Kwenye harakati zangu za kufuatilia majukwaa mbalimbali ya kampeni ya wagombea Urais mbalimbali, kwa hali isiyotegemewa ghafla nimemsikia mgombea Urais wa Chadema Ndugu Tundu Lissu akiongea kwenye mkutano wake wa kampeni kule Karagwe, Bukoba kuhusu viongozi wetu wa dini.
Kwenye mkutano huo, Lissu licha ya mambo mengine aliyoyazungumza lakini zaidi alitamka hadharani kwamba katika nchi hii yote ya Tanzania viongozi wa dini wenye akili na waliobaki ni watatu tu. Lissu aliwataja kwa kile alichokiita viongozi hao ndio national conscious yaani ndio viongozi wenye akili na wanaojitambua kuwa ni Askofu Bagonza, Askofu Mwamakula na Sheikh Katimba nje ya mamia ya viongozi wetu wa dini.
Lissu anasema hao watumishi wa umma watatu ndio viongozi pekee wanajitambua nje ya mamia kwa mamia ya viongozi wetu wa dini. Wakati nikitafakari kauli hii, ghafla nakumbuka namna sasa ilivyokuwa ni kama tabia iliyoota mizizi kwenye chama hicho na mwendelezo wa Lissu na chama chake kushambulia, kutweza utu, heshima na kutukana makundi mbalimbali kwenye jamii yetu na mara hii kwa viongozi wetu wa dini.
Baada ya kutweza na kuwavunjia utu waandishi wa habari kwa kuwafukuza kwenye mikutano yao, kukashfu wasanii kwa kuwaita watu wanaojipendekeza na wanaoburuzwa, kuwaita watumishi wa umma watu wa majalalani na makundi mengine mengi kwenye jamii sasa Lissu amevuka mipaka mpaka kuwavunjia adabu viongozi wetu wa dini. Hivi kwenye nchi hii viongozi wenye akili ni watatu tu? Hao wengine wote kwa mujibu wa Lissu ni hovyo na wala hawana akili yoyote ile. Lissu anakashfu watu hawa muhimu kwa ustawi wa nchi yetu mbele ya mkutano unaorushwa mpaka na vyombo vya habari. Dharau gani hii?
Viongozi wa dini ni kama Baba, Walezi wa amani na wapatanishi kwenye nchi, leo mtu mmoja tu tena anayetaka ridhaa ya cheo kikubwa kama cha Urais anakaa hadharani mchana kweupe kukashfu na kutukana waziwazi viongozi wetu wa dini. Watu wanaofanya kazi kubwa namna hii kwenye nchi.
Hii, moja ni dharau kwa watumishi wenyewe wa dini, familia zao na kundi kubwa la waumini walioko nyuma yao. Mtu kama Askofu Kakobe au Mufti Zubeir unamvunjia heshima maana yake umekashfu kundi kubwa la watu lililoko nyuma ya watu hawa. Pili ni hatari kwa mtu anayetaka Urais wa nchi kufanya kejeli kiasi hiki ambapo hana hata huo Urais, kushambulia na kutukana makundi mbalimbali kwa jamii.
Hili ni la kukemewa na kupigwa vita na watu wote. Na viongozi wa dini kama walezi wanalo jukumu la kutoa tamko kukemea vitendo hivi. Tunafahamu nyakati za kampeni ni za kuomba kura na kujinyenyekea kwa watu ili wakuchague. Sasa hawa ambao hata kabla hawajapata huo Urais wanakuwa viburi na kejeli namna hii kesho wakiupata huo Urais itakuwaje? Mtu mwenye shida anakuwa jeuri namna hii mkimpa hicho cheo hali itakuwaje? Watanzani twende tukawanyime kura watu hawa Oktoba 28.
Bwanku M Bwanku