnunuzi wa chuma hicho. Aliwapeleka hadi kwenye mnara kwa ziara maalum, akazungumza kwa kujiamini, akataja takwimu za uzito wa chuma, gharama za matengenezo, na taratibu za zabuni.
Mmoja wao, André Poisson, aliona fursa ya maisha. Lakini Lustig kutokana na ujanja wake hakuuza tu mnara; aliuza pia hofu ya kukosa nafasi. Alimshawishi Poisson kwamba kulikuwa na ushindani mkali, na kama angeongeza “kiasi kidogo cha ziada” kwa ajili ya kurahisisha mchakato, mambo yangekwenda haraka.
Poisson alitoa hundi kubwa, inayokadiriwa kufikia karibu franc milioni moja, pamoja na rushwa ya ziada.
Lustig alipokea pesa, akafunga mizigo yake, na kutoweka Paris mara moja.
Cha kushangaza, Poisson baada ya kutapeliwa hakuenda polisi mara moja. Aibu ilimzuia. Aliogopa kuonekana mjinga mbele ya jamii ya wafanyabiashara. Poisson akaona mambo yasiwe mengi akakausha.
Baada ya mwezi mmoja tu, Lustig alirudi Paris na kujaribu kuuza mnara huo tena kwa kundi jipya. Safari hii, mmoja alishtuka mapema na kuwasiliana na polisi. Lakini Lustig alikuwa tayari ametorokea na kukimbilia Marekani.
Alivyofika marekani akafanya tukio lingine. Kwa kuuza “Rumanian Box” kifaa kidogo kilichodaiwa kuchapisha noti halisi za dola mia moja. Aliweka noti halisi ndani kama mfano, mashine “ikatoa” noti nyingine. Mnunuzi alipoenda nyumbani, mashine ilifanya kazi kwa muda mfupi kisha ikanyamaza milele. Watu walilipa kati ya dola 20,000 hadi 50,000 kwa kifaa hicho.
Hata jina la Al Capone liliingia kwenye orodha ya waliokutana naye. Lustig alimshawishi Capone ampe dola 50,000 kwa uwekezaji fulani. Badala ya kukimbia nazo, alizihifadhi kwa muda kisha akazirudisha akidai biashara haikufanikiwa. Capone alivutiwa na “uaminifu” huo na akampa zawadi ya pesa kama shukrani. Hivyo Lustig alimlaghai bila hata kuiba rasmi.
Baadaye alihusika katika uchapishaji wa noti bandia za dola mia moja nchini Marekani, kiasi kikubwa cha fedha bandia kikaingia katika mzunguko wa pesa. Hatimaye, mwaka 1935, maafisa wa Secret Service walimkamata New York. Alihukumiwa miaka 20 gerezani na kupelekwa katika gereza maarufu la Alcatraz, kisha baadaye Springfield, Missouri.
Inasemekana aliwahi kuandika ukutani mwa seli yake ujumbe mfupi kuhusu Mnara wa Eiffel, akijivunia kwamba aliwahi kuuuza kwa franc 100,000. Hadi gerezani, alibaki kuwa muuzaji wa hadithi.
Alikufa Machi 11, 1947 kwa nimonia, akiwa na umri wa karibu miaka 57.
Hakuwahi kutumia bunduki. Hakuvunja milango kwa nguvu. Silaha yake ilikuwa saikolojia .... tamaa ya faida ya haraka, hofu ya kukosa nafasi, na aibu ya kukubali kudanganywa. Aliwafanya watu matajiri, wasomi, na wenye mamlaka waamini ndoto isiyowezekana.
Na hapa ndipo funzo linapojitokeza: mara nyingi si ujinga unaotuangusha, bali uchoyo na kiburi. Watu hawadanganywi kwa sababu hawana akili. Wanadanganywa kwa sababu wanataka kuamini kitu kinachowanufaisha.
Huyu mwamba hakuiba tu pesa. Alikuwa anaanza kwanza kuuza matumaini, kisha hadhi, na watu walikuwa wanaingia kwenye mitego yake kirahisi tu.
Naam namaliza namna hiyo.... Hii nimoja ya story za kufurahisha tu hasaa kujua kuwa ulimwengu unawatu wajanja wasioogopa.