Thiologia, yaani ilimu ya Ungu, ya Mtakatifu Paulo iliikuza hiyo imani ya Dhambi ya Asili kuthibitisha imani nyengine, yaani imani ya kuokoka kwa kifo cha Yesu msalabani.
Katika barua yake aliyowapelekea Warumi Paulo aliandika hivi:
Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi; maana kabla ya sheria dhambi ilikuwamo ulimwenguni, lakini dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria; walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, aliye mfano wake yeye atakayekuja. Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi.
Warumi 5.12-15
Pia vile vile Paulo aliwaandikia Wakorintho:
Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhaalika na katika Kristo wote watahuishwa.
1 Wakorintho 15.22
Paulo anakusudia kusema kuwa wanaadamu wote, wameingia makosani kwa vile Adam alivyovunja amri ya Mwenyezi Mungu, ndio maana ya kufa kwao; mpaka kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo ndiko kumeleta uhai kwa wenye kumuamini kuwa yeye ni Mwana wa Mungu aliyekuja duniani kwa ajili ya kuwaokoa walimwengu kwa kuteswa na kutundikwa msalabani na kufa na kuingia Jahannam na kisha kufufuka na kupaa mbinguni.
Haya ni mafunzo ambayo Paulo amejaribu kufunza katika barua zake.
Lakini imani aliyofunza Paulo ya Dhambi ya Asili ya kurithiwa inapingwa na vifungu vingine kutokana na Biblia.
Katika Kumbukumbu la Torati, kwa mfano (na hicho ni katika vitabu vitano vinavyohisabiwa kuwa ndiyo Torati inayoaminiwa na Mayahudi na Wakristo) Musa anasema:
Mababa wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuwawe kwa ajili ya baba zao; kila mtu na auawe kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe.
Kumbukumbu 24.16
Hali kadhaalika tunasoma neno la Mungu katika kitabu cha Yeremia:
Siku zile, hawatasema tena, Baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi. Bali kila mtu atakufa kwa sababu ya uovu wake mwenyewe; kila mtu alaye zabibu kali, meno yake yatatiwa ganzi.
Yeremia 31.29-30
Tena Neno la Mungu linaendelea kusema katika kitabu cha Ezekieli kwa uwazi zaidi:
Lakini ninyi mwasema, Kwani yule mwana asiuchukue uovu wa baba yake?
Yule mwana atakapofanya yaliyo halali na haki, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, hakika ataishi. Roho itendayo dhambi, ndiyo itayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe; haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake.
Ezekieli 18.19-20
Hayo tuliyoyanukulu kutokana na vitabu vya Yeremia na Ezekieli ni maneno ya Bwana Mungu, na yale yaliyotoka katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati ni maneno ya Musa, ambaye alileta sharia itokayo kwa Bwana Mungu na ambayo Yesu alisema kuwa yeye hakuja kuitengua hata nukta moja bali amekuja kuitimiza tu.
Ni wazi kabisa kuwa nadhariya ya Paulo ya dhambi ya asili ya kurithiwa inagongana na neno la Mungu kama lilivyo katika Biblia.