Sanamu katika maana halisi ya Kibiblia ni mtu au kitu chochote kile cha Mbinguni au Duniani ambacho binadamu anakipa hadhi sawa na au kupita Mwenyezi Mungu, anakitegemea kupita ambavyo anamtegemea Mungu, anakiamini kuliko anavyomwamini Mungu, anakipenda kuliko anavyompenda Mungu. Kwa maneno mepesi kabisa, ni kitu chochote au mtu yeyote ambaye binadamu husika anakitumainia au kumtumainia na kukithamini au kumthamini kuliko Mwenyezi Mungu. Kwa ufupi kabisa, ni kitu au mtu yeyote kinachopewa au anayepewa hadhi sawa na Mwenyezi Mungu.
Kila mtu katika udhaifu wake, kwa namna moja au nyingine ana mungu wake; kama unapenda mpira kuliko Mungu, mungu wako ni mpira; kama unapenda pesa kuliko Mungu, mungu wako ni pesa; kama unamwamini na kumtegemea mganga wa kienyeji kuliko Mungu, mungu wako ni huyo mganga; kama unamheshimu binadamu yeyote kuliko unavyomheshimu Mungu, huyo binadamu ni mungu wako; kama unayapa kipaumbele masomo kuliko Mungu, hayo masomo ndio mungu wako; kama unapenda kuchat kuliko Mungu, hizo chattings ndio mungu wako; kama unapenda pombe kuliko Mungu, pombe ndio mungu wako; na mambo mengine kama hayo.
Ukitaka kujua kitu gani unakipenda, kukiamini na kukithamini kuliko Mungu, ujiulize tu maswali mepesi; ni mara ngapi umeshindwa kuhudhuria misa au ibada kwasababu una mitihani siku za usoni na umetingwa ukijiandaa na mitihani? Mara ngapi umeshindwa kuhudhuria misa au ibada ikiwemo jumuia eti kisa kuna mechi unaenda kutazama? Mara ngapi umeshindwa kuhudhuria ibada eti kuna mtu muhimu anakuja kukutembelea? N.k
Kiuhalisia kuabudu sanamu ni dhambi. Mungu alipokuwa anampa Musa amri kumi mlimani Sinai, hii ni amri ya kwanza ambayo anampa “Usiwe na miungu mingine, ila mimi. Usijifanyie sanamu ya miungu wa uongo, au kinyago chochote kilicho mbinguni, katika nchi au majini chini ya dunia” Kutoka 20:3-4 Kujifanyia sanamu zetu wenyewe, kama nilivyoainisha hapo juu, ni dhambi; kwasababu inaenda kinyume na mapenzi ya Mungu, inaonesha kukata tamaa, kwamba Mungu si kitu katika maisha yako; kwamba hawezi kukupa furaha, amani, ushindi, n.k ambavyo unaweza kuvipata kwa kitu au mtu unayemuabudu.
Tuna mifano mingi katika Biblia inayoenesha kuwa Mungu anachukizwa na ibada ya sanamu kitu kinachopelekea awaadhibu wale wote wanaokiuka amri hii. Hapa tutaona michache;
Baada ya Musa kukawia kurudi kutoka mlima Sinai, tunawaona Waisraeli wanamshinikiza Aaron awatengenezee mungu, naye anawatengenezea mungu wa dhahabu ambae wanamtolea dhabihu na kumwabudu wakisema “Ee Israeli, huyu ndiye mungu wetu aliyetutoa nchini Misri” Kut 32:4 Pamoja na maombezi ya Musa kwa Mungu, na msamaha ambao Mungu anawapa Waisraeli, tunaona anawapa adhabu kwasababu wametenda dhambi, dhambi ya kumwabudu mungu (sanamu ya ndama wa dhahabu) waliojifanyizia.
Katika kitabu cha Wafalme; tunamwona mfalme Hezekia akimpendeza Mungu baada ya kuharibu mahali pote pa kuabudia miungu ya uongo na kuvunja nguzo za mungu Ashera, pamoja na Nehushtani, nyoka ya shaba ambayo ilitengenezwa na Musa ili kuwaponya waliokuwa wakiumwa na nyoka kule jangwani. 2Fal 18:4-5 Mungu anapendezwa na Hezekia kiasi ambacho mwandishi anakilinganisha na upendo wa Mungu kwa Daudi.
Kwasababu anapinga kwa vitendo na kuharibu mambo yanayomchukiza Mwenyezi Mungu, ibada kwa miungu ambayo ni sanamu.
Kutokana na mifano michache kutoka kwenye Biblia Takatifu hapo juu, sina wasiwasi na ukweli kuwa ibada yoyote kwa sanamu ni ya uongo na ni dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na kama tunavyojua kuwa mshahara wa dhambi ni mauti.
Je, Wakatoliki wanaabudu sanamu?
