Mimi hofu yangu ni wale wanaopotoshwa na wakapotea. Yesu aliwahi kusema hata kama una kondoo mia, moja akipotea unaacha 99 na kumtafuta mmoja aliyepotea. Swali la kijiuliza haya makanisa yanayoibuka Kila kukicha wanapata wapi waumini?
Kanisa Katoliki kazi yake kubwa ni kuwapa mafundisho ya kweli ya Kristo, na siyo kubishana na watu wasioelewa. Kama kuna muumini ataamua kutosikiliza mafundisho yaliyo sahihi, hakuna namna ya kufanya.
Kumbuka kuwa hakuna Kanisa lenye hazina kubwa ya historia ya ukristo kama Kanisa Katoliki, labda mtu aamue kutotaka kujifunza na kutafuta majibu kwa mambo asiyoyajua au yanayomtatiza.
Fahamu kuwa hata Biblia hii ambayo makanisa yote yanatumia, ni Kanisa Katoliki ndiyo lililokusanya na kuweka katika muundo huo uliopo sasa. Kristo alipoondoka hakuacha Biblia, hakuacha kitabu, bali aliacha mitume, na akawapa maagizo.
Biblia unayoiona leo, ilikuja kuwa katika muundo unaokaribia na tulio nao leo, kama miaka 300 baada ya Kristo.
Kwa hiyo huko nyuma kote, ukristo ulienezwa kwa njia ya mafundisho ya mitume. Ndiyo maana tunasema imani ya Kanisa Katoliki imejengeka kwenye mapokeo (yaani wakristo wa mwanzo walifanya nini, katika jambo gani) na neno la Mungu ambalo ni biblia.
Wale wanaotegemea tu kilichoandikwa kwenye Biblia pekee, wanakosa mengi. Kwa maana sehemu nyingine ni maagizo tu lakini yasiyo na ufafanuzi au maelekezo ya namna ya kutenda.
Kwa mfano, Kristo alisema hakuna amri iliyokubwa kuliko amri ya upendo. Baada ya hapo unaenda kwenye mapokeo, unaenda kuona ni namna gani wakristo wa mwanzo waliitekeleza amri hii ya upendo.
Kristo alisema, salini. Tunaenda kuangalia kwenye mapokeo, wakristo wa mwanzo walikuwa wanafanya namna gani ibada zao. Hata kama kutakuwa na mabadiliko ya kiasi fulani kutokana na hali ya wakati (kama vile wakati wa kale watu walikuwa wachache sana, sasa hivi tupo wengi sana) lakini msingi wa kufanya ibada ni lazima uwe ni ule ule maana ndivyo walivyofundisha na kutenda mitume na wakristo wa mwanzo.