Moja ya maswali na tuhuma kuu na ya mara kwa mara kwa Kanisa Takatifu Katoliki la Mitume, ni ibada juu ya sanamu; Wakatoliki wanatuhumiwa kuabudu sanamu kinyume na agizo la Mwenyezi Mungu kwenye hicho kipengele cha Biblia cha Kutoka 20:3-4
Katika ibada ya kukumbuka mateso makali na kifo cha Mwokozi wetu, Bwana Yesu Kristu, siku ya ijumaa kuu; Wakatoliki pamoja na mambo mengine huabudu msalaba, kitendo kinachounganishwa na ibada kwa sanamu. Wanaotuhumu, hudai kuwa sanamu ni huo msalaba. Pamoja na msalaba pia vielelezo mbali mbali kama vile picha, sanamu ya Bikra Maria, Watakatifu, n.k Je, kuna ukweli wowote katika tuhuma hizi?
“Huu ndio mti wa msalaba, ambao wokovu wa dunia umetundikwa juu yake.., Njoni, njoni, njoni; tuuabudu” Ni sehemu ya ibada hiyo kwa msalaba siku ya Ijumaa kuu.
Kuna vitu viwili ambavyo watuhumu, aidha kwa kujua au kutokujua, huvichanganya.
- Mosi; maana halisi ya ibada kwa sanamu kama nilivyoeleza kwa ufupi hapo juu na
- Pili; mafundisho ya Kanisa Katoliki katika Fumbo hili Kuu la Pasaka.
Wakatoliki wanapoabudu Msalaba, akili na malengo yao ya kufanya hivyo huenda mbele zaidi (beyond) ya sanamu ya Msalaba iliyopo mbele yao.
Katika Biblia Takatifu, tunaona Waisraeli wanamnung’unikia Mungu baada ya kufa moyo walipokuwa wakitoka mlima Hori mpaka Edomu kupitia bahari ya Shamu. Tunaona Mungu anawapelekea nyoka wenye sumu wanaowauma na wanaoumwa wanakufa. Tunawaona wanajirudi na kumwomba Musa awaombee ili Mwenyezi Mungu awaondoe nyoka wale. “Tengeneza nyoka wa shaba, umtundike juu ya mlingoti. Mtu yeyote atakae umwa na nyoka, akimtazama nyoka huyo wa shaba, atapona” Hesabu 21:8
Mungu anamwamuru Musa, Musa anatekeleza na kila anaefanya hivyo anapona.
Je, nyoka huyo anawaponya? La hasha, anaewaponya ni Mungu mwenyewe aliemwingi wa Huruma. Nyoka anakuwa chombo cha Huruma na Msamaha wa Mungu; kwamba kila anaemtazama yule nyoka anakiri na kushuhudia Upendo na Msamaha wa Mungu. Kwahiyo nyoka wa shaba anakuwa ni kiungo cha mawasiliano kati ya Mungu na Waisraeli.
Wanachofanya Wakatoliki, ni kumwabudu Mungu mwenyewe, ule msalaba ni kielelezo kinachowasaidia kutimiza lengo lao la kumwabudu Bwana Yesu. Wanaabudu wokovu wenyewe uliowafikia kupitia msalaba na sio ile sanamu.
Uhalisia katika mashule, vyuo na sehemu nyingine za mafunzo zinaonesha kuwa watu huelewa zaidi wakifundishwa au kuelekezwa jambo fulani kwa vielelezo kuliko bila vielelezo; hivyo, kwa Wakatoliki, Msalaba huwasaidia katika tafakari.
Waha ni kabila linalosifika sana kwa ubishi nchini Tanzania, siku moja Muha mmoja alimtembelea Msukuma. Wakiwa katika kikome usiku; Muha, baba mwenye ile nyumba pamoja na watoto walikuwa wanachoma viazi. Yule baba mwenye nyumba ghafla akainua kidole juu akiashiria kuonyesha kitu. Yule Muha akamuangalia yule mzee, mpaka kidole kilipoishia. Wale watoto wakaangalia mawinguni na kustajaabu, yule Muha akawashangaa, akawadharau na kuwaona kuwa hawana akili. Lakini kumbe wale watoto walipoangalia mawinguni waliona nyota nzuri sana iliowafanyanya wastaajabu, they went beyond.
Kutokana na maelezo yangu hapo juu, japo ni mafupi ila yanaeleweka; kwamba Wakatoliki popote duniani huwa hawaabudu sanamu. Hawaupi mti wa msalaba hadhi sawa na Mungu, bali msalaba unakuwa kiunganishi kizuri kati yao na Mungu. Mkatoliki anapouona msalaba, anakumbuka upendo wa Bwana Yesu, aliyemfia pale msalabani. Na huo ndio uhalisia.
Habari zenu